Habari yako mpenzi msomaji?
Najua si jambo geni kusikia swala la upungufu wa damu hasa kwa watoto, wajawazito, pamoja na wasichana walio katika umri wa kuzaa. Kwa wengi wetu imekua ni kawaida kutafuta namna mbalimbali ambazo zinaweza kusaidia kutatua changamoto hii ya upungufu wa damu mwilini hasa tukiamini kwamba vitu kama soda zenye rangi nyekundu huongeza damu mwilini, jambo ambalo si la kweli!
Ongezeko la damu hutokana na ulaji bora wa vyakula hasa vya asili vinavyolimwa na kufugwa kama vile matunda, mboga mboga pamoja na nyama ambavyo vitaupatia mwili kirutubishi cha madini chuma pamoja na vitamini zingine kama vitamini C ambayo husaidia katika ufyonzwaji wa madini chuma mwilini na kupelekea ongezeko la damu.
Ngoja nikupe story kidogo…
Siku chache zilizopita nilitembelea duka moja kubwa katika eneo la mji ninaoishi na pale nilikutana na mwanaume mmoja akimuuliza muuzaji “Juisi nyekundu ya kuongeza damu ipo?”
Aliitaja kwa jina , ilikua ni mojawapo ya juice ambazo hutengenezwa viwandani na mara nyingi huwa zinachanganywa na maji wakati wa kunywa.
Nilitambua kuwa yupo katika hali ya kutamani kutatua tatizo la kupungukiwa damu kwa ndugu yake, au yeye mwenyewe lakini hakuwa na uelewa wa namna sahihi ya kufanya hivyo.
Hizi zilikua elimu za mitaani ambazo huenea kutokana na imani za watu juu ya vyakula; hii hujulikana kitaalamu kama “Food Fallacies”.
Wakati mwingine watu huenda kutafuta soda/juice hizi kutokana na ushauri waliopata kwa wataalamu wa Afya wengine ambao si maafisa lishe.
Ukweli kuhusu soda/juisi hizi…
Gazeti la Reuters la nchini Uingereza, mwaka 2007, liliandika juu ya kisa cha wanafunzi wawili wa kike walioshtaki kampuni ya Ribena ambayo hutengeneza juisi ya blackcurrant ambayo ilitangaza kwamba ina kiwango kikubwa cha vitamin C katika kinywa chake kuliko inayopatikana katika machungwa.
Wanafunzi hawa walifanya tafiti juu ya hilo na kubaini kuwa jambo hilo si la kweli na hivyo waliishinda kampuni ya Ribena mahakamani na kulipwa fedha ambayo ni fidia ya fedha za Newzealand $227,500 “(sawa na dollar za marekani $163,700 ambazo kwa fedha zetu za kitanzania ni Milioni 387,940,799.40)”.
Nini cha kujifunza?
Japo kampuni hio haikufungwa na bidhaa zake zinaendelea kutumika duniani lakini ninachotaka ujifunze hapa ni kwamba matangazo ya bidhaa mbalimbali hasa vinywaji kama hivi na kadhalika hujikita katika kufanya biashara na kumvutia mtumiaji.
Unapaswa kuweza kuchagua vyakula mbalimbali vya kiasili ambavyo hupatikana katika masoko yetu ili kuweza kukusaidia kutatua matatizo yako ya kiafya kama vile kuongezeka kwa damu.
Mfano wa vyakula hivi ni vile vinavyopatikana katika kundi la mbogamboga za kijani pamoja na matunda.
Mbali na hili, kuna supplements kama vile Fefo, Folic acid pamoja na Vitamini B mbalimbali (mfano vitamin B12) ambazo hutolewa kwa mpangilio maalum wa kitaalamu na sio kununua tu na kutumia mwenyewe.
Nini hasa kiko katika juisi/soda za aina hii?
Juisi za aina hii huwa na sukari nyingi ambayo si nzuri katika afya ya kwasababu sukari ikizidi hubadilishwa na kupelekwa kuwa mafuta ambayo hutunzwa mwilini na kama yakijaa katika mifumo mbalimbali hupelekea magonjwa yasioambukizwa.
Zingine huwa na kiwango kikubwa cha caffeine ambayo hupelekea kuzuia ufyonzwaji wa madini na virutubisho mbalimbali mwilini.
Vyakula na vinywaji vinavyoweza kuongeza damu mwilini ni vipi?
Kabla ya kuongelea vyakula hivi, ningependa kukuambia kwamba vyakula hivi (nitakavyopendekeza) huhitaji ushauri zaidi wa wataalamu wa lishe pamoja na madaktari kwasababu kuna baadhi ya vyakula watu wengine hawataweza kutumia kabisa au hupaswa kutumia kwa kiasi kidogo kutokana na matatizo ya kiafya mfano nyama nyekundu.
Hivyo fahamu machaguo ya vyakula hutegemea kwanza hali ya kiafya ya mtu binafsi. Mifano ya vyakula ambavyo vina sifa ya kuongeza damu ni kama ifuatavyo:
- Vyakula vyenye madini chuma kwa wingi kama vile nyama nyekundu na mboga za majani yenye ukijani.
- Vyakula vyenye kirutubishi cha vitamin C kama vile maembe, machungwa, strawberries na kadhalika.
- Vyakula vyenye kirutubishi cha folate kama vile broccoli, spinachi, njegere, maharage na kadhalika.
- Vyakula vyenye Vitamin B12 kama vile mayai, maziwa , samaki, dagaa na kadhalika.
Hivi ni vyakula ambavyo hupatikana kwa urahisi masokoni, na ni vya asili hapa kwetu Tanzania, hivyo jitahidi kuvitumia ili uweze kuboresha afya yako.
Asante, tukutane katika makala nyingine ya lishe.

Providing nutrition education and counselling in Tanzanian local communities, currently in Mkuranga – Pwani region. My goal is to raise awareness on how to improve our health through nutrition – in all human life stages.