Njia Kuu 4 za Kujikinga na Malaria

“Mwaka 2015 mtoto wetu wa miaka 6 alifariki kwa sababu ya ugonjwa wa malaria.” Alisema mama mmoja kwa uchungu wakati tukizungumza mawili matatu.

 

“Hatukuwahi kabisa kuzingatia maagizo ya afya ya kujikinga na malaria na ndio sababu.” Aliongezea mama huyo huku machozi yakimlenga.

 

Ni rahisi sana kupuuzia maagizo ya wataalam kuhusu namna ya kujikinga na malaria, lakini yanapotokea majanga, hasa ya vifo au gharama nyingi za matibabu,  inaumiza sana.

 

Malaria inazuilika?

Jibu ni ndio kwa herufi kubwa!

 

Mnamo tarehe 17 october mwaka 2024, Naibu Waziri wa Afya Dr. Godwin Mollel alisema Tanzania imefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria kwa asilimia 45%.

 

 

Idadi hii ni kubwa na ni dalili kwamba jitihada za ushirikiano kati ya wananchi, Wizara ya Afya na wadau zikiendelea kuwa kubwa basi tunaweza kufikia malengo makubwa ya kufikia maambukizi sifuri kama ilivyokuwa nchi ya Misri mwaka jana.

 

Unawezaje kujikinga na malaria?

1. Matumizi ya vyandarua

Kulala chini ya chandarua ni tabia ya kila mtanzania muwajibikaji. Wewe unawajibika?

 

Wakati tukiwa wadogo, Baba alihakikisha kama kweli tumelala chini ya chandarua au la. Bila shaka aliogopa tukiumwa ni gharama sana lakini pia nadhani alithamini uhai wetu sana.

 

Kama wewe ni baba au mama ambaye hulali ndani ya chandarua na hauakikishi wanao wanalala ndani ya chandarua maana yake wewe huna malengo yoyote kama ya baba hapo juu. Kwahiyo wewe malengo yako kwa familia kama sio afya ni nini?

 

Kulala chini ya chandarua imekuwa njia kubwa ya kupunguza maambukizi kwanzia serikali ilivyoanzisha jitihada zake za kugawa vyandarua vyenye dawa, bure, hasa kwa mama wajawazito.

 

Upatikanaji wa chandarua umekuwa rahisi na gharama nafuu sana kwa sasa. Maamuzi yako ya kulala chini ya neti yataikinga familia yako na janga la malaria

 

2. Kuondoa maji yaliyotuama

Maji yaliyotuama ni mazalio makuu ya mbu wa malaria. Ukiwa karibu na madimbwi ya maji uwezekano wako wa kupata malaria huwa ni mkubwa.

 

Ndio maana watu wanaoishi karibu na madimbwi ya samaki na tingatinga huathiriwa sana na malaria, mfano kanda ya ziwa.

 

Hupaswi kuruhusu maji kutuama kwa zaidi ya masaa 24 karibu na nyumba au makazi yako,unapaswa kuyatoa mapema.

 

Kama siwezi kuondoa maji yaliyotuama nafanyaje?

Kama unakaa karibu na madimbwi yenye maji yaliyotuama, jambo la kufanya ni kupulizia au kumwagilia dawa ya kuuwa mayai ya mbu  na kuzuia mbu kuzalishwa. Dawa hizi hupatikana madukani.

 

Kama huwezi kununua basi waweza kumiminia mafuta ya taa au oil chafu  ya gari kwenye maji yaliyotuama. Vyote hivi huua mazalia ya mbu.

 

3. Weka nyavu kwenye madirisha na milango

Hii ni njia moja wapo ya kuzuia mbu kuingia ndani ya nyumba hasa mida ya jioni. Hii ni njia maarufu sana na imesaidia sana kupunguza maambukizi ya malaria. Bahati nzuri nyavu hizi sio gharama sana na zinapatikana kiurahisi madukani.

 

4. Matumizi ya dawa za kufukuza mbu (mosquito repellents)

Hizi husaidia sana kufukuza mbu na kuzuia kuumwa na mbu hasa unapokuwa nje ya nyumba, usiku au hata ndani. Matumizi ya dawa hizi za kujipaka, au kuchoma ni njia ya kijadi ambayo imetumika toka enzi za baba zetu na zimefanya kazi vizuri.

 

Dawa hizi haziui mbu bali huwazimisha au kuwafukuza na wanaweza kurudi mara tu dawa ikiisha nguvu.

 

Dawa za mbu za kupaka au kuchoma zisitumike kama mbadala wa chandarua. Dawa hii huisha nguvu baada ya muda fulani na hivyo kama hauko ndani ya chandarua mbu watakung’ata kama kawaida. Na unakuwa katika nafasi kubwa ya kupata malaria.

 

Angalizo: Matumizi ya feni kufukuza mbu usiku sio mbadala ya njia nyingine muhimu za kuzuia maambukizi ya malaria. Mbu wana tabia ya kuzoea feni na usiku wa manane wanaweza kukuuma kama kawaida.

 

Pia umeme ukikatika usiku ukiwa umelala utageuka kitoweo cha mbu. Chandarua bado ina nafasi yake ya kipekee.

 

Mwisho, kila ifikapo tarehe 25 April huwa ni maadhimisho ya siku ya malaria duniani. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imejitahidi sana kuhakikisha inafikia malaria sifuri (zero malaria). Wewe umejiandaaje kushirikiana na serikali kufanikisha adhima hii?

 

Tokomeza malaria kuanzia kwenye familia yako na taifa litakuwa salama!

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW