Muda wa Kula Unavyoathari Afya na Maisha Yako

Kuna maana yoyote kuzingatia unakula muda gani? Tulipokuwa watoto, chochote unachoshika au kupewa mwisho wa siku unaelekeza mdomoni. Ila baada ya kukua, kabla hujaweka kitu mdomoni, lazima ujiulize maswali matatu: Je! Ni muhimu? Ni lazima? Ni muda sahihi?

 

Maswali mawili ya kwanza (muhimu na lazima) kila mtu mwenye ufahamu lazima ajiulize. Swali la tatu ndio nguzo ya makala hii. Mara ngapi tunajiuliza swali hili?

 

Basi kama hujui, utekelezaji wa hili swali ndio huleta tofauti ya kiafya kati yako na mtu unayetamani kuwa kama yeye.

 

Unajua kwamba muda unaokula una mahusiano ya moja kwa moja na afya yako? Miaka ya 2005 mpaka 2009 wakati nipo sekondari, pale Katoke Seminari, swala la msosi lilikuwa gumu sana. Ilikuwa nadra sana mimi kushiba. Uji wa asubuhi ilikuwa nadra kupata kikombe kilichojaa, ugali vile vile ilikua ni bahati kubwa ikitokea siku nimeshiba.

 

Kwa maisha kama yale niliapa nikikua nikapata pesa yangu nitahakikisha napiga misosi hasa. Hicho ndicho kilichotokea, baada ya kuwa daktari nilianza kuuwasha msosi balaa. Asubuhi saa 3 mimi na rafiki yangu, Dk. Aziz, ilikuwa kawaida kugonga supu, chapati tatu na maji halafu tunashushia Pepsi baridi.

 

Hapo hapo mida ya saa 6 akipita mtu wa maandazi basi nanunua, achana na kutafuna jojo muda wowote ninaojiskia. Usiku tukiagiza bia lazima tuagize na nyama choma.

 

Niliendelea na utaratibu huo mpaka baadaye nilipokuja kugundua kitu: Sikuwa na utaratibu wowote wa nile saa ngapi na kwa nini. Baada ya muda, katika safari yangu ya kuijua afya, nilikuja kujifunza vingi hasa nilipokuwa nahangaika kukata kitambi na uzito.

 

Muda wa kula ni muhimu sana kwenye afya yako kwa ujumla. Issue sio kula bali unakula saa ngapi na kwanini?

 

Katika ulaji kuna mambo mawili ambayo unaweza kuwa unafanya: Inawezekana unakula au unakula-kula. Kula ni sawa ila kula- kula ni mbaya kwa afya yako.

 

 

Mwili wako ni mashine inayoendeshwa na utashi au tabia zako. Ukiamua ule kila baada ya nusu saa mwili utaendana na wewe tu. Ukiamua ule mara moja kwa siku basi mwili utafuata lakini tambua kila tabia itakuwa na matokeo yake mwilini mwako.

 

Kiuhalisia mwili unahitaji nafasi ya kutumia kile kilichoingia kabla haujapokea kingine, tofauti na hapo mwili utakachokifanya ni kuvikusanya tu vile unavyovila na kuviweka kwenye store ya mwili wako na vitakaa bila matumizi.

 

Vile vile mwili ukikaa muda mrefu bila kupata nguvu ya chakula bado ni changamoto sana na inaweza kuleta madhara mbalimbali katika mwili.

 

Kula ni muhimu na lazima, swali linakuja: Ule saa ngapi?
Mwili wako una saa ya asili inayoitwa circadian rhythm, saa hii ndio hujua mwili unalala saa ngapi, unaamka saa ngapi, unakula vyakula vya aina gani saa ngapi na mwili umezoea kuchakata chakula fulani muda gani.

 

Kufaidika na saa hii, ni lazima uutengenezee mwili utaratibu wa kufanya vitu fulani katika muda fulani. Ulishawahi kugundua kama umeuzoesha mwili kula saa saba kila siku, muda huo ukifika njaa inaanza kukamata? Au kama umezoea kulala saa tano usiku, muda huo ukifika utaanza kuhisi usingizi hata kama mchana ulilala?

 

Utafiti uliofanywa mwaka 2022 na Chuo Kikuu cha John Hopkins ulionyesha kwamba kuvurugika kwa saa hii ya asili kutokana na mwili kutojua unakula saa ngapi hasa kutokana na mtu kula kila mara umekuwa kisababishi kikuu cha kuongezeka kwa ugonjwa wa kisukari cha pili (Diabetes type 2) na maradhi mengine ya mishipa ya damu (cardiovascular diseases).

 

Ni muhimu sana kuwa na muda maalum wa kula chakula. Tabia ya kula kila kinacholetwa mbele yako ni hatari sana kwa afya yako. Pia kukaa muda mrefu kupitiliza bila kula muda maalum ni hatari kwa afya yako.

 

Mfano wewe umezoea kula saa 7 mchana halafu leo imefika saa saba hukula umekula saaa 12 jioni; sasa kitakachotokea ni kwamba mwili wako una saa ambayo imeshasetiwa kula saa 7 hivyo kila kitu kitaendelea kama kawaida. Mwili utatoa asidi kwa ajili ya kuja tumboni kuchakata chakula na kama hamna chakula basi asidi ile hushambulia tumbo wazi na hivyo kuumiza kuta za tumbo.

 

Hali hii ikiendelea husababisha kuvimba kwa kuta za tumbo (Gastritis). Haiishii hapo, ukila baadaye mmeng’enyo wa chakula hautakuwa mzuri na ndio maana utashangaa tumbo linauma au chakula kinakaa tumboni muda mrefu kwa sababu muda uliokula sio muda mwili uliouzoea.

 

Unamjua mtu mwenye tabia ya kula hovyo?
Saa 8 umekula lunch nzuri tu, hujakaa sawa saa 9:30 mtu kapita na bisi au karanga, utasikia “unauzaje? nipe moja!”. Saa 11 jioni umeona mahindi, nipe hindi la buku na juice ya azam. Saa mbili usiku unashindilia msosi kama kawaida nyumbani.

 

Ni bora hiyo ndio iwe routine ya kila siku, lakini kesho tena mara chai unywe saa 2 mara siku nyingine saa 4 asubuhi, mara muda mwingine saa 6 – kiufupi mwili wako umechanganyikiwa, hauna nafasi ya kutengeneza ratiba maalum kwa ajili ya kufanyia kazi chakula unachokula.

 

Ulishawahi kuona mtu anakula sana lakini hapendezi na wala hanenepi? Au ananenepa kupitiliza? Watu hawa huwa wanalalamika kwamba wanakula msosi mdogo tu lakini wanashangaa unene unakujaje wasijue kwamba tatizo lao wanakula hovyo! Mwili haupati nafasi ya kuchakata vizuri.

 

Dk. Janabi kutoka muhimbili anashauri,

“…walau upe nafasi mwili wako upate hata njaa basi, sio kushindilia msosi kama
unapakia lumbesa!”

Angalizo: Kama unajikuta na njaa mara kwa mara (hata masaa machache baada ya kula) ni vyema ukafanya uchunguzi kuhakikisha huna minyoo au tatizo la sukari maana kwa kawaida ukila chakula vizuri unaweza kukaa mpaka masaa 8 badaye, labda kama unafanya kazi ngumu sana.

 

Fanya yafuatayo ili muda unaokula uendane sambamba na kujenga afya yako:

1. Tawala hisia zako

Hisia zetu ndizo hutuongoza kufanya maamuzi mbalimbali kuhusu kula hivyo usipozitawala utajikuta unakula vitu kwa sababu vinakuvutia machoni lakini mwili hauvihitaji kwa wakati huo.

 

Watu wengi wanaokula kila mara hufanya hivyo kwasababu wanapenda kula vitu fulani bila kuangalia vinaathiri vipi mwili na afya zao. Afya yako ni muhimu kuliko Pepsi au hizo juice unazokunywa kila mara. Jenga tabia ya kuupa mwili wako nafasi ya kuchakata ulichokula muda uliopita.

 

Kuendesha maisha kwa hisia za kutamani kumeathiri afya za watu wengi mfano kuogezeka uzito au kupata athari za tumbo.

 

Pia ni vizuri kuwa na subira. Ndio muhogo ni mzuri kwa afya lakini sio lazima ule sasahivi, unaweza kununua ukautunza ukaja kula katika muda wako wa kula wa kila siku.

 

Mfano, ukimpa embe mtu aliye katika mfungo hatokakaa lakini hatolila muda ule, ataliweka mpaka muda wa kufuturu jioni. Nidhamu hii ni muhimu kwa ajili ya afya yako. Ni lazima ujue kwamba muda huu kwangu sio wa kula, nakulaga mida fulani, full stop!

 

2. Sio lazima ule milo mitatu kwa siku

Miaka mitatu iliyopita nilikuwa miongoni mwa watu walioamini kwamba nisipokula milo mitatu kwa siku nitakonda na mwili utadhoofika. Kumbe ilikuwa ni ukosefu wa elimu ya afya mpaka niliposoma kitabu kimoja kinaitwa Fast This Way by Dave Aspray.

 

Kilinipa mwanga ambao mpaka leo ndio umekuwa maisha yangu. Huitaji milo mitatu kuwa na afya nzuri wala kuwa na mwili mzuri, unahitaji mlo mmoja mpaka miwili tu ndani ya masaa 24.

 

Binafsi niliacha kula breakfast asubuhi zaidi ya chai kavu tu na maji. Niligundua breakfast sio muhimu na inachangia kuleta uvivu na kusinzia kazini.

 

Unapopiga breakfast, baada ya nusu saa, ubongo wako huingia katika hali ya kupumzika kwa sababu nguvu nyingi muda huo inaelekezwa kwenye matumbo ili kuwezesha mmeng’enyo wa chakula. Kwa maana hiyo ubongo unapumzika kidogo, focus yako huondoka, utakuwa mzito kiasi fulani, utasinzia na kuharibu siku yako mpaka kufika muda wa launch.

 

Kama ni mwalimu na ulitakiwa usahihishe karatasi 30 utasahihisha 15 kwasababu utakuwa mvivu sana.

 

Niligundua kuacha breakfast kuliniongezea umakini sana na uwezo mkubwa wa kukamilisha malengo yangu kwa wakati. Nilianza kufanya kitu kinaitwa intermittent fasting: Asubuhi chai kavu ya rangi na maji ya kunywa. Napiga kimya mpaka saa 7:30 mchana, nakula lunch safi ya kushiba kabisa na maji au juice.

 

Baada ya hapo tutafutane saa 2 usiku napiga wastani tu na baada ya hapo siweki kitu kingine mpaka kesho saa saba mchana zaidi ya chai kavu ya rangi asubuhi. Basi afya yangu iko poa tu, napiga na zoezi, huwezi jua kama naruka breakfast asubuhi.

 

Hakuna kitu kitakufanya uwe na focus kubwa kama kuwa na tumbo wazi. Kwa taarifa yako ndio maana watu wakifanya sala kama kipindi cha Kwaresma au Ramadhan wanafunga kula pia.

 

Sio ishu ya dini tu, ile ni Sayansi ya kweli kabisa! Tumbo likiwa wazi basi damu nyingi ina’flow kwenda kwenye ubongo na kuufanya uwezo wako wa kusali na kutafakari kwa umakini bila kusinzia kuwa mkubwa.

 

Ili mwili uwe imara haukuhitaji wewe ule kila mara, unakuhitaji wewe ule kwa wakati maalum na ukishazoea tu baasi.

 

Faida kubwa ya kuuachia mwili wako mwanya wa kutosha ni kwamba utapata nafasi ya kula kwa uhuru bila kujibana pale muda unapofika, tumbo linakuwa wazi kabisa kusubiria msosi.

 

Faida tatu za kula kwa muda maalum:

1. Huongeza ufanisi katika utendaji wa kazi

Unapokula chakula mwili huanza kukimeng’enya. Mmeng’enyo wa chakula huchukua walau masaa mawili mpaka chakula kiishe tumboni. Wakati mmengenyo unatokea huwa kuna hali fulani ya uchovu na kuhisi usingizi.

 

Hali hii hutokea kwasababu ubongo hupumzika kidogo kwasababu damu nyingi huelekezwa katika matumbo kuwezesha mmeng’enyo wa chakula.

 

Sasa mtu anayekula muda wowote bila utaratibu hujikuta katika hali hii mara kwa mara. Watu hawa huwa wanasinzia mara kwa mara, wanakuwa na uvivu fulani na hiyo hupelekea kupungua kwa umakini na ufanisi kwenye utendaji. Kumaliza kazi kwa wakati ni jambo la maajabu kwao.

 

Mtu anayeupa mwili wake walau masaa nane ya tumbo kukaa tupu huwa na nguvu na makini kwasababu ubongo umeamka kwa muda huo wote.

 

Unataka kuongeza ufanisi kwenye shughuli zako hasa mida ya asubuhi mpaka saa nane? Usile msosi mzito na wala usile snacks katikati. Kunywa chai kavu na maji halafu usile kitu mpaka saa saba au nane.

