Fahamu vyakula vya kumpatia mtoto wako baada ya kufikisha miezi 6

Wazazi wengi na walezi wa watoto waliokamilisha miezi sita, na wanaotakiwa kuwaanzishia watoto vyakula vya nyongeza, huwa na maswali mengi sana ya vyakula vya kutumia katika kuwalisha watoto wao.

 

Wengi wao huishia kuogopa kuwapa watoto vyakula vya aina mbalimbali wakihofia labda hawatakua wanafanya kitu sahihi kuwalisha watoto wao vyakula mbalimbali.

 

 

Je! Unajua namna ya kumuanzishia mtoto vyakula vya nyongeza?

Kama hufahamu namna ya kufanya, usijali! Kupitia makala hii nitaelezea namna ya kumuanzishia mtoto wako chakula cha nyongeza akishafika miezi 6. Utaweza kujifunza vyakula ambavyo mtoto anapaswa kula na kwa umri gani mpaka pale atakapofika mwaka mmoja.

 

Uzito wa chakula (Consistency of the food)

Tuanze na namna ambavyo chakula kinapaswa kiwe. Chakula kinatakiwa kisiwe chepesi, kwa maana ya kwamba hakitakiwi kuwa na urahisi wa kumiminika katika kijiko – yaani kisiwe majimaji. Faida ya chakula kizito ni uwepo wa virutubishi vya kutosha kwa ajili ya mtoto.

 

Watoto wa Miezi 6

Watoto wanapotimiza miezi sita wanatakiwa kuwa bado wananyonya maziwa ya mama kwa sababu ndio chanzo muhimu cha virutubishi mwilini.

 

Katika kipindi hichi, japo maziwa ni chanzo muhimu cha virutubishi, lakini kinakua hakitoshi hivyo inabidi kuanza kumpa mtoto vyakula vingine.

 

Kwa upande huu wa chakula, watoto hawa wanapaswa kuwa wanakula mara mbili mpaka tatu kwa siku na hii inaweza kuhusisha vijiko viwili mpaka vitatu vikubwa vya chakula.

Muhimu: Bado mtoto anapaswa kuendelea kunyonyeshwa mara kwa mara.

 

Namna ya kumpa mtoto chakula katika kipindi cha miezi sita ni kama ifuatavyo:

Mama anapaswa kuwa anamnyonyesha mtoto halafu katikati anampa chakula na kisha anamnyonyesha tena. Kumbuka kuwa watoto wana matumbo madogo kwa kipindi hiki hivyo hawapaswi kula chakula kwa kiasi kingi.

 

Mfano wa ukubwa wa tumbo la mtoto afikapo miezi sita, ambao napenda kuwapa akina mama na walezi wanaokuja katika kliniki ya watoto, ni sawa na ngumi ya mkono wake hivyo mtoto hapaswi kupewa chakula kingi kuliko uwezo wa tumbo lake.

 

Vyakula vya kumpa mtoto anapotimiza miezi 6

Mtoto anapotimiza miezi sita anapaswa kuwa anatumia vyakula vilaini kama vile uji na matunda yaliyosagwa.

 

Vyakula hivi havipaswi kuwa katika mfumo wa majimaji mengi, vinapaswa kuwa na uzito ambao haumiminiki kirahisi katika kijiko cha chakula kwa sababu vikiwa na majimaji mengi huwa havina virutubishi vya kutosha.

 

Kidokezo: Mtoto wa miezi sita anapoanza kula anakua na hali ya mshangao kwa sababu ya vyakula vipya.

 

Lishe kwa Mtoto Kipindi cha Miezi 7 Mpaka 8

Mtoto anapotimiza miezi 7 mpaka 8 unaweza kuanza kumlisha vyakua kiasi cha nusu kikombe cha kawaida (kikombe cha kawaida kinachotumika kwa ajili ya chai). Chakula hichi kinatakiwa kuwa kilaini na mtoto anapaswa kula mara mbili mpaka tatu kwa siku.

 

Kumbuka: Mtoto alipoanza kula kipindi anafika miezi sita alianza na vijiko viwili mpaka vitatu vya chakula. Hivyo anapofika miezi 7 hadi 8 atakua anakula chakula kiwango cha nusu kikombe.

 

Kama unajiuliza ni vyakula gani vya kumlisha mtoto katika kipindi hiki, jibu ni vyakula vyote isipokua asali mpaka pale atakapofika miezi 12. Hapa inabidi kuongeza asusa zenye virutubishi vya kutosha kama vile matunda yaliyopondwa mfano ndizi, papai na parachichi.

 

Jambo la kuzingatia ni kwamba kadiri mtoto anavyoendelea kupata vyakula vya nyongeza anatakiwa pia kupata maziwa ya mama kama kawaida.

 

Lishe kwa Mtoto wa Miezi 9 Mpaka 11

Mtoto wako anapofika miezi tisa mpaka kumi na moja anapaswa kula chakula kiasi cha nusu kikombe kama ilivyo kawaida. Kinachobadilika ni idadi ya milo; unapaswa kuwa unampa milo mitatu mpaka minne kwa siku.

 

Katika kipindi hichi unaweza kuwa unakatakata vyakula vilaini katika size ndogondogo na unampatia mtoto anakula; na hata wakati mwingine kwa kutumia mikono yake mwenyewe kwani kipindi hichi anakua anaandaliwa kwa ajili ya kuhitimu vyakula vya majimaji na kwenda katika darasa la kula vyakula vyenye ugumu kiasi (solid foods).

 

Muhimu: Utaendelea kumyonyesha mtoto pindi anapokua na njaa. Ili kujua kama mtoto wako ana njaa, anaweza kuwa anaweka vidole vyake mdomoni.

Vyakula hivi anavyopewa mtoto vinapaswa kuwa na nguvu na kumpa mtoto virutubishi vya kutosha.

 

Swala la muhimu sana kuzingatia katika kipindi hichi cha kumuanzishia mtoto vyakula kwa ujumla ni kwamba mbali na vyakula vya jamii ya nafaka kama vile mahindi na vyakula kama viazi na ndizi, pia mtoto anapaswa kuwa anakula mboga za majani, matunda, pamoja na vyakula jamii ya mikunde kunde kama vile maharage na njegere.

 

Vyakula vingine ni nyama, samaki, kuku, mayai na maziwa. Kwa upande wa maziwa ya ng’ombe, tunashauri mtoto kutumia maziwa haya pale tu anapokua amefika umri wa mwaka mmoja. Chini ya hapo mtoto huyu atafaidika zaidi kwa kutumia maziwa yanayotoka kwa mama pekee.

 

Nimeona nisisitize swala hilo kwasababu katika eneo langu la kazi nimekutana na malalamiko mengi ya wazazi kuhusu watoto kutokupenda kula lakini nikiuliza huwa anapewa vyakula gani ninagundua kwamba watoto wengi hupewa vyakula vya kundi moja kwa muda mrefu mfano Uji wa sembe au dona pekee.

Hii husababisha mtoto kukataa chakula kile kwasababu anapatwa na hali ya kukichoka

 

Lishe kwa watoto wasionyonya maziwa ya mama

Ikitokea kuna changamoto ya mtoto kutokupata maziwa ya mama labda kwa sababu mama ana changamoto isiyomuwezesha kunyonyesha au mama amefariki, zingatia yafuatayo:

1. Mtoto chini ya miezi sita anapaswa kuwa anapata maziwa mbadala yaliyotengenezwa tayari kwa ajili ya watoto walio na umri chini ya miezi sita.

 

2. Anapotimiza miezi 6 na kuanza kula, anapaswa kupata vyakula laini na matunda yaliyopondwa na atakua anatumia vijiko viwili mpaka vitatu mara nne kwa siku.

 

3. Anapofika miezi 7 mpaka nane anapaswa kuwa anakula nusu kikombe cha chakula mara nne kwa siku pamoja na asusa yenye virutubishi mfano matunda yaliyopondwa.

 

4. Anapofika miezi 9 mpaka 12 anapaswa kuwa anakula nusu kikombe cha chakula mara nne mpaka tano kwa siku pamoja na asusa zenye virutubishi mara mbili kwa siku.

 

Kumbuka: Vyakula vinatakiwa kuwa na uzito usioweza kumwagika kirahisi katika kijiko cha chakula. Hii inaashiria kwamba chakula hichi kina virutubishi vya kutosha tofauti na chakula ambacho kimeandaliwa na kuwa na majimaji (chakula chepesi).

 

Ukihitaji kuwasiliana na mimi kwa ajili ya kupata mpangilio wa chakula wa mtoto wako, weka booking yako hapa.

3 thoughts on “Fahamu vyakula vya kumpatia mtoto wako baada ya kufikisha miezi 6”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW