Kumekuwa na kampeni nyingi za kuhamasisha watu kuchangia damu kwa hiari. Mara nyingi, mtu anapokuwa ana mgonjwa hospitali anayehitaji damu, ndugu wanahamasishwa kuchangia damu ili kuweza kurejesha ile ambayo mgonjwa wao amepatiwa.
Je, umeshawahi kujiuliza ni kwanini damu inahitajika kila siku? Na kuchangia damu kuna athari gani mwilini mwako?
Hali kadhalika mgonjwa wako anapopokea damu, nini kinatokea?
Kwanini Unashauriwa Kuchangia Damu?
Kuchangia damu ni kitendo cha hiari kinachohusisha utoaji wa sehemu ya damu yako ambayo itakusanywa, kupimwa, na kutumika kwa mgonjwa anayehitaji.
Damu inahitajika sana kwa watu wanaofanyiwa upasuaji (operation) mkubwa, walioumia na kupata ajali zinazosababisha kupoteza damu nyingi, wanaoishi na maradhi ya damu kama vile sickle cell, upungufu wa damu na wagonjwa wa kansa, magonjwa ya ini, wajawazito, watoto, n.k.
Kila chupa ya damu unayochangia inatenganishwa katika sehemu tatu zenye matumizi tofauti na zinaweza kuongezwa kwa watu wenye mahitaji tofauti ya kuongezwa damu, ambazo ni; seli hai nyekundu, seli sahani na plasma.
Hivo basi kuchangia chupa moja ya damu inaweza kusaidia kuokoa maisha ya watu watatu tofauti ndio maana utasikia taasisi nyingi, pamoja na serikali, zinahimiza sana watu kuchangia damu.
Nani Anaweza Kuchangia Damu?
Watu wengi, kwa jinsia zote, kati ya umri wa miaka 17 hadi 65 wana uwezo wa kuchangia damu. Japokuwa wanaume wana damu iliyo sawa kipindi chote cha maisha yao tofauti na wanawake ambapo kiwango na wingi au uchache wa seli mbalimbali katika damu yao unabadilika kipindi cha hedhi, wakati wa ujauzito na kunyonyesha.
Kwa mantiki hiyo Mwanamke anaweza kuchangia damu kila baada ya miezi minne na mwanaume anaweza kuchangia kila baada ya miezi mitatu.
Kwa ujumla wafuatao wanaweza kuchangia damu kwa Tanzania:
- Mwanamke au mwanaume mwenye umri kati ya miaka 18 na 65.
- Mwanamke asiwe mjamzito au ananyonyesha
- Mtu asiwe na magonjwa ya muda mrefu kama vile kisukari, presha, kifafa, n.k
- Uzito juu ya kilo 50.
- Asiwe anaumwa homa au ugonjwa au kutumia dawa kipindi cha kutoa damu.
- Asiwe na mazingira hatarishi ya kupata maradhi kama UKIMWI, Homa ya Ini n.k.
- Asiwe ameongezewa damu au kupandikizwa kiungo cha mwili kama vile ini, figo, moyo n.k
- Asiwe anajidunga dawa kama vile za kuongeza misuli ya mwili au kupendezesha ngozi.
Ninawezaje Kuchangia Damu?
Unaweza kutembelea kituo cha kutoa huduma za afya mbalimbali chenye huduma za kuchangia damu au kushiriki kampeni zinazotangazwa na serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS).
Baada ya kutoa ridhaa ya kuchangia damu kuna vipimo vya awali vitafanyika, kama vile:
- Wingi wa damu – mwenye damu ndogo chini ya 13g/dl kwa wanaume na 12.5 g/dl kwa wanawake hawachangii damu
- Uzito – chini ya 50 kg hairuhusiwi kuchangia damu
- Shinikizo la damu – Presha ikiwa juu ya 180 mmHg au chini ya 90mmHg wakati wa kuchangia damu, pia hairuhusiwi kutoa damu kwa wakati huo.
Baada ya vipimo na kuwa na sifa stahiki za kuchangia damu, utawekwa kwenye kiti au kitanda maalum. Taarifa zako muhimu kama jina, umri, unapoishi, n.k zitachukuliwa kwa kumbukumbu.
Kisha mkono utaotoa damu utakaguliwa na kufungwa mkanda wa kusaidia kusukuma damu.
Mfuko wa kukusanya damu utaunganishwa kwenye sindano iliyowekwa mkononi kwako; mfuko ambao unakua na namba maalum ya mchangiaji. Damu itaacha kutolewa pale utakapochangia 470 mL (chini ya nusu lita).
Kwa kawaida zoezi linakamilika ndani ya dakika 5 mpaka 10. Hautakiwi kujisikia hali yoyote au maumivu wakati wa zoezi hili, hivyo ni muhimu kuwasiliana na mtoa huduma pindi utakaposikia hali ya tofauti wakati wa kutoa damu.
Ni Zipi Faida za Kuchangia Damu?
Faida kubwa ya kuchangia damu ni kuokoa maisha. Chupa moja ya damu unayochangia inaweza kuokoa maisha ya watu hadi watatu.
Tanzania inakadiriwa kuhitaji takriban chupa 550,000 za damu kila mwaka wakati uchangiaji umefikia chupa 330,000 tu! Ni sawa na upungufu wa 40% wa mahitaji ya damu nchini (NBTS – 2020/21).
Mimi kama mchangiaji nitapata faida gani kupitia mchakato huu wa uchangiaji damu?
1. Kupata vipimo vya afya kwa wakati mmoja bure
Uchunguzi wa damu yako utaendelea baada ya kutoa damu ili kuona kama inafaa kupewa mtu mwingine. Kati ya vipimo vinavyofanyika ni pamoja na Kiwango cha damu, UKIMWI (VVU), Kaswende, Homa ya Ini (Hepatitis B na C), na Makundi ya Damu.
Majibu ya vipimo hivi utapatiwa, kwa usiri mkubwa, wewe mwenyewe – bila kuambiwa mtu mwingine yoyote.
2. Kurekebisha kiwango cha madini chuma mwilini
kuchangia damu kunazuia mwili wako kuwa na uhifadhi wa madini chuma uliopitiliza (madini muhimu katika seli nyekundu za damu).
Madini chuma yakizidi yanahatarisha afya ya ini, moyo na kongosho hivyo kuchangia damu kunalinda hivi viungo muhimu.
3. Kusaidia mzunguko wa damu
Damu ni mujumuiko wa seli, protini mbalimbali na maji, ndani na nje ya mishipa ya damu.
Unapochangia damu kunakua na mzunguko wa maji na ubadilishaji wa viambata mwilini na kuchochea mzunguko mzuri wa damu.
4. Kupata kusudi na kujitolea
Kuchangia damu kunaleta hali ya kujisikia vizuri na kuridhika katika kusaidia wengine. Hii inasaidia kuwa na mood nzuri, kupunguza mawazo na kuwa na afya ya njema ya akili.
5. Kuchangia ustawi wa jamii
Kuchangia damu hakutakupa faida binafsi pekee, bali utaokoa pia maisha ya wajawazito, watoto, wagonjwa wa kansa, na waliopata ajali; ni mchango mkubwa sana katika ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.
Nini Kinatokea (Athari) Mwilini Baada ya Kuchangia Damu?
Mara baada ya kuchangia damu, mwili unaanza mchakato wa kurejesha kiasi cha damu kilichotolewa. Maji kati ya seli (yana virutubisho na baadhi ya viambata muhimu vya damu kama madini chuma) mwilini yanaanza kuingia katika mzunguko wa damu.
Kiasi cha ujzao wa damu huanza kurejea kwa kasi kati ya 9 mls – 120 mls kwa saa ndani ya masaa mawili ya kwanza na kupungua kuwa 40mls -60 mls ndani ya masaa 6 hadi 10 yanayofuata.
Baada ya masaa 30-40 ujazo wa damu unakua umekamilika, na ndio maana inashauriwa kurejea kwenye shughuli nzito kama mazoezi/michezo na kunyanyua vitu vizito angalau saa 48 baada ya kuchangia damu ili kuupa mwili muda kurejesha kiwango cha damu cha awali.
Kurejea kwa seli nyekundu za damu kunachukua muda mrefu kidogo. Kunakua na ongezeko la seli nyekundu changa ambazo hazijakomaa kwenye mzunguko katika siku 10 za kwanza baada ya kutoa damu. Na kufikia wiki 4 na zaidi, wingi wa seli unarejea katika kiwango chake cha awali kabla ya kuchangia damu.
Hii inatofautiana na mtu kulingana na kiasi cha seli kilichochoka mwilini wakati wa kuchangia, kiwango cha chakula (na maji) unachotumia.
Wachangiaji wengi wanahimili kuchangia damu bila kujisikia hali yoyote baadae. Na kawaida kiasi cha damu kinachotolewa hakizidi 15% ya ujazo wa damu mwilini mwako.
Zaidi ya hiyo, unapojisikia hali ya tofauti wakati wa kuchangia damu, toa taarifa kwa mtoa huduma ya afya. Huwa wako tayari muda wote kusaidia mabadiliko yanayojitokeza.
Hata hivyo hizi ni kati ya athari zinazoweza kujitokeza wakati wa kuchangia damu:
Kuzimia kwa hofu au mshtuko: Hii inasababishwa aidha na kuona damu, kuona wengine wakitoa damu au mshtuko wa mwili. Dalili zake ni pamoja na uchovu, kizunguzungu, kutoka jasho, kupoteza fahamu, kutokwa haja ndogo au kubwa bila kukusudia.
Kichefuchefu na Kutapika: Mwili unaweza kupata mshtuko wa ghafla unaosababisha kushuka kwa shinikizo la damu na kupelekea kichefuchefu na kutapika. Ikitokea hivi lala ubavu na vuta hewa kwa nguvu, taratibu taratibu.
Kuvilia damu: Sehemu ambayo sindano imeingizwa kwa ajili ya kutoa damu inaweza kuvimba na kuvia damu. Kwa kawaida sindano itatolewa na kugandamiza eneo hilo; baada ya muda huisha yenyewe.
Kutoboa mishipa ya ateri: Damu inatoloewa katika mishipa ya vein, lakini napotokea damu inaruka kwa kasi, nyekundu sana na inatoka kwa kuambatana na maumivu inawezekana ni msipa wa ateri umeguswa. Sindano itatolewa mara moja na kupewa msaada wa kitaalamu.
Mwisho
Naamini utakua umejifunza kitu kwenye makala hii fupi; kwa maswali na maoni, tafadhali naomba uniandikie kwenye comments section au unitumie ujumbe kupitia barua pepe yangu.
Makala yangu ijayo itahusu “Sababu zinazoweza kukupelekea kuhitaji huduma ya damu ya ziada na nini hutokea mwilini baada ya kupokea damu”. Unaweza kuisoma kwa kubonyeza hapa!

Analytical, energetic, and detail-oriented medical doctor and researcher with experience supporting qualitative and quantitative research-related activities. My skill set spans from conducting interviews, coding qualitative data materials, and analyzing qualitative and quantitative data materials as well as English- Swahili transcription and translation.
Also, I have experience in stakeholder meetings, workshop facilitations, evidenced-based dissemination and policy and strategic planning.
