Unapoweka malengo ya kupunguza uzito huwa unalenga nini hasa?
Je unataka muonekano mzuri? Unataka kuongeza ujasiri (confidence)? Au unataka kumfurahisha mchumba wako? Wengine hupunguza uzito ili waigize filamu au watoe wimbo fulani.
Kwa bahati mbaya asilimia 95% ya watu wanaojaribu kupunguza uzito hushindwa. Kama umeweza basi kuna sababu ya ziada na ya kipekee iliyokusaidia zaidi ya hizo nia nilizozitaja hapo juu.
Kushindwa kunasababishwa na nini?
Nia nyingi zinazowekwa hazina uhalisia. Mfano mtu anayejaribu kupunguza uzito kwa sababau ya kazi fulani, akikosa au kuacha hiyo kazi, hurudi hali yake ya zamani.
Au kama sababau ni kumfurahisha mpenzi, akiondoka basi mtu hujikuta anarudi kule kule kwenye ubonge na kadhalika.
Njia pekee ya kuweza kupunguza uzito ni kuwa na sababau thabiti ambazo hazibadiliki kulingana na mazingira. Sababau hizi ni za kiafya.
Ukiwa na nia ya kupunguza uzito ili kuepuka kisukari ambacho unajua madhara yake yalivyo, lazima utafanikiwa kupungua tu. Au nikikwambia “kwa kila kilo unayopunguza unaongeza umri wa kuishi kwa siku 3 zaidi utashindwa kupungua?
Kama una mpango wa kupunguza uzito fanya hivyo kwa sababau za kiafya zaidi kama nitakavyokuonyesha hapa chini.
Hizi ndio faida tatu za kupunguza uzito wako mkubwa:
1. Kupunguza uwezekano wa kupata kisukari na ugonjwa wa moyo
Hivi leo hii ukiambiwa ukipunguza uzito wako ugonjwa wa moyo na kisukari ndio bye bye, utalichukuliaje hilo swala? Bila shaka utachukua hatua mara moja.
Hakuna anayependa kupata kisukari na shida ya moyo. Ni magonjwa yanayotesa kimwili, kiakili na kiuchumi. Kama kuna namna ya kuyaepuka lazima hatua hizo zichukuliwe.
Uwepo wa kitambi ni moja ya kisababishi kikuu cha mtu kupata kisukari (diabetes type 2) kwakuwa hupunguza uwezo wa seli za mwili kupokea homoni ya insulin ambayo ndio husaidia kuweka sukari sawa.
Sasa ukiwa na makandokando mengine ya vinasaba basi wewe uwezekano wa kupata kisukari huongezeka maradufu.
Utafiti wa kiafya umeonyesha kwamba mtu mwenye uzito mkubwa ana nafasi ya kupata kisukari mara tatu zaidi ya mwenye uzito wa kawaida. Vilevile mwenye kitambi ana anafasi ya kupata kisukari mara saba zaidi ya kawaida.
Kizuri zaidi ni kwamba ripoti za afya zimeonyesha kwamba hata kupunguza kilo chache tu kuna faida kubwa ya kupunguza sana uwezekano wa ugonjwa wa kisukari.
Bahati mbaya hata hizo chache huwa sio rahisi kuzipunguza kama hujadhamiria na hauna mipango ya kiafya ndani yake.
Uzito mkubwa huambatana pia na maradhi ya joint, maumivu ya visigino na nyayo, presha na kansa.
Mfano, asilimia 70% ya watu wanaolalamika maumivu ya viungio vya miguu (joint, visigino na nyayo ni wale wenye uzito mkubwa na vitambi).
2. Mwili kuwa mwepesi
Umeshawahi kusikia mtu mnene anakwambia mimi ni mnene lakini ni mwepesi?
Uwepesi hauwezi kuwepo wakati una uzito mkubwa sana, ni kwamba mtu huyo amezoea tu hali kadhaa kama kutembea au kufanya shughuli fulani hivyo anajikuta mwepesi. Wepesi asilia ni pale unapokuwa na kilo ambazo ziko kwenye kiwango sahihi.
Kilo zako zikiwa za kawaida hata seli zako zinafanya kazi vizuri kuchakata kemikali mbalimbali za mwili kama insulin, kwa haraka, na kuruhusu mwili kufanya shughuli nyinginezo kwa haraka zaidi. Mwili ukiwa na mafuta mengi unakuwa taratibu na unatumia nguvu nyingi kufanya jambo dogo.
Mtu mnene na mwembamba wakitembea kilomita moja kwa pamoja, mnene atatokwa na jasho jingi sana na atahitaji kupumzika walau katikati ya safari au kutembea taratibu.
Mtu mwenye uzito mkubwa uwezo wa mwili wake kuchakata chakula na shughuli nyingine huwa ni taratibu sana. Ndio maana watu wenye uzito mkubwa husinzia kirahisi sehemu yoyote wanapokuwa.
Mfano akikaa kwenye kochi kidogo tu kashasinzia, akimaliza kula anasinzia zaidi ya mtu mwenye uzito wa kawaida kwa sababu mwili unatumia nguvu kubwa kuchakata chakula hivyo ubongo unapumzika muda mrefu. Umewahi kujiuliza kwanini watu wenye kilo nyingi hupenda sana usingizi?
Cha kushangaza, mtu akishaanza kupunguza unene na kilo, vitu vingi hapo juu huondoka! Mwili unaaanza kuwa sharp na hapo ndipo wepesi wa mwili unapokuja.
Patia mfano unaendesha gari halafu kuna ukungu. Kama wipers za gari yako ni mpya basi zitafuta vizuri na utakwenda kwa spidi. Kama wipers ni mbovu au zimeisha, kioo kitakuwa bado kina ukungu na utalazimika kwenda taratibu sana kuepusha ajali.
Mafuta mengi na kilo nyingi kwenye mwili ni sawa na ukungu kwenye kioo cha gari. Mwili unafanya kazi taratibu na kwa nguvu nyingi. Sasa ukipunguza kilo zako utaongeza wepesi kwenye mwili wako na itakusaidia sana kiafya kwa baadhi ya mambo niliyoyasema hapo juu.
Kiufupi wepesi wa mwili unakuja pale mwili wako unapokuwa na uwezo wa kufanya shughuli zake kwa wakati bila mawaa. Mwili wa mtu mwenye kilo nyingi unakuwa taratibu sana.
3. Kupona haraka maradhi
Ni ukweli usiopingika kwamba mtu mwenye uzito mwingi huchukua muda mwingi kupona, sababu kubwa ni kwamba kinga ya mwili hushuka pale unapokuwa na uzito na mafuta mengi mwilini.
Hii husababishwa na seli za mwili kushindwa kufanya kazi kwa uharaka unaotakiwa kutokana na mlundikano wa mafuta kati ya seli na seli.
Mfano, kipindi cha mlipuko wa korona, watu wanene na wenye uzito mkubwa waliathirika sana na wengi walilazwa mahospitalini tofauti na weneye uzito wa kawaida.
Pia mtu mnene akifanyiwa upasuaji huchukua muda mrefu kupona kidonda. Au akivunjika, mfano mguu, huchukua muda mrefu kupona kwa sababau ya uzito mkubwa.
Mtu mwenye uzito wa kawaida ni rahisi kupona kidonda au maradhi ya aina mbalimbali kwa sababu kinga ya mwili wake iko juu .Ni rahisi seli zake za mwili kupambana na maradhi.
Utafiti wa kisayansi umeonyesha kitambi cha wastani (moderate obesity) kinapunguza muda wa kuishi kwa miaka mitatu na kitambi kilichopitiliza (severe obesity) kinapunguza muda wa kuishi kwa miaka 10 sawa na mtu anayevuta sigara.
Pia utafiti umeonyesha wale wanaokuwa na uzito mkubwa kwenye umri mdogo huwa na matokeo mabaya sana kiafya kwa baadaye.
Kiimani binadamu hana uwezo wa kujiongezea urefu wa maisha yake, lakini kisayansi mtu anauwezo wa kuongeza maisha yake kwa kutunza afya yake.
Ukiondoa changamoto za ajali, mtu mwenye uzito wa kawaida ni rahisi sana kupambana na maradhi na kuyashinda kuliko mweneye uzito mwingi.
Hii inaelezewa vizuri na ile falsafa ya bwana Charles Darwin ijulikanayo kama “Survival for the fittest”. Dunia ina tabia ya kuwaheshimu na kuwaogopa watu wenye afya thabiti ambao wako fiti.
Mwisho
Dunia ina mitihani mingi sana ya kupambana nayo na swala la afya ni sehemu mojawapo. Afya njema ndiyo itaamua unakwenda umbali gani katika maisha na kwakuwa hatujui ni muda gani halisi wa kufikia malengo yetu, basi hatuna budi kuiandaa miili yetu kukabiliana na changamoto hizo.
Mojawapo ya hatua za kuchukua ni kuhakikisha uzito wetu ni wa kawaida. Uzito wa kawaida moja kwa moja hufanya mwili kuwa fiti kukabiliana na changamoto.
Siku zote kuwa mfatiliaji mzuri wa mwili wako. Kagua tumbo lako na kupima kilo zako mara kwa mara na kuhakikisha unachukua hatua stahiki kabla hakijawa kikubwa .
Kumbuka, wakati kwenye jamii kitambi ni dalili ya afya njema na maisha mazuri, kiafya kitambi kimebeba mabomu ya nyuklia ya kukatisha uhai wako mapema. Chukua hatua!
Katika makala yangu ijayo nitakuelezea namna ya kupunguza uzito, usikose.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.