Tambua jinsi ya kujiandaa na kuufurahia uzee wako kila sekunde

Uzee ni lazima uje, hauwezi kuwa kijana maisha yako yote. Kuna muda utafika, utazeeka tu!

 

Lakini swala la muhimu sio kuzeeka, ni utazeeka vipi? Uzee wako utakuwa wa aina gani? Huzuni, maumivu au furaha?

 

Makala hii inalenga kukuonesha namna ya kuufanya uzee wako kuwa wa furaha pamoja na changamoto zinazojitokeza ukizeeka.

 

Mtu unapozeeka nini hutokea?

Uzee kwa tafsiri ya kijamii huanzia miaka 60 kwenda juu. Hapa kama ni muajiriwa wa serikali huwa ndio muda wa kustaafu na kuanza kukaa nyumbani.

 

Ndio muda ambao watoto wameshakuwa na wameanza kujitegemea, hivyo unaweza kubaki na mwenza wako nyumbani, wajukuu au mtoto wa mwisho, kama umebahatika.

 

 

Uzee unapoingia, mwili wako huanza kuchoka na maradhi huanza kuingia. Magonjwa kama tezi dume, kansa, shinikizo la damu, sukari, kuvimba kwa joints (Arthritis), Gout, magonjwa ya kusahau na kadhalika.

 

Lakini pia mambo kama upweke huingia, hasa kama umezoea kukutana na rafiki zako kazini au kukukumbuka ratiba ya kazi.

 

Mambo yote hayo hufanya uzee kuwa na changamoto mbalimbali kama kuhitaji faraja, furaha, matibabu, msaada wa watu wa karibu wa kifedha, na mengineyo.

 

Nimewaona wazee waliozeeka vizuri, nimewaona pia wazee waliozeeka vibaya katika miaka yao ya mwisho.

 

Kwa uchunguzi wangu mdogo, niegundua tofauti ya makundi haya mawili ipo kwenye malengo. Kuzeeka vizuri inapaswa iwe target yako kama mzee, maana maisha ndiyo haya haya, hamna mtu anayehitaji kuteseka hapa duniani hasa muda wa uzeeni.

 

Mambo yanayoweza kupelekea kuzeeka vibaya kwa mzee ni kama:

  • Matatizo ya afya
  • Hali mbaya kiuchumi
  • Ukosefu wa furaha
  • Upweke
  • Ugomvi na watoto
  • Kukosa maandalizi ya mapema ukiwa kijana.

 

Unawezaje kuzeeka vizuri?

Kuzeeka vizuri maana yake ni kuishi bila majuto katika uzee wako, ukiwa na afya nzuri kiujumla.

 

Sio kila mzee hupata bahati hii kutokana na sababu mbalimbali lakini hasa ikiwa ni kushindwa kujua namna ya kutafuta hii furaha.

 

Matatizo katika maisha huwa hayakosi, hilo halina ubishi, lakini swali kubwa la kujiuliza ni kwamba “Nawezaje kuishi katikati ya matatizo ya uzee na bado nikawa na maisha yenye furaha?”

 

Katika tafiti mbalimbali zilizofanywa kuhusu maisha ya uzeeni, mambo mbalimbali yalionekana kupaswa kuwepo ili kumsaidia mzee kuishi vizuri kwa furaha.

 

Mambo haya mzee unaweza kujifanyia au kufanyiwa na watu wako wa karibu:

1. Kuimarisha afya yako

Maisha ya wazee yanaandamwa na maradhi mengi kama tulivoyataja kule juu, lakini tatizo kubwa huwa sio haya magonjwa, bali ni kukosa uangalizi wa karibu.

 

Kukosa matibabu ya msingi hufanya afya za wazee kuharibika na maisha yao kuwa magumu. Baadhi ya changamoto zinazowakumba wazee wengi ni matatizo ya joint (Arthritis), tezi dume kwa wanaume, kansa ya  kizazi, macho kutoona vizuri (cataracts) n.k.

 

Haya matatizo yanatokea kwa sababu ya uzee lakini hayapaswi kuwa chanzo cha kukosa furaha na kuzeeka vibaya. Kinachohitajika hapa ni huduma ya afya ya karibu.

 

Moja ya changamoto ya wazee wengi huwa ni kutopenda na kukataa kwenda hospitali, na kwa sababu hiyo huamua kuficha maradhi yao na kuendelea kuteseka nyumbani.

 

Hivyo kuweza kuzeeka vizuri ni lazima kuwa na huduma ya afya nyumbani. Walau daktari kuweza kumtembelea mzee nyumbani na kumuona bila ya yeye kutakiwa kwenda kupanga mstari hospitali.

 

Huduma ya namna hii itampa nafasi ya kuwa na furaha kwa kutibiwa nyumbani huku akiwa karibu na wajukuu zake.

 

Hali hii pia huimarisha afya zao kwakuwa ni rahisi kwa daktari kuja mara kwa mara na kufuatilia maradhi yao kwa ukaribu ikiwa ni pamoja na kusaidia matumizi ya vifaa mbalimbali vya kutembelea na kupunguza maumivu.

 

Ni jukumu la wajukuu na watoto kuhakikisha mzee wao anapata huduma nzuri za afya ili kurefusha maisha yake na kumpa furaha zaidi.

 

Hapa sio swala la kuwa na pesa kwasababu gharama za kuonwa nyumbani sio kubwa sana ukizingatia faida atakazopata mzee akitibiwa nyumbani.

 

Nikuibie siri?

Ukitaka mzee wako aishi muda mrefu, wekeza kwenye afya yake. Hakikisha anakula chakula bora, analala mahala salama, anavaa nguo safi na anapata matibabu nyumbani.

 

Siku hizi ni rahisi kupata watu wa afya wa kumfata mzee wako nyumbani. Namna ya kulifanikisha hii ni kukutana kama ndugu na kujichanga walau kila mwezi.

Kama mnaweza kuchangisha pesa ya msiba na mazishi, mnashindwaje kumpatia mzee wenu pesa ya bima kila mwaka?

 

2. Kuhudhuria sehemu zenye ukumbusho wa enzi zake

Hakuna kitu kinachompa Mama yangu furaha kama nikimpeleka kwenye live band ambayo wanapiga nyimbo za zamani za enzi zake. Basi utaona jinsi anavyofurahi na kujihisi mpya kama karudi zama zake za ujana.

 

Mazingira kama haya huwapa wazee wetu furaha na kuridhika hata kama wana maumivu ya mwili. Hali hii wanaweza kuipata katika maeneo mbalimbali yenye burudani zinazomkumbusha enzi zake mfano, kanisani, matamasha, shule zao za zamani walizosoma au makumbuso ya kisiasa.

 

Hali hii huwafanya wazee kujiona wapya, kuwa na furaha, na kutaka kuishi zaidi ili waone zaidi.

 

3. Kuwa na “kampani”

Kampani inaweza kuwa ya kikundi, kwaya, wajukuu au watu ambao huwafanya kutabasanu.

 

Katika utafiti uliofanyika mwaka 2018 nchini Marekani ulionyesha wazee wengi wenye kampani (Wanaoishi na wajukuu au walioendelea kujihusisha na mambo ya kijamii kama vikundi vya siasa, dini, kwaya na jamii) walikuwa wanaishi kwa furaha na muda marefu kwa sababu kampani inawapa sababu ya kuendelea kuishi.

 

Rafiki yangu David ana mama yake mwenye miaka 72 ambaye husumbuliwa sana na tatizo la magoti (arthritis), lakini mara nyingi huyu mama ana furaha na sababu kubwa ni kwamba mama huyu aliamua kujiweka katika mahusiano ya kanisa, pamoja na kujitolea kuwafundisha watoto wadogo kwaya.

 

Hivyo muda wake mwingi huutumia kanisani na kampani anayoipata huko humpa furaha na afya njema; pamoja na maumivu makali ya magoti lakini sijawahi kuona kama anawaza kufa leo wala kesho.

 

Hakuna kitu kinachowaua wastaafu haraka kama kujitenga na kuwa wapweke nyumbani.

Jitahidi mzee wako apate kampani walau ya kikundi au wajukuu wa kufanya awe mchangamfu na kukimbia huku na huku.

 

Mfano, mama anayelea mjukuu anaweza kuishi kwa furaha zaidi kwa sababu anahisi ni mama na ana majukumu ya kumkuza mjukuu wake.

 

4. Matembezi ya jioni

Hii ni muhimu sana kwa wazee, huwasaidia kufanya mazoezi kila siku, kupata hewa safi na kuwapa wasaa vijana zao kuona uasili wa dunia.

 

Hali hii huwafanya kujisikia wapya na kuwakumbusha baadhi ya mambo ambayo wanapaswa kuyafanya kabla hawajafa.

 

Huwapa sababu ya kutaka kuishi zaidi na kuwaongezea furaha kwa kuwafanya watambue kwamba bado wanahitaji kuishi.

 

Matembezi yahusishe sehemu za wazi ambazo hazina usumbufu wa magari na pikipiki, sehemu ambayo ina hewa ya kutosha na ana uwezo wa kuona uso wa dunia.

 

Ukiachana na kutembea ambako humfanya mzee kushughulisha viungo vyake, utafiti unaonyesha hata kusimama tu sehemu yenye uwazi na kupata upepo na kuangalia uso wa dunia ni dawa tosha.

 

 

Hivyo hata kama mzee wako hawezi kutembea bado unaweza kumsukuma kwenye wheelchair yake na kupata hewa safi.

 

Evening walk ina mchango chanya kwenye kushughulisha viungo (huimarisha mifupa na joints) na kupata muda wa kutafakari maisha na kuota ndoto mpya.

 

Kitaalamu inashauriwa mzee kuanzia miaka 60 atembee dakika walau kuanzia 150, sawa na nusu saa kila siku. Na walau siku mbili za mazoezi magumu kidogo kama kukimbia (jogging), push ups au kuruka kamba.

 

Mambo haya mawili ni muhimu kwa ajili ya furaha ya mtu yeyote. Mzee usikubali kukaa tu, tembea upate furaha.

 

5. Kufanya “meditation”

Meditation ni moja ya tabia zinazoleta kujiskia vizuri na furaha. Hali ya kupata muda wa peke yako wa walau dakika 10, 20 au 30 na kupata utulivu kiasi cha kusikia upumuaji wako, na kujaribu kuondoa mawazo yote yanayokujia kichwani ni jambo zuri sana kiafya.

 

Kutokana na utafiti wa wanasayansi, kitendo hiki huweza kufanya mudi yako kuwa nzuri, kuongeza uwezo wa kumbukumbu na kuondoa mawazo yanayoweza kuleta msongo wa mawazo.

 

Utafiti uliochapishwa katika mtandao wa JAMA Internal Medicine mwaka 2014 ulibainisha faida mbalimbali katika ubongo wa watu, hasa wazee wanaofanya meditation, kama ifuatavyo:

  • Kupunguza msongo wa mawazo (sonona) kwa kiasi sawa na kumeza dawa za sonona (depression)
  • Kupunguza hofu
  • Kuongeza uwezo wa kumbukumbu na furaha
  • Kushusha shinikizo la damu, na
  • Kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa wa alzehmer disease.

 

Hivyo mzee kufanya meditation ni dhahiri itamsaidia kuwa na furaha zaidi. Bahati mbaya uelewa wa jambo hili ni mdogo na wengi wao huishia kuishi tu kwa kusubiria kesho.

 

Haya mambo sio ya wazungu tu, wazee wa zamani walikuwa wanatumia njia hii kuupa mwili nguvu na kuboresha kumbukumbu zao.

 

 

Jishughulishe…

Baada ya kufika miaka 60, kitakachomfanya mzee kuishi kwa furaha ni shughuli mbalimbali anazoshughulika nazo. Kukaa tu kila siku huleta huzuni kwa wazee.

 

Shughuli hizi zinaweza kuwa bustani ya mboga, kusimamia ujenzi, kukamua maziwa ya ngombe au hata kupalilia shambani.

 

Mara nyingi wazee wakifika miaka 60 na kuendelea hujikuta wana muda mwingi sana na muda unakuwa kama hauendi. Hali hii inaweza kuwafanya kuchanganyikiwa na kupoteza furaha hivyo kujishughulisha na kazi ni muhimu.

 

Chapisho moja lililotolewa na Australian Department of Health and Aged Care (May 6, 2021) lilionyesha wazee kwanzia miaka 65 hupaswa kupata walau dakika 30 kila siku ya kufanya kazi ngumu kwa wastani

 

Mfano kupalilia au kufagia uwanja, kudeki nyumba, kutembea kwenda sokoni kama sio mbali sana, kusafisha nyumba, kuosha vyombo, kulima shamba, kupanda na kushuka ngazi, na kadhalia.

 

Ukimuoma mzee wako anajishughulisha, usimkataze muache ajishughulishe. Inamuongezea furaha hiyo.

 

Mwisho

Sio lazima uteseke ukiwa mzee, bado unaweza kufurahia maisha ya uzee na ukaishi zaidi. Hela ni muhimu Uzeeni Lakini epuka kuhusianisha pesa na furaha yako, jipe furaha mwenyewe kwa kufanya mambo hayo hapo juu.

 

Kijana unayesoma makala hii hakikisha wazee wako wana furaha kwa kuhimiza mambo kadhaa niliyoyasema hapa.

 

Makala hii naituma kwa wazee wangu: Mzee Bitegera, Bi Joan Maria (Mama Muta), Mzee Henerico, na shangazi zangu wote. Hakikisha mnafuata hizo kanuni kupata furaha na kuzeeka vizuri.

1 thought on “Tambua jinsi ya kujiandaa na kuufurahia uzee wako kila sekunde”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW