Wakati watu walio wengi wanahangaika kupunguza uzito wao kila siku bila mafanikio, yupo kijana mahali anahangaika kuongeza uzito wake walau ufike kilo 50.
Kama jinsi ambavyo uzito wa kupitiliza ni tatizo kiafya, uzito mdogo nao huweza kuwa tatizo kwa afya ya mtu.
Uzito mdogo unaweza kupelekea:
- Mifumo ya mwili kuathiriwa. Mfano mtu mwenye uzito mdogo anaweza kupata matatizo ya kupoteza uwezo wa kushika au kutungisha mimba.
- Baadhi ya viungo (kama Figo, ini na moyo) kutofanya kazi kwa kiasi kinachotakiwa kutokana na kukosa nguvu ya mwili ya kutosha.
Nitajuaje kama uzito wangu ni mdogo au umepitiliza?
Makadirio ya uzito wa mtu mzima, kuanzia miaka 20, hufanywa kwa kutumia vipimo vya BMI (njia hii hutumia uwiano wa urefu wako na uzito ulionao).
Kama BMI yako ni chini ya 18.9 maana yake una uzito mdogo; 18.5 mpaka 24.9 una uzito wa kiwango cha kawaida, unaotakiwa; BMI kuanzia 25 mpaka 29.9, uzito wako umezidi; BMI zaidi ya 30, wewe ni obese (mnene/bonge).
Muhimu: Kujua BMI yako unaweza kuwasiliana nasi tukakuelekeza namna ya kuikakatua.
Sababu za kutoongezeka uzito
Sasa kwako wewe ambaye uzito wako upo chini ya viwango vya BMI (18.9) na umeshindwa kuongezeka, na inawezekana usijue sababu ya uzito wako kutoongezeka japo unafanya juhudi. Basi soma hapa na uelewe sababu Nne kuu Kwanini uzito wako hauongezeki.
Chukulia mfano wa kufungua akaunti ya Benki. Kuna kuweka pesa pamoja na kutoa pesa. Sasa Ili account iyongezeke lazima uweke pesa ya kutosha, na ukiwa unatoa lazima uibalance ili akaunti isiyumbe.
Lakini pia imagine unaweka hela ya kutosha halafu kuna majambazi wanadokoa bila wewe kujua, akaunti haitakua. Pia kama akaunti au benki unayoweka hela wana makato makubwa, akaunti haitakua.
Kutoka kwenye mfano huu, tujadiri sababu gani zinaweza kufanya usiongezeke uzito:
1. Hauli chakula cha kutosha
Chakula cha kutosha sio kile tu kinachokufanya ushibe, bali kinachokupa virutubisho kamili vya protini, wanga, mafuta, vitamini na maji.
Chakula chenye hivyo vitu ukikipata katika kiasi kinachotosheleza kuupa mwili nguvu (calories) ya kuendesha mifumo yake, hapo ndipo uzito huongezeka.
Inawezekana tatizo lako unakula kushiba lakini mwili haupati virutubisho muhimu, au unavipata lakini havitoshi.
Gram moja ya protini hutoa calories 4 za energy; wanga hutoa calories 4; wakati mafuta hutoa calories 9. Mwili wako kama mtu mzima unahitaji calories kuanzia 2,500 mpaka 3,000 kwa siku!
Mwili unaweza usipate calories hizo kutokana na kiasi kidogo unachopata lakini unapoteza zaidi. Ndio maana mtu anayetaka kupunguza uzito hula wastani na kupoteza zaidi kupitia mazoezi.
Kama unataka uzito wako uongezeke, huna budi kuupa mwili chakula zaidi ila ubaki na ziada ya kujenga mwili.
2. Una maradhi ya mwili
Mwili ili uweze kukua na kuongeza uzito lazima uwe unapata virutubisho vya kutosha zaidi kuliko unachopoteza. Mwili ukiwa na maradhi – mfano, Rovu (kuvimba tezi ya shingo), Ini (liver), HIV/Ukimwi, Ugonjwa wa Figo na Moyo, au Kisukari – hufanya upoteze zaidi ya kinachoingia na kupelekea kupoteza uzito.
Baadhi ya maradhi hupunguza hamu ya kula na hivyo kufanya mwili kudhoofika kwa kukosa virutubisho muhimu na kupelekea kupungua uzito. Inawezekana hujui kama unaumwa. Hatua ya kuchukua kama uzito wako hauongezeki ni bora kutembelea hospitali na kumwelezea daktari matatizo yako Ili akupime na kubaini tatizo lolote linalokusumbua.
Kupambana na sababu ya kwanza hapo juu bila kuhakikisha sababu hii ya pili ni upotevu wa muda.
Kumbuka: Usipojua afya yako, mwili unaweza kupoteza uzito kwa mwendelezo mpaka ukapata utapiamlo. Pima afya yako kama huuelewi uzito wako!
3. Ulevi wa pombe na uteja wa madawa
Mwili unahitaji kuchoma energy nyingi sana, kuvunjavunja na kumeng’enya pombe unayokunywa. Kama ukinywa kiasi, unaweza kupungua uzito kwa wastani, lakini kama ni mlevi tatizo linaanzia hapo.
Unywaji sugu wa pombe hupelekea mwili kuwa na upungufu wa vitamini B 1 (thiamine). Upungufu huu hufanya mtu kukosa hamu ya kula, na hivyo akinywa pombe hali na akila hutapika.
Mtu huyu hunywa pombe zaidi ya chakula na kumbuka pombe nyingi uhitaji energy ya mwili nyingi ili iweze kubadilishwa katika ini, hivyo mwili wako kama mlevi hupoteza nguvu nyingi zaidi ya unavyoingiza.
Hali hii hufanya miili ya walevi wengi kushindwa kuongezeka, na kama tayari ni mnene, basi huwa unashuka. Wewe kama ni mlevi na uzito wako hauongezeki, dawa ni kupunguza pombe.
Kumbuka kuna athari nyingi za kuwa na uzito mdogo na moja wapo kwa mwanaume ni kutoweza kutungisha mimba, na kwa mwanamke ni kuwa na matatizo ya mzunguko wa hedhi na ugumba (hii tutaijadili siku nyingine)
4. Una msongo wa mawazo
Msongo wa mawazo (stress) hufanya mwili ufanye kazi katika metabolism kubwa hivyo mwili hupoteza nguvu zaidi ya ile inayoingia. Stress pia hupunguza hamu ya kula kwa waliowengi na kupelekea kutoongezeka kwa uzito.
Vitu vikubwa vinavyoweza kuleta stress kubwa ni mapenzi, gari bovu, mkopo benki, kushabikia Man united (hahah) na kadhalika.
Kama upo katika mpango wa kuongeza uzito, basi jaribu kuondoa au kubalance stress zako na furaha.
Sababu hizo zinaweza kufanya uzito wako ugome kupanda, hivyo jitahidi kuzibalance. Kumbuka, uzito mdogo ni tatizo kubwa kiafya kama uzito mkubwa.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.