Afya ya akili ni nini?
Ni hali ya ubongo wako kungamua mambo mbali mbali yanayohusisha kufikiria, kumbukumbu, hisia, maamuzi, kuona kwa usahihi na jinsi ya kuhusiana na jamii kwa ujumla. Afya ya akili sio ukosefu wa magonjwa ya akili.
Shirika la afya duniani (WHO) hutambua afya ya akili kama mojawapo ya mahitaji muhimu ya kibinadamu (basic life needs).
Kuwa na afya mbaya ya akili sio lazima uwe chizi, unaweza kuwa katika utimilifu wa akili na bado afya yako ya akili ikawa mbovu.
Zipi ni dalili za afya nzuri ya akili?
Kwanza huwa na furaha mara nyingi, huweza kuzitawala hisia zako, huwa na mitazamo chanya ya mambo, huwa na shukrani kwa kila hatua ya maisha, huwa na mahusiano mazuri na jamii inayokuzunguka.
Mtu anapokosa vitu hivyo mara nyingi afya yake ya akili sio nzuri na huwa ni watu wa lawama, hawaridhiki na chochote, wagomvi mara kwa mara, wabishi bila sababu, walevi na wengi hupenda shortcut sana mfano kuvuta sigara iIi kupunguza mawazo badala ya kutatua matatizo.
Hizi ndizo tabia tatu zinazoleta afya nzuri ya akili:
1. Kujenga mahusiano salama
“Ndege wanaofanana huruka katika kundi moja”
Je, unajua kwamba mahusiano yako – yawe ya urafiki wa kawaida au mapenzi – ndiyo hutoa picha halisi ya afya yako ya akili na kwa upande mwingine huwa na mchango wa moja kwa moja katika afya yako ya akili?
Ukimuona mtu ambaye haeleweki kazini au mtaani, angalia kwanza watu wake wa karibu. Utagundua kitu.
Tabia kuu ya watu wenye afya njema ya akili ni kutengeneza mahusiano na watu wenye mchango chanya katika maisha yao na sio kila mtu. Huusiana zaidi na watu wenye mitazamo chanya, wasiolalamika mara kwa mara, watu wawajibikaji, watu wenye juhudi ya kazi na wasio na majungu. Watu ambao wamefanikiwa.
Kuhusiana na watu wa aina hii humpa mtu mtazamo chanya wa maisha, kupambana kutaka kuwa kama wao. Hivyo hujikuta na mawazo mazuri, msaada mzuri na mwishowe hupata ile saikolojia nzuri ya kuishi kwa furaha na amani.
Saikolojia nzuri hupelekea mtu kuwa na afya njema ya akili na watu hawa huwa watu wa kutabasamu, kushukuru na kadhalika.
Chukua mfano, wewe ni kijana ukahusiana na binti asiye mlalamishi, mwenye kushukuru na kile unachoweza kumpa, pamoja na upendo kwa nduguzo. Utajikuta baada ya muda mambo yako yanaanza kunyooka na unakuwa na furaha na kujiamini kwa sana.
Lakini ukitengeneza mahusiano na binti ambaye haliziki, kila kukicha ni kuomba hela, kukutukana unapochelewa kupokea simu, kuwatukana ndugu zako na vitu vingine. Mara nyingi utajikuta una msongo wa mawazo, haufikiri vizuri na ni rahisi kugombana au kufanya vibaya kazini.
Au ukiwa na mpenzi tapeli na mwizi, utakuwa vizuri kichwani? Mara nyingi unawaza jela, au kukamatwa siku moja. Afya yako ya akili haiwezi kuwa sawa. Ili Afya yako iweze kuwa sawa lazima kuwe na amani.
Mahusiano unayotengeneza ndiyo huamua mudi yako. Kuna baadhi ya watu ukiwa karibu nao mambo yako yataenda vibaya kwa sababu watakuambukiza mtazamo hasi (victim mind-sets).
Ukiwa na rafiki anayelalamikia kila kitu, baada ya miezi mitatu nawewe utakuwa mlalamishi. Ukishakuwa mlalamishi tayari ni dalili akili yako haiko sawa.
Mwaka huu kuwa wa tofauti. Jenga mahusiano na watu ambao watakutoa hatua moja kwenda nyingine. Kumbuka afya nzuri ya akili ndio ufunguo wa kutimiza malengo yako. Angalia tabia za watu wenye afya mbaya ya akili hapo juu na ukiwagundua kaa nao mbali.
Kumbuka afya mbovu ya akili inaambukizwa. Epuka kukaa na watu wenye tabia mbaya kwa kudhani utawabadilisha. Mara nyingi watu wa namna hii huwa tayari wanaumwa na wanahitaji wataalam wa saikolojia, sio wewe.
Baadhi yao wanaweza kuwa ndugu zako lakini hamna namna, wasiliana nao inapobidi lakini usitumie muda mwingi nao. Tumia muda wako na watu wachangamfu, wenye furaha na mtazamo chanya.
Ukiona kila siku mambo yako hayaendi, usitafute mchawi mbali. Angalia mahusiano yako kuanzia ndani mpaka kwa washkaji zako. Utagundua mchawi.
2. Kutumia muda wako vizuri
Muda ni mali, ukitumika vizuri huweza kumpa mtu matokeo ya mapema na furaha. Nikwambie kitu? Watu wenye afya njema ya akili wana matumizi mazuri ya muda na wanajali muda wao vizuri.
“The way we spend our time defines who we are” – Jonathan Estrin.
Utafiti unaonyesha matumizi mabaya ya muda huleta majuto ambayo badaye hupelekea msongo wa mawazo. Kila jambo na muda wake. Kuna fursa ikipita huwezi kuikamata tena.
Watu wenye afya njema ya akili hutumia muda vizuri kwenye mambo mbalimbali kama;
Kujali muda wao wa kulala. Watu hawa hulala walau masaa 6 hadi saba na kesho yake huamka wakiwa na vichwa vilivyotulia na hivyo kufanya kazi kwa nguvu na ubora sana.
Moja ya shida ya watu wenye afya mbovu ya akili ni kutolala muda wa kutosha. Mtu akitoka kazini anaingia mtandaoni mpaka saa saba usiku na hulala masaa manne tu. Matokeo yake, siku inayofuata huwa mchovu na mudi mbaya, hivyo ni rahisi sana kugombana na wenzake kazini au majirani. Ubongo ukiwa mchovu, afya ya akili huathiriwa pia. Bila shaka wote ni mashahidi wa hili.
ANGALIZO: Bahati mbaya kuna watu wanafanya kazi zinazowafanya wasilale vya kutosha. Bado ukweli haupingiki kwamba kulala muda wa kutosha ni dawa nzuri ya afya ya akili, hivyo jitahidi kupata muda wa kufidia usingizi wako.
Mwaka 2020 Mtandao wa afya wa PUBMED ulitoa report iliyohusisha msongo wa mawazo na ukosefu wa usingizi wa kutosha. Hii husababishwa na mvurugiko wa homoni za cortisol pamoja na homoni za ukuaji.
Pia ilihusisha kutolala vizuri na ongezeko la mawazo ya kujiua, usahaulifu na kuzeeka mapema.
Watu wenye afya njema ya akili huweka mipango thabiti na kuifanyia kazi kwa wakati. Mafanikio ni safari ndefu na mtu anapaswa kuanza mapema kutimiza ndoto zake.
Kiufupi inabidi kuwa mbele ya muda. Kuchelewa kufanya mambo kwa wakati baadaye huleta majuto na majuto huvuruga afya ya akili. Hauwezi kuwa sawa.
Ili uweze kuwa na amani ya moyo na kuepuka msongo wa mawazo ni lazima ujue kutumia muda wako vizuri. Kupanga mambo vizuri na kuanza kutekeleza mapema husaidia kuwa na amani na furaha.
Mtu asiyeenda na muda hujikuta nyuma ya wengine mara kwa mara na hali hii huathiri saikolojia yake na kupoteza kujiamini na baada ya hapo huwa mlalamishi na kuona kama wengine ndio sababu yupo hapo alipo.
Hupoteza muda kwa kufanya vitu tofauti tofauti bila kukamilisha chochote na baadaye hupata msongo wa mawazo. Tayari afya yake ya akili haiko sawa.
Jifunze:
Ili uweze kuwa na furaha na kujivuna, jaribu kuwa mbele ya muda. Fanya linalowezekana kufanya leo. Usighairishe mambo kila wakati.
Watu wengi wanaopata msongo wa mawazo kuanzia miaka 40 ni wale waliopoteza muda kwenye mambo yasiyokuwa na faida za mbeleni mfano umalaya, kufanya kazi za kipato cha chini kwa muda mrefu, kugombana na mke kwa muda mrefu, kupoteza mali walizozikusanya mapema na kadhalika.
Mwanafalsafa Muse alisema “Usipoteze muda au muda utakupoteza”.
3. Kufanya ulichopanga kufanya
Mara ngapi umeweka mipango yako na umeshindwa kuitimiza kila mwaka?
Waangalie watu wenye afya nzuri ya akili utagundua wana furaha, wanajiamini na wana shukurani kwa sababu wanatimiza ahadi wanazojiwekea. Hakuna kitu kinacholeta majuto na msongo kama kutokamilisha mipango yako kwa muda mrefu.
Watu wenye afya nzuri ya akili utagundua huwa wanaweka malengo na kuyatimiza.
Wanayatimizaje?
Wanaweka nia thabiti ya kutimiza malengo yao. Wanafanya maamuzi ya uhakika bila kusita. Watu hawa huwa wana furaha kwa sababu wakiamua kufanya jambo lao hawawi na visababu vingi katikati. Kinachowapa furaha ni ile hali ya ushindi wa kila hatua wanayoipata.
Unataka kujenga afya nzuri ya akili?
Fanya mambo yako kama watu hawa. Jiwekee malengo ya size yako, halafu jisukume kuyafanya. Ushindi utakaopata utakupa furaha na kujiamini kufanya tena na tena. Mafanikio hata kama ni madogo huleta furaha na afya nzuri ya akili.
Watu wengi wenye afya nzuri ya akili ni waliofanikiwa katika jambo fulani Mfano mahusiano mazuri, kazi zao zinaenda au malengo yao yanatimia. Hawa ndio utasikia wanasemwa wana roho nzuri na husaidia jamii.
Watu waliofeli mara nyingi huwa na roho majuto na roho mbaya. Wanakuwa na ile roho ya kwanini. Hali hii huchangiwa na afya zao za akili kuwa mbaya kutokana na kutofikia malengo yao.
Usiwe mtu wa kughairisha mambo. Kumbuka kila jambo lina wakati wake wa kufanyika, muda ukikuacha ni ngumu kuukamata.
Mwisho
Afya yako ya akili ndio kila kitu. Ilinde kama mboni ya jicho. Ubongo wako ukiwa umechoka kwa sababu ya msongo wa mambo mengi, hutaweza kufanya jambo lolote la maana.
Afya yako ya akili itategemea sana tabia zako za kila siku. Jenga tabia zenye afya Ili uwe na afya.
Kumbuka, maisha ni mipango. Ukishindwa kupanga, unapanga kushindwa.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.
Makala nzuri sana hasa jamii ikipata ujumbe huu hakika itasaidia kwa kiasi kikubwa sana.
Ahsante!
Karibu mayala, Unaweza kushare kwa ndugu na jamaa..