“Mama, nguzo ya afya ya familia”, ni kweli?

Kuna msemo unasema ‘ukimuelimisha mwanamke, umeelimisha dunia’, Je ni kweli? Mwanamke ana uhusiano gani na afya ya familia?

 

Mwandishi maarafu wa Marekani, Zig Ziglar, katika kitabu chake cha “See You at the Top” kuna mahala anasema “The best way to love your children is to love their mother”.

 

Unaisi aliona nini kwa mwanamke? Mwanamke ana nguvu kiaisi gani katika afya ya familia?

 

Kabla hatujaingia ndani zaidi embu tujiulize maswali mawili:

Kuna tofauti yoyote ukiwa unaishi na mke na ukiwa bachela (single)? Mfano, ukiwa na mke halafu akaondoka, upungufu wa kwanza kuugundua huwa ni sekta gani?

 

Au kwa wale walioishi na mama halafu akafariki au kuondoka, ni maeneo gani yalianza kulegalega?

 

Moja ya nguzo kubwa za amani katika familia huwa ni afya. Magonjwa ya muda mrefu ya watoto, mme au mke huleta wasiwasi katika familia maana hugharimu muda na uchumi.

 

Nani anahusika na afya ya familia?

Afya ya familia inaletwa na mambo makuu 4 ambayo ni usafi, lishe, saikolojia ya familia na uchumi.

1. Nani huwa ni kiongozi wa usafi nyumbani?

Kila mmoja huwa ana jukumu la kuhakikisha nyumba ni safi kuanzia mazingira mpaka chakula. Lakini nani kiongozi wa usafi?

 

Ukitembelea nyumba ya bachelor wa kike na bachelor wa kiume bila shaka utagundua kwamba usafi uko kwenye vinasaba vya mwanamke zaidi na malezi yao yamewaandaa kuwa wasafi kutokana na hali ya miili yao n.k.

 

Ukiwa bachela ukatembelewa na mwanamke, hata kama umefanya usafi, akifika utashangaa anaanza upya na anaona kama hujafanya lolote.

 

Kwa haraka mwanamke ndio kiongozi wa usafi. Pua zao zinanusa haraka uchafu, macho yao yanaona haraka uchafu na hisia zao huisi haraka uchafu.

 

 

Haimaanishi kwamba wanaume sio wasafi na hawana hisia hizo, hapana! Mwanamke anaandaliwa mapema sana kuona uchafu na kusafisha mazingira.

 

Usafi ndio kila kitu kwenye afya ya familia.

Vyombo vichafu, chakula kichafu, nyumba chafu na mashuka machafu lazima vikupe maradhi ya kuhara, typhoid, allergy na kuugua mafua mara kwa mara.

Mara nyingi watoto kuharisha mara kwa mara huwa ni dalili ya nyumba kuwa na hali mbaya ya usafi kuanzia kwenye vyakula mpaka mazingira.

 

Nyumba ambayo Mama ni mchafu ni kichaka cha maradhi ya familia hivyo ni muhimu sana Mama kujitahidi kuwa msafi.

 

Sio vizuri kuwa na mtazamo wa kukimbilia hospitali tu bila ya kuwa na utaratibu wa kuhakikisha familia inapata mazingira safi.

 

Usafi ni kinga ya kupunguza wanafamilia kuumwa mara kwa mara. Familia yenye mama anayezingatia usafi husahau kabisa maradhi ya mara kwa mara ya watoto.

 

Tuboreshe wapi?

Kumbuka watoto wadogo huokota vitu chini na kula bila kujua, hivyo wakati unapiga deki lazima uweke sabuni itakayoua bakteria wa sakafuni.

 

Watoto wanakojoa kwenye viti na chini, ni muhimu kujitahidi walau kuvisafisha kwa sabuni na kuhakikisha ni visafi na havitoi harufu ili visiwe chanzo cha maambuki ya kuhara.

 

Mfano, kuna nyumba moja niliwahi kwenda, sitasahau. Ile nyumba ilikuwa na harufu mbaya sana tena kwenye makochi. Inaonekana kila watoto wanapokojoa viti havisafishwi. Harufu ilikuwa kama ya uozo, na hapo hapo nikaletewa chai na chapati, nusura nitapike, ila sikuwa na namna. Sikuwahi kurudi tena nyumba ile!

Kumbuka: Uchafu unapokuwa wa kawaida nyumbani, wanafamilia huzoea harufu mbaya na kuona kawaida, tatizo linakuja wageni wanapokuja, huwa ni aibu kubwa.

 

Mama hakikisha vyombo vinaoshwa na vinakaa visafi muda wote, sio vyombo vinashinda na inzi siku nzima. Vyakula vipashwe moto na viwe vya moto.

 

Nguo za watoto na mume lazima ziwe safi na zinukie vizuri. Haya ndio mambo ya msingi anayopaswa kufanya mama yeyote, kabla ya taaluma zozote!

 

Tip kwa wanaume: Mume kabla ya kuoa hakikisha mchumba wako ni msafi, la sivyo hilo litakuwa chanzo cha ugomvi mara kwa mara. Mfano, mwanamke ambaye hajisafishi vizuri na kutoa harufu mbaya humfanya mumewe kupoteza hamu ya kula chakula pamoja na tendo la ndoa.

 

Zaidi, Mume mchafu mara nyingi huweza kusaidiwa na kubadilika kama mke wake ni msafi.

 

Sasa pigia picha familia ambayo mke na mume wote ni wachafu. Jibu baki nalo!

 

2. Nani huwa ni kiongozi wa Lishe bora katika familia?

Katika utafiti wa haraka ni asilimia 15 tu ya wanaume hujihusisha na ratiba za chakula na aina ya chakula nyumbani. Asilimia 85 huwa wanawaachia wake zao.

 

Mfano, mwanamke akiamua msile mchicha au dagaa nyumbani, inawezekana kabisa maana yeye ndio anaenda sokoni kununua hivyo vitu, na mara chache kwa wanaume.

 

Mwanamke akiamua mle nyama, hata usipoacha hela, atajua pa kupata lakini utakuta nyama mezani ila mwanaume asipokuwa na hela basi mtakula kabeji mpaka ziwaote usoni.

 

 

Kwa haraka utagundua Lishe bora ya familia inategemea zaidi mama kuliko baba. Ndiomaana mama asipokuwa na elimu ya afya ni hatari sana kwa familia. Hapa ndipo watoto hupata utapiamlo wakati vyakula vipo.

 

Hivyo ni muhimu sana kama mama kujieleimisha zaidi kuhusu Lishe na kupambana kuhakikisha familia inapata mlo kamili.

 

Ni vizuri pia mama kuwa mwaminifu hasa katika matumizi ya fedha ya familia. Sio vizuri kuminya pesa ya chakula cha familia kwa ajili ya mambo binafsi. Ni vizuri kupambana kuwa na kipato cha ziada cha kuhudumia haja zingine.

 

Ukiwa kama mama ni jukumu lako kuhakikisha familia wanapata mlo kamili. Mlo kamili sio lazima iwe nyama kila siku. Ni mchanganyiko wa vyakula vinavyoleta nguvu (wanga), vinavyojenga mwili (protini), vinavyolinda mwili (vitamini, matunda na mboga za majani, mafuta na maji).

 

Unaweza kuisoma zaidi hii katika makala yangu ya utapiamlo.

 

Lengo la mlo kamili ni kuhakikisha walau unaepusha wanafamilia kupata utapiamlo ambao ni hatari kwa kizazi chako.

 

Watoto ni taifa la kesho, wakipata utapiamlo wa mapema wa chini ya miaka 5, basi akili yao huwa haiwi sawa tena hata wakikua. Sasa kwanini ukubali kukuza mazombi?

 

Mume pia anapaswa kula vizuri, ili awe na nguvu ya kutosha kuipambania familia.

 

Mume wako akipata kitambi kwa sababu ya kula wanga peke yake ni hatari kwako na familia kwa ujumla, hasa akianza kupata magonjwa ya moyo na sukari.

 

Hata kama mume ni mlevi, ni vizuri kuhakikisha anakula vizuri. Mambo ya kumlisha mume mikate na chips kila siku kwasababu ya uvivu wa kupika sio sawa. Inamfanya mume anakuwa dhaifu, hana nguvu na hii inaathiri familia kwa ujumla.

 

3. Nani anahusika na saikolojia nzuri ya familia?

Mama huwa ndio nguzo ya saikolojia ya familia. Mama akiwa waruwaru, hata familia kuanzia baba mpaka watoto huvurugika.

 

Mama mtulivu na mwenye heshima humpa mume wake saikolojia nzuri na amani. Watoto pia wanakuwa na amani zaidi mama akiwepo.

 

Wanawake wana moyo mkubwa wa ku’balance changamoto za familia. Baba katika familia anaweza kuwa mkali au muonevu, lakini uwepo wa mama husaidia kubalance hali hii.

 

 

Bila kuwepo mama, sisi wanaume ni ngumu kuishi na watoto bila kugombana nao.

 

Kuna changamoto nyingi ambazo mama anazitatua za kifamilia ambazo hata baba hazijui. Mfano, mkiwa na changamoto ya kipesa, mama ana uwezo wa kukopa katika kikundi na kutatua tatizo kwa moyo mmoja.

 

Katika kuishi kwangu na mke wangu, mara nyingi niligundua kitu kimoja. Ukitaka kuwa na amani kama mume, mjali mke wako vizuri.

 

Pia niligundua mke ambaye hajatulia na mkorofi huweza kuathiri afya ya mume wake moja kwa moja.

 

Mume mwenye mke mkorofi na muhuni ni rahisi kupata presha, kiharusi na kufa mapema au kuwa na msongo wa mawazo na kufanya vibaya kazini.

 

Hivyo mke mtulivu ni chanzo cha amani na afya nzuri ya mumewe na familia kwa ujumla. Mume mwenye mke wa namna hii mara nyingi huishi muda mrefu.

 

Mke akiwa anapata upendo thabiti na akajiamini ana uwezo wa kuipambania familia katika kiwango kikubwa sana.

 

Maneno ya kutia moyo anayokupa mwanamke wako ukiwa katika tatizo ni chanzo cha afya nzuri ya akili na hukupa nguvu ya kupambana tena.

 

Mfano, wakati nimeachishwa kazi ghafla mwaka 2020, mke wangu alikuwa nguzo kubwa sana kwangu kwa kuniamini, kunitia nguvu na kunisapoti kifedha walau kupata mahitaji yangu muhimu wakati najitafuta tena.

Bila yeye nani angenifariji?  Marafiki wengi ukishaishiwa wanakimbiaga lakini mke wako atabaki na wewe na kukufariji.

 

Ndiomaana kwa mwanaume, ukitaka amani na maisha bora kifamilia, kwanza hakikisha unamjali mke wako, mpe kujiamini, mpe uhuru wa kufanya majukumu yake, mtie moyo na kadhalika.

 

Lengo ni kutengeneza nguzo imara ya familia. Hata ukifa, unajua umeacha jembe na watoto watakuwa salama.

 

Wanawake ni viumbe wenye nguvu na ushawishi mkubwa sana. Ukitaka kufanikiwa katika maisha kama mume lazima utengeneze mazingira ya kutumia vizuri uwezo wa mke wako.

 

Chuo Kikuu cha Carnegie Mellon University kilifanya utafiti huu kwa kuhusisha wanandoa 163.

Asilimia 95 ya wale waliokuwa na mafanikio walisema mafanikio yao yametokana na wake zao kuwa na msaada mkubwa hasa kisaikolojia kwa kuwapa msukumo wa kufanya makubwa.

Baadhi yao ni Raisi wa zamani wa Marekani, Barack Obama, mwanzilishi wa Facebook Marc Zuckerberg na Rapa maarufu Jay Z.

 

4. Nani ni nguzo ya uchumi wa familia?

Bila shaka jibu lako ni Baba. Lakini nitaenda kinyume na wewe. Baba anaweza kuwa mtafutaji mkuu wa familia ila muhasibu mkuu wa pesa ya familia mara nyingi huwa ni mama.

 

Katika utafiti wangu wa haraka, asilimia 75 ya wanaume wanapopata mshahara, pesa ya matumizi ya familia huwapa wake zao kuhakikisha kila kitu kiko sawa. Maana yake nini?

 

Mume akimpa mke pesa anapumzika kwamba tayari kila kitu kiko sawa. Sasa itakuwaje kama mama sio mwaminifu au sio muhasibu mzuri?

 

Bila shaka familia itajikuta inakula aina moja ya chakula au chakula kuisha mapema kabla ya muda wake kwa sababu tu mama alitumia pesa kwa manufaa yake.

 

Mama mzuri wa familia na anayejali familia huwa anatumia pesa anayopewa lakini huficha akiba kidogo kwa ajili ya dharula.

 

Ndiomaana wakati mwingine Baba anaweza kuwa anarudi nyumbani anajua leo majanga lakini mkewe atampakulia msosi mzuri tu, atashangaa, kumbe mke alitunza akiba.

 

Mama anajukumu na nafasi kubwa ya kuwa nguzo ya uchumi wa familia.

Mama akiwa muhasibu mzuri huweza kubalansi hata kile kidogo anachokipata mumewe kununua mahitaji muhimu ya familia na hivyo husaidia kushusha presha ya mumewe na kuleta amani.

 

Mama asiyekuwa mchumi mzuri ni chanzo cha mgogoro katika familia na hii huathiri afya kwa ujumla. Kununua vitu vichache na hela inayobaki huweka kucha za gharama, wigi la gharama n.k.

 

Mapema tu chakula huisha na huanza kumsumbua tena mumewe kutuma hela ya kula. Hapo ndipo ugomvi wa baba na mama huanza.

 

Kumbuka, mume anafanya kazi ngumu sana kuhakikisha analeta chochote, ni muhimu kumtia moyo na sio kila siku kumuonyesha kwamba anachokileta hakitoshi wakati unatumia vibaya.

 

Ni vizuri mama pia kufanya shughuli za kuongeza kipato cha familia, hii inachangia sana afya ya familia. Mama anayejishughulisha ni dhahabu katika familia na huongeza chachu ya maendeleo.

 

Wakati mama analisha familia, baba anajenga nyumba au kununua usafiri wa familia au kulipa ada ya shule za watoto. Hali hii huleta afya bora na furaha katika familia.

 

Mwanamke mvivu ni kikwazo katika afya ya familia.

Ewe mwanamke, wewe ni chachu na nguzo ya afya ya familia, fanya mishe mishe, itakuongezea heshima na utaongeza thamani ya familia.

 

Baba anayemzuia mama kujishughulisha ni mpumbavu hasa katika karne hii ya teknolojia na viwanda. Mambo ya Baba ndio mtafutaji pekee yameshapitwa na wakati.

 

Wanawake wameonesha uwezo mkubwa wa kusaidia familia. Ushirikiano wa Mama na Baba utaleta mafanikio zaidi.

 

Bonus: Nani huwa ana jicho la tatu katika familia?

Mwanafamilia akiumwa, mama ndio huwa wa kwanza kulazimisha kumpeleka hospitali kwasababu mara nyingine Baba hana hela au huchukulia powa, huwa na kusitasita kidogo na kadhalika.

 

Mwisho

Mambo manne niliyoyazungumzia hapo – usafi, lishe, saikolojia nzuri (afya ya akili) na uchumi – ndio nguzo ya afya ya familia.

Mwanamke yuko katika nafasi nzuri ya kuhakikisha anawezesha haya mambo.

Haimaanishi wanaume hawawezi, hapana! Bali wanawake wako katika nafasi nzuri ya kutekeleza haya kulingana na majukumu na malezi yao.

 

Ni muhimu sana kwa mwanamke kulitambua hili na kutimiza wajibu wako. Wewe una nguvu na uwezo mkubwa na wajibu wa kuhakikisha familia inasimama imara.

 

Epuka kulaumu wanaume kila matatizo ya familia yanapotokea bali uwe mstari wa mbele kuhakikisha familia inasimama.

Mama bora lazima aangukie katika vitu hivi vinne.

 

Kwa kumalizia, naomba nikuachie maswali haya katika makundi mawili:

1: Kwanini mume akiwa mchafu, huwa analaumiwa mama? Na Kwanini mama akiwa mchafu huwa analaumiwa yeye na sio baba? Jibu baki nalo.

 

2: Baba, mara ya mwisho kudeki nyumba ni lini? Mara ya mwisho kununua chakula sokoni ni lini? Mara ya mwisho kununua mashuka ni lini? Mara ya mwisho kujinunulia nguo za ndani ni lini?

 

Mama ni nguzo ya afya ya familia, tumpe maua yake.

 

Endelea kupitia blogu yetu kujielimisha kiafya zaidi.

 

Tembelea duka letu kupata vitabu vyangu mbalimbali. Unaweza pia kufanya booking ya kuongea na mimi ili kupata ushauri wa mambo mbalimbali ya kiafya.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW