Mwaka 2005, wakati nikiwa kidato cha kwanza, nilikuwa kwenye taxi ambayo mimi na wenzangu tuliikodi wakati tunarudi shule.
Kipindi hiko madereva taxi walikuwa wanatujaza sana kwenye gari dogo, wakati mwingine mpaka kwenye buti.
Wakati niko kwenye taxi niligundua kwamba milango ikishafungwa nahisi kama vile sina hewa pamoja na gari kuwa na AC. Nilikuwa nahisi naweza kufa muda wowote na kuna muda nilianza kupiga kelele kumwambia dereva asimame nishuke.
Nilikuwa na hofu kubwa mpaka wenzangu walinishangaa sana. Nilishuka nikachukua boda mpaka shule kwa gharama kubwa ya buku mbili; kwa kipindi kile ilikuwa kubwa sana lakini mimi nilihisi nafuu.
Niliendelea kuwa na hofu za namna hiyo lakini sikujua tatizo ni nini mpaka baadaye nilipoenda Chuo kikuu.
Wakati nipo Chuo Kikuu, mwaka 2013, ikatokea kizaa zaa kingine. Wakati tunaenda kupanda lift, baada tu ya kuingia, mlango ulipofungwa nilihisi kufa! Nilitamani wafungue mlango nitoke japo nilikuwa nimechelewa, lift ilishaanza kupanda juu.
Nilitoka jasho na kutetemeka sana mpaka aibu.Wakati wa kurudi chini nilikomaa kutumia ngazi. Sikukutaka kutumia lift tena.
Inaonekana sikuwa napenda kabisa kuwa sehemu iliyofungwa ambayo najua siwezi kutoka kirahisi, hivyo kila nikijikuta katika mazingira hayo naingiwa na hofu kubwa sana.
Ndipo nikaamua kuingia kwa Dr. Google ili kujua tatizo langu ni nini maana ilifikia mahala ikawa inaingilia furaha yangu. Niligundua tatizo langu lilikuwa ni hali inaitwa Claustro-Phobia – fear of closed spaces.
Ni hofu ya mahala palipobanwa au kufungwa ambapo kutoka sio rahisi, mfano nikiwa kwenye gari linalotembea, ndege, lift, chumbani nk. Baada ya hapo niliamua kuchimba zaidi kujua aina za Phobia.
Nikaja kugundua kwamba watu tuliokuwa tunawacheka zamani kwamba ni waoga sana wa vitu – kama wadudu, kusimama mbele za watu wengi, wanyama kama mbwa au paka, mahusiano, kufeli n.k – haikuwa tu hofu ya kawaida.
Ni hofu ambayo iko katika saikolojia na ndio maana ukimtishia mtu hicho kitu anaweza mpaka kuzimia kwa hofu kubwa.
Tofauti kati ya hofu ya kawaida na Phobia ni nini?
Phobia ni hofu iliyopitiliza ya kitu fulani ambayo huingilia mpaka hali yako ya afya na ubora wa maisha yako.
Mara nyingi hicho kitu huwa hakina madhara kama kinavyoogopwa, ni hofu tu ambayo umeijenga mwenyewe kwenye ubongo wako.
Mfano, hofu ya sisimizi. Kuna mtu alishawahi kufa kwa kuumwa na sisimizi? Lakini utashangaa hofu uliyonayo ni kama sisimizi wakikuuma utakufa, jambo ambalo halina uhalisia wowote!
Sifa kubwa ya Phobia ni kwamba mara nyingi huwezi kuelezea hasa unaogopa nini, ila wewe unaogopa tu (The fear is not justifiable).
Katika uzoefu wangu wa Phobia, ni ngumu sana kuidhibiti kwasababu huwa imejificha kwenye ubongo wa ndani (subconscious mind).
Haijitokezi mara kwa mara hivyo hukufanya usahau au udhani imeisha mpaka pale utakapokutana na hali inayoileta (trigger).
Aina za phobia ni zipi?
Kuna aina nyingi sana za Phobia lakini unaweza kuziweka katika makundi matatu:
1. Hofu ya vitu fulani (specific phobias)
Mfano, wadudu, wanaume, wanawake, wanyama, kuendesha gari, kuogelea, hofu ya kina kirefu, hofu ya kukaa kwenye majengo na kadhalika.
2. Hofu ya kuwa kwenye sehemu za umati (Social phobia)
Mfano, kuogopa kuongea mbele ya umati au kuogopa kwenda sehemu ambayo mtu huisi anaweza kunyanyasika au kukosa uhuru wake binafsi Mfano kanisani na baa. Watu hawa hupenda kukaa ndani tu.
3. Hofu ya kuwa katika sehemu ambayo huwezi kutoka kirahisi (Agoraphobia)
Watu wa namna hii huogopa mikusanyiko au sehemu zilizofungwa ambapo sio rahisi kutoka, mfano hofu ya kupanda ndege (Aerophobia).
Watu wa namna hii hawapendi kuzungukwa na watu wengi na wanapoenda mahali hupenda kukaa karibu na mlango au dirisha na wakiona watu wanaongezeka wanaweza kutoka nje au kuondoka.
Namba mbili na tatu ni changamoto kubwa sana kwa sababu katika maisha ya kila siku ni ngumu sana kuepuka mikusanyiko na sehemu zilizofungwa.
Hivyo hofu hizi huathiri ubora wa maisha ya mtu binafsi na mwisho inaweza kuleta msongo wa mawazo.
Piga picha unatakiwa kusafiri kwa Ndege kwenda Africa kusini. Kampuni imeshakukatia tiketi halafu ukifika kwenye ndege, kwa sababu ya Phobia, unaamua kushuka au kugoma kusafiri kabisa.
Phobia husababishwa na nini?
Kumekuwepo na theory mbili zinazoelezea sababu ya watu kuwa na Phobia.
Theory ya Kwanza inaongelea kuzaliwa na vinasaba (Genetics) vya kuogopa sana vitu fulani.
Theory hii hutumia ushahidi wa watoto mapacha waliozaliwa na kukua katika mazingira tofauti. Utafiti ulionyesha japo mapacha walikulia katika mazingira tofauti walionekana kuwa na Phobia ya kitu kile kile.
Hii inaonyesha uwezekano wa kurithi au kuzaliwa na vinasaba vya hofu hiyo.
Utafiti huu umeonyesha pia mtoto aliyezaliwa na Baba au Mama mwenye Phobia ya kitu Fulani, mfano wadudu, ana asilimia 39% ya kupata phobia hiyo.
Theory ya pili inaelezea kuhusu kujifunza (learned experience) baada ya kupitia hali hiyo ukiwa mdogo au kuona wengine wakiogopa hali au kitu fulani.
Mnamo mwaka 1904, Mwanasayansi wa Urusi, Bwana Ivan Pavlog alishinda tuzo ya Nobel baada ya kuja na utafiti uliojulikana kama “classical conditioning”
Katika utafiti huu maarufu kama Pavlog’s dogs, mbwa walikuwa wakiitiwa chakula kwa kugonga kengele. Baada ya muda kadhaa aligundua kwamba kila kengele ilipokuwa ikilia, hata kama sio muda wa chakula, mbwa walijua ni muda wa chakula na walikuwa wakitokwa na mate mdomoni.
Hali hii inamaanaisha walijifunza kuhusianisha kengele na Chakula na hivyo kutokwa na mate.
Miaka kadhaa badaye, utafiti huu ulitumiwa na wanasaikolojia mbalimbali kuelezea jinsi Phobia inavoweza kutokea kutokana na kukutana na jambo au kusikia jambo (classical conditioning).
Mfano, mtoto mdogo anaweza kuangalia TV akaona mtu anadondoka kutoka ghorofani na kufa hapo hapo, hivyo hali hiyo ikamfanya ahusishe urefu wa juu na kifo.
Hali hiyo huweza kumjengea hofu kubwa sana na baadaye huwa Phobia ya kupanda kwenye majengo marefu au kukwepa kuangalia TV kabisa.
Pia mtu aliyeumwa na nyoka au mdudu wakati wa utoto – au kuona mtu anakufa kwa kuumwa na nyoka – anaweza kupata hofu hiyo kubwa.
Kwahiyo kama una hofu kubwa na jambo fulani, inawezekana ilitokana na mazingira kama hayo wakati wa utoto wako.
Uzoefu wangu na nadharia hii…
Siku moja wakati nikiwa mdogo nilikuwa navua shati la shule chumbani likang’anga’nia shingoni.
Nilipiga kelele bila msaada, nikawa kama nashindwa kupumua ila baadaye kwa mbinde sana kishikizo kikaachia nikaweza kutoka. Baada ya hapo niliingiwa na hofu sana ya kuvaa nguo iliyobana ambayo najua itakuwa ngumu kuivua.
Hadi leo nikiwa nachagua nguo ya theatre huwa nachagua shati bwanga kwa hofu ya kwamba inayobana inaweza ikanikaba nikakosa pumzi, nikafa. Hofu ambayo nadhani nilipata kipindi nikiwa mdogo.
Huu ndio Mfano mzuri wa phobia zinavojengeka kwa watu Wengi. Ukiskia mtu anakwambia hapendi mashati au tisheti za kubana, anapenda kuvaa tisheti na mashati makubwa, basi inawezekana ana hii phobia.
Utajuaje kama una Phobia?
Sio kila hofu ni Phobia. Mfano, unaweza kuwa na uoga kwa mwanamke fulani lakini sio wanawake wote. Sasa Phobia ni pale ambapo wewe unawaogopa wanawake wote (Gynophobia).
Hizi ni baadhi ya dalili zinazoonyesha kwamba Hofu uliyonayo ni Phobia:
- Unafanya kila uwezavyo kukwepa kitu au hali fulani na unaweza kubuni njia za kuepuka jambo fulani. Mfano kuamua kutumia ngazi za kawaida wakati Kuna lift.
- Kupata Hofu ya ghafla unapoona kitu au unapokuwa katika hali fulani. Kupanic na kukosa Amani kabisa.
- Kushindwa kufanya shughuli zako za kawaida kwasababu tu una Hofu na jambo, Mtu au hali fulani. Mfano, Kupigwa na ganzi unapokutana na wanawake au kuingia chumba chenye wadudu na kushindwa kabisa kufanya kilichokupeleka.
- Kuwa na Hofu inayoongezeka kadiri kitu unachokiogopa kinapokaribia.
- Huwa Unajua Hofu yako haina msingi au uhalisia wowote Lakini huwezi kuishinda.
- Kushindwa kuelezea ni nini hasa unakiogopa na mara nyingine unajishangaa unaogopa nini hasa. Mfano, unaweza kuhisi kama sehemu fulani hamna hewa wakati wengine wanaona kawaida tu.
Kama una hofu ya namna hiyo juu ya jambo au hali fulani basi inawezekana una Phobia. Hofu ya kawaida sifa yake ni kwamba unaweza kuogopa jambo kwa mwanzoni lakini ukigundua sio hatarishi basi inaondoka.
Unawezaje kutibu Phobia?
Sio kila phobia inapaswa kutibiwa kwani baadhi ya phobia ni za kawaida kiasi cha kutoleta hatari katika maisha ya kawaida; na zingine ni rahisi kuzikwepa.
Tatizo linakuja pale phobia inapohusisha mazingira au hali ambayo huwezi kukwepa. Mfano, hofu ya mikusanyiko na majengo.
Hapo lazima utafute namna ya kuitibu la sivyo inaweza kuingilia ubora wa maisha ya kawaida, kazi, kipaji na afya yako kwa ujumla.
Mfano, mtu mwenye sauti nzuri ya kuimba lakini ana hofu ya umati anaweza kuzeeka au kufa na kipaji chake bila kuleta tija yoyote katika jamii.
Hizi ndizo njia za kutibu Phobia yako:
1. Njia ya kujiweka Katika mazingira ya Phobia yako (Exposure Therapy)
Mfano, unaweza kuwa muoga wa lift za maghorofa, lakini ukipata kazi katika hotel ambayo lazima utumie lift, utajikuta unazoea taratibu na baada ya muda utaweza kupanda na kushuka bila hofu tena.
Njia hii husaidia ubongo kupata tafsiri mpya ya jambo ulilofikiria kwamba ni hatari na hivyo hofu hupungua kwa kuona hamna kilichotokea baada ya kuwa katika hali ile.
Mwaka 2015, katika jimbo la Arizona Marekani, utafiti mdogo ulifanywa kwa watu wenye hofu ya kupanda ndege.
Baada ya watu hawa kuelezewa kuhusu hofu zao na kuonyeshwa kwamba hofu yao ya ndege kuanguka ikiwa angani ni kwa asilimia chache na kuambiwa pia kwamba ndege ni moja kati ya usafiri salama katika vyombo vya usafiri.
Asilimia 84 ya watu hao walikubali kupanda ndege na miaka mitatu baadaye walipofatiliwa na watafiti, asilimia 60 ya watu hao walisema bado wanatumia ndege kama usafiri wao wa mara kwa mara.
Wanasaikolojia wamekuwa wakitumia njia hii ya Psychotherapy with exposure kuwasaidia watu kutibu phobia zao na imeleta mafanikio makubwa sana.
Unataka kutibu Phobia yako? Onana na wanasaikolojia wakupe tiba hii au anza mwenyewe kufanya majaribio ya kujiweka katika mazingira hayo mara kwa mara.
Kumbuka Hofu hii huwa haina uhalisia bali inakuwa kwenye ubongo wako wa ndani (subconscious mind) na ukijiweka katika mazingira ya hatari mara kwa mara inaweza kuisha kwani ubongo utagundua kwamba hamna hatari yoyote baada ya kuwa katika hali hii.
2. Njia ya dawa
Njia hii husaidia kwa kipindi kifupi tu pale unapokuwa katika hali ya wasiwasi lakini baada ya hapo Phobia yako huendelea.
SIO njia inayoshauriwa sana maana haileti msaada wa muda mrefu. Ni kama mtu mwenye malaria kumeza panado kushusha homa bila kutibu malaria.
Dawa zinazopunguza hofu au wasiwasi mfano Propranolol, Amitryptiline, fluexetin huweza kutumika hasa kwa watu ambao wana muambatano wa matatizo ya akili au msongo wa mawazo.
Kama ni kwa muda mfupi, mfano kupanda kwenye Ndege au kutoa speech, dawa hizi zinaweza kusaidia kukupa confidence.
Angalizo: Pata ushauri wa daktari kwanza kabla ya kutumia hizi dawa hasa kwa watu wenye shida za pumu, presha ya kushuka, na moyo.
Mwisho
Phobia zipo nyingi sana, baadhi zinaweza kuhatarisha maisha yako au afya yako. Ni vizuri kutambua Phobia yako na kuitafutia matibabu kama nilivyosema hapo juu.
Kuna watu wameshindwa kuoa au kuolewa kwa sababu ya Phobia ya wanawake au wanaume.
Kuna watu wamejirusha kutoka ghorofani na kuvunjika au kufa kwa sababu ya hofu ya Mende.
Kuna watu wamefeli mtihani kwa sababu ya phobia.
Wengine wameharibu au kukosa kazi kwa sababu ya uoga uliopitiliza wa watu au mikusanyiko.
Unashangaa ukiwa nyumbani vitu viko kichwani, ila ukifika mbele ya interview panel material yote yanayeyuka (Panic attack). Utaishia kusema umerogwa kumbe ni Phobia.
Kumbuka: Kitakachofanya Phobia yako iwe kubwa ni kuikubali. Ikatae na tafuta namna ya kuitibu. Habari njema ni kwamba inawezekana ukiamua.
Kama unataka niwe daktari wako katika ushauri wa afya yako binafsi au familia yako, ingia hapa.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.