“Daktari nina kikohozi cha zaidi ya wiki mbili sasa na nikikohoa makohozi yanatoka yaliochanganyika na damu, pamoja na kuchoka mwili, vilevile nikilala usiku natokwa na jasho sana”

Hiyo hapo juu ni nukuu ya maelezo ya mgonjwa mmoja alipoamua kufika hospitali baada ya kujaribu kutibu kikohozi kwa zaidi ya wiki mbili bila kupona, alizidi kuona hali yake inakuwa mbaya zaidi.
Baada ya maelezo yake kueleweka, uchunguzi na vipimo kufanyika, aligundulika kuwa anasumbuliwa na maambukizi ya kifua kikuu (TB) na bila kuchelewa alianza hatua muhimu za matibabu.
Kwanza, alipatiwa elimu kuhusu ugonjwa wake na umuhimu wa kutumia dawa kila siku bila kuruka. Kisha akaanzishiwa dawa za kifua kikuu (TB) kulingana na mwongozo wa matibabu.
Pili, kwa mujibu wa muongozo wa Shirika la Afya Dunia (WHO) na National Tuberculosis and Leprosy Program (NTLP) Tanzania, matibabu ya kifua kikuu hufuata hatua mbili kuu:
1. Hatua ya mwanzo: Miezi 2
Mgonjwa huanza na dawa nne kwa pamoja kila siku. Na Mgojwa huyu alipatiwa hizo dawa na kuanza kutumia. Hizi dawa kazi yake ni kupunguza bakteria haraka mwilini na kupunguza maambukizi.
2. Hatua ya pili: Miezi 4
Baada ya hapo mgonjwa huendelea na dawa mbili. Mgonjwa huyu alipatiwa hizo dawa na kuanza kuzitumia.
Hii husaidia kuua bakteria waliobaki na kuhakikisha ugonjwa haujirudii.
Katika kipindi chote cha matibabu, mgonjwa hufuatiliwa na wahudumu wa afya ili kuhakikisha anatumia dawa vizuri. Baada ya kumaliza miezi sita, mgonjwa hupimwa tena ili kuthibitisha kama amepona.
Mgonjwa huyu alifuata maelekezo yote, alimeza dawa kila siku bila kuruka, na baada ya miezi sita alipimwa tena na kuonekana hana tena kifua kikuu (TB). Alipona kabisa.
Hii inaonyesha kuwa kifua kikuu (TB) kinatibika. Zaidi ya watu 90 kati ya 100 wanaofuata matibabu sahihi na kumaliza dawa hupona kabisa.
Mambo yanayochangia kupona ni pamoja na:
● Kuanza matibabu mapema
● Kutumia dawa kila siku bila kuruka
● Kumaliza dozi yote
● Kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya
Mambo yanayochangia kutopona ni:
● Kuacha dawa katikati
● Kusahau dozi mara kwa mara
● Kuchelewa kuanza matibabu
● Kupuuza ushauri wa wataalamu wa afya
Vilevile, ni muhimu sana kujua kuwa si kila mtu mwenye bakteria wa kifua kikuu (TB) huugua. Wengine hubaki nao mwilini bila dalili na ugonjwa huanza pale kinga ya mwili inaposhuka.
Hivyo kama una kikohozi cha zaidi ya wiki mbili, au dalili kama kutokwa jasho sana wakati wa usiku na kupungua uzito, usisubiri.
Nenda hospitali ukapimwe mapema na ukigundulika kuwa una maambukizi ya kifua kikuu, anza dawa mara moja na malizia dozi.
“Kumbuka, kifua kikuu kinatibika. Anza matibabu mapema, maliza dawa zako, na utaweza kupona kabisa”.
Je, una ndugu au mtu wa karibu aliyegundulika na kifua kikuu lakini hajaanza dawa au hajaimaliza?
Usikae Kimya! Msaidie afike mapema kituo cha afya cha karibu ili aanze au aendelee na matibabu.
Hii itamsaidia kupona na kuepuka madhara kama kuharibika kwa mapafu, kuenea kwa ugonjwa kwenye viungo vingine, au kufanya dawa kushindwa kufanya kazi.
Kuchelewa au kuacha dawa katikati kunaweza kufanya ugonjwa kuwa mgumu kutibika na kuongeza hatari ya kuambukiza wengine.
Kwa maelezo zaidi na ushauri sahihi, tembelea kituo cha afya kilicho karibu nawe.
I am a healthcare provider. I focus on sharing clear, evidence based health information through articles and social media.
My goal is to help you understand healthily life. I believe accurate health information improves decisions and lives.
