Umuhimu wa Kupima Malaria Kabla ya Kuanza Matibabu

Naomba usome makala hii polepole na kwa utulivu sana, kwa sababu ninakuandikia wewe na sio orodha ya watu, wala takwimu za hospitali. 

Ninakuandikia wewe ambaye labda jana au wiki iliyopita umehisi mwili wako haupo sawa sababu unahisi maumivu ya kichwa, baridi kali, joto la ghafla, uchovu usioelezeka.

Unakaa chini na kujiuliza, “Nina nini hasa?

Na pengine, kama wengi wetu, umekimbilia duka la dawa au unamuomba jirani akupe dawa za malaria tu, au pengine unakunywa dawa za miti shamba bila kupima na ujajua sababu hasa ni nini.

Hilo ndio tatizo na leo ningependa tuzungumze hili kwa ukweli wote

Malaria na magonjwa mengine yanafanana sana. Huu ni ukweli ambao mara nyingi watu hawausemi wazi. Unapopata maumivu ya kichwa, homa, au mwili kuchoka, si lazima iwe malaria. 

Dalili hizo hizo zinaweza kuonekana kwenye magonjwa mengine kama typhoid, dengue, UTI, au hata mafua ya kawaida. Ndiyo maana hata daktari mwenye uzoefu hawezi kukutegemea kwa kukuangalia tu. Ili kupata jibu sahihi, anahitaji kipimo kwanza!

“Unapoanza kutumia dawa za malaria bila kupima, unajitibu ugonjwa ambao huenda hata haupo kwenye mwili wako”

Fikiria hivi: Unaenda hospitali ukiwa na maumivu ya tumbo, halafu unapewa dawa ya kikohozi bila kufanyiwa hata kipimo kimoja. Unaweza kuhisi nafuu kidogo, lakini chanzo cha tatizo bado kipo.

Hivyo ndivyo inavyotokea unapopewa dawa za malaria wakati ugonjwa wako ni typhoid, au unapewa za typhoid wakati una malaria. Unatibu kitu kisicho sahihi, na ugonjwa halisi unaendelea.

Dawa za malaria zina nguvu na hufanya kazi vizuri unapozitumia kwa kutibu Malaria tu. 

Lakini nguvu hiyo inakuja na tahadhari…

Unapomeza dawa hizi bila kupima, unalazimisha mwili wako kubeba dawa nzito wakati hujui ugonjwa uliopo. Watu wengine hupata kichefuchefu, kizunguzungu, maumivu ya tumbo, au mapigo ya moyo kwenda kasi ambayo siyo kawaida. Mwili unapata mzigo bila sababu ya msingi.

Changamoto kubwa zaidi ipo nyuma ya pazia. Vimelea vya malaria hubadilika polepole. Kila mara dawa hizi zinapotumika bila ulazima, vimelea hupata nafasi ya kujifunza jinsi ya kuziepuka. Baada ya muda, dawa ambazo leo zinaokoa maisha zinaweza kushindwa kufanya kazi vizuri.

Hapo ndipo hatari halisi huanza

Uamuzi mdogo wa leo wa kunywa dawa bila kipimo haukuathiri wewe peke yako bali  unaweza kuchangia tatizo kubwa zaidi litakalowagusa watu wengi baadaye.

Kupima Malaria  ni bure wala haichukui muda

Najua unachoweza kusema: “Hospitali iko mbali. Nina kazi nyingi. Pesa ya usafiri sina.” 

Ninaelewa hilo. Lakini ukweli ni kwamba  kipimo cha malaria – Malaria Rapid Diagnostic Test  (mRDT) kinaweza kutoa jibu ndani ya dakika 15 na vinatolewa bila malipo yoyote na majibu ya vipimo unapatiwa mara moja na yanakuambia kama una malaria au hauna. Hapo ndipo matibabu sahihi yanaanza.

Hapa ndipo Malaria ya kweli inahitaji matibabu ya kweli

Upande mwingine wa jambo hili ni muhimu pia. Malaria isipotibiwa kwa wakati inaweza kuwa hatari sana. Aina ya Plasmodium falciparum, inayopatikana sana Afrika Mashariki, inaweza kubadilika haraka na kumfanya mgonjwa kuwa mahututi ndani ya muda mfupi.

Unaweza kuona mtu anaanza na homa ya kawaida tu, lakini baada ya muda mfupi hali inazidi kuwa mbaya. Mwili unadhoofika, kupumua kunakuwa shida, kizunguzungu kinaongezeka, na wakati mwingine hali inafika hatua ya hatari kubwa sana. Watoto wadogo, wajawazito, na watu wenye magonjwa mengine wako kwenye hatari zaidi.

Ndiyo maana kupima si suala la kuepuka dawa zisizo za lazima tu. Ni pia njia ya kuhakikisha unapopata Malaria kweli, unapata matibabu sahihi mapema kabla hali haijawa mbaya.

Nini Kifanyike Ukihisi Dalili?

Jibu ni moja tu, nenda kapime! Usisubiri hali kuwa mbaya. 

Usimuombe jirani akupe dawa zake na wala usiamini tu kwa sababu mtu mwingine alikuwa na homa akatibiwa malaria, eti na kwako itakuwa hivyo hivyo.

Ukifanyiwa kipimo na ikaonekana una Malaria, fuata maelekezo ya mtaalam wa afya  kama yalivyo. Maliza dozi yote kwa siku zote ulizoandikiwa. Usiache katikati hata kama unaanza kujisikia vizuri.

Kama kipimo kinaonyesha huna malaria, maana yake chanzo cha dalili zako ni kingine. Hapo unahitaji uchunguzi zaidi, na daktari au mtaalam wa afya atakusaidia kuelewa tatizo halisi lilipo.

Mwisho

Katika kuadhimisha siku ya Malaria Duniani kote ambayo ni  Tarehe 25 Aprili, inayoambatana na kauli mbiu ya“Tumedhamiria kutokomeza Malaria, Wakati ni sasa, Tunaweza”, weka nadhiri kutoka moyoni kwamba kuanzia sasa unadhamiria kwamba hautatumia dawa ya Malaria bila kupima, kwasababu wakati sahihi wa kufanya hilo jambo ni sasa na kwasababu ni nadhiri basi utaweza.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW