Mfungo sio dhana mpya kabisa. Tumekuwa tukifunga kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kidini – wakati wa Kwaresma au Mwezi Mtukufu wa Ramadhani – au kupunguza uzito.
Miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na uelewa mpana wa faida za mfungo kutokana na tafiti za kisayansi kuendelea kuonyesha jinsi ambavyo utaratibu wa kufunga husaidia kupunguza uzito na kuboresha hali ya ubora wa maisha kwa ujumla.
Faida za mfungo tiba
Zipo faida mbalimbali za mfungo tiba. Faida hizi hutokana na hali inayojulikana kama ketosis ambayo hutokea mwilini pale ambapo mwili unaacha kutumia sukari na kuanza kuchoma mafuta yaliyohifadhiwa mwilini.
Hali hii huchochea uzalishwaji wa baadhi ya homoni kama homoni ya ukuaji yaani Human Growth Hormone (HGH) na Testostreni.
Pia ketosis husaidia kuanzisha ukarabati mkupwa ndani ya mwili. Hali hii hujulikana kama autophagy. Seli za mwili zilizoharibika au kuchoka, hufanywa upya.
Hivyo zifuatazo ni baadhi ya faida kuu za mfungo tiba katika mwili wako;
1. Kupunguza uzalishwaji wa homoni ya insulin
Homoni hii husaidia kuhifadhi sukari mwilini kama mafuta. Mfungo hupelekea kuchochea mwitikio wa homoni kwa wagonjwa waliokwisha kutengeneza ukinzani (insulin resistance).
2. Husaidia kupunguza uzito, kurudisha nyuma athari za kisukari, kupunguza makali ya magonjwa yanayosababishwa na shambulio ndani ya mwili yaani inflammation – magonjwa haya ni kama mafua ya mara kwa mara, pumu ya mfumo wa upumuaji na ile ya ngozi, pamoja na matatizo katika kuta za mfumo wa mme’ngenyo wa chakula.
3. Hupelekea kupungua uzito mkubwa
Uzito mkubwa na unene ni hali ya kuwa na mafuta mengi yaliyohifadhiwa katika sehemu mbali mbali za mwili.
Ukiwa katika mfungo tiba, mwili huanza kuyatumia mafuta hayo kama chanzo kikubwa cha nishati. Hivyo kukufanya upungue kilo kwa urahisi na ndani ya muda mfupi.
4. Kama Rumi alivyosema “kufunga ni kanuni ya kwanza ya matibabu, funga na ufahamu uwezo wa nafsi yako”. Basi kufunga humiarisha kinga ya mwili wako kwa kuharibu seli hai nyeupe za mwili zilizochakaa na kutengeneza nyingne mpya.
Faida nyingine ni pamoja na kupunguza cholesterol mbaya mwilini, kuongeza utulivu wa fikra na ubunifu.
Pia mfungo tiba husaidia mwili kuhimili njaa na kukata shauku ya chakula hasa vyenye sukari kila wakati.
Nini huendelea mwilini wakati ukiwa umefunga?
Masaa 0 mpaka 4 baada ya kula chakula chako: Mwili huzalisha homoni ya insulin ambayo husaidia kutumia na kuhifadhi sukari (glucose) katika seli za mwili wako.
Masaa 4 mapaka 16: Mwili huanza kutumia glucose aliyokwisha kuhifadhia katika misuli na ini kama chanzo kikuu cha nishati mpaka pale hazina itakapoisha.
Masaa 16 mpaka 24: Mwili huingia katika hatua ya kuchoma mafuta. Mapema kiasi gani utaingia katika hatua hii hutegemea na kiasi cha hifadhi ya sukari katika mwili wako na mazoea yako ya kufanya mfungo.
Wengine huanza masaa 14 baada ya kula na baadhi masaa 16 mpaka 20.
Masaa 24 mpaka 72: Mwili rasmi huingia katika hali iitwayo ketosis. Ndani ya muda huu, mwili wako hutumia mafuta kama chanzo pekee cha nishati.
Mafuta yakichomwa huzalisha aina ya kemikali iitwayo ketones. Kama tulivyoona hapo awali, ketones ndio msingi wa faida zote za mfungo tulizoziorodhesha.
Masaa 72 na zaidi: Mwili huendelea kuwa katika hali ya ketosis ambapo mabadiliko mbalimbali hutokea mwilini ikiwemo kuongezeka kwa homoni ya ukuaji na testosteroni.
Kiasi cha insulin kinachozalishwa hupungua na kukaribia/kufikia sifuri.
Katika hali hii ya deep ketosis, seli hutengenezwa upya, kinga ya mwili kuimarishwa, shambulio ndani ya mwili kupungunzwa na seli za saratani hudhaniwa kuaanza kufa kutokana na kukosa chakula.
Namna tofauti za mifungo
Zipo namna tofauti za mifungo. Namna hizi zote hutegemea mpangilio wako wa ulaji wa chakula.
Aina hizi tunaweza kuziweka katika makundi matatu: mfungo wa muda mfupi, mfungo wa kubadilishana, na mfungo wa muda mrefu.
1. Mfungo wa muda mfupi
Huu hujulikana kama Intermittent Fasting ambapo mfungaji huchagua masaa kadhaa ambayo anakuwa hali au kunywa chochote chenye chanzo cha sukari.
Mfungo maarufu hapa ni ule wa 16:8 ambao humaanisha mtu anakaa kwenye mfungo wa masaa 16 wakati milo yake ikiwa imepishana masaa 8.
Kwa mfano kama ukila mlo wako wa mwisho saa 2:00 usiku, mlo wako unaofuata unapaswa kuwa kesho saa 6:00 mchana.
Aina zingine za mifungo ya muda mfupi ni 18:6, 20:4, 21:1 na ule wa mlo mmoja tu kwa siku yaani OMAD (One Meal a Day).
2. Mfungo wa kupokezana siku
Mfungo wa aina hii hujulikana pia kama Alternate-day Fasting. Unapokezana siku za kufunga. Unaweza kufunga leo kisha ukaruka siku moja au mbili.
Pia unaweza kula milo yote kwa siku tano, ukafunga siku za wikiendi yaani 5:2, au kinyuma chake.
3. Mfungo wa muda mrefu
Mfungo huu ni wa muda wa kuanzia siku mbili, tatu na kuendelea. Kwa mfungo unaozidi siku tano ni muhimu ufanywe chini ya usimamzi wa mtaalamu wa mfungo tiba.
Muhimu: Mifungo tiba tunayopendekeza katika makala hii ni ile inayoambatana na kunywa maji pamoja na madini ya chumvichumvi.
Mfungo tiba na kupunguza uzito
Kufunga, kama tulivyoona, ni njia rahisi na nafuu ya kupunguza uzito. Isitoshe unaweza kuingiza mfungo katika mfumo wako wa maisha wa kila siku.
Kwa mfano, wapo watu wanaoruka kifungua kinywa cha asubuhi, na kula mlo miwili, mchana na usiku. Na wengine wanakula mlo mmoja tu, wa asubuhi au usiku. Unaweza kupanga ratiba zako sawa ili kuendana na utaratibu wako wa maisha wa kila siku.
Siku za kwanza za mfungo utapukutika uzito. Hali hii hujulikana kama water weight. Baadae utaanza kuona mabadiliko kidogo kidogo na mwili utaendelea kupungua.
Kufunga ni vigumu katika siku za mwanzo lakini baada ya muda uwezo wa kustahimili njaa huongezeka na linakuwa zoezi rahisi kabisa.
Namna na aina ya mfungo hutegemea na malengo yako. Ila namna rahisi ya kuanza ni mfungo wa muda wa mfupi wa 16:8, baadae unaweza kuongeza mpaka mlo mmoja kwa siku au mfungo wa siku mbili au tatu.
Mambo ya kuzingatia wakati wa ‘kufungua’
Jambo jingine la muhimu kuzingatia ni namna unavyofungua mfungo wako. Ni vyema kufungua mfungo wako kwa kula vyakula vyenye kiasi kidogo cha sukari kwenye damu.
Kwa mfungo mfupi, unaweza kufungua kwa kula supu, nyama, mayai, mboga za majani, na nafaka ambazo hazijakobolewa.
Lakini ukiwa umefunga zaidi ya siku mbili, kula vitu laini katika mlo wako wa kwanza, mfano juisi ya parachichi, ukwaju na kabeji (isiyo na sukari), mayai, mtori, na makongoro.
Unakusudia kuanza kufunga kwa ajili ya afya yako au sababu nyingine? Unaweza kuongea moja kwa moja na daktari wetu ili akupe ushauri wa kina.

Medical Writer | Offering top-notch writing services in the medical, scientific, and academic realms | I share practical insights on weight loss, fasting, nutrition, sleep, productivity and longevity.
Madini mengi sana daktari, ahsante
Interermitent fasting sio tu ilinisaidia kumantain mwili na uzito bali hata budget yangu ya chakula ilipungua…