Dalili Kuu 5 Zinazoashiria Una Tatizo la Moyo

Mwili wa binadamu umeumbwa na mifumo mbalimbali inayofanya kazi pamoja kuhakikisha wewe unakuwa hai. Katika mifumo hiyo yote moyo ndio kiunganishi kikuu. Nitakosea nikiufananisha moyo wako na injini ya gari? Kama una ufahamu na gari utanielewa.

 

Moyo na injini ya gari ni kama vinafanya kazi zinazofanana. Bila injini kuwa imara, mafuta na maji kwenye gari haviwezi kusukumwa ipasavyo na hivyo gari haiwezi kwenda umbali wowote wa maana. Itashindwa!

 

Moyo wako pia ndio injini ya mwili wako. Damu, maji na virutubisho haviwezi kuzunguka kama moyo hausukumi ipasavyo. Moyo wako umeanza kupiga kuanzia wiki ya 4 ya maisha ukiwa bado tumboni na utasimama pale tu utakapokufa.

 

Unapokuwa umepumzika moyo wako unasukuma kiasi cha lita 5.7 za damu kwa dakika, na unaweza kusukuma mpaka lita 15 hadi 20 kwa dakika ukiwa katika mazoezi.

 

Mwaka 2023, Shirika la World Health Federation (WHF) lilitoa report kuhusiana na hali ya magonjwa ya mishipa ya damu na moyo (cardiovascular diseases) duniani kote na ripoti ilibainisha kwamba kwa miaka mingi sasa magonjwa ya moyo yamekuwa yanaongoza kwa kusababisha vifo.

 

Mfano, mwaka 2023 viliripotiwa vifo milioni 20.5 kutoka vifo milioni 12 mwaka 2009.

Katika ukanda wa Sub-Saharan, ikiwemo Tanzania, hali sio nzuri pia ambapo mnamo mwaka 2013 ripoti ilionyesha magonjwa ya moyo yamesababisha vifo kwa asilimia 38.3 ya watu wenye magonjwa hayo. Kufikia mwaka 2023, hali ya magonjwa na vifo yamekuwa mara mbili zaidi.

 

Pia ripoti hii imeonyesha asilimia 34 ya watoto waliozaliwa na magonjwa ya moyo walifariki kati ya mwaka 2015 na 2017.

 

Hii inatoa picha ya namna magonjwa ya moyo yanavyokua kwa kasi huku ikitoa rahi kwa kila mtu kujua visababishi na kuviepuka kwanzia wanaume mpaka wajawazito.

 

Baadhi ya visababishi vilivyoripotiwa ilikuwa ni presha ya kupanda, ulaji mbaya, mafuta mengi mwilini (high cholesterol), kisukari, kuvuta hewa chafu, kitambi au uzito mkubwa (obesity), uvutaji wa sigara, ugonjwa wa figo, kutofanya mazoezi, na unywaji wa pombe kupita kiasi.

 

Nitajuaje kama moyo wangu una shida yoyote kiafya?

Una dalili kama hizi hapa chini? Basi ni wakati wa kuonana na wataalam wa afya na kufanya vipimo mbalimbali kwasababu inawezekana kabisa ukawa na tatizo la moyo.

 

1. Maumivu ya kifua

Maumivu haya yanachoma katikati mwa kifua halafu yanapanda kwenda bega la kushoto mpaka kidevuni na pia husambaa mpaka mkono wa kushoto.

 

Wakati mwingine maumivu haya huwa yanakuja kama yanaminya (constrictive) na mtu anaweza kuhisi kama amewekewa tofali au mzigo kifuani. Maumivu haya hutokea pale mishipa ya damu inapokuwa haipeleki damu ya kutosha kukidhi mahitaji ya misuli ya moyo.

 

Umeshawahi kupata maumivu ya kifua? Sizungumzii maumivu unayoyapata kwasababu ya kikohozi, au kupigwa na kitu, hapana. Maumivu ya moyo huanza tu yenyewe na mara nyingi ukijaribu kutafuta sababu hutaipata mpaka pale uchunguzi utakapofanyika.

 

 

Kinachotofautisha maumivu ya kawaida na maumivu ya moyo ni dizaini ya maumivu yanavyokuja. Maumivu ya moyo yanafuata njia fulani kama nilivyosema hapo juu mwanzoni. Kuanzia kifuani kwenda kwenye bega la kushoto, mara nyingine huusisha kidevu na kuelekea mkono wa kushoto.

 

Ukipata maumivu ya namna hii basi inaweza ikawa ni shida ya moyo (Angina Pectoris/Myocardial infarction). Maumivu haya mara nyingi huanza ghafla na yanaweza kuambatana na kichefuchefu au kutapika, moyo kwenda kasi, kukosa nguvu, kushindwa kupumua vizuri na wakati mwingine kupoteza fahamu.

 

Maumivu mengine ya kifua (ya kawaida) huwa hayasambai, hubaki kifuani pale pale.

Maumivu haya ya moyo hutokea kwa sababu misuli ya moyo inakuwa haipati damu ya kutosha. Hii husababishwa na mambo mawili:

 

Kwanza, kama mishipa yako ya damu haitanuki kiasi cha kutosha kupitisha damu ya kutosha.

Hii mara nyingi hutokea kwa watu ambao mishipa yao ya damu imekuwa myembamba kutokana na mkusanyiko wa mafuta au sababu nyingine za kuzaliwa nazo.

 

Pili, kama wewe una damu chache unaweza kupata maumivu haya hasa pale unapofanya jambo linalohitaji moyo kupiga kwa kasi, hivyo mahitaji ya moyo hayatimii kwakuwa damu inayoenda ni chache.

 

Au pia ukifanya mazoezi makali kuzidi ustahimilivu wa moyo wako. Hali hii hutokea kwa wanarihadha na michezo mingine.

 

Ulishawahi kupata maumivu ya kifua ukifanya mazoezi kwa siku za mwanzoni? Hii huwa sio dalili ya tatizo la moyo bali ni kwamba mishipa yako ya damu haijazoea kupitisha kiasi kikubwa cha damu, hivyo unapofanya mazoezi moyo unadai kiasi kingi na mishipa yako inapeleka kidogo hivyo utapata maumivu kwasababu ya mishipa ya damu kukosa hewa ya kutosha.

Ndiomaana unashauriwa kuanza mazoezi kidogo kidogo huku unaongeza kila wakati.

 

Hali ya awali ya maumivu hujulikana kama Angina Pectoris, na isipotibiwa vizuri kwa kuondoa tatizo basi baada ya muda ile sehemu ya moyo isiyopata damu ya kutosha itakufa (Myocardial infarction) na utaanza kupata maumivu ya muda wote na badaye moyo unaweza kufeli.

 

Dalili ya namna hii sio ya kufanyia masihara, na bahati mbaya ukiwa na kisukari unaweza kupata mabadiliko kama haya na usisikie maumivu yoyote kwasababu ya mishipa ya fahamu inayosafirisha maumivu kuwa haifanyi kazi na hivyo utakuwa kwenye hatari ya kupata shambulio la moyo (heart attack).

 

Hivyo kwa mtu mwenye sukari ni muhimu kufanya check-up ya moyo na mafuta walau kila baada ya miezi 6.

 

Umekuwa ukipata maumivu kama haya? Basi ongea na daktari hapa, ili aweze kukisikiliza na kukupa ushauri unaofaa.

 

2. Kuchoka kirahisi

Ni jambo la kawaida mtu kuchoka hasa akifanya shughuli fulani nzito. Uchovu huu unatofautiana kulingana na ustahimilivu wa mtu.

 

Lakini uchovu unaosababishwa na moyo ni tofauti. Ukiwa na tatizo la moyo unachoka haraka kwa kufanya kazi ndogo tu, ambayo kama ungekuwa mzima wala usingehisi chochote.

 

Tired because of heart problems?

 

Mfano, ukitembea umbali mfupi basi utaanza kuhema sana, utalazimika kusimama na kupumzika halafu badaye utaendelea, na hivyo utatumia muda mrefu kutembea umbali mdogo au kufanya kazi fulani.

 

Uchovu huu huwa hauendani na ukubwa wa shughuli na mara nyingi huambatana na kifua kujaa na kubana, na mtu hutakiwa kusimama au kupumzika kabla hajaendelea.

 

Hali hii inaweza kuonekana kwa watoto?

Kwa watoto utagundua utofauti katika kucheza kwao. Mara nyingi utagundua mtoto hachezi sana na wenzake kama zamani, akikimbia kidogo utashangaa anakaa au anachuchumaa au kama ananyonya atachoka haraka na kuachia nyonyo mapema.

 

Kwa watoto, kunyonya ni shughuli kubwa sana na huitaji wawe fiti. Kama mtoto ana tatizo la moyo, basi hatoweza kunyonya vizuri maana kunyonya kunahitaji nguvu na hapa moyo huwa unafanya kazi kubwa.

 

Ukiwa na hitilafu, utashangaa mtoto kila akinyonya kidogo tu anaachia nyonyo. Hali hii huweza kufanya mtoto kushindwa kukua vizuri, kupoteza uzito na anaweza kupata utapiamlo.

 

Hali ya uchovu wa namna hii ni dalili kwamba moyo wako hauwezi kukidhi mahitaji ya mwili hivyo unafeli (heart failure).

 

Kitengo cha Afya ya Moyo Marekani (New York Heart Association), wameweza kuchambua viwango vya moyo kufeli kama ifuatavyo:

NYHA Class 1: Mtu ana shida ya moyo lakini bado anaweza kufanya kazi kama kawaida bila kuchoka kama mtu asiye na shida ya moyo. Hapa mara nyingi moyo unafeli lakini bado unaweza kufidia na hatua hii huchukua muda.

 

NYHA Class 2: Hapa mtu ana shida ya moyo na akifanya kazi ngumu basi huweza kuchoka haraka tofauti na kawaida.

 

NYHA Class 3: Hapa kazi ndogo sana inatosha kumfanya mtu achoke. Mfano, kutembea umbali mfupi tu hufanya mtu asimame, apumzike, hivyo anaweza kuchukua muda mrefu kufika mahali fulani.

 

NYHA Class 4: Hapa mtu huchoka hata akiwa amekaa, huwa na shida ya kupumua na hawezi kwenda umbali wowote.

 

Mara nyingi namba 1 na 2 watu huwa wanaishi nazo na hawaji hospitali, na huja tu pale wanapoanza kufika 3 na 4, maana hapo ndipo huwa wanaanza kuona dalili zingine nitakazozitaja hapo chini.

Je! Unajua kwamba tatizo la kuwa na uwezo kidogo wa kufanya tendo la ndoa, unaoambatana na kuchoka haraka, na kushindwa kuendelea kabisa baada ya mshindo inaweza kuwa dalili mojawapo ya tatizo la moyo?

Taadhari: Kuwa makini, dalili hizi najaribu kukuelezea ili ujitambue na utafute msaada wa afya mapema na sio kukwambia uende duka la dawa kutafuta dawa ya moyo!

 

Jua kwamba moyo kushindwa kufanya kazi vizuri husababishwa na hali mbalimbali, na hivyo wewe kupona ni mpaka chanzo kigundulike kwa vipimo maalum na kitibiwe. Tofauti na hapo hauwezi kupona.

 

Unahitaji kujua ufanyeje baada ya kuona dalili hizi? Usijali ongea na daktari hapa, ili upate ushauri kabla hujaenda hospitali.

 

3. Kikohozi kisichopona

Kikohozi kinachosababishwa na ugonjwa wa moyo huwa kina tabia zake maalum. Huwa hakiponi kwa dawa za kikohozi, na mara nyingi hutokea usiku mtu anapokuwa analala; wakati mchana huwa ni kidogo sana.

 

Kikohozi cha namna hii huweza kuwa kama pumu na hivyo watu wengi bila kujua huisi ni pumu ya ukubwani na mara nyingi utakuta mtu tayari anatumia dawa za pumu.

 

Mwaka 2022 nikiwa nchini Namibia nilikutana na mama mmoja aliyekuwa na tatizo la moyo. Bahati mbaya, kwasababu alikuwa anakohoa zaidi usiku na kifua kubana anapolala, moja kwa moja akajua ni pumu kwasababu kazoea kuwaona watu wenye pumu wakipumua na kukohoa vile.

 

Kila akienda hospitali kwasababu ya ujuaji mwingi anasema kabisa, “Daktari mimi nina pumu naomba niandikie dawa ya Pumu”. Madaktari walikuwa wanamtibu Pumu mpaka nilipokutana naye. Nilimuuliza tabia ya kikohozi chake akaniambia, niliposikiliza moyo wake nikagundua haupigi vizuri, kulikuwa na viashiria vya moyo kufeli.

 

Nilimuandikia dawa na kumshauri kufanya vipimo maalum, toka kipindi kile aliendelea kuwa mgonjwa wangu, na yuko fiti sana sasahivi, anaendelea vizuri na shughuli zake za mapambo. Hivyo hatua ya kwanza ya kutibu ugonjwa huu ni kujua chanzo.

 

Moyo unapofeli, huwa unashindwa kusukuma damu vizuri, hivyo huongeza presha kwenye mapafu na matokeo yake maji hujaa kwenye mapafu na kusababisha Kikohozi cha usiku mtu anapolala.

 

Kikohozi hiki huwa kama kinabana kifua na hutoa mlio kama filimbi. Ukianza kupata dalili kama hii, basi pata ushauri wa daktari, inawezekana kabisa ukawa na tatizo la moyo.

 

Zaidi kikohozi cha moyo huchanganya mara nyingi mtu akilala, na hupoa akiamka na kukaa au kutembea. Akilala huisi kama anabanwa na kifua na hivyo watu hawa mara nyingi huogopa kulala.

Vikohozi vingine mtu hukooa muda wowote haijalishi kalala, amekaa au anatembea.

 

Una kikohozi cha namna hii? Wasiliana na daktari kwa ajili ya ufafanuzi kabla hujaenda hospitali.

 

4. Kuvimba miguu

Miguu kuvimba ni dalili mojawapo ya moyo kushindwa kufanya kazi vizuri (kufeli). Kuna maradhi mengi yanayoweza kusababisha miguu kuvimba, Mfano, utapiamlo, magonjwa ya ini, magonjwa ya figo, na kadhalika.

 

Lakini tofauti ya kuvimba kwa miguu kunakosababishwa na moyo ni kwamba, kuvimba huku huambatana na dalili zingine hapo juu kama kuchoka haraka, kukohoa usiku, kifua kubana na kuuma.

 

Katika jamii yetu, kuvimba miguu huusishwa na kurogwa. Utaskia mtu anasema “Kuna madawa niliruka njiani ndio maana navimba hivi…”. Basi wataanza kwenda kwa mganga kuchanja miguu lakini bila mafanikio!

 

Kuvimba miguu husababishwa na moyo kufeli. Hivyo moyo unafikia mahali kwamba hauna nguvu ya kusukuma damu yote inayoingia na hivyo kusababisha presha kubwa kwenye mishipa ya damu. Hii pia huweza kusababisha jam kwenye maini na kufanya mtu kuwa na maumivu ya tumbo.

 

Kumbuka: Kuvimba miguu hakusababishwi na moyo kufeli peke yake, zipo sababu nyingine nyingi. Vipimo zaidi vitahitajika kuhakikisha hauna shida nyingine kama utapiamlo,  tatizo la Figo (nephrotic/nephritic syndrome), tatizo la Ini, damu kuganda (Deep venous thrombosis), na kadhalika.

 

Ndio maana ukiwa na daktari wako binafsi ni rahisi kuepuka matumizi mabaya ya dawa bila ushauri. Jipatie daktari binafsi au wa familia kutoka Abite Nyumbani leo. Tembelea duka letu hapa.

 

5. Kupoteza uzito

Moyo kufeli ni mojawapo ya kisabababishi cha kupungua kilo. Moyo ni kiungo ambacho hufanya kazi kubwa sana katika mwili wa binadamu na hivyo huitaji nguvu kubwa mwilini.

 

Moyo unapofeli hutakiwa kufanya kazi mara mbili au tatu zaidi ya kawaida kuhakikisha kila kitu kinabaki sawa (compensatory mechanisms). Hali hii huuweka mwili katika uhitaji mkubwa wa lishe na nguvu ya mwili.

 

Losing weight because of heart failure?

 

Kwa bahati mbaya, mtu anapoanza kupata maradhi ya moyo, hamu ya kula hupungua sana wakati uhitaji umeongezeka na hivyo kusababisha uzito kupotea. Dalili hii kwa watoto hujidhiirisha kwa kushindwa kukua kwa wakati (failure to thrive), kutoongezeka uzito na wengine huishia kupata utapiamlo.

 

Mtoto mwenye tatizo la moyo katika uchanga wake huwa hawezi hata kunyonya maana kila akianza kunyonya ndio pumzi inakata na anaacha kunyonya. Kama mtoto wako haongezeki kilo na anazidi kukonda, hakikisha unapata vipimo mbalimbali vya mwili ikiwemo moyo.

 

Wazazi wengi huchelewa kuligundua hili mapema mpaka baadaye kabisa watoto wanapokuwa wamedhoofika mno.

 

Mwisho

Una dalili yoyote hapo juu? Ni vyema ukafika hospitali kwa ajili ya kupata vipimo na matibabu ya mapema kwakuwa moyo ukishafeli huchukua nguvu kubwa na muda mwingi kurudi katika hali ya kawaida na pengine moyo wako unaweza kufeli moja kwa moja.

 

Moja ya njia ya kuhakikisha hauchelewi hospitali ni kuwa na huduma ya daktari binafsi kutoka Abite Nyumbani. Huduma hii itakuwezesha kuwa na daktari wako binafsi kwa gharama ya kawaida tu.

 

Daktari huyu utamtumia kwa ushauri wa kiafya na atasaidia kugundua mapema tatizo lako na kukuagiza matibabu au kukushauri ufanye nini kwa hatua inayofuata.

 

Wagonjwa wengi wanaotumia huduma hii wametupongeza kwa kuwasaidia kupunguza kwenda hospitali kiholela au kuchelewa hospitali kwa sababu tu ya kukosa ushauri wa kitaalamu. Ingia “hapa” kupata huduma hii.

2 thoughts on “Dalili Kuu 5 Zinazoashiria Una Tatizo la Moyo”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW