Watu wengi sana tuna Google dalili tulizonazo kabla na baada ya kwenda hospitali, bila shaka hii inaweza kuwa njia ya kuokoa muda, lakini kwa upande mwingine wa shilingi, hatua hii ni hatari kwa Afya yako.

Fikiria ni usiku wa manane unashtuka kutoka usingizini, na kinachokupokea cha kwanza ni maumivu makali ya kichwa. Na badala ya kupiga simu kwa Daktari au kwenda kituo cha Afya unachukua simu yako iliyokuwa pembeni yako na unafungua Google na kuandika “maumivu makali sana ya kichwa wakati wa usiku”.
Ndani ya sekunde chache, screen yako imejaa kurasa mbalimbali za majibu na ushauri. Na bila shaka wengi wao wanakwambia majibu mabaya na makali zaidi kuliko hata yale ulioyatarajia.
Google inaweza kukwambia kuwa una uvimbe kwenye kichwa, lakini Daktari atakwambia ni kwasababu ya hali ya mafua uliyonayo.
Sasa ngoja nikwambie kidogo kuhusu Google: GOOGLE ni chombo cha kutafuta taarifa na wala si Daktari. Algorizimu zake zinafanya kazi kwa kukuonyesha maudhui yanayolingana na maneno unayoyaandika, si kwa kuchunguza mwili wako, historia yako ya kiafya, umri wako, au hali yako ya sasa.
Unapoandika “maumivu ya kichwa,” Google hajui kama una msongo wa mawazo au kama una mafua pia.
Google ina tatizo kubwa moja ambalo kitaalamu huitwa “availability bias”. Ni kama ubaguzi wa upatikanaji wa taarifa kwa maana ya kwamba taarifa nyingi zinazopatikana mtandaoni huhusisha hali mbaya au za kushangaza kama saratani, ugonjwa wa moyo, maambukizo ya hatari sana.
Hii ni kwasababu tovuti/blogu nyingi zinaandika maudhui yanayovutia wasomaji. Hali za kawaida kama “uchovu wa kawaida” hazifatiliwi lakini pia haziandikwi sana.
Hatari Kuu 5 za Kujitibu Kupitia Google
1. Utambuzi Potofu (Misdiagnosis): Dalili moja inaweza kuashiria magonjwa kumi tofauti. Google hawezi kufanya uchunguzi wa damu, X-ray, au kusikiliza moyo wako lakini daktari anaweza.
2. Utachelewa Kupata Matibabu ya Kweli: Kila saa inayopita katika hali kama kiharusi, mshtuko wa moyo, au sumu inaweza kuwa tofauti kati ya maisha na kifo chako.
3. Overdose ya Dawa za Dukani: Dawa nyingi zinaonekana salama lakini zina hatari kubwa unapozichanganywa au kuzitumia vibaya. Mfano mzuri ni paracetamol ambayo inaweza kuharibu ini lako.
4. Wasiwasi wa Kupita Kiasi (Cyberchondria): Kusoma kuhusu magonjwa makubwa kunaweza kusababisha wasiwasi mkubwa wa kiafya, hata kama ulikuwa mzima kabisa.
5. Taarifa za Uongo na Propaganda: Mitandao imejaa “madaktari wa bandia” wanaouza tiba za mitishamba, maji ya ajabu, au njama za kupinga dawa za kisasa.
Hadithi za Baadhi ya Watu Walioumia kwa “Daktari Google”
Kijana mmoja wa kiume alikuwa na maumivu ya kichwa kwa wiki mbili. Alitumia Google na kupata jibu: “maumivu ya kichwa yanaweza kuwa tumor ya ubongo.”
Kwa wiki mbili zaidi aliishi katika wasiwasi mkubwa, akijificha, akiogopa kwenda hospitalini kwa sababu “hakutaka kujua ukweli mbaya.” Alipofika hospitalini hatimaye, daktari akamwambia kuwa hana shida kwenye ubongo bali alikuwa na shinikizo la macho linalohitaji tiba ya miwani tu.
Lakini kuna hadithi nyingine zenye mwisho mbaya zaidi:
Kiijana wa miaka 32 alihisi maumivu ya mguu wa kushoto. Google ikamwambia ni “misuli iliyochoka tu” na aliamini. Kwa wiki tatu alijifanyia massage na kupumzika lakini hakupata nafuu.
Alipoenda hospitali, madaktari walikuta damu iliyoganda kwenye mshipa mkubwa wa mguu (hali inayojulikana kama deep vein thrombosis) ambayo ingeweza kumsababishia hatari zingine kubwa zaidi.
Hadithi hizi mbili zinaonyesha pande mbili za tatizo: Wasiwasi usio wa lazima kutokana na taarifa za kutisha na uzembe wa hatari kutokana na taarifa zinazotuliza lakini zisizo sahihi.
Mtandao una taarifa nzuri na mbaya kwa uwiano sawa. Tatizo ni kwamba huwezi kujua upi ni upi bila elimu ya matibabu.
Uongo Husambaa kwa Kasi Kama Mwanga
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), “infodemic” yani mlipuko wa taarifa potofu za kiafya ni moja ya hatari kubwa za afya ya umma katika karne ya 21.
Wakati wa janga la COVID-19, taarifa potofu zilisambaa haraka zaidi kuliko virusi vyenyewe, na kusababisha vifo vya wengi waliokunywa dawa za mifugo au sumu kwa kuwa na taarifa potofu ya kujitibu.
Kwetu Afrika Mashariki swala la upatikanaji wa madaktari bado ni changamoto kwani uwiano wa daktari 1 kwa watu 1,000 bado upo kwenye maeneo mengi.
Hii inamaanisha watu wengi wana sababu halisi ya kutafuta msaada mtandaoni. Lakini pia inamaanisha wahusika wabaya wana fursa kubwa ya kusambaza taarifa za uongo kwa watu wasio na namna nyingine ya kupata msaada wa kiafya.
Kwa upande mwingine wa mitandao ya kijamii kama WhatsApp na Instagram, imekuwa chanzo kikubwa cha “tiba” za uongo kama mafuta ya kupika yanayodaiwa kutibu saratani, miti shamba isiyokuwa na uthibitisho, na hata maombi ya “kuondoa mapepo” kama tiba za magonjwa ya akili.
Hatari ya maudhui haya si tu kwamba hayasaidii bali yanaweza kudhuru moja kwa moja.
Si Yote Mabaya: Jinsi ya Kutumia Intaneti kwa Usalama
Hata hivyo, si sahihi kusema Google na intaneti hazina nafasi katika afya. Lakini pale unapotumia Google na mitandao mingine uku tayari unajua ni ipi njia sahihi ya kupata taarifa sahihi basi mitandao itakusaidia sana.
Taarifa za mtandaoni zinaweza kukusaidia kuelewa utambuzi uliotolewa na daktari, kujua maswali ya kuuliza daktari wako, kutambua dalili za dharura zinazohitaji kwenda hospitali mara moja, na kupata msaada wa kisaikolojia wa awali wakati haupatikani na hivyo vyote ni kwa kujua namna sahihi ya matumizi yake.
Tovuti kama WHO.int, Mayo Clinic, MedlinePlus, abiteafya.com na WebMD zinasimamiwa na wataalamu wa afya na kurekebishwa mara kwa mara – kama ikitokea mabadiliko ya taarifa.
Zinaweza kutoa muhtasari wa kweli wa magonjwa na dalili zake tofauti na blogu za watu binafsi, ukurasa wa Facebook wa “mganga wa asili,” au video za TikTok zinazodai kutibu magonjwa kwa limao na miembe.
Hivyo:
● Tumia Vyanzo Vinavyoaminika Pekee: WHO, Mayo Clinic, MedlinePlus na Abite Afya.
● Google ni kwa Maelezo, Si Utambuzi: Tumia intaneti kuelewa maneno ya kimatibabu baada ya daktari kukuambia kitu, si badala yake.
● Dalili za Dharura Hazihitaji Google: Maumivu makali ya kifua, ugumu wa kupumua, ulemavu wa ghafla wa mkono/mguu/uso hivyo nenda hospitalini leo bila kufungua simu.
● Jiulize: Ni chanzo cha kweli? Tovuti yenye makosa ya sarufi, inayouza bidhaa, au inayodai tiba ya “magonjwa yote” ni ishara ya hatari.
● Shauriana na Daktari Halisi: Hata madaktari wengi sasa wana huduma za simu na ujumbe, hivyo tumia hilo kabla ya kuamini taarifa za Google.
● Vumilia Kutojua: Si aibu kusema “sijui” na kwenda hospitali. Wasiwasi wa “kuonekana dhaifu” unaweza kukugharimu afya yako.
“Simu Yako ni Chombo, Lakini Si Daktari Wako”
Teknolojia imefanya maisha yetu kuwa rahisi kwa njia nyingi za kushangaza. Lakini afya yako ni ya thamani na kipekee sana kuwekwa mikononi mwa algorizimu inayolenga kukupa matokeo ya utafutaji yanayovutia, si yanayokuwa ya kweli kwa hali yako mahususi.
KUMBUKA: Daktari alisoma miaka mitano au zaidi kujifunza mwili wa binadamu. Alifanya mazoezi ya kliniki kwa miaka mingine miwili hadi mitano.
Ana vifaa vya kupima damu yako, moyo wako, macho yako. Ana uwezo wa kukuuliza maswali kwa undani, kukuchunguza kwa mikono yake, na kuzingatia historia yako yote ya kiafya.
Google ana nini?
Ana maneno uliyoyaandika kwenye sanduku dogo la utafutaji.
Tumia intaneti kwa busara. Tumia kwa uelewa. Lakini usikubali simu yako iwe daktari wako wa kwanza, wa mwisho, na wa pekee. Maisha yako yana thamani zaidi ya click moja ya Google search.
Mwili wako ni zawadi ya kipekee uliyopewa mara moja tu. Usimkabidhi Google. Mpe daktari.
I am a healthcare provider. I focus on sharing clear, evidence based health information through articles and social media.
My goal is to help you understand healthily life. I believe accurate health information improves decisions and lives.