 

Muhimu: Chai haifanyiwi mmeng’enyo kwasababu sukari tayari ni final product hivyo ubongo haujishughulishi nayo sana.

 

Zoezi hili kwa wiki ya kwanza huwa ni gumu mno ila ukishazoea kwanzia wiki ya pili utashuhudia utofauti mkubwa katika umakini wako kwani ubongo unakuwa umeamka muda wote.

 

2. Huleta afya ya mwili

Mwili unapokaa zaidi ya masaa nane bila chochote huingia katika ketogenic state. Huanza kuvunja akiba ya mafuta ili kuzalisha nguvu.

 

Ketones zinazotoka kwenye mafuta haya huwa ni chanzo kizuri sana cha nishati ya ubongo na inasemekana huimarisha seli za ubongo na kuongeza uimara wa ubongo kufanya kazi kwa umakini mkubwa.

 

Pia mafuta yanapotumiwa badala ya chakula cha nje huusaidia mwili kuwa na nguvu; pia kitambi huondoka.

 

Watu waliojitahidi kupunguza idadi ya mlo na kutokula sana hasa usiku wameripoti vitambi kupungua sana. Mke wangu, Ms. Agness, ni shahidi mzuri wa jinsi kula milo miwili tu inavyoweza kuondoa tumbo na kukupa nguvu.

 

3. Hupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya mwili

Kula kwa muda fulani maalum (kuzoea muda fulani wa kula) husaidia kuiweka vizuri saa yako ya kibaiologia (circadian rhythm).

 

Utafiti umeonyesha kupungua kwa maradhi ya kisukari, presha na moyo kwa watu ambao wanakula kwa muda maalum tu. Pia kuongezeka kwa uwezekano wa kupata kisukari (Dm-2) kwa watu ambao hawana muda maalum wa kula(wanakula hovyo)

 

Kwa kumalizia…
Kuwa na muda maalum wa kula milo yako na punguza ulaji wa hovyo na muda wowote. Lazima uwe na ratiba yako ambayo inaruhusu walau tumbo kukaa wazi masaa sio chini ya nane.

 

Kwa wenye madonda ya tumbo, inawezekana pia kuwa na muda maalum, mwili ukishazoea huwa haisumbui. Cha kufanya: unaweka kitu asubuhi halafu unaliacha tumbo lako wazi kwa walau saa 8,
mara nyingi haisumbui ila kama inasumbua sana basi unaweza kuweka chochote katikati lakini kwa muda fulani.

 

Mfano, mwili ukizoea kila ikifika saa 6 mchana unapata juice au karanga kidogo kusukumia masaa mpaka lunch hamna shida. Shida hapa ni kula tu kila unapojisikia.

 

Kama una tatizo la kisukari, unaweza kujua uweke vipi masaa ya milo yako kupitia kitabu hiki cha “How to Reverse Type 2 Diabetes” ambacho kinapatikana dukani kwetu.

 

Angalizo: Ulaji wa chakula usiku uendane na mahitaji ya usiku. Kama wewe ni mfanyakazi wa shift za usiku unaweza kuhitaji kula kushiba vizuri. Lakini kama usiku unarudi kulala basi tumia busara kwa kula kwa wastani mdogo na sio kushindilia kwa maana uhitaji wa chakula, usiku, kwenye mwili sio mkubwa.

 

Vyovyote vile unavyokula, mchawi ni muda tu. Unaweza kula sana usiku ila ukihakikisha baada ya hapo unafunga mpaka kesho mchana basi itaupa nafasi mwili wako kutumia kilichopo. Hii ni aina ya mfungo unaitwa 8:16 formula. Soma zaidi kupitia makala hii.

 

Pia kadri umri unavyoongezeka, epuka kula kila kitu unachokutana nacho na punguza idadi ya milo, sio lazima upate milo mitatu kwa siku. Hii ni mazoea tu lakini sio lazima. Milo miwili mizuri inatosha kukupa afya njema.

 

“Nambie unachokula nitakwambia wewe ni nani ” – Brillat Savarin.

 

 

Usisahau pia kutembelea duka letu lenye vitabu mbalimbali vya afya ambavyo naamini vitakupa mwanga mpya kwenye maisha yako. Asante sana.

2 thoughts on “Muda wa Kula Unavyoathari Afya na Maisha Yako”

    1. DR ANSBERT MUTASHOBYA

      habari chazy, hapana sema kuna namna ya kuanza ,ni vizuri kuongea na mtaalamu wa afya.Tupigie tukupe ushauri-0767226702.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW