Dalili 5 za Kuonyesha Unajali Afya Yako

Kuwa na afya nzuri kuna maana gani?

Afya nzuri ni hali ya mwili wako kuwa katika usawa mzuri wa kuendesha majukumu yake kwa mtiririko sahihi – kwa maana ya kwamba mifumo yake yote inabalance.

 

Kuwa na afya nzuri ni mafanikio kama mafanikio mengine. Bila afya nzuri mwili hushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu yake na hivyo kupelekea maradhi mbali mbali, uchovu na mtu kushindwa kufika kiwango cha juu cha utendaji kazi.

 

Mwili una mifumo, na mifumo hufanya kazi kwa muingiliano; mfumo mmoja ukishindwa, huathiri mifumo mingine na mingine na mingine, hivyo kupelekea kupunguza ufanisi wa mwili mzima.

Zifuatazo ni tabia zitakazoonyesha unajali afya yako kuliko mtu mwingine:

 

1. Unalala muda wa kutosha

Hata ukatae vipi, hakuna sababu yoyote inayoweza kutolewa ya kuhalalisha kutopumzisha ubongo na akili yako. Unaweza kusingizia kazi au ubize wa aina yoyote ile, ila bado sio kigezo cha kushindwa kupumzisha ubongo wako.

 

Ni dhahiri kwamba ubongo haupumziki kwa asilimia 100%, hata ukilala bado kuna shughuli za mwili huendelea kufanyika. Mfano upumuaji, utoaji wa homoni, mizunguko ya misuli ya mwili, metabolism mbali mbali za mwili na kadhalika.

 

Lakini ubongo uhitaji kupunguza mambo mengi ili seli zake nyingi zipate mapumziko kwa ajili ya kuweka upya mifumo yake kwa siku nyingine. Hivyo ikiwa unalala walau kuanzia masaa 6 mpaka 8 unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuamka ukiwa na kichwa kipya kabisa huku mambo yako yakiwa yameandaliwa vema kichwani na uwezo wako wa kufikiri ukiwa juu kuliko mtu anayelala masaa chini ya hapo.

Utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Havard (chapisho la mwaka 2005) ulionesha kwamba mtu anayelala masaa 6 – 8, uwezo wake wa kufanya maamuzi ni mkubwa mara 3 zaidi ya mtu aliyelala chini ya hapo. Utafiti huo pia ulihusisha uwezo wa kufanya maamuzi kazini kwa kuangalia maamuzi yaliyochukuliwa na watu wawili waliolala muda tofauti; Kulala muda wa kutosha hukupa timamu ya akili, na kuongeza uwezo wa kuchukua maamuzi sahihi.

Utafiti mwingine huonesha asilimia 55 ya maamuzi mabovu hufanywa wakati mtu akiwaza amechoka ubongo. Kama unalala muda wa kutosha basi unajali afya yako na uwezekano wa wewe kufanikiwa kazini, shuleni au kwenye maisha ni mkubwa.

Kulala muda wa kutosha sio uvivu bali ni hali ya kujali afya yako ya mwili na akili.

 

2. Unakula kwa mpangilio

Chakula ni lazima kwa ajili ya mwili kufanya kazi. Lakini mwili utafanya kazi vizuri ukiwa na usawa sahihi wa chakula katika mwili wako – kwa maana, kisiwe chini ya kiasi au juu ya kiasi.

 

Kikiwa chini ya kiasi hapo afya yako hukosa virutubisho muhimu na hushindwa kufikia utendaji kamili, na kikiwa zaidi ya kiasi basi hupelekea mwili kuzidiwa na mzigo mzito.

 

Hakuna sababu ya kuelezea kwanini ule chakula chini ya kiwango kinachotakiwa. Inaweza kuelezewa kwa upande wa umaskini na kipato duni, lakini utafiti unaonesha watu wengi hawali vizuri sio kwa sababu ya kukosa pesa bali kukosa elimu na ufahamu ya mlo kamili, na kuwa na tabia ya kutoweka kipaumbele mlo sahihi.

 

Mfano, kama uko tayari kunywa pombe ya Tshs 20,000 halafu ukala msosi wa buku, ni dhahiri kwamba wewe kipaumbele chako ni pombe, sio chakula. Au kama unamiliki simu ya Laki nane alafu muda wa chakula unapiga chipsi kavu ya 1,000; utaona kabisa kipaumbele chako sio afya.

 

Ni muhimu uweke afya yako kipaumbele namba moja kwa sababu mwili wako ni mashine, na mashine ikiwa mbovu hakuna kazi itakayofanyika.

 

Mpangilio sahihi ni pamoja na kula kwa wakati na kwa ratiba maalum ili kuupa mwili nafasi ya kukitumia chakula vizuri na kwa manufaa. Ulaji holela na wa kupitiliza hupelekea uzito wa mwili kuongezeka, vitambi na shape mbaya.

 

Kiafya uzito mwingi hufanya mwili kuwa na speed ndogo ya kufanya kazi.

 

3. Unapenda kufanya mazoezi

Mwili unafanya kazi kwa kuunganisha mifumo mbalimbali. Ubongo ndio huendesha mifumo yote ya mwili kwa kutuma homoni mbali mbali. Mwili kwa jumla ili uweze kufanya kazi vizuri unahitaji uhimara kuanzia kwenye ubongo mpaka kwenye misuli.

Watu wengi hudhani kufanya kazi za kawaida kama kuandika, kupika, kudeki au kufanya kazi zinazochosha ni mazoezi tosha na huwa wabishi wanapoambiwa anapaswa kufanya ziada. Unapaswa ufahamu kwamba kufanya mazoezi ya kuu’challenge mwili kama kukimbia, au kunyoosha misuli faida yake kubwa inaanzia kwenye ubongo wako, sio tu swala la kuchoka mwili bali ubongo wako kufunguka na kufanya kazi kwa mpangilio mzuri.

Mazoezi hupelekea mwili wako kutoa homoni inaitwa endorphins ambayo huitwa homoni ya furaha (happiness hormone), hii ndiyo huwapa watu kujiskia vizuri na kupunguza stress mara tu baada ya kufanya mazoezi.

 

Homoni hii haizalishwi katika kazi ngumu za kila siku, bali katika mazoezi ya viungo na ubongo. Ndio maana ni lazima kuuwendesha mwili wako kwa mazoezi ya ziada.

 

Asilimia 55 ya watu wanaofanya mazoezi huwa na mafanikio katika nyanja mbalimbali za maisha. Sababu ya hii ni kwamba mazoezi huongeza homoni za furaha (endorphins) na kupunguza homoni za stress (cortisol) hivyo dakika kadhaa baada ya mtu kuanza mazoezi, hali ya ubongo wake hufunguka, akili kuongezeka na ufikiri mkubwa hivyo ni rahisi kupata mawazo mapya na suluhisho ya matatizo yako.

 

Kumbuka majibu mengi ya maswali yako huwa yapo kwenye ubongo wako, tatizo ni kwamba mara nyingi ubongo wako haufunguki kirahisi. Nitajie tajiri ambaye hafanyi mazoezi, nitakutajia maskini wengi ambao mazoezi kwao ni mateso!

 

Utafiti uliofanywa na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Stamford mwaka 2015 ulionesha watu wenye tabia ya kufanya mazoezi hufanikiwa kitaaluma na kibiashara. Pia wana mafanikio mazuri katika mahusiano na familia zao. Sababu kubwa?  Wanajali afya zao. Kama una tabia hii basi jipongeze.

 

4. Unafanya mahusiano mazuri

Mahusiano uliyo nayo yana mchango sana katika afya yako ya mwili. Mtu mwenye mahusiano mazuri na mwenza, wazazi, rafiki na hata nchi yake, huwa katika nafasi nzuri ya kuwa na afya nzuri.

 

Afya nzuri huanza na saikolojia yako. Ukiwa na mahusiano mazuri basi saikolojia yako huwa nzuri na hivyo furaha huongezeka na stress hupungua, na hivyo kuongeza ufanisi wa mwili wako. Mahusiano mabovu na watu wako wa karibu inaweza kuwa sababu ya wewe kuumwa mara kwa mara na kukosa furaha.

 

Tabia nzuri kiafya ni tabia ya kuchagua au kujiweka katika mahusiano bora – rafiki bora, mpenzi bora, kikundi bora na kadhalika. Mzunguko wa watu bora hukupa nafasi ya kujifunza mambo mapya, kuusukuma ubongo wako kuwa na fikra mpya, na kukupa saikolojia njema ya kuwa na afya safi.

 

Kumbuka mahusiano mabovu huleta msongo wa mawazo na kuufanya mwili wako kushindwa kuprocess mifumo yake vizuri. Hii inaweza kupelekea kuongezeka uzito, kupata maradhi ya moyo, magonjwa ya presha na kiarusi.

 

Lakini pia kukaa karibu na mahusiano mabaya kunaweza kukupa mawazo ya kujiona huna thamani, kujidhuru kwa kujiua, na kadharika. Jenga tabia ya kujiweka katika mahusiano yenye afya ili uwe na afya njema.

Utafiti unaonesha watu waliozungukwa na mahusiano mazuri – kama ya wazazi, majirani, wafanyakazi, n.k – hawaugui mara kwa mara na huweza kufanya shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.

Usiwe miongoni mwa watu wa mahusiano mabovu, ina madhara makubwa kwenye afya yako. Tazama watu wanaojiua au wanaojidhuru au kutumia dawa za kulevya, pombe na kubeti; mara nyingi huwa wako kwenye mahusiano mabovu ya kimazingira.

 

Kama una tabia ya kufanya mahusiano mazuri na kuchagua watu wanaoongeza faida katika maisha yako, basi unajali afya yako.

5. Unafanya ulichopanga kufanya

Afya yako inaanzia kwenye mafanikio unayoyapata kila mara kwa kufanya ulichopanga kufanya. Ulishawahi kujiuliza kwanni mtu anaweza akawa mgonjwa lakini bado ana furaha? Unapaswa kujua kinachokufanya uwe na afya njema mara nyingi ni namna unavotimiza mipango yako.

 

Ukiwa na tabia ya kufanya ulichopanga na kuona matarajio yako, hata afya yako huimarika. Huimarika kwa sababu ya furaha unayoipata. Tambua kadiri unavopata ushindi mdogo ndio hamu yako ya kuishi zaidi huongezeka na hivyo hukupa sababu ya kujali afya yako.

 

Mtu aliyekata tamaa kwa sababu hamna kinachoenda sawa kwenye kazi zake huwa hajali hata afya, ndio maana hujiingiza katika tabia ya ngono, ulevi, ugomvi, uchawi na chuki.

 

Target yako wewe iwe kwenye kutimiza malengo yako hatua kwa hatua, kila hatua ya ushindi itakupa furaha na afya ya akili, na hivyo vyote huupa mwili wako nguvu ya kupambana na magonjwa kutokana na kinga yako kuongezeka. Kinga ya mwili huongezeka pale homoni zako za stress zinapokuwa chini, na endorphin homoni zinapokuwa juu.

 

Kama wewe unatimiza majukumu ya malengo yako, hongera, unajali afya yako.

3 thoughts on “Dalili 5 za Kuonyesha Unajali Afya Yako”

  1. Umenigusa sana Dr. Hasa swala la kufanya mazoezi ili kuwa sawa kiakili, pia kula mlo kamili. Asante sana kwa somo zuri. Nitafanyia kazi, endelea kutupa elimu zaidi.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW