Athari 7 za Kukosa Lishe Bora kwa Mama Mjamzito

Kipindi cha ujauzito ni kipindi ambacho mama anapaswa kuwa anakula vyakula vinavyompatia virutubisho vya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya kiafya yanayotakiwa katika mwili wake na pia kwa ajili ya ukuaji bora wa mtoto tumboni mwake.

 

Vyakula vinavyompatia mama virutubishi vya kutosha katika kipindi cha ujauzito huimarisha afya ya mama na humsaidia mtoto kukua vizuri kimwili na kiakili.

 

lishe bora kwa mama mjamzito

 

Vyakula hivi ni vile ambavyo vinatoka katika makundi yote ya vyakula kama ambavyo nimewahi kuongelea katika makala ya sahani inayofaa.

 

Baadhi ya mifano ya vyakula ambavyo mama mjamzito anapaswa kula ni kama: Nyama, samaki, maini, nyama ya kuku, maharage, choroko, njegere, kunde na kadhalika.

 

Vyakula hivi vina kirutubishi cha protini ambacho husaidia katika kuimarisha kinga ya mwili ya mama kwasababu protini inahusika moja kwa moja katika uumbwaji wa seli kinga za mwili zinazofanya kazi ya kupambana na magonjwa mbalimbali.

Vyakula hivi pia hufanya kazi ya kusaidia ukuaji wa mtoto aliyeko tumboni.

 

Vyakula vingine ambavyo unatakiwa kula katika kipindi hichi cha ujauzito ni matunda na mboga mboga za majani ambazo mojawapo ya kazi zake ni kukupatia kirutubishi muhimu cha madini kiitwacho madini chuma.

 

Kirutubishi hichi kinasaidia katika kuongeza damu mwilini ambapo damu hii ni kisafirishaji cha virutubishi vingine vyote mwilini. Hivyo kama kutakua na upungufu wa damu, utakua unaingia katika hali duni ya lishe.

 

Ukosefu wa lishe bora wakati wa ujauzito huweza kusababisha changamoto mbalimbali za kiafya kama vile:

1. Mama kutokuongezeka uzito kama inavyotakiwa

Katika kipindi cha ujauzito mama anapaswa kuongezeka uzito ili kuonyesha kuwa kuna ukuajia wa mtoto lakini ikitokea kuna upungufu wa virutubishi muhimu, mwili hautaweza kuongezeka kwa kiwango sahihi kwasababu mtoto atakua anakua kwa taratibu sana.

 

Hali hii ya kuongezeka uzito haitakiwi kuwa kwa kiwango cha kupitiliza; na ni kwa watu ambao wanakua na uzito wa kawaida na uzito usiokua umezidi.

Nimeona nisisitize hili kwani katika kipindi cha ujauzito mama, ambaye kabla ya kupata ujauzito alikua na uzito uliozidi, anakua anaongezeka uzito zaidi hali ambayo si nzuri kwa afya.

Kinachotakiwa kufanya ni kuhakikisha hauwi na uzito mkubwa katika vipindi vya kabla ya kupata mimba kwani uzito uliozidi huweza kusababisha changamoto katika kipindi cha kujifungua.

 

2. Upungufu wa damu kipindi cha ujauzito

Wakina mama wengi, katika swala la upungufu wa damu, wamekua wakiamini kwamba vidonge vya kuongeza damu pekee vinaweza kuwasaidia kuongeza damu.

 

Hii dhana si kweli kabisa kwasababu vile vidonge huwa vinaitwa vidonge vya nyongeza, ikimaanisha ni lazima kuwe na sehemu ambayo vinakua vinaongeza! Na sehemu hio huwa ni katika vyakula unavyotumia.

 

Ili damu iyongezeke mwilini, unapaswa kutumia vyakula vyenye madini ya chuma pamoja na vyakula vitakavyowezesha ufyonzwaji wa madini haya mwilini.

 

Hivyo vidonge vya kuongeza madini chuma huja baada ya kula vyakula hivi na sio kwamba vinakua mbadala wa vyakula hivi.

 

3. Kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu

Hali hii hutokana na kutokupata virutubisho vya kutosha kuwezesha mtoto kukua vizuri anapokua tumboni kwa mama yake.

Kumbuka: Mama mjamzito anapaswa kula kwa ajili yake na mtoto wake tumboni.

 

Mfano: Kuna mama ambaye alijifungua mtoto mwenye uzito pungufu pamoja na kwamba mtoto amezaliwa katika kipindi cha mimba iliyokomaa, yaani miezi tisa.

 

Katika kuhojiana, mama huyu alitoa ripoti ya kwamba alikua akila milo mitatu kwa siku. Nilipomuhoji zaidi niligundua alikua anakula vitumbua au mandazi mawili tu na chai asubuhi.

 

Mchana alikua akila ugali na samaki wawili. Msosi wa jioni ulikua hauna tofauti sana na wa mchana. Kwa lishe ya namna hii, mtoto utakayejifungua lazma atakua na uzito pungufu (njiti).

 

4. Ongezeko la magonjwa kwa mama

Hii ni kwasababu, katika kipindi cha ujauzito, kinga ya mwili ya mama hupungua kutokana na mabadiliko ya kifiziolojia ya mwili.

 

Seli za kinga ya mwili huwa na asili ya protini hivyo inabidi kula vyakula vya protini vya kutosha kwa kiwango kinachotakiwa mwilini ambacho ni gramu 0.8 mpaka gramu 1 kwa kila kilo ya mtu kwa siku moja (0.8 -1 gram/kg/day).

 

Kama unahitaji kujua namna ya kuzipata gramu hizi, tafadhali wasiliana nami kwani inategemea na kilo za mtu na chakula gani kinachotumika kwa wakati huo.

 

5. Kuzaa mtoto mfu. Hii ni kwasababu mtoto hutegemea virutubishi ili kukua vizuri.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba hali duni ya lishe kwa mtoto aliyeko tumboni huweza kupelekea changamoto katika ukuaji wa mtoto na pia katika kondo la uzazi ambalo ndio chanzo la chakula kwa mtoto.

Hali hii ikitokea huweza kusababisha mtoto kupoteza maisha anapokua tumboni mwa mama.

 

6. Kujifungua kabla ya wakati na hivyo kupelekea kuzaa mtoto njiti pia ni changamoto inayoweza kutokea kutokana na hali duni ya lishe kipindi cha ujauzito.

 

7. Kukosa nguvu za kufanya shughuli mbalimbali za kila siku kutokana na hali duni ya lishe inayopelekea kuchoka sana.

 

 

Mambo muhimu ya kuzingatia kukabiliana na changamoto za lishe duni kipindi cha ujauzito
  1. Uhudhuriaji wa kliniki ya ujauzito pindi tu unapojua wewe ni mjamzito. Usisubirie miezi mitatu, anza leo kama umeshajua una ujauzito!
  2. Kula milo minne kwa siku na asusa mara nyingi kadri uwezavyo ili uweze kupata virutubishi vya kutosha kwa ajili ya afya yako na afya ya mtoto wako.
  3. Epuka kunywa kahawa au majani ya chai wakati wa mlo kwani huingiliana na ufyonzwaji wa madini chuma mwilini.
  4. Meza vidonge vya kuongeza damu (FEFO) katika kipindi chote cha ujauzito. Unaweza kuendelea kumeza mpaka kipindi cha miezi mitatu baada ya kujifungua.
  5. Kunywa maji ya kutosha kila siku; angalau glasi nane mpaka lita moja na nusu kwa siku. Husaidia umeng’enywaji wa chakula kuwa rahisi.

 

Mwisho

Baada ya mazungumzo na mteja wangu, huwa nampatia orodha ya vyakula anavyotakiwa kula. Orodha hii inazingatia upatikanaji wa vyakula hivi katika maeneo yake na hali yake ya kiuchumi ambayo hupelekea kuwezesha upatikanaji wa vyakula mbalimbali.

 

Hivyo basi nichukue fursa hii kukukaribisha katika huduma yetu ya kupatiwa muongozo wa chakula (mpangilio wa mlo) katika kipindi cha ujauzito ili uweze kupiga hatua moja kwenye safari ya lishe bora kipindi cha ujauzito.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW