Jibu ni NDIYO yenye herufi kubwa!
Matumizi ya tumbaku, iwe kwa kuvuta sigara au kutafunwa, yanaweka tishio kubwa katika afya yako ya mdomo. Athari hizi huonekana kwenye meno hadi fizi zako.
Unaweza uliza ni athari gani hizo unaweza kupata na ni kwa namna gani hiyo. Basi acha nikueleze zaidi kuwa matumizi ya tumbaku hupelekea yafuatayo:
Magonjwa wa fizi na kuoza kwa meno
Ukivuta sigara au kunusa tumbaku kunachangia sana magonjwa ya fizi (gingivitis and periodontitis) na kuoza kwa meno. Kemikali zilizo kwenye bidhaa za tumbaku zinaweza kusababisha kudhohofika kwa fizi, kusababisha uvimbe na kuacha wazi fizi.
Haya yote hufungua njia kwa bakteria kuongezeka, kusababisha uharibifu na hatari ya kupoteza meno.
Hatari ya kupata saratani ya mdomo
Athari mbaya zaidi na kubwa ya matumizi ya tumbaku ni hatari ya kutokea kwa saratani ya mdomo. Tishu za mdomo, ulimi, na koo zinaweza kuathiriwa kwa ukuaji wa kansa kutokana na kemikali zilizomo kwenye tumbaku.
Ishara za mapema unazoweza kupata ni pamoja na vidonda vinavyodumu, mabadiliko kwenye sauti, na ugumu wa kumeza.
Kubadilika kwa rangi ya meno na harufu mbaya ya mdomo
Matumizi yako ya tumbaku ni mojawapo ya sababu kuu za kubadilika kwa rangi ya meno, ikiacha meno yakiwa ya njano na baada ya muda meno huwa na rangi nyeusi.
Tumbaku pia inasababisha harufu mbaya ya mdomo kwa muda mrefu ambayo inaweza kuwa na athari kijamii. Wanawake wenye wanaume ambao huvuta sigara wananielewa sana hapa.
Hata wewe ulishawahi kaa karibu na mtu anayevuta sigara hata kwenye usafiri, je ulionaje harufu ya kinywa cha mtu huyo?
Upungufu wa mtiririko wa damu na kupona kwa vidonda kinywani
Mkondo wa damu utembeapo mpaka kwenye fizi huleta pamoja nayo virutubisho na vimelea vya mwili ambavyo husaidia katika matibabu ya majeraha na ushawisho wa viungo mbali mbali vya mwili.
Nikotini katika tumbaku inapunguza mtiririko wa damu, hivyo kusababisha upungufu wa damu kwenye ufizi. Hii inazuia uwezo wa ufizi kupona na kuongeza hatari ya maambukizi kwani kinga huwa chini.
Kuchelewa kupona baada ya kung’oa meno au katika matibabu ya kupanga meno (orthodontics)
Watumiaji wa tumbaku mara nyingi hupata matokeo yaliyodhohofishwa kutokana na matibabu ya upandikizaji wa meno. Hata kusafisha kawaida kunaweza kupelekea changamoto ya kupona kuliko dhoofika na ongezeko la hatari ya maambukizi yaani infection kwenye jeraha.
Kuwapa athari wengine karibu na wewe
Ni muhimu kutambua kwamba athari mbaya za tumbaku husambazwa kwa wengine pia zaidi ya mtu yule anayevuta. Kuchangamana na moshi wa pili kunaweza kuathiri afya ya wale wasiovuta, hasa watoto, kuongeza hatari ya matatizo ya kupumua.
Utegemezi wa Nikotini
Nikotini, kiungo kinachosababisha uraibu katika tumbaku, sio tu kinaleta hatari kwa afya lakini pia kinachangia kuleta uraibu au kwa lugha ya mtaani uteja.
Kitendo cha kuvuta sigara au kutumia tumbaku bila kuteketezwa huwaweka watu katika hali ya utegemezi. Kuachana na uraibu huu ni muhimu kwa afya kiujumla, pamoja na ustawi wa mdomo.
Athari kwa tezi za kuzalisha mate
Kuvuta sigara kunaweza kuathiri vibaya kazi za tezi zinazozalisha mate. Mate huwa na jukumu muhimu katika kudumisha afya ya mdomo kwa kusawazisha asidi, kusaidia kumeng’enya chakula, na kuzuia kuoza kwa meno.
Uzalishaji mdogo wa mate unaosababishwa na kuvuta sigara unaweza kusababisha kinywa kuwa kikavu, kuongeza hatari ya meno kuoza na matatizo mengine ya mdomo.
Husababisha kinga dhaifu kinywani
Matumizi ya tumbaku yanadhoofisha mfumo wa kinga, ikifanya mwili kuwa dhaifu katika kupambana na maambukizo, ikiwa ni pamoja na yale ya kwenye ufizi. Udhaifu huu wa kinga huongeza hatari ya magonjwa ya fizi na kuchelewesha mchakato wa uponyaji baada ya upasuaji wa mdomo au taratibu za meno.
Hubadilisha mzunguko wa vimelea hai kinywani
Kinywa ni nyumbani kwa jamii mbalimbali za bakteria, ambao wengine ni muhimu kwa ustawi wa kinywa chako. Kuvuta sigara kunavuruga usawa wa vimelea hvi hivyo kutoa nafasi kwa bakteria hatari kustawi.
Hii inachangia maendeleo ya plaki, ugaga kwenye meno, na kuongeza hatari ya meno kuoza na magonjwa ya fizi.

“For the love of words”