Madhara Matano ya Uzito Mdogo 

Mara nyingi tukiongelea uzito watu wengi huangalia uzito mkubwa kama tishio kwenye afya.  

Ulishawahi kujiuliza mtu akiwa na uzito mdogo kupita kawaida ina athari gani kwenye afya? Usiumize kichwa sana kwasababu makala hii itakupa majibu ya swahi hilo. 

 

Uzito kiasi gani huesabika kama uzito mdogo?

Jibu ni kwamba hakuna uzito maalum unaohesabika kama mdogo kwasababau uzito wa mtu hutegemea na vigezo vingine kama urefu, misuli, mifupa, n.k. 

 

Kwa hali ya kawaida uzito kisayansi hujulikana kwa kutumia viwango viitwavyo BMI (body mass index). BMI hupatikana kwa kutumia uzito wa mtu kugawanya kwa ‘urefu mara urefu’ (W/H^2). 

 

Kwa kawaida uzito wa mtu mwenye afya nzuri huanzia BMI ya 18.5 mpaka BMI ya 24.9, tofauti na hapo kuna uwezekanao mkubwa afya yako haiko sawa. 

 

Sasa ni madhara gani utayapata ukiwa na uzito mdogo kupita kawaida?

1. Upungufu wa damu wa muda mrefu (chronic anemia) 

Uzito mdogo huwa unaambatana na upungufu wa virutubisho na madini muhimu mwilini hasa madini ya chuma.  

 

Madini ya chuma ni muhimu sana katika utengenezaji wa chembe nyekundu za damu. Hivyo kama chembe hizo hazitengenezwi kwa wingi mwisho wa siku damu yako itakuwa haitoshi na kupelekea kuwa na upungufu wa damu wa muda mrefu. Hali hii inaweza kuathiri viungo muhimu vya mwili kama ubongo, figo na moyo. 

 

2. Mifupa kuchuja (osteoporosis) 

Mifupa ni sehemu muhimu sana ya mwili, ikiwa dhaifu ni hatari. Kwa kawaida mifupa imetengenezwa kwa madini ya Phosphate pamoja na Calcium.

 

Sasa mtu mwenye uzito mdogo ana uwezekano mkubwa wa kuwa na kaisi kidogo cha haya madini ambayo ni muhimu kwenye kutengeneza mifupa migumu. 

 

Hii hufanya mifupa kuwa kama imechuja (shallow) hivyo kuwa laini na kuweka hatari ya kuvunjika kirahisi hata kwa kuanguaka chini kidogo tu. 

 

Ulishawahi kuona mtu anasukumwa kidogo kwenda chini na anavunjika? Kuna uwezekano mkubwa akawa na upungufu wa phosphate, ana mifupa ni laini. 

 

Zaidi kwa wanawake, uzito mdogo unaweza kuambatana na upungufu wa homoni za oestrogen ambazo ni muhimu kufanya mifupa iwe na ujazo wa kutosha na hivyo ni rahisi mifupa kuchuja. 

 

3. Ugumba (infertility)

Hatua za utengenezaji na upevushaji wa mayai ya kike hutegemea zaidi utoaji wa homoni za uzazi. Mtu mwenye uzito mdogo ana uwezekanao wa kutoa homoni kidogo hivyo kupelekea mwili kushindwa kutoa mayai ya kutosha au yai kushindwa kutolewa (ovulation) kwa ajili ya hatua zingine.

 

Ndio maana wanawake wengi wenye uzito mdogo huwa na hedhi ambazo hazina mtiririko mzuri. Badala ya siku tano inaweza kuja siku mbili ikakata au pia anaweza kukaa muda mrefu bila kushika mimba. Uzito mdogo ni moja ya sababau. 

 

Kwa mwanaume pia, uzito mdogo huambatana na utoaji wa shahawa kidogo zaidi (chini ya mil 15). Pamoja na uchache wa shahawa bado ubora wa shahawa unaweza kuwa mdogo na hivyo kuzifanya zishindwe kuwa na nguvu ya kuogelea kufika kwenye yai. 

 

4. Mwili kukosa nguvu 

Kuna kiasi fulani cha nguvu mtu wa kawaida anapaswa kuwa nacho ili mwili ufanye shughuli zake na shughuli za ziada. Pale mwili unapotakiwa kufanya nguvu za ziada kama kubeba mizigo, kutembea umbali fulani, kufanya sex au kazi muhimu ndipo nguvu zaidi huitajika. 

 

Mtu mwenye uzito mdogo huwa na uwezekano wa kuchoka haraka anapokuwa anajaribu kufanya shughuli kama hizo. Kuchoka huko na kukosa nguvu huchangiwa na changamoto mbalimbali za uzito mdogo kama damu chache mwilini au utapiamlo. 

 

5. Matatizo ya akili 

Hivi unajua uzito mdogo unaweza kuambatana na changamoto za akili? Ukiwa na uzito mdogo ni rahisi kupata msongo wa mawazo, hofu, kupoteza kujiamini na uwezo mdogo wa kufikiri na kufanya maamuzi. Hali hii ikiendelea ni rahisi sana mtu kupata matatizo ya akili.  

 

Shida hii inatokea zaidi kwa watoto wanaopata utapiamlo kutokana na kukosa lishe nzuri na matokeo yake huathiri uwezo wao wa ubongo na baadaye huwaweka kwenye hatari ya kupata shida ya akili. 

Kwa changamoto hii, soma zaidi makala yangu ya “UTAPIAMLO: Adui wa akili ya mwanao“. 

 

Pia watoto wenye utindio wa ubongo hukumbwa na tatizo la kutoongezeka uzito kutokana na ulaji mgumu na shida kwenye mifumo ya mwili inayomsukuma mtu kula. 

 

Muhimu: Jambo la kufahamu pia ni kwamba uzito mdogo unaweza kuwa dalili mojawapo ya tatizo la akili au kisaikolojia. Moja ya tatizo la kisaikolojia linaloweza kuleta uzito mdogo ni Anorexia Nervosa. 

 

Hili ni tatizo la kisaikolojia ambapo mtu hugoma kula sana kwasababu hataki kuongezeka uzito; anapenda sana mwili mdogo (obsession). Watu hawa hula kidogo sana au kujikondesha makusudi. Kisaikolojia huwa na hofu kubwa ya kunenepa.  

 

Kutokana na hali hii, ambayo wao wenyewe hawaitambui, wanaweza mpaka kufikia hatua ya kupata utapiamlo. 

 

Ukiwa na mtu mwenye tatizo kama hili ni muhimu kuonana na wataalamu kwa ajili ya kumfanyia uchunguzi zaidi. 

 

Nifanyeje ili kuongeza uzito wangu?

1. Kwanza onana na wataalamu wa afya 

Uzito kushindwa kupanda pamoja na kujitahidi kula inaweza kuwa dalili ya magonjwa kama ya figo, ini, moyo, kansa, HIV na magonjwa ya akili. Ni vyema kumuona daktari kwanza na kuhakikisha huna tatizo lolote la kiafya. 

 

Kwa watoto, uzito kugoma inaweza kuwa dalili ya magonjwa mbalimbali hivyo jaribu kumuona daktari kwanza. 

 

2. Jisukume kula vyakula vya kujenga mwili (vyakula vyenye protini, wanga, mafuta na maji). Vyakula hivi viliwe kwa wingi ukiongeza na mbogamboga.  

Siri ya kuongeza uzito ni kula zaidi ya unachotoa. Vyakula kama nyama, samaki na maziwa ni vizuri sana kwenye kuongeza uzito. 

 

Wakati mwingine watu hukonda kwasababau ya uchumi mbaya hivyo jitahidi kupambana kutafuta pesa, na kama huna usisite kuomba msaada kwa wasamalia wema. 

 

3. Badili mtindo wa maisha 

Hakuna kitu kinachoshusha uzito kama pombe, sigara, bangi, mapenzi na kuwaza sana. Jua kwamba kunywa sana bila kula vizuri ni chanzo cha kushuka uzito.  

 

Punguza pombe, acha sigara na bangi; pia epuka mazingira yenye stress kama kuchukua mikopo mikubwa ambayo huwezi kuilipa, kuishi na mpenzi pasua kichwa, kufanya kazi mazingira yasiyo na utulivu/amani n.k. 

 

Angalizo: Njia bora ya kuongeza uzito ni kupata lishe bora na kuondoa visababishi vya uzito kushuka kama maradhi na mtindo wa maisha. Matumizi ya dawa za kunenepesha na kuongeza uzito yanaweza kuathiri mwili wako na kuwa na madhara ya muda mrefu kama kansa, matatizo ya mifupa, figo na ini. 

 

Mwisho 

Ukweli ni kwamba kupandisha uzito ni gharama kweli; inahitaji pesa, muda na maamuzi! Hivyo usichezee afya yako kwani inaweza kuwa chanzo cha kuwa na afya mgogoro kwa muda mrefu. 

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW