Wiki hii ya Disemba iliyoisha (18th mpaka 22nd) nilipata nafasi kama mhudumu wa afya ya kinywa na meno kusaidia katika matibabu kwenye kambi ya ugonjwa wa hemangioma katika kitengo cha meno, hospitali kuu ya Muhimbili.
Niliona watoto wengi katika umri wa kwanzia miezi na hata watu wazima, vijana na wazee wakiwa na vimbe hizi katika maeneo mbali mbali ya nyuso zao.
Niliweza kuonana na wamama wengi ambao haikuwa mara ya kwanza kuja katika kambi kama hiyo lakini pia walikuwamo wamama ambao hiyo ndiyo ilikuwa kambi ya kwanza kushiriki kwaajili ya kutibia watoto wao.
Nilijikuta nikikumbwa na maswali mengi kutoka kwa mama hao juu ya ugonjwa huu na jinsi gani huduma inayotolewa itafanyika kwani kama mama unakuwa umejawa na wasiwasi mwingi.
Inawezekana kabisa ulishawahi kuona uvimbe huu au mwanao anao uvimbe kama huu hivyo basi kupitia makala hii nitakufahamisha juu ya visababishi, namna inavyojitokeza, uchunguzi wa kufanya kuufahamu uvimbe huu kwa mwanao, na chaguzi za matibabu kwa hemangioma ya uso, ikizingatia therapia ya dawa iitwayo bleomycin.
Ugonjwa Hemangioma ni nini?
Hemangiomas ni uvimbe unaotokana na utengenezekaji mbaya wa mishipa ya damu wakati wa utungaji wa mimba tumboni. Mara nyingi uvimbe huu hupatikana sehemu mbalimbali za mwili lakini zaidi sana katika maeneo ya usoni na shingoni mwa mtoto.
Uvimbe huu unapotokea kwenye eneo la uso, huitwa hemangioma ya uso.
Chimbuko la ugonjwa huu ni nini?
Chanzo halisi cha hemangioma hakijulikani kikamilifu, lakini inaaminika kuwa uvimbe huu hutokana na ukuaji usio wa kawaida wa mishipa ya damu. Genetics ya mwilini na mabadiliko ya homoni zinaweza kuchangia katika ukuaji na maendeleo ya uvimbe huu. Ingawa hemangiomas nyingi huwapo tangu kuzaliwa, mara nyingine hutoweka au kuwa dhahiri katika miezi ya kwanza ya maisha ya mtoto.
Visababishi vya hemangioma
Hemangioma ya uso mara nyingi huwepo tangu kuzaliwa kwa mtoto, hata hivyo huenda zikawa hazionekani papo kwa papo na kuanza kuonekana na kukua kadiri mtoto anavyoendelea kukua.
Zingine huwa hazionekani wakati wa utotoni na kuja kutokea mtoto akiwa amekwisha kukua mtu mzima. Vitu vinavyoweza kuchangia sana kutokea kwa vimbe hizi ni kama kuzaliwa kabla ya wakati, uzito mdogo wa kuzaliwa, na jinsia ya kike, hizi zote zinaweza kuongeza hatari ya kupata hemangioma.
Dalili zake
Hemangioma za uso hutofautiana sana katika muonekano. Zinaweza kuonekana kama alama za rangi nyekundu au zambarau kwenye ngozi, au kama uvimbe ndani ya tishu za uso.
Awamu ya ukuaji wa haraka sana. Hapa kama mzazi utaona uvimbe huu ukiongezeka kila siku kuwa mkubwa zaidi ya hapo awali.
Mara nyingi hatua hii hufuatwa na awamu ya kustawi, wakati huu uvimbe hubakia katika saizi yake hiyo hiyo bila kuongezeka wala kupungua na hatimaye involution, au hatua ya kunywea, wakati ambapo hemangioma inaweza kupungua ukubwa wake na kupotea kabisa.
Kiwango cha kupungua hutofautiana kati ya watu.
Uvimbe huu huwa hauumi wala kusababisha hali yoyote ya usumbufu kwa mtoto ila kama ikitokea shingoni na kukua sana, huweza kusababisha kuziba kwa njia ya hewa kwa mtoto hivyo ni vyema kpata ushauri wa daktari mapema.
Vitu gani vinaweza kukujulisha kuwa uvimbe huo ni hemangioma?
Ingawa mtaalamu wa afya ndiye mwenye uwezo zaidi wa kutambua hemangioma, kuna dalili ambazo mtu asiye mtaalamu anaweza kuziangalia.
Hizi ni pamoja na kuonekana kwa alama nyekundu au zambarau kwenye uso, ukuaji wa haraka wa uvimbe katika miezi ya kwanza ya maisha ya mtoto, au uwepo wa uvimbe usio na rangi kama ngozi nyingine inayozunguka uso.
Vilevile unaweza kugundua uvimbe huo huwa na joto zaidi kuliko sehemu zingine za uso. Vilevile uvimbe huo huweza kujaa wakati mtoto amelala au analia na kupungua akikaa au kuacha kulia.
Ikitokea umeona dalili yoyote kati ya hizo, ni muhimu kutembelea kituo cha afya haraka na kushauriana na daktari kwa uchunguzi wa kitaalamu zaidi.
Je, hemangioma hutibiwaje?
Matibabu ya hemangioma za uso hutegemea mambo kadhaa kama vile ukubwa wa uvimbe, eneo uliopo uvimbe, na awamu ya ukuaji.
Ingawa baadhi ya hemangioma zinaweza kutoweka bila matibabu, nyingine zinaweza kuhitaji matibabu. Therapia ya bleomycin imejitokeza kama chaguo linalofaa kwa matibabu ya hemangioma.
Bleomycin, dawa ya antibiotiki na kupambana na kansa, huingizwa moja kwa moja ndani ya uvimbe, na huwezesha kupungua kwake.
Mbinu nyingine za matibabu zinaweza kujumuisha therapia ya leiza, au upasuaji kulingana na hali ya mgonjwa na upokeaji wa uvimbe kwa dawa kama bleomycin.
Therapia ya Bleomycin hufanyikaje?
Therapia ya bleomycin inahusisha sindano ya dawa moja kwa moja ndani ya uvimbe wa hemangioma. Dawa hii hufanya kazi kwa kuharibu mishipa ya damu ndani ya uvimbe, na hivyo kusababisha kupungua kwake.
Hatua hii ya kuelekeza dawa moja kwa moja katika uvimbe ulio ugonjwa inapunguza madhara kwa tishu za kawaida zilizo karibu na uvimbe huo.
Mtoto wako anaweza hitaji sindano mara moja au zaidi ya moja ambapo itapelekea haja ya vikao kadhaa na daktari husika ili kufikia matokeo bora.
Kutambua na kutafuta huduma ya matibabu mara moja
Ni muhimu kwa wazazi na walezi kufuatilia ngozi ya watoto wachanga na wadogo kwa mabadiliko yoyote ya kawaida. Ikiwa alama ya rangi nyekundu au zambarau inaonekana kwenye uso, hasa ikiwa inakua haraka, ni muhimu kutafuta huduma ya matibabu haraka.
Kuingilia kati mapema kunaweza kusaidia kusimamia hali hii kwa ufanisi na kuzuia matatizo yanayoweza kutokea.
Kwa sasa matibabu haya ya vimbe hizi hufanyika hospitali kuu ya taifa Muhimbili katika idara ya meno. Kambi hutangazwa hususani kwaajili ya hemangioma na wakati muafaka hutengwa kwaajili ya kutibu huu ugonjwa.
Mtoto wako atahitajika kurudi miezi 3 baada ya kuchomwa sindano ya bleomycin ili kuangalia maendeleo yake na kufahamu uhitaji wa matibabu zaidi au la.

“For the love of words”
Shukran daktari…
Karibu
Hongera sana dr
Hongera sana
Thanks