Bila shaka swala la kuvimba miguu sio geni kwako. Linaweza kuwa limeshakutokea au kumtokea ndugu na jamaa yako wa karibu.
Miguu kuvimba huwa ni hali ya kushtua kidogo na hupelekea watu wengi kuzunguka huku na kule kutafuta matibabu.
Matibabu ya hali hii yamekuwa magumu sana kwasababu matabibu wengi wanatoa dawa bila kujua nini hasa chanzo cha kuvimba miguu.
Kumbuka, kuvimba miguu huwa na visababishi mbalimbali, hivyo kabla ya kutibu lazima ujue kwanza sababu ni nini, sio kutoa matibabu ya aina moja kwa kila Mtu mwenye tatizo hilo.
Kwanini miguu huvimba?
Kiufupi miguu kuvimba husababishwa na mishipa ya damu ya miguu (veins) kushindwa kusukuma damu kurudi juu.
Hali hii hufanya damu kubaki muda mrefu kwenye mishipa hii na Baadaye kusababisha mgandamizo mkubwa hivyo maji (plasma), huvuja na kutoka kwenye mishipa kwenda kwenye tishu, hivyo miguu huvimba.
Kwa maelezo mengine hali yoyote inayoweza kufanya maji yatoke kwenye mishipa ya damu na kwenda kwenye tishu inapelekea miguu kuvimba.
Tambua: Kuvimba miguu sio ugonjwa bali ni dalili ya ugonjwa fulani mwilini.
Hizi ndio sababu tatu kwanini miguu yako inaweza kuvimba:
1. Maradhi ya Mwili
Kuvimba miguu inaweza kuwa dalili ya maradhi mwilini. Mfano, dalili ya mapema ya ugonjwa wa Moyo inaweza kuwa kuvimba kwa miguu yote miwili.
Hii husababishwa na Moyo kushindwa kupokea damu kwa spidi inayotakiwa kutokana na kukosa nguvu ya kusukuma damu iliyo ndani yake kwenda kwenye mapafu kwa wakati na hivyo kuzalisha mgandamizo mkubwa kwenye mishipa inayoleta damu kwenye Moyo.
Hivyo damu inayopaswa kupanda hushindwa kupanda vizuri na kupelekea mkusanyiko.
Dalili yake huanza kwa kuvimba miguu.
Ukitaka kujua kwamba shida ni Moyo, hali yako ya kuvimba itaambatana na kuchoka haraka, shida ya kupumua unapolala, Moyo kwenda mbio pamoja na kizunguzungu.
Hali nyingine inazoweza kufanana na Shida ya moyo ni kuganda kwa damu kwenye mishipa ya mapafu (Pulmonary embolism).
Magonjwa yanayosababisha kupungua kwa Protein mwilini kama Ugonjwa wa Ini na Utapiamlo husababisha maji kuondoka kwenye mishipa na kwenda kwenye tishu na hivyo huanza kwa kuvimba mwili kuanzia miguu mpaka sehemu zingine.
Mfano wa Magonjwa mengine ni haya: Matende, kuganda damu ya mishipa (Deep venous thrombosis) na Cellulitis (maambukizi ya bacteria kwenye ngozi).
Magonjwa haya yote huambatana na Dalili kama :kushindwa kupumua au maumivu makali ya mguu/miguu yote.
Ukiona hali hizi, usikae nyumbani muda mrefu, muone daktari.
2. Ujauzito
Ujauzito ni moja ya hali ambayo huleta mabadiliko makubwa ya vichocheo vya mwili (hormones).
Hali hii huleta mabadiliko mengi mwilini ikiwemo: kuongezeka kwa kiasi cha maji, kuongezeka kwa presha katika mishipa, moyo kufanya kazi kwa kasi zaidi kwa sababu ya Kuongezeka kwa ukinzani mkubwa zaidi ya kawaida.
Kuongezeka kwa presha katika mishipa ni moja ya sababu ya kuvimba miguu kwa mwanamke mwenye mimba.
Hali hii huchochea maji kutoka kwenye mishipa ya damu kwenda kwenye tishu. Hali hii huanza mara nyingi mimba inapokuwa kubwa kuanzia wiki ya 28 kwenda juu.
Hali hii huwa haiambatani na hatari zingine kama presha kupanda na mara nyingi huchukuliwa kama hali ya kawaida ya mabadiliko ya mwili wakati wa mimba.
Angalizo: Kuvimba miguu mapema kuanzia wiki ya 20 ambapo huambatana na dalili zingine kama: Kichwa kuuma mara kwa mara, Kizunguzungu na maumivu ya tumbo, yaweza kuwa dalili za mapema za Presha ya mimba ijulikanayo kama Pre eclampsia.
Hivyo, kuvimba miguu kokote kwa mama mjamzito ni lazima kufanyiwe uchunguzi na daktari kutambua kama ni hali ya kawaida au kuna dosari.
Miguu yako ikivimba, usikae nyumbani. Nenda ufanyiwe vipimo kadhaa vya presha na mkojo katika kituo cha afya au hospitali ya karibu, sio maabara.
3. Kusimama au kukaa muda mrefu
Kama nilivyokuelezea kuhusu mishipa ya damu kusukuma damu kutoka chini kwenda juu, fahamu kwamba ili mishipa ya vena (veins) iweze kusukuma damu uhitaji misuli yako kutanuka na kusinyaa. Kitendo hiki huitaji mwili wako kuwa kwenye mwendo (movement).
Sasa ukisimama au kukaa muda mrefu, misuli yako haitanuki na kusinyaa, hivyo damu yako katika vena haitembei ipasavyo na baada ya muda miguu huvimba.
Hali hii huwatokea kwa haraka watu wenye umri kuanzia miaka 45 na kuendelea. Hutokea mara chache kwa vijana wadogo.
Kuzuia hali hii
Jitahidi kuwa unatembea walau kila baada ya lisaa na nusu, Mfano kwenda chooni au kwenda nje (kama upo kwenye kikao). Au kwenye Basi, jitahidi kutoka nje na kunyoosha miguu kidogo.
Ukipatwa na tatizo hilo basi ufikapo nyumbani jaribu kulala ukiwa umeinua miguu yako (leg elevation). Mara nyingi huwa sio shida kubwa.
Mwisho
Kuvimba miguu katika sababu ya kwanza na ya pili ni muhimu sana kwako kumuona daktari mapema. Epuka kuanzia kwa waganga, watakupotezea muda, hilo sio tatizo la kurogwa bali ni hitilafu ya mwili na mara nyingi hutibika vizuri.
Kuna sababu nyingine za kuvimba miguu na zingine uhitaji vipimo zaidi kugundua tatizo.
Angalizo: Kuvimba miguu kwa watoto inaweza kuwa dalili ya mapema ya utapiamlo. Ni vyema ukiona hali hii uwahi mapema hospitali ili mtoto aangaliwe.
Endelea kusoma makala zetu kuelimika zaidi. Ingia kwenye duka letu kupata vitabu vya afya vilivyoanadikwa kwa ajili yako na familia yako.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.
Imekaa powa Sana….
congratulations for ur kindness heart