Fahamu usichokijua kuhusu “Kichaa cha Mbwa”

Ulishawahi kuona mtu mwenye dalili za kichaa cha mbwa? Kama bado, usiombe kuona, itakuathiri kisaikolojia.

 

Wengi wetu dalili ambayo huwa tunaijua ya kichaa cha mbwa ni ile hali ya kubweka kama mbwa lakini hatujui kwamba hiyo ni dalili ya baadaye kabisa.

 

Kichaa cha Mbwa (Rabies) ni ugonjwa ambao huwa hauzungumziwi sana lakini naweza kusema ni jinamizi lililonyamaza.

 

Sifa yake kuu ni hii:

Ukishapata dalili za kichaa cha mbwa ndio basi tena, hakuna dawa! Ni ugonjwa unaoua kwa asilimia 100, lakini cha ajabu ni ugonjwa unaoweza kuzuiliwa (prevention) kwa asilimia 100 pia.

Hadi sasa ni watu 20 tu, dunia nzima, walioripotiwa kupona baada ya kuambukizwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa, na mmoja wapo ni mwanadada anayeitwa Jeanna Giesse (35).

 

 

Aliripotiwa katika jarida maarufu nchini Marekani la Scientific American (SciAm) mwaka 2008, ambalo lilimuhoji. Japo baada ya kupona alibaki na changamoto kadhaa za viungo na upumuaji, na baadaye aliamua kuwa daktari wa wanyama.

 

Yeye alipata ugonjwa huo baada ya kuumwa na popo aliyemuokota chini akiwa ameanguka.

 

Sasa mambo gani unapaswa kuyajua kuhusu Kichaa cha Mbwa?

1. Huambukizwa kwa kuumwa na mnyama mwenye ugonjwa huo ambapo virusi vya ugonjwa huo hutoka kwenye mate yake na kuingia katika mwili wako kupitia ngozi yako iliyoumwa.

 

Sio kwa kumgusa/kumshika mnyama au kutemewa mate na mnyama.

 

Pia huambukizwi kwa kula nyama ya mnyama mwenye ugonjwa huo. Japokuwa muandaaji wa nyama hiyo (namaanisha mchinjaji au/na mkataji) akipata kidonda kwa kuchomwa na mfupa wa nyama ya mnyama mwenye kichaa cha mbwa, basi atakua kwenye hatari ya kupata maambukizi.

 

2. SIO lazima iwe kidonda kikubwa kupata maambukizi.

Maana yake ni kwamba hata mkwaruzo mdogo, ilimradi umechubua ngozi yako, unaweza kukupelekea kupata kichaa cha mbwa.

 

Hivyo usichukulie poa mkwaruzo ilimradi mnyama aliyekuuma au kumuuma mwanao ana dalili ambazo hazieleweki.

 

Japo kadiri kidonda kinapokuwa kikubwa mpaka kufikia kuvuja damu ndivyo hatari huongezeka.

 

3. SIO mbwa pekee husababisha maambukizi ya kichaa cha Mbwa, bali wanyama wote wenye damu ya moto.

 

Mbwa ndio mnyama anayeongoza katika kusababisha kichaa cha mbwa lakini kuna kesi nyingi sana zimeripotiwa kutoka kwa wanyama wengine kama Nyani, Mbwa mwitu, Swala, Popo, Fisi, na hata ng’ombe.

 

Wanyama jamii ya Panya wana nafasi ndogo sana lakini usidharau kama damu imetoka, maana kwa kawaida panya huwa wanakula ngozi ya juu lakini mpaka wakuume utoke kidonda kunaweza kuwa na uwalakini.

 

Wadudu na wanyama wenye damu baridi kama nyoka, kenge, kiboko n.k. hawaambukizi Kichaa cha Mbwa. Kesi ya Jeanna Giesse iliyoriportiwa hapo juu ilisababishwa na kuumwa na Popo.

 

Kumbuka hata mtu mwenye dalili tayari za ugonjwa huu akikuuma utapata Kichaa cha Mbwa.

 

4. Mnyama mwenye Kichaa cha Mbwa hufa ndani ya siku 7 mpaka 10.

Hivyo kama uliumwa na mbwa halafu ukakuta mbwa kafa ndani ya muda mfupi au katoweka kabisa hajulikani alipo, hiyo ni hatari kubwa lazima uwahi hospitali kupatiwa chanjo.

 

Pia kama mnyama amekuuma bila sababu ya msingi, ameuma watu wengine kadhaa ndani ya muda huohuo, hajachokozwa au anatoa mate mengi, na kukimbia kimbia kijijini au mtaani bila sababu, basi ana uwezekano mkubwa wa kuwa na Kichaa cha Mbwa.

 

Pia mnyama kama swala kuja jikoni au nyumbani kwako sio kawaida lazima ushtukie. Au mtu kuumwa na ng’ombe aliyekuwa anamkamua maziwa sio kawaida kwasababu Ng’ombe akihudhika hutumia mapembe na miguu sio meno, shtuka!

 

5. Kichaa cha Mbwa kinaweza kukupata siku chache, miezi, au miaka kadhaa baada ya kuumwa na Mbwa.

 

Hivyo hauko salama mpaka umepata matibabu ya mwanzo ikiwemo kumaliza chanjo. Kuna kesi nyingi ambazo watu wamekuja hospitali na dalili za Kichaa cha Mbwa baada ya kuumwa na mnyama miaka 2 iliyopita.

 

Usichukulie poa, kumbuka nafasi ya kupona baada ya dalili kuanza ni sifuri.

 

Nifanyeje nikiumwa na mnyama?

1. Kwanza usichukulie poa kuumwa na mnyama hasa niliowataja hapo juu, au hata mkwaruzo ambao haueleweki na mnyama haeleweki. Fika hospitali kwa ajili ya watu wa afya kufanya ufatiliaji wa mnyama.

 

Pia fuatilia huyo mnyama, mf. Mbwa, amechanjwa lini.

 

Record zake zipo? Anapata chanjo kila mwaka kama inavyotakiwa? Mbwa ana dalili ambazo hazieleweki kama kubweka hovyo, hasira kali, kutoa mate mengi n.k.? Amewauma watu wengine?

 

2. Safisha eneo uliloumwa au mwanao/jamaa aliloumwa kwa kutumia maji mengi na sabuni walau dakika 15 kabla ya kumpeleka au kwenda hospitali.

 

Hii imeonyesha kuwa na msaada mkubwa sana kwa kuosha yale mate yenye vimelea vya virusi wa kichaa cha mbwa.

 

Usikimbilie hospitali hapo hapo isipokuwa kama mgonjwa anavuja damu sana.

 

3. Nenda hospitali kupata chanjo mapema iwezekanavyo, hii ni muhimu sana. Chanjo huwa ni nne katika vipindi tofauti lakini siku ya kwanza na ya tatu ni muhimu.

 

Usijaribu kuishia njiani, hakikisha unamaliza chanjo zako. Kumbuka ukipata dalili tu za ugonjwa huu, safari yako imeisha! Hakuna dawa, kuna chanjo pekee, ya kuzuia.

 

Pia huwa kuna matibabu mengine muhimu kama sindano ya tetenus na antibiotic pamoja na kusafisha kidonda, lazima ufike kituo cha afya kwa hivi.

 

Zaidi usihofie kwamba siku kadhaa zimepita haujaenda kuchoma chanjo, maadamu umegutuka we nenda tu watakupa chanjo muda wowote, ila jua kuchelewa kunaongeza hatari.

 

Kuna wagonjwa ambao wamekuja kuonesha dalili za kichaa cha Mbwa miaka kadhaa baada ya kuumwa.

 

Utajikingaje na janga hili la Kichaa cha Mbwa?

1. Elimu hii uliyopata waelimishe na ndugu zako, jamaa na familia.

Hasa watoto wana tabia ya kuficha wakiumwa na kitu kwa kuhofia kupigwa na wazazi. Wape elimu wajue hatari ya kuumwa na mnyama na kunyamaza. Kuripoti kesi ya kuumwa na mnyama yoyote. Usidharau.

 

2. Kupata chanjo mapema bila kukosa ndio njia pekee ya kuzuia maambukizi. Kumbuka usipofanya hivyo, ukipata ugonjwa ndio kwaheri.

 

3. Kama unamiliki Mbwa au ni Afisa Mifugo hakikisha Mbwa wanachanjwa kila mwaka.

Mbwa anapopatiwa chanjo huwa inachukua siku 28 mpaka kupata kinga, lakini lazima achanjwe booster kila mwaka ndipo atakuwa na kinga ya kutosha kuzuia maambukizi.

 

 Mwisho

  1. Usichukulie poa ukiumwa na mnyama, pata chanjo.
  2. Kichaa cha Mbwa hakina dawa, ukipata unakufa. Kinga ya elimu ya afya na chanjo ndio kipaumbele.
  3. Kumbuka kumaliza chanjo zote, usiishe njiani, na kikubwa hakikisha Mbwa wako wanapata chanjo kila mwaka.

 

Endelea kufurahia makala zetu za Abite Afya.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW