Sumu Kuvu: Maana, Madhara na Jinsi ya Kuiepuka

Wakati ninaandika makala ya “Njia 2 za kutengeneza unga wa lishe kwa ajili ya mtoto wako na familia“, nilizungumzia utumiaji wa nafaka aina ya mahindi na hapo ndipo nikapata wazo la kuandika makala nyingine itakayokusaidia wewe msomaji kufahamu namna ya kuchagua nafaka salama kwa ajili ya utengenezaji wa unga huo wa uji wa lishe.

 

Kwa ajili ya usalama wa chakula, unapaswa kufanya machaguo ya nafaka hizi ukizingatia swala la kuepuka sumu kuvu.

 

 

Kupitia makala hii, utaweza kufanya maamuzi sahihi kwenye chaguzi za vyakula vya nafaka ambavyo vinatumika kama chakula katika hali yake ileile vikitoka shambani mfano mihogo au mahindi ya kuchemsha, pamoja na unga sahihi wa Lishe.

 

Pia wale wenye kupendelea matumizi ya karanga mbichi na mihogo mibichi, somo hili linawahusu.

 

Nini maana ya Sumu Kuvu?

Taasisi ya Viwango Tanzania (TBS, 2022) imetoa maana ya sumu kuvu, mycotoxin, kama ni sumu inayozalishwa na kuvu (fungi) ambao wanapatikana kwa asili kwenye mazingira na wanaathiri mazao na kusababisha athari za kiafya kwa binadamu na mifugo.

 

Sumu hii huathiri nafaka mbalimbali mfano mahindi, mtama, ngano, uwele na ulezi, karanga, korosho, viungo vilivyokaushwa, mbegu za mafuta (alizeti na pamba) na mazao yatokanayo na mifugo mfano maziwa na mayai.

 

Muonekano wa chakula kilichoathiriwa na sumu kuvu unakuwaje?

Uotaji/ukuaji wa kuvu unaweza kutokea kabla au baada ya kuvuna, kipindi cha uhifadhi na kwenye chakula chenyewe hasa kwenye mazingira ya joto, unyevu na uchafu.

 

Mazingira haya hutengeneza hali rafiki kwa uotaji wa fangasi wanaoleta sumu kuvu.

 

Muhimu: Sumukuvu ni sumu ambazo haziwezi kuondolewa kwa kupikwa au kusindikwa hivyo basi hufanya sumukuvu kuwa sumu ambayo ni hatari sana katika afya na ina madhara ambayo yanaweza kuonekana hapo hapo au kwa kipindi cha muda mrefu.

 

Mara nyingi unaweza kukuta mahindi ya kuuzwa yana weusi na mfanyabiashara akakuambia hayana shida; usikubali maneno yake na usinunue kwasababu weusi huo unamaanisha uwepo wa sumu kuvu kwenye hayo mahindi.

 

Hivyo hivyo ukiwa shambani na kukutana na hindi kama hili lenye weusi, usilitumie kwa kuchemsha au kuchoma kwani ni hatari sana kwa afya yako.

 

Kama umenunua unga wa ugali au uji, na ukawa na uchungu, hii huashiria kwamba fangasi hawa wameshaingia katika chalupa hicho na kimeshakua si salama kwa kuliwa.

 

Sumukuvu hii pia inaweza kupatikana katika viungo vya kupikia mfano mdalasini, viungo vya samaki, viungo vya nyama na kadhalika.

 

Viungo hivi vikishakua vimepata unyevu na kuwa na hali ya kuganda au kutengeneza mabonge, na wakati huu unaweza kukuta chakula hichi kinakua kimetengeneza  ukungu unaojivuta, hali hii huashiria kwamba fangasi hawa wameshawasili katika viungo hivyo na hufanya chakula kutokua salama kwa kula.

 

“Undugu wa Achari na Sumu Kuvu”

Kuna dada mmoja aliwahi kuniambia kuwa kwenye ukoo wao wana kawaida ya kutengeneza achari na kama achari hii itakua inakaa muda mrefu na kutengeneza ukungu, huwa wanafanya kuuondoa tu huo ukungu na achari ile huendelea kutumika.

 

Nilimuuliza kama anafahamu ule ukungu unamaanisha nini, hakuwa anafahamu!

 

Ndipo nikamuelewesha kwamba ukungu ule huashiria fangasi na ni hatari kwani fangasi si rahisi sana kuondoka katika chakula na hata mwilini kwasababu fangasi hana tabia ya kufa kirahisi.

 

Hivyo kama chakula kikiharibika kinatakiwa kisitumike tena kwani si salama kwa afya ya mlaji.

 

Madhara yatokanayo na ulaji wa vyakula vyenye sumu kuvu

Tafiti zinaonyesha kwamba kula chakula kilicho na zaidi ya Miligramu 1 kwa kila Kilo 1 kunaweza kusababisha ugonjwa wa ‘aflatoxicos’ ambao ni kula sumu

 

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kutapika, kuumwa na tumbo, kuwa na maji kwenye mapafu, kuharibikwa kwa maini na hata kupoteza maisha.

 

 

Jinsi ya kuepuka ulaji wa sumu kuvu

Ili uweze kuepukana na kula vyakula vyenye sumu kuvu, fanya yafuatayo:

 

  1. Chagua vyakula ambavyo ni visafi na nafaka ambazo ni nzima nzima zisizo na rangi nyeusi na hali ya kuharibika.

 

  1. Acha kutumia vyakula ambavyo vimekaa muda mrefu sana. Mfano, kuna watu wenye tabia ya kutumia nyanya zilizoharibika na kukata palipooza kisha kutumia panapoonekana ni pazima kwa macho tu.

 

Kumbuka: Fangasi wanaweza kuwa vimelea visivyoonekana kwa macho ya kawaida mpaka kutumia microscope (kifaa cha kimaabara) na vinaweza kuishi katika mazingira magumu na kushamiri katika ukuaji.

Hivyo kutambua kama chakula chako kina fangasi, kwa macho, ni ngumu sana.

 

  1. Tumia viungo ambavyo sio vya muda mrefu na vilivyotengenezwa katika hali ya usafi.

 

  1. Tunza vyakula vyako katika hali ya usafi isiyo na unyevunyevu kwasababu mazingira ya uchafu na unyevunyevu huchochea mazalia ya vimelea vya wadudu na fangasi.

 

  1. Epuka kutumia vyakula vilivyotengeneza weusi au ukungu kwani huashiria fangasi ambao hutengeneza sumu kuvu.

 

 

Muhimu: Ni vizuri ukawa unatengeneza vyakula mbalimbali mwenyewe ili uwe na uhakika na hali ya usafi pamoja na malighafi zilizotumika kuandalia vyakula hivyo.

8 thoughts on “Sumu Kuvu: Maana, Madhara na Jinsi ya Kuiepuka”

    1. Ester Mndeme

      Nafurahi kusikia umejifunza . Endelea kufuatilia makala zetu za lishe utajifunza zaidi.

    1. Ester Mndeme

      Asante sana Suleiman. Amina. Nitafanya kadri ya uwezo wangu kuisaidia jamii yetu ya kitanzania.

    1. Ester Mndeme

      Nimefurahi kusikia umejifunza Eric . Endelea kufuatilia makala zetu zq lishe utajifunza zaidi.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW