Je, umewahi kuamka asubuhi na ulipoweka mguu chini kupiga hatua ya kwanza, ukasikia maumivu makali ya kuchoma kwenye kisigino chako?
Au labda baada ya kukaa kwa muda mrefu unaposimama unahisi kama unakanyaga kigingi au sindano chini ya kisigino?

Katika jamii yetu, watu wengi wakipatwa na changamoto hii wanakimbilia kuamini kuwa ni maumivu ya “asidi kujaa mwilini”, “dalili ya uchawi”, au “tatizo la figo”.
Hata hivyo, kisayansi na kitiba, maumivu haya mara nyingi husababishwa na hali inayojulikana kama Plantar Fasciitis.
1. Plantar Fasciitis ni Nini?
Chini ya mguu wako kuna utepe au utando mpana na imara wa tishu unaoitwa Plantar Fascia. Utando huu unaunganisha mfupa wa kisigino (calcaneus) na vidole vya mguu. Kazi yake kuu ni:
- Kubeba uzito wa mwili mzima unapotembea au kukimbia.
- Kufanya kazi kama chemchemi (shock absorber) inayopunguza mshituko kwenye mguu.
- Kuupa mguu wako umbo la stendi au upinde (arch of the foot).
Inapotokea kwamba utando huu unavutika au kupata msongo uliopiliza mara kwa mara, husababishwa mijeraha midogo midogo (micro-tears) na uvimbe (inflammation).
Matokeo yake ni maumivu makali, hasa pale unapoanza kutembea baada ya kupumzika.
2. Dalili Kuu za Maumivu ya Kisigino
Maumivu Makali Asubuhi
Maumivu kuwa makali zaidi unapoamka kitandani na kupiga hatua za kwanza, au unaposimama baada ya kukaa muda mrefu.
Auuena Bafuni / Baada ya Mazoezi
Unapotembea kidogo, maumivu yanaweza kupungua kwa sababu misuli inapata joto, lakini hurudi tena baada ya kukaa au baada ya kukamilisha mazoezi.
Maumivu Unapovuta Vidole Juu
Unapojaribu kuvuta vidole vya mguu kuelekea mwilini kwako, maumivu ya kisigino huongezeka.
3. Nani Yuko Kwenye Hatari Zaidi ya Kupata Tatizo Hili?
Watu Wanaoajiriwa/Kufanya Kazi za Kusimama Muda Mrefu: Walimu, askari, wafanyakazi wa viwandani, na wahudumu wa migahawa/mabar.
Wenye Uzito Mkubwa wa Mwili: Uzito wa ziada huongeza msukumo na shinikizo kwenye utando wa plantar fascia.
Aina ya Viatu: Kutumia viatu vilivyo bapa sana visivyo na sponji (flat shoes), viatu vya kisigino kirefu sana (high heels), au viatu vilivyochakaa chini.
Watu Wanaofanya Mazoezi Bila Maandalizi: Wanaokimbia sana ghafla au kubadilisha uwanja wa mazoezi (kama kutoka kwenye nyasi kwenda kwenye lami) bila kutoa muda kwa mguu kuzoea.
Anatomy ya Mguu: Mtu mwenye mguu ulio bapa kabisa (flat feet) au mwenye upinde wa mguu uliorudi juu sana (high arch).
4. Jinsi Physiotherapist Anavyoweza Kusaidia (Tiba Viungo)
Watu wengi hujaribu kutatua maumivu haya kwa kumeza dawa za kutuliza maumivu (painkillers) kila siku.
Dawa hizi zinaweza kupunguza maumivu kwa muda, lakini hazitatui chanzo cha tatizo. Hapa ndipo mtaalamu wa tiba viungo (physiotherapist) anapohusika:
Kufanya Tathmini ya Biomechanics ya Mguu: Physiotherapist ataangalia mkao wa mguu wako (foot posture), mtembeo wako, na uimara wa misuli ya paja na ugoko ili kubaini kwanini kisigino kinapata shinikizo kubwa.
Mazoezi ya Kuvuta Kano na Misuli (Stretching Exercises): Physio atakufundisha mazoezi mahsusi ya kuvuta kano za nyuma ya mguu (Calf stretch) na kano ya chini ya kisigino (Plantar fascia stretch) ili kupunguza msukumo na kurudisha unyumbulifu.
Mazoezi ya Imara ya Misuli (Strengthening): Kujenga uimara wa misuli midogo midogo ya ndani ya mguu (intrinsic foot muscles) na misuli ya kifundo cha mguu (ankle) ili kuboresha msaada wa uzito wa mwili.
Tiba ya Mikono (Manual Therapy & Soft Tissue Release): Physio hutumia mbinu za kukanda kwa utaalamu (soft tissue mobilization) kwenye misuli ya ugoko (calf muscles) na chini ya mguu ili kuachanisha misuli iliyokaza na kuboresha mzunguko wa damu.
Ushauri wa Viatu na Insoles (Footwear & Orthotics): Physio atakushauri aina sahihi ya viatu kulingana na muundo wa mguu wako, au kupendekeza soli za ziada (arch supports/orthotics) za kuweka kwenye viatu ili kupunguza presha kwenye kisigino.
Mbinu Nyepesi za Kujisaidia Nyumbani (Self-Care Tips)
- Zoezi la Chupa ya Maji ya Baridi: Chukua chupa ya plastiki yenye maji yaliyoganda (barafu), iweke chini ya mguu kisha weka mguu juu yake na uirudishe mbele na nyuma kwa dakika 10-15. Hii husaidia kupunguza uvimbe na maumivu.
- Kuvuta Mguu Kabla Hujashuka Kitandani: Unapoamka asubuhi, kabla hujakanyaga chini, tumia kitambaa au mikono yako kuvuta vidole vya mguu kuelekea mwilini kwako na kushikilia kwa sekunde 20-30.
- Punguza Viatu Bapa Sana au Vya Kisigino Kirefu: Epuka kutembea peku kwenye sakafu ngumu, tumia ndala zenye sponji unakapokuwa nyumbani.
Hitimisho
Maumivu ya kisigino siyo tatizo la kutishia maisha, lakini yakipuuzwa yanaweza kubadilisha mtembeo wako na kusababisha maumivu ya magoti, nyonga, na mgongo baadaye.
Badala ya kutegemea vidonge vya maumivu kila siku, muone mtaalamu wa Physiotherapy akusaidie kurudisha afya na mtembeo wako sahihi.
UNAHITAJI TIBA NA USHAURI WA KITAALAMU?
Unasumbuliwa na maumivu ya kisigino, viungo, au mgongo? Weka miadi (Consultation Session) na Mtaalamu wa Tiba Viungo (Physiotherapist), kupitia simu namba/WhatsApp +255 686 552 952, upate tathmini ya kina na programu maalum ya mazoezi ya kuondoa tatizo lako kabisa.

Erick Myenda ni mtaalamu wa physiotherapy (physiotherapist) na mwelimishaji wa afya mwenye shauku ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu physiotherapy, urekebishaji wa uwezo wa mwili na afya ya jamii kupitia elimu inayozingatia ushahidi wa kisayansi.
Maeneo yake ya kuvutiwa kitaaluma ni pamoja na afya ya misuli na viungo, udhibiti wa maumivu, urekebishaji wa uwezo wa mwili, afya ya uzee na uhamasishaji wa afya. Kupitia makala zake, analenga kuunganisha maarifa ya kitaalamu ya afya na maisha ya kila siku kwa kuwasilisha taarifa sahihi kwa lugha rahisi, inayoeleweka na inayoweza kutumika katika vitendo.
Kama mtaalamu wa physiotherapy na mwelimishaji wa afya, Mr. Erick analenga kuwasaidia watu na jamii kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao, kutambua changamoto zinazoweza kuhitaji tathmini ya kitaalamu na kuelewa mchango wa physiotherapy katika kuboresha uwezo wa kufanya shughuli za kila siku na ubora wa maisha.
