Nani Mwenye Jukumu la kudhibiti Malaria Kwenye Jamii Yangu?

Kama Baba Mateso angekuwa ananunua dawa ya mbu ya kuchoma mara kwa mara, familia hii tusingekuwa na Malaria!”  Mama Mateso akiwa analalamika. 

Unatamani umuulize swali: Jukumu la kukinga familia dhidi ya malaria ni la nani?  

Mama Mateso ni mama wa familia na Mwenyekiti wa Mtaa wa kiongoleni, Kata ya Goba. Familia yake inawindwa sana na Malaria na mwanae amelazwa mara mbili ndani ya miezi mitatu kwa sababu ya malaria. Hajawahi kudhani kwamba yeye anapaswa kupambana na Malaria bali ni mume wake. 

Hayuko peke yake, wananchi wengi pia huamini kwamba serikali ndio yenye jukumu la kupambana na malaria, sio wao. Mtazamo kama huu ndio chanzo cha kutofikia mpango wa Ziro Malaria mapema.

Jukumu la kudhibiti malaria ni la kila mwanafamilia na mwana jamii kulingana na nafasi yake aliyonayo. Hebu kwanza tuangalie chanzo cha mbu waenezao Malaria halafu tujue kila mwanajamii anaweza kushiriki vipi.

Mbu aina ya Anofelesi Jike ndio hueneza vimelea vya  ugonjwa wa Malaria, mbu hawa hupata nafasi ya kukuuma kutokana na sababu hizi:

  1. Kulala kwenye chandarua kisicho na dawa au kutotumia chandarua kabisa kwa walio wengi.
  2. Mazingira machafu yenye maji yaliyotuama au nyasi ndefu ambazo huruhusu mbu kutaga, kuzaliana kwa wingi na hivyo kuwauma na kuleta Malaria.
  3. Kuacha milango na madirisha wazi nyakati  za jioni na usiku.
  4. Dhana potofu juu ya malaria kwa kuonekana kama ni mapepo na haihitaji matibabu ya Hospitalini. . Hii hufanya wanajamii wasijifunze zaidi kuhusu mbinu za kupambana na Malaria.
  5. Kukaa nje wakati wa jioni na usiku bila kufunika mwili wako.

Sasa hebu tazama visababishi hivi, huoni nafasi yako katika kupambana na Malaria?

Mama Mateso ana jukumu kubwa la kuilinda familia pamoja na wananchi wake dhidi ya  Malaria kwa kuhakikisha anahamasisha wanafamilia na jamii kufanya  mambo kadhaa.

Akihakikisha mazingira ya nyumba yake ni masafi, hayana maji  yaliyotuama kwa muda mrefu, hamna nyasi ndefu au hamna vifaa vyovyote vinavyoweza kusababisha maji kutuama kama vile vifuu vya nazi, makopo,chupa au matairi ya gari yasiyotumika karibu na nyumba, mbu watazaliana wapi? 

Maana yake ni swala la usafi na utunzaji wa mazingira tu hapa amabalo ni jukumu lake na halipaswi kumsubiri Mume wake.

Wewe unayesoma makala hii ukihakikisha familia yako inalala ndani ya chandarua chenye dawa kila siku, unafunga milango na madirisha mapema au kuweka nyavu kwenye madirisha na milango kuzuia mbu, Malaria itatokea wapi? Maana yake ni swala la kuwa muwajibikaji tu hapa.

Ukihakikisha unatunza mazingira na kudhibiti mazalia ya mbu, Malaria itatoka wapi?

Mama Mateso ni mwenyekiti wa mtaa na anahudhuria vikao mbalimbali vya serikali vinavyosisitiza mapambano dhidi ya Malaria, akiweza kutoa elimu hii kwa watu anaowaongoza ili nao walinde familia zao dhidi ya Malaria tutaona mabadiliko makubwa kwenye jamii.

Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) imeendelea kupambana na Malaria hasa kwa wajawazito na watoto kwa kuhakikisha kila mama mjamzito anapata chandarua kila wanapohudhuria udhurio la kwanza kliniki pamoja na kupatiwa dawa ya kujikinga na malaria (SP).

Vilevile vyandarua vyenye dawa hugawiwa kwa watoto wanapofikisha umri wa miezi 9 (wakati wa kupatiwa chanjo ya surua lubella.

Kupitia kampeni   ya “Ziro Malaria Inaanza na Mimi,” Wizara imefanikiwa kuongeza uelewa wa wananchi juu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria ikiwemo utunzaji wa mazingira, umuhimu wa kupima kabla ya kutumia dawa pamoja na kuzingatia tiba sahihi ya malaria.

Kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria katika jamii kimepungua  kwa takribani asilimia 30 kutoka asilimia 8.1 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 5.7 mwaka 2025. Lengo ikiwa ni kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria na hatimae kufikia Ziro Malaria ifikapo mwaka 2030.

Tukiwa tunaadhimisha siku ya Malaria Dunia ambayo huazimishwa tarehe 25 Aprili kila mwaka ambapo kwa mwaka  huu 2026,  Kauli mbiu inasema “Tumedhamiria Kutokomeza Malaria, Wakati ni Sasa, Tunaweza”.

Hivyo basi tuendeleze mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa kuhakisha jamii inashiriki ipasavyo katika mapambano dhidi ya malaria na kuhakikisha tunafikia lengo la kutokomeza malaria nchini.

Mwisho

Fanya wajibu wako kama mwana jamii na serikali ifanye kazi yake, halafu tukutane katikati Malaria ikiwa imefika ziro. Ungependa kujifunza zaidi kuhusu njia za kujikinga na Malaria? Soma makala yangu ya “Njia Kuu 4 za Kujikinga na Malaria”.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW