Vidonda vya tumbo (peptic ulcers) bila shaka sio jina geni kwako na inawezekana umewahi kupata tatizo hili au unalo muda mrefu na haliondoki.
Vidonda vya tumbo ni hali ya sehemu ya ukuta wa tumbo kulika au kuchubuka na hivyo kutengeneza vidonda ambavyo huchukua muda kupona na huambatana na maumivu makali hasa wakati wa usiku.
Kama yalivyo matatizo mengine, tatizo la vidonda vya tumbo linaweza kuwa sugu na kupelekea hali mbaya kiafya.
Vidonda hivi vinaua, moja ya tatizo lake kubwa ni kusababisha tumbo kutoboka na kuvujia ndani, kama huduma ya kwanza ikichelewa, unaweza kufa.
Ni miongoni mwa magonjwa yanayohitaji nidhamu ya hali ya juu, na kukosa nidhamu hii kumepelekea watu kuishi na madonda ya tumbo muda mrefu.
Kiuhalisia, tatizo la vidonda vya tumbo halipaswi kuwa sugu, linapaswa kutibiwa na kupona.
Sababu mbalimbali huweza kusababisha mtu kupata madonda ya tumbo kama ifuatavyo:
- Maambukizi ya bakteria aina ya h-pylori
- Kushinda njaa muda mrefu
- Kuwa na msongo wa mawazo
- Hali ya mwili wako kutoa asidi nyingi hivyo kupelekea ukuta wa tumbo kulika
- Utumiaji wa vinywaji au kemikali yenye asidi kali
- Utumiaji wa spicy zenye pili pili kali
- Uvutaji wa sigara, na kadhalika.
Dalili za vidonda vya tumbo huwa:
- Maumivu ya tumbo ya kuwaka moto ambayo huja kabla au baada tu ya kula
- kiungulia cha mara kwa mara
- Tumbo kujaa gesi
- Kichefuchefu na kutapika
- Kupungua uzito, na wakati mwingine kutapika damu
- Choo ngumu, na wakati mwingine kupata choo cheusi.
Dalili zipi kati ya hizo unazo?
Sababu hizo huweza kupelekea kupata vidonda vya tumbo, na namna pekee ya vidonda kupona ni kuziondoa sababu hizo.
Kwanini baadhi ya watu wakiugua vidonda vya tumbo na kutibiwa hupona na wengine hawaponi? Hapa nitakupa sababu tano zinazofanya vidonda vyako vya tumbo visipone.
Kwanza kabisa unapaswa kujua matibabu ya vidonda vya tumbo hayapo tu kwenye kumeza dawa peke yake, bali yanahitaji nidhamu ya hali ya juu ya dawa na kuepuka vichonganishi (risk factors).
Matibabu yake sio kama ya malaria au UTI, kwamba ukimeza dawa tu kwishnei, bali matibabu yake uhitaji zaidi ya hayo, na hivyo kufanya tatizo hili kuwa kati ya matatizo magumu kutibika.
Hizi hapa sababu tano kwanini vidonda vyako vya tumbo haviponi:
1. Haupati tiba sahihi
Kama nilivyotaja hapo juu, visababishi huwa ni vingi na nidhamu ya kutibu vidonda vya tumbo ni tiba sahihi kwa ya kujua kisababishi na kukiondoa. Tatizo lako bado hujajua kisababishi ni nini.
Mfano kama kisababishi ni bakteria aina ya pylori, basi unapaswa kwanza upime damu au choo na baada ya hapo upate tiba.
Tiba anayoipata mtu mwenye vidonda vinavyosababishwa na h-pylori bakteria ni tofauti kabisa na mwenye vidonda vinavyosababishwa na mambo mengine.
Mtu mwenye tatizo la kuwa na asidi nyingi tumboni anaweza kuwa na vidonda vya tumbo sugu, lakini usipopima na kujua utaendelea kuwa na vidonda kwa muda mrefu.
Tatizo ni pale unapopata tiba ambayo haiyendani na kisababishi cha vidonda vyako. Kila ukisikia maumivu unaenda pharmacy unapewa magnesium, unameza, maumivu yakipungua kidogo, uunaendelea na maisha. Hapo ndipo kosa lako lipo.
Unapaswa kwenda hospitali kupima na kujua sababu hasa ni nini. Kama sababu ni matumizi ya kemikali fulani, vidonda vyako vitapona endapo utapata dawa na kuacha matumizi ya kemikali hiyo.
Fanya hili sasa: Nenda kwanza hospitali upime choo au damu ili daktari aweze kutofautisha sababu ya tatizo lako. Baada ya hapo pata matibabu kulingana na kisababishi chako.
Vipimo vingine vya vidonda vya tumbo ni kwa kutumia OGD au Endoscopy. Vifaa hivi huweza kuchungulia tumboni na kuangalia ukubwa wa vidonda na pengine kuvikausha kabisa.
Acha kukaa mtaani na kulalamika tumbo linauma mwaka mzima! Pata tiba sahihi.
2. Haumalizi dawa
Pamoja kwamba umepima na kuambiwa una maambukizi ya bakteria wa h-pylori na kupewa dawa ya kutumiwa; kuna uwezekano mkubwa haumalizi dozi yako unayopewa au unasahau kumeza.
Endapo umegundulika na vidonda vya tumbo vinavyosababishwa na h-pylori, basi hupewa dozi ya dawa tatu ambayo humezwa kwa muda wa wiki mbili na uhusisha umezaji wa dawa nyingi.
Watu wengi hawamezi hiyo dawa kwa wiki mbili, wengi wao huishia njiani baada ya kupata nafuu. Mtu atameza kwa siku saba za kwanza na baada ya hapo zitamchosha na ataziacha kwa kisingizio kwamba anahisi amepona.
Kama nilivyosema, matibabu ya vidonda vya tumbo yanahitaji nidhamu kubwa na ya hali ya juu.
Kiuhalisia kumeza dawa aina tatu kwa wiki mbili na mara nyingine mpaka mwezi ni mtihani mkubwa, lakini ndio njia pekee ya kutibu bacteria wa h-pylori.
Unapaswa kuwa na nidhamu kubwa na wengi wenye nidhamu hii hupona haraka na kuendelea na Maisha mengine, wakati wale wasiokuwa na nidhamu ya kumaliza dawa hujikuta wakipata tatizo la kujirudia mara kwa mara.
Utafiti unaonyesha kutotibu vizuri bakteria wa h-pylori na kuwaaacha kushambulia tumbo kwa muda mrefu yaweza kupelekea kupata maradhi ya saratani ya tumbo. Utafiti uliofanywa mnamo mwaka 1994 na kitengo cha kimataifa cha utafiti wa saratani cha shirika la afya duniani lilibainisha bakteria aina ya h-pylori kama moja ya visababishi vya kansa ya tumbo.
Hivyo ni muhimu kuwa na nidhamu na kukamilisha matibabu yake.
3. Unashinda njaa muda mrefu
Moja kati ya vitu vinavyoweza kufanya vidonda kuchimbika na kuwa sugu ni kutokula kwa wakati sahihi.
Muda ambao unapaswa kula, asidi ya tumbo inatolewa. Asidi hii ni kwa ajili ya kumeng’enya chakula. Sasa asidi inapokuja na kukuta hamna chochote tumboni huenda kuunguza kuta za tumbo na kusababisha kuvimba kwa kuta hizo (gastritis).
Kama ukiendelea kutokula au kuvuka muda wa kawaida wa kula, asidi inapokuja huja kuchimba zaidi kuta zako na kuvifanya vile vidonda kuchimbika zaidi na kupelekea kuwa ngumu kupona.
Ni vyema ukaheshimu ratiba ya chakula. Kula kwa wakati ni nidhamu ya kiafya, haipaswi kupuuzwa. Kama vidonda vyako vya tumbo haviponi, inawezekana hauli kwa wakati sahihi hivyo hata ukitibu, bado vidonda huendelea kuchimba, kuwa vikubwa na usugu wa kuchelewa kupona.
Mimi ni muhanga wa vidonda vya tumbo kwa njia hii na nilivipata wakati nipo sekondari, Katoke Seminary. Nilikuja kugundua njia nzuri ni kuweka chochote tumboni, hata kama ni sukari kavu, bado itasaidia.
Unataka kuepuka adha hii?
Kama una vidonda vya tumbo, hakikisha muda wa kula ukifika – wakati haupo sehemu ya kula – jenga tabia ya kutembea na chochote cha kutafuna hasa karanga au popcorn.
Weka pakiti hata mbili za karanga kila siku, muda ukifika na ukaanza kujiskia kama tumbo linawaka moto, tafuna karanga zako au popcorn, tumbo liwe na chochote wakati unaelekea nyumbani kupata msosi.
Nitafanya nini msimu wa kufunga ukianza?
Mtu mwenye vidonda vya tumbo sugu inaweza kumuwea ngumu kufunga, na kama unavyojua tunafunga ili kuupa mwili afya zaidi, sasa kama kufunga kwako kunafanya vidonda vyako viwe vibaya zaidi, ni bora kutofunga chakula, ukafunga mambo mengine kama matendo na kudaidia wasio nacho.
4. Unavuta sigara na kunywa pombe kupita kiasi
Uvutaji wa sigara ni adui wa tumbo. Moja kati ya visababishi vya vidonda vya tumbo ni ile nikotini kwenye sigara. Nikotini hufanya ukuta wa tumbo kupoteza uwezo wake wa kuhimili adui na kuwa rahisi kulika.
Pombe vile vile ina asili ya asidi ambayo huweza kula kuta za matumbo na kusababisha vidonda vya tumbo.
Sasa pigia picha kuna mtu anatumia vyote viwili kwa pamoja, tumbo lake litakuwa katika hali gani?Hapo vidonda vitapona kweli?
Ndio maana tunasema, kupona vidonda vya tumbo kunahitaji nidhamu kubwa sana na ndio sababu asilimia kubwa huishi na vidonda vya tumbo muda mrefu.
Nifanye nini sasa?
Kwa wanywaji wa pombe, unaweza kupunguza madhara ya moja kwa moja kwenye tumbo lako kwa kufanya mbinu hizi mbili:
- Hakikisha umekula kwanza kabla ya kunywa pombe: Hii husaidia uasidi wa pombe kupunguzwa nguvu kwa kutofika moja kwa moja kwenye tumbo.
- Kunywa walau nusu lita ya maji kabla ya kuanza kunywa pombe, kwa ajili ya kusaidia kupunguza ukali wa asidi ya pombe.
Njia hizi mbili sio kwamba huzuia kabisa vidonda bali hupunguza uwezekano wa vidonda vyako kuwa sugu.
Epuka pombe kali (Mfano Konyagi, KVant, Valuer, Whiskey nk.) kwasababu huwa na kiwango cha kilevi kwanzia asilimia 35 mpaka 40, ambayo ni kali sana na inaweza kusababisha kulika kwa vidonda na kuvifanya visipone na kuwa sugu; bia ina pombe asilimia 4.5, hivyo ni bora zaidi.
Kama navuta sigara na siwezi kuacha?
Hakuna stadi yoyote inayoweza kutetea uvutaji wa sigara. Kama una vidonda vya tumbo na unavuta sigara, ningeomba nikwambie, havitokaa vipone.
Suluhisho ni moja tu, kuacha sigara!
Iwapo imetokea umeanza kusikika tumbo linawaka moto na kuuma, basi jaribu kuacha pombe na sigara walau kwa wiki mbili Ili vidonda vikauke. Unaweza kuanza kunywa tena vidonda vikishakauka.
Usikilizie mwili wako, mwili unaongea.
5. Matumizi ya muda mrefu ya dawa za maumivu.
Dawa za maumivu zinatumika na watu wengi sana. Watu wenye magonjwa sugu na maumivu ya muda mrefu ya mifupa – hasa wazee na wale kutokana na mvunjiko, au matokeo ya ajali.
Kwa namna dawa hizi zinavyofanya kazi, mojawapo ya madhara yake huwa ni kuongeza umwagaji wa asidi nyingi tumboni hivyo Kuongeza nafasi ya kupata madonda ya tumbo.
Mfano wa dawa hizo ni Aspirin, Ibuprofen, Diclofenac, Aceclofenac, Panadol na kadhalika.
Dawa hizi ni moja ya sababu ya kupata vidonda vya tumbo na matumizi ya muda mrefu hupelekea kuwa na vidonda sugu.
So unashauri nini? Kwa sababu hizi dawa ndo maisha yangu!
Kuna mazingira unaweza usiepuke matumizi ya dawa hizi lakini lazima kuwa na namna ya kutumia dawa nyingine ya kupoza makali ya dawa hizi.
Mfano kwa wagonjwa wanaomeza Aspirin kwa zaidi ya mwezi, huwezi kupewa dawa nyingine ya kuasidia kupunguza asidi mfano Omeprazole. Hii husaidia kupunguza madhara ya dawa hizi za maumivu.
Kama una maumivu yanayoweza kukuhitaji kumeza dawa za maumivu muda mrefu, basi ni vizuri kumuona daktari ili aweze kukuongezea dawa nyingine ya kupunguza makali ya dawa ya maumivu kwenye tumbo lako.
Sababu gani hapo juu imekugusa? Kama ipo, jaribu kuifanyia kazi ili uweze kupona vizuri.
Fomula ya kutibu vidonda vya tumbo
Dawa + Nidhamu = Matibabu
Dawa – Nidhamu = Vidonda Sugu
Nidhamu – Dawa = Vidonda Sugu
Matibabu ya vidonda vya tumbo yanaweza kutaka mpaka oparesheni. Jitahidi usifike hatua hii, fanya juhudi ya kuwa na nidhamu.
Kama utakua na swali lolote, usisite kutuuliza hapo chini. Ukitaka kuwa wa kwanza kusoma posts zetu, unaweza ukajiunga kwa kututumia email yako.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.
Nimepata elimu ya kutosha. Asante sana daktari kwa elimu nzuri, nimejua dalili na jinsi ya kuepuka vidonda vya tumbo. Asante sana.
I offer mutually beneficial cooperation https://zetds.seychellesyoga.com/info