Jinsi ya kuishi muda mrefu na ugonjwa sugu

Mnamo July 21, 2022 mtandao wa Centre for Disease Control and Prevention (CDC) nchini Marekani ulitolea ufafanuzi kuhusu maana halisi ya magonjwa sugu.

 

Ulielezea kwamba, magonjwa sugu ni magonjwa ambayo hukaa mwaka au zaidi na huitaji matibabu endelevu.

 

Pia huweza kuathiri utendaji wa kawaida wa mtu au vyote kwa pamoja.

 

Mfano wa magonjwa sugu ambayo yanajitokeza kwa wingi ni magonjwa ya moyo, kisukari, kansa, shinikizo la damu (high blood pressure), kuvimba kwa joints (arthritis), kiharusi, kifafa, mtindio wa ubongo, sonona, magonjwa ya akili na kadhalika.

 

Magonjwa sugu hutoka wapi?

Mara nyingi magonjwa sugu hutokana na sababu mbalimbali kama kuambukizwa au kutokana na mfumo wa maisha, au hata vinasaba vya kifamilia.

 

 

Tabia za kimaisha hujumuisha uvutaji wa sigara, lishe mbovu, ukosefu wa mazoezi, matumizi ya vilevi, maambukizi ya magonjwa na mengineyo.

 

Nawezaje kuishi maisha ya kawaida nikiwa na ugonjwa sugu?

Baadhi ya magonjwa sugu huja tu bila sababu au kujua yametoka wapi hivyo kuishi na ugonjwa wa aina hii ni jambo gumu sana katika maisha na linahitaji kuhusisha mambo kadhaa ili ufanikiwe.

 

Ndio maana watu wengi hukata tamaa, kuwa na majuto mengi, na wakati mwingine kuanza kulaumu ndugu wa karibu pale tu wanapoambiwa ugonjwa wao utakaa muda mrefu,

 

Baadhi huenda mbali zaidi na kuanza kujichukia na kujaribu kujiua.

 

Lakini pamoja na hayo yote bado ni muhimu kuishi kwasababu bado una ndoto zako amabazo hujazitimiza, una watoto wako ambao unahitaji wakue ukiwa bado uko hai, bado una ahadi zako ulizoweka kwa ndugu na jamaa, bado una kampuni au biashara ambayo unahitaji kuona ikikua.

Basi haya ndio mambo matatu yaliyothibitishwa kisayansi ya namna ya kuendelea kuishi maisha ya kawaida kama wengine ukiwa na ugonjwa sugu:

 

1. Kuukubali ugonjwa

Ulishawahi kusikia msemo mtaani unasema “mchawi tunamjua ila tunaishi nae tu“?

 

Huu ni msemo wa kisaikologia ukimaanisha kukubali jambo na kuendelea na maisha yako bila kuangalia nyuma.

 

Fikra ya namna hii hukuepusha na vita zisivyo na tija. Hukusaidia kutunza nguvu na akili yako kwa hatua inayofuata.

 

 

Kwa upande wa ugonjwa, maana yake ni kwamba kuukataa ugonjwa hakuondoi ugonjwa bali kunamaliza nguvu kwa kupambana na jambo ambalo limeshatokea tayari.

 

Ukiamua kuishi nao maana yake unaamua kuisamehe nafsi yako na kuamua kufungua ukurasa mpya wa namna ya kupata suluhu ya changamoto.

 

Mnamo mwezi Aprili 2023, utafiti uliofanywa na mwanasaikolojia Grzegor Wysoski et Al na wenzake wanne kuhusu watu wenye ugonjwa wa joint uitwao Ankylosing spondylosis – ugonjwa ambao ni endelevu, huaribu joint na kusababisha vilema kwa baadhi ya watu – ulichapishwa.

 

Utafiti huu ulilenga kuangalia tofauti ya wagonjwa walioukubali hali yao na ambao hawakuukubali.

 

Katika matokeo ya utafiti huu ilionekana kwamba wagonjwa ambao hawakuukubali ugonjwa waliandamwa sana na kulazwa hospitali mara kwa mara, kupata vilema ndani ya muda mfupi, kuhitaji dawa nyingi na kupata maumivu kwa muda mrefu.

 

Kundi la walioukubali ugonjwa walionekana kuwa na ubora mzuri wa kimaisha. Kwa kuendelea kuishi na ugonjwa kwa furaha, kupata maumivu machache, kulazwa mara chache, kutumia matumizi madogo ya dawa na kuishi muda mrefu bila madhara zaidi ya kiafya.

 

Tafsiri yake ni nini?

Unapokubali ugonjwa maana yake unakuwa tayari kufata masharti na kusaidiwa kwa urahisi na hivyo afya yako huwa bora.

 

Kukataa ugonjwa maana yake ni kutoa mwanya wa kuendelea kudhoofika kiafya kwa sababu ya Kukataa dawa, kutofata masharti ya ugonjwa na mwisho wake mashambulizi huwa ya mara kwa mara na baadhi ya viungo muhimu vya mwili kama magoti, figo, ini na moyo kuanza kuathirika kwa kuzidiwa na ugonjwa.

 

Mfano, mgonjwa wa UKMWI aliyekubali hali yake na kukubali kumeza dawa vizuri na kwenda clinic kwa wakati, mwili wake huwa na hali ya kawaida tu kama mtu mwingine na huweza kuishi maisha yake kwa miaka mingi kama watu wengine.

 

Lakini kwa wagonjwa wa UKIMWI Walioshindwa kuukubali ugonjwa wao na kuamua kuishi bila dawa, huugua mara kwa mara na wengi wao huwa hawaishi zaidi ya miaka mitano!

 

Umekutwa na ugonjwa utakaokuwa sugu? Ishi nao tu mkuu, ukubali kwanza halafu tafuta namna ya kukabiliana nao. Hali yako ya afya itakuwa bora kama huumwi vile.

 

“Be water my friend ” – Bruce Lee.

 

2. Uelewe ugonjwa wako kwa undani

“Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa” – Hosea 4:6

 

Katika uzoefu wangu wa miaka 6 kama daktari, nimekuwa nikijaribu kuwachallenge wagonjwa wangu hasa wenye magonjwa sugu kama presha, sukari, UKIMWI, cancer, na arthritis.

Katika kufanya hivi niligundua wagonjwa wawili tu kati ya 10 niliowauliza walionekana kuwa na uelewa wa ugonjwa wanaoumwa wakati 8 huwa hawana taarifa ya kutosha ya ugonjwa wao na wala hawajui vitu gani hufanya ugonjwa wao kutokea.

Mfano, magonjwa ya sukari na presha ni magonjwa ambayo yanategemea zaidi mtindo wa maisha hasa aina ya vyakula lakini asilimia kubwa ya wagonjwa hawa huwa wana elimu ndogo juu ya lishe na mambo wanayopaswa kufanya kusaidia miili yao.

 

Matokeo yake yamekuwa magonjwa magumu kutibika na kupelekea madhara mengi katika afya za wagonjwa.

 

Kuwa na elimu nzuri ya ugonjwa wako ni kama nusu ya kuukabili ugonjwa huo. Kutibia ugonjwa bila kuwa na elimu nao ni sawa na kukata nyama na kisu butu, utatumia nguvu kubwa sana na mwisho wake utachoka.

 

 

Jifunze ugonjwa wako umesababishwa na nini. Fahamu mambo gani ya kuepuka au kufanya ili ugonjwa utulie.

 

Fahamu ni dawa gani nzuri ya ugonjwa wako. Fahamu unapaswa kumeza dawa kiasi gani. Fahamu unapaswa kuudhuria clinic mara ngapi kwa mwaka.

 

Mfano, unajua kwamba chumvi mbichi ni adui wa presha yako? Unajua kwamba mazoezi ya dakika 30 tu kila siku yanaweza kushusha presha yako?

 

Unajua kwamba uzito wako mkubwa ndio chanzo cha sukari yako kuwa juu? Unajua kwamba kuvuta sigara kunafanya madhara ya kisukari kuwa mara 4 zaidi ya kawaida?

Utafiti unaonyesha kati ya wagonjwa 10, watano huwa hawataki kabisa kujua au kusikia kuhusu ugonjwa walioambiwa hospitali kwa dhana kwamba huwaongezea msongo wa mawazo! Na hawa ndio huongoza kwa kutokubali ugonjwa na hivyo hali zao huishia pabaya.

Kati ya watano waliobaki, watatu hukubali ila huwa hawajishughulishi zaidi ya kumeza dawa tu na kuendelea na maisha yao kama kawaida. Hawafanyi juhudi kufahamu zaidi ugonjwa wao.

 

Wawili waliobaki ndio huwa na nidhamu na ugonjwa wao na kujaribu kwenda kwa wataalamu au kujisomea na hivyo huweza kuishi na ugonjwa kama hawaumwi vile maana hatua stahiki zote wanazijua kuanzia muda mzuri wa kumeza dawa hadi vyakula gani wale au wasile – na wale lakini kiasi gani.

 

Marehemu Lowasa alipokuwa akigombea kiti cha urais mwaka 2015 alipoulizwa vipaumbele vyake vitatu vitakua nini, alisema:

 

“Cha kwanza Elimu; cha pili Elimu; cha tatu Elimu”

 

Tumia vizuri smartphone yako kujielimisha. Inashangaza sana mtu ana smartphone halafu hajui hata kwa ugonjwa wake anapaswa kula vyakula gani! Unajiuliza huyu smartphone kanunua ya nini?

 

“Kama ningepewa masaa sita ya kukata mti, ningetumia masaa matano ya kwanza kunoa shoka” – Abraham Lincoln

 

4. Fuatilia ugonjwa wako

Umeenda hospitali umeambiwa presha yako iko juu, ukaanzishiwa dawa, ukaambiwa urudi baada ya wiki mbili kupima tena presha ili kuona imeshuka kiasi gani; ukarudi, daktari akaangalia na kukupa ushauri zaidi.

 

Akakwambia kila baada ya miezi mitatu urudi kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa presha yako na ukafanya hivyo.

 

Presha yako ikakaa vizuri na ukaendelea na maisha yako kama kawaida.

 

Hadithi yangu imeisha hapo. Asante!

 

Hiyo ndio namna ya kufuatilia ugonjwa wako na ndio njia sahihi ya kufuatilia afya yako hasa ukiwa na ugonjwa Sugu. Je huwa unafanya hivyo?

 

Mara ya mwisho kurudi hospitali baada ya kuambiwa una tatizo la moyo ilikua lini? Sana sana unaenda tu pharmacy kununua dawa na kumeza na kuona kama kila kitu kiko sawa tu sio?

 

Faida ya kumuona tena daktari walau kila baada ya miezi mitatu ni kwamba, baada ya muda madaktari huwa wanabadili dozi ya dawa waliyokupa.

 

Mfano kushusha dozi kulingana na nafuu unayoipata baada ya muda fulani. Usipo rudi maana yake kuna hatari ya kuendelea kumeza dozi kubwa na kuathiri maini na figo zako.

 

Pia daktari huwa anapaswa kurudia baadhi ya vipimo kama x-ray na figo ili kujua maendeleo yako baada ya kuanza matibabu. Lakini kwakuwa hupendi kufuatilia mwenendo wa ugonjwa wako basi hayo yote hupati, matokeo yake baada ya muda fulani unarudi hospitali ukiwa na hali mbaya zaidi.

 

Kufanya follow up ya ugonjwa wako ni moja ya nidhamu muhimu katika kuhakikisha ugonjwa sugu ulionao unabaki katika kiwango cha chini. Usisubiri mpaka uzidiwe tena.

 

Mfano ugonjwa wa akili na kifafa ni moja ya magonjwa ambayo yanadai sana ufatiliaji. Kila unapopata shambulio (attack) la ugonjwa wa akili au kifafa hupelekea kuharibika kwa sehemu ya seli za ubongo ambazo hazirudi tena.

 

Kwa magonjwa haya, mgonjwa anapaswa kuhudhuria hospitali mara kwa mara kwa ajili ya ufatiliaji na madaktari kugundua mapema dalili za hatari.

 

Mwisho

Katika kuumwa, ishu sio kuwa na ugonjwa, ishu ni unaishi kwa muda gani baada ya kuanza kuumwa?

 

Hivi unafahamu kuna watu wanaishi na ugonjwa wa kifafa na akili lakini wala hawajawahi kuanguka au kukimbia huku na huku?

 

Unajua kuna watu wana tatizo la sukari au presha kama wewe ila hawalazwi hospitali mara kwa mara kama wewe?

 

Unajua kuna watu waliopata ugonjwa wa UKIMWI miaka 20 kabla yako na bado hawana hata dalili ya kufa? Ila wewe umeugua miezi miwili tu afya yako imedorora!

 

Kuna mambo matatu ambayo wao wanafanya, ambayo wewe hufanyi na ukifanya utakuwa kama wao.

 

Kwanza waliamua kuukubali ugonjwa wao na kuuchukilia kawaida. Pili, waliamua kujielimisha na kujua kiundani kuhusu ugonjwa wao na matakwa yake. Tatu, waliamua kuwa wafatiliaji wazuri wa ugonjwa wao na kuhudhuria hospitali mapema kabla hawajapata dalili.

 

Hizi ndio nidhamu tatu kubwa za kuishi na ugonjwa sugu.

 

Endelea kusoma makala zetu kwa ajili ya kupata elimu ya afya thabiti. Unaweza kubook consultation hapa na nikawa daktari wako binafsi au wa familia.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW