Unaamka na Maumivu ya Mgongo Kila Asubuhi? Huenda Godoro Lako Lina Jibu!

Wiki iliyopita Rally Polyclinic tulipokea mgonjwa, kwa jina anaitwa Mr. Juma (si jina halisi), mwenye umri wa miaka 38. Ni mfanyakazi wa ofisini ambaye hutumia muda mwingi wa siku akiwa amekaa kwenye kompyuta. 

Alinilalamikia kuwa kila asubuhi anapoamka huhisi maumivu na kukakamaa sehemu ya chini ya mgongo. Anapojaribu kuinuka kitandani au kuinama kuvaa viatu, maumivu huongezeka na kumfanya atembee kwa shida kwa dakika chache. 

Hata hivyo, baada ya kuoga, kutembea na kufanya shughuli zake za kawaida, maumivu hupungua taratibu na wakati mwingine hupotea kabisa. Mchana na jioni hujisikia vizuri bila maumivu makubwa. 

Hali hii imeendelea kwa wiki kadhaa sasa, na nilipojaribu kumuuliza godoro analotumia ana muda gani nalo alinijibu kuwa amekuwa akilala kwenye godoro hilo kwa miaka kadhaa. 

Sababu hiyo ikanifanya kuanza kufikiria huenda tatizo ni godoro kuchakaa na kuamua kuja Rally Polyclinic kwa msaada. Nilimpokea na kumhudumia, pia nilimfundisha namna ya kukagua godoro lake kama lina ubora unatakiwa na aniletee majibu siku nyingine tutakapoonana.

Utafiti Unasema Nini?

    Utafiti uliochapishwa katika jarida la The Lancet mwaka 2003 ulihusisha watu wazima 313 wenye maumivu ya muda mrefu ya sehemu ya chini ya mgongo. Washiriki walitumia magodoro magumu au yenye ugumu wa wastani kwa siku 90.  

    Matokeo yalionyesha kuwa asilimia 82 ya waliotumia magodoro yenye ugumu wa wastani walipata nafuu wa maumivu, ikilinganishwa na asilimia 68 ya waliotumia magodoro magumu. 

    maumivu ya mgongo yaliyosababishwa na godoro baya

    Utafiti mwingine uliochapishwa mwaka 2021 ulihusisha vijana 366 wenye umri wa miaka 18 – 35. 

    Matokeo yalionyesha kuwa vijana 208 (sawa na 56.8%) walikuwa na maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo. Kati yao, 105 (50.4%) walikuwa hawajabadilisha magodoro yao kwa zaidi ya miaka mitatu. 

    Vile vile, utafiti mwingine uliofanyika mwaka 2023 kwa wagonjwa 130 wenye maumivu ya mgongo ulibaini uhusiano wa kitakwimu kati ya muda mrefu wa matumizi ya godoro na kuongezeka kwa ukali wa maumivu. 

    Aidha, utafiti wa mwaka 2009 uliohusisha watu wazima 59 ulibaini kuwa kubadilisha vitanda vya zamani kwa mifumo mipya ya kulalia kulihusishwa na kupungua kwa maumivu ya mgongo na kuboreka kwa usingizi. 

    Kwa Nini Mgongo Wangu Unauma Ninapoamka Asubuhi? 

      Je, umewahi kulala usiku mzima lakini unapoamka asubuhi unahisi maumivu ya mgongo, kukakamaa kwa misuli au uchovu wa mwili? Huenda ukajiuliza kama godoro lako linachangia hali hiyo. 

      Godoro ni sehemu muhimu ya mazingira ya kulala. Godoro lisilotoa msaada unaofaa kwa mwili linaweza kuongeza usumbufu wakati wa kulala na kuchangia maumivu ya mgongo kwa baadhi ya watu.  

      Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kwamba si kila maumivu ya mgongo husababishwa na godoro. 

      Kwa Nini Godoro Linaweza Kuchangia Maumivu ya Mgongo? 

        Wakati wa kulala, mwili unahitaji godoro linalosaidia kusambaza uzito wake vizuri na kuuweka mgongo katika mkao unaostarehesha (relaxation). 

        Godoro likiwa limechakaa, limezama katikati au ni laini sana kiasi cha kutounga mkono mwili ipasavyo, linaweza kufanya baadhi ya sehemu za mwili kuzama zaidi kuliko nyingine.  

        Hali hii inaweza kusababisha usumbufu na kuongeza maumivu kwa baadhi ya watu. 

        Vivyo hivyo, godoro gumu kupita kiasi linaweza kusababisha shinikizo kwenye mabega, nyonga na sehemu nyingine za mwili, na kufanya iwe vigumu kupata mkao wa kulala unaostarehesha. 

        Utafiti unaonyesha kwamba kwa watu wenye maumivu ya mgongo yasiyo maalumu, godoro la ugumu wa wastani (medium-firm) linaweza kusaidia zaidi kuliko godoro gumu sana.  

        Hata hivyo, mahitaji hutofautiana kulingana na mtu na chanzo cha maumivu. 

        Ni Mambo Gani Yanayochangia Maumivu ya Mgongo Wakati wa Kulala? 

          Mbali na ubora wa godoro, mambo yafuatayo yanaweza kuchangia maumivu ya mgongo: 

          1. Godoro Kuchakaa au Kuzama

          Godoro lililotumika kwa muda mrefu linaweza kupoteza uwezo wake wa kuusaidia mwili. Dalili zinaweza kujumuisha kuzama katikati, kutokuwa sawa au kuhisi sehemu fulani za mwili hazipati msaada wa kutosha. 

          Kwa mfano: Mr. Juma aliporudi awamu nyingine aliniambia kuwa godoro lake limedidimia katikati na akiamka huacha shimo mahali alipolala.  

          Hii inaweza kuwa sehemu ya kwanza ya kufikiria kama chanzo cha maumivu Juma anayoyahisi. 

          2. Ugumu au Ulaini Usiofaa

          Godoro linalomfanya mtu azame kupita kiasi au linalosababisha shinikizo kwenye nyonga na mabega linaweza kupunguza faraja (comfort) wakati wa kulala. 

          Kwa mfano:

          Kuna mgonjwa mwingine, kwa jina anaitwa Janeth (sio jina halisi), alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo kwa muda mrefu na akashauriwa kulala chini sakafuni kama tiba ya maumivu hayo.  

          Maumivu yalipungua kwa siku chache ila baada ya muda yaliongezeka zaidi ya ilivyokuwa mwanzo, ikamlazimu kuja Rally Polyclinic kwa uchunguzi na matibabu. 

          3. Mkao wa Kulala

          Kulala katika mkao unaoongeza maumivu kunaweza kuchangia usumbufu. Kwa mfano, baadhi ya watu hupata nafuu wanapolala ubavuni huku wakiweka mto kati ya magoti yao. 

          (Soma zaidi kuhusu mikao mbalimbali ya kulala kupitia “link hii“) 

          4. Kukaa Muda Mrefu na Kutofanya Mazoezi

          Kukaa kwa muda mrefu, kutofanya shughuli za mwili na udhaifu wa misuli inayosaidia mgongo vinaweza kuchangia maumivu, hata kama godoro ni zuri. Hivyo unapaswa kufanyiwa uchunguzi sahihi kujua chanzo cha maumivu unayoyapata. 

          5. Matatizo Mengine ya Kiafya

          Maumivu yanaweza pia kusababishwa na matatizo ya misuli, viungo vya uti wa mgongo, diski za uti wa mgongo au magonjwa mengine. Kwa hiyo, ni muhimu kutodhani kuwa godoro ndilo chanzo pekee. 

          Unaweza kufanya nini ili kupunguza maumivu ya mgongo yanayohusiana na godoro? 

            Suluhisho la 1: Chagua Godoro Linalounga Mkono Mwili Vizuri 

            Unaponunua godoro, zingatia uwezo wake wa kutoa support kwa mgongo na kukupa faraja. Kwa watu wengi wenye maumivu ya mgongo yasiyo maalumu, godoro la ugumu wa wastani linaweza kuwa mwanzo mzuri wa kujaribu hasa magodoro ya “orthopedic mattress”. 

            Usichague godoro kwa kuzingatia bei, unene au chapa pekee. Jaribu kulalia godoro kwa mkao unaotumia mara nyingi na uangalie kama mwili unapata msaada na faraja inayofaa. 

            Suluhisho la 2: Kagua Hali ya Godoro Lako 

            Angalia kama godoro limezama, limeharibika au lina sehemu zisizo sawa. Ikiwa halitoi msaada unaofaa na linaonekana kuchangia usumbufu, fanya maamuzi ya kulibadilisha. 

            Kumbuka kwamba hakuna muda mmoja unaofaa kwa kila godoro wa kulibadilisha; hali yake na uwezo wake wa kusaidia mwili ni muhimu zaidi. 

            Kwa mfano: Mgonjwa wangu Mr. Juma (jina sio halisi) aliponiambia hali ya godoro lake, mbali na matibabu mengine ya fiziotherapi kama vile ya joto, umeme, mikao sahihi awapo kazini na mazoezi maalumu, pia nilimshauri kubadilisha godoro na nikapendekeza “orthopedic mattress”.  

            Baada ya wiki moja, maumivu yalikuwa na unafuu mkubwa na yalipotea kabisa baada ya wiki mbili. 

            Suluhisho la 3: Rekebisha Mkao Wako wa Kulala 

            Unaweza kujaribu njia hizi: 

            • Kulala ubavuni: Weka mto kati ya magoti ili kusaidia nyonga na mgongo kuwa katika mkao unaostarehesha. 
            • Kulala chali: Jaribu kuweka mto chini ya magoti ili kupunguza usumbufu kwenye sehemu ya chini ya mgongo. 
            • Epuka mkao unaoongeza maumivu: Ikiwa mkao fulani unazidisha maumivu, jaribu mkao mwingine unaokupa faraja. 

            Soma zaidi kuhusu mikao ya kulala na mito ya kulalia kupitia makala yangu ya “Je, Ni Sahihi Kutumia Mto Wakati wa Kulala?“

            Suluhisho la 4: Endelea Kushughulisha Mwili Wako, Usipumzike Kupitiliza 

            Kutembea, kufanya mazoezi yanayofaa na kuepuka kukaa muda mrefu bila kusimama kunaweza kusaidia afya ya mgongo. 

            Mazoezi maalumu ya kuimarisha misuli na kuboresha unyumbufu yanaweza kusaidia baadhi ya watu. Chagua mazoezi yanayolingana na uwezo wako, na pata ushauri wa mtaalamu ikiwa maumivu ni makali au mazoezi yanaongeza maumivu.  

            Kulala sana au kupumzika kupitiliza kutokana na maumivu huongeza maumivu na kuongeza muda wa kupona. 

            Suluhisho la 5: Tafuta Uchunguzi wa Kitaalamu  

            Ikiwa maumivu yanaendelea, yanajirudia mara kwa mara au yanaathiri shughuli zako za kila siku, wasiliana na mtaalamu wa afya ili kubaini chanzo na kupata mpango sahihi wa matibabu. 

            Usinunue godoro jipya ukidhani litaponya kila aina ya maumivu ya mgongo. Godoro linaweza kusaidia kuboresha faraja, lakini matibabu yanapaswa kuzingatia chanzo halisi cha tatizo. 

            Ni wakati gani unapaswa kutafuta msaada wa kitaalamu? 

              Tafuta uchunguzi wa mtaalamu wa afya ikiwa: 

              • Maumivu ya mgongo yanaendelea kwa wiki kadhaa bila nafuu. 
              • Maumivu yanazidi au yanakuzuia kulala, kutembea au kufanya shughuli zako za kawaida. 
              • Maumivu yanaambatana na homa, kupungua uzito bila sababu au historia ya ugonjwa mkubwa. 
              • Maumivu yalianza baada ya kuanguka au kupata jeraha kubwa. 

              Nenda hospitalini haraka ikiwa maumivu ya mgongo yanaambatana na kushindwa kudhibiti mkojo au choo, kushindwa kukojoa, ganzi katika eneo la sehemu za siri au makalio, au udhaifu mpya au unaozidi wa miguu. Dalili hizi zinaweza kuashiria tatizo linalohitaji huduma ya dharura. 

              Muhimu: Kutoka kwa PT. Joseph Kisima

                Godoro bora si lazima liwe ghali zaidi au gumu zaidi. Jambo muhimu ni uwezo wake wa kuusaidia mwili vizuri na kukupa faraja wakati wa kulala. 

                Ikiwa una maumivu ya mgongo, kagua godoro lako, zingatia mkao wako wa kulala, endelea na shughuli za mwili zinazofaa, na tafuta ushauri wa kitaalamu ikiwa maumivu yanaendelea au yanaambatana na dalili za hatari. 

                Kulala vizuri ni sehemu ya kujitunza, lakini maumivu ya mgongo yanayodumu yanahitaji kutafutiwa chanzo na kutibiwa kwa usahihi.

                Wasiliana nasi leo kupitia simu namba +255 786 240 204 kwa ushauri kamili kutoka kwa wataalamu wetu.

                Leave a Comment

                Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

                swSW