Kiharusi, au stroke, ni hali ya sehemu ya upande wa mwili kudhoofika (to paralyze), kwa muda au moja kwa moja, ambayo husababishwa na sehemu ya seli za ubongo kuharibika kutokana na kutopata kiasi cha damu ya kutosha au kutopata kabisa kwa zaidi ya sekunde 30 na zaidi.
Kutofika kwa damu kwenye ubongo huweza kutokana na sababu kuu mbili; Moja inaweza kuwa sababu ya mishipa mikuu ya damu inayoenda kwenye sehemu hiyo ya ubongo kupasuka, au…
Kutokea mgando wa damu kwenye mishipa ya damu mwilini na hivyo kwenda kuziba mshipa huo na kusababisha damu isifike kweye sehemu ya ubongo na hivyo kufanya sehemu hiyo kuharibika na kuathiri sehemu zote za mwili zinazotegemea eneo hilo.
Mambo yanayoweza kukuweka katika hatari ya kupata kiharusi
1. Presha ya damu iliyopitiliza
Shinikizo kubwa la damu kwa zaidi ya 160/110, kwa muda mrefu, bila matibabu hupelekea mgandamizo mkubwa kwenye mzunguko wa damu na hivyo kupelekea moyo kushindwa kusukuma damu kwenda kwenye sehemu muhimu za ubongo na hivyo kusababisha kiharusi.
Presha kubwa kwenye mishipa ya damu pia huweza kusababisha mishipa ya damu kwenye ubongo kupasuka na kupelekea kiharusi.
2. Mafuta mengi kwenye damu (High cholesterol)
Kiwango kikubwa cha Mafuta (cholesterol) kwenye mishipa ya damu ni moja ya visababishi vya kiharusi. Mafuta haya huweza kuganda na kufanya mshipa wa damu kuwa mwembamba (Atherosclerosis) na baadaye kuzuia damu kufika katika sehemu muhimu ya ubongo.
3. Matatizo ya moyo, kansa na sukari
Ugonjwa wa moyo wa muda mrefu unaweza kuwa chanzo cha kiharusi kutokana na uwezekano wa kutokea damu kuganda Katika sehemu zenye tatizo Katika moyo na kupelekea damu mgando (blood clots) kuziba mishipa ya ubongo.
Pia ugonjwa wa kisukari na kansa humuweka mtu kwenye hatari kubwa ya kupata kiharusi (stroke) kutokana na uwezekano mkubwa wa kupelekea mafuta kukusanyika kwenye mishipa ya damu.
4. Matumizi ya dawa za kulevya
Matumizi ya dawa za kulevya mfano cocaine yamekuwa moja ya chanzo cha kusababisha kiharusi kwa watumiaji walio wengi hasa hasa kwa vijana wadogo.
Katika moja ya utafiti uliofanyika katika jimbo la Washington – Baltimore nchini Marekani iligundulika katika vijana wadogo waliolazwa hospitali kwasababu ya stroke, asilimia 12 mpaka 33 walikuwa wanatumia cocaine.
Katika kipindi cha miaka 4, ndani ya jimbo hilo hilo, hospitali 46 ziliripoti kiasi cha wagonjwa wenye stroke 240 ambao pia walikuwa wakitumia dawa za kulevya kama cocaine.
5. Mambo mengine yanayoweza kuleta hatari ya kiharusi ni kama mivunjiko ya mifupa mikubwa mfano mfupa wa paja (femur).
Pia kuganda kwa damu kwenye mishipa ya mguu (DVT), kusimama ghafla hasa kwa wazee wakiwa wanaamka ghafla kwenda kukojoa usiku, n.k.
Utamtambuaje mtu mwenye kiharusi?
- Kuanguka ghafla, kutokana na upande mmoja kukosa balance. Mara nyingi stroke huathiri upande mmoja kutokana na upande wa ubongo ulioathiriwa. Hivyo kama shida imetokea upande wa kushoto wa ubongo, upande wa kulia wa mwili ndio huwa dhaifu na kupoteza nguvu, hivyo mtu akiwa amesimama au anatembea atadondoka ghafla chini.
- Kushindwa kutumia upande mmoja wa mwili, mfano mkono mmoja kushindwa kufanya chochote. Pia kushindwa kusimama au kutembea mwenyewe au kushindwa kuamka asubuhi kutoka kitandani.
- Kushindwa kutamka sentensi au kuongea kwa ufasaha hasa kwa mtu aliyekuwa anaongea vizuri kabla, ikiambatana na mdomo kupinda upande mmoja.
- Dalili zingine ni kama maumivu makali ya kichwa, kupata ugumu wa kuona, kupata ugumu wa kuelewa mazungumzo, na kadhalika.
- Stroke nyingi hutokea muda wa kuamka asubuhi – hasa kwa wazee.
Juhudi gani muhimu zifanyike kuepuka kiharusi?
1. Kama una tatizo la presha, hakikisha unafata maelekezo ya daktari ambayo yanahusisha kumeza dawa kwa wakati pamoja na kufata kanuni za mlo ambao unashusha presha.
Mfano matumizi kidogo ya chumvi, mazoezi ya viungo, kupunguza uzito, na kuepuka msongo wa mawazo kila mara.
Lakini pia kuhudhuria clinic au kuonwa na daktari walau mara mbili kwa mwezi kwa ajili ya kufuatilia hali ya afya yako.
2. Ukiwa na magonjwa ya moyo, sukari na wingi wa mafuta mwilini, daktari atakuandikia dawa za kusaidia kuzuia uwezo wa kuganda damu kwenye mishipa. Dawa hiyo unapaswa uimeze ipasavyo.
Pia ni vizuri kufanya vipimo vya damu walau kila baada ya miezi 3 mpaka 6.
3. Epuka matumizi ya dawa za kulevya
Kumbuka ukipata kiharusi cha ‘milele’ (moja kwa moja), kama ni kijana shughuli yako imeisha hapo! Jihadhari sana na makundi na kufanya vitu ambavyo huna taarifa navyo.
Epuka dawa za kulevya, jikinge na kiharusi. Kumbuka hata matumizi ya sigara yanakuweka karibu kabisa na uwezekano wa kupata kiharusi hasa ukiwa na matatizo mengine kama presha, sukari na kitambi (obesity).
4. Usichukulie poa kuvimba kokote kwa miguu, hasa mguu mmoja. Pata ushauri wa daktari mapema iwezekanavyo.
5. Kufanya mazoezi mara kwa mara
Utafiti unaonyesha mazoezi ya walau dakika 30 kila siku kwa siku 5 yanapunguza uwezekano wa kupata kiharusi kwa asilimia 25%.
6. Matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za uume (viagra) yafanywe kwa kuzingatia ushauri wa daktari na sio binafsi.
Ikitumika katika kiwango cha juu inaweza kusababisha kiharusi.
7. Ni muhimu kuanza mazoezi mepesi (ambulatiion) mapema baada ya upasuaji mkubwa (major surgery) ili kuepusha mgando wa damu kwenye mishipa.
Nini kifanyike ukishapata kiharusi?
Fahamu kwamba ugonjwa wa kiharusi unaweza kuwa wa muda mfupi au muda mrefu au kubaki na kilema maisha yako yote.
Inategemea na kiasi cha madhara ya ubongo, umri, na sababu zingine ambatanishi kama uzee, ugonjwa wa moyo, sukari na kadhalika.
1. Unapopata kiharusi ni vyema kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu na vipimo vya awali vya kutambua tatizo.
Kukaa nyumbani muda mrefu kunaweza kufanya tatizo kuwa kubwa zaidi na kupelekea kifo au kilema cha muda mrefu.
Kumbuka katika kila dakika moja unayopoteza bila sehemu ya ubongo kupata damu unapoteza selli milioni 2.
2. Baada ya matibabu hospitalini ni muhimu kuendelea na mazoezi nyumbani kwa ajili ya kuboresha kuongea, mazoezi ya viungo (physiotherapy) na msaada mwingine wa afya.
Sio vyema kumrudisha mgonjwa nyumbani na kumuweka tu bila kuendelea na huduma ya afya.
3. Kumbeba mgonjwa kurudi hospitali mara kwa mara huwa ni changamoto hivyo ni bora kuwa na daktari wa nyumbani wa kumuangalia kwa ukaribu na kufuatilia muenendo wake wa presha, moyo na mambo mengine.
4. Huduma ya afya nyumbani (home health care) inaweza kusaidia mgonjwa kurudi katika hali yake ya mwanzo na kutembea tena kwa sababu ya huduma ya ukaribu anayoipata.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.