Lishe bora kwa wagonjwa wa kisukari

Kisukari ni ugonjwa usioambukiza unaogundulika baada ya vipimo vya kimaabara kuonyesha viwango vikubwa vya sukari katika damu kwa nyakati tofauti tofauti.

 

Ili uweze kugunduliwa kuwa una kisukari unapaswa kuwa umepimwa zaidi ya mara moja.

 

Unapokua umegundulika na ugonjwa wa kisukari unapaswa kubadilisha mtindo wako wa maisha na hii huhusisha maswala mawili muhimu:

  1. Kuongeza mazoezi katika ratiba yako ya kila siku.
  2. Kuwa na taarifa sahihi za jinsi ya kula.

 

Maswala haya mawili ni muhimu sana kukusaidia katika kudhibiti viwango vya sukari katika damu pindi ambapo umeshagundulika na ugonjwa huu.

 

Mazoezi

Tukianza na swala la mazoezi, unapaswa kuwa unafanya mazoezi yanaochangamsha mwili walau kwa muda wa nusu saa kwa siku.

 

Unaweza kuanza na mazoezi ya kutembea kwa kutembea mwenyewe au na ndugu, jamaa au rafiki. Kwa wale wanaofuga mbwa, unaweza pia kwenda nae kutembea jioni (dog walking).

 

 

Makala mbalimbali zimethibitisha kufanya huku mazoezi (mepesi) husaidia kupungua kwa kiwango cha sukari mwilini. Lakini kuna baadhi ya mazoezi ambayo yanaweza kupelekea ongezeko la sukari mwilini kama vile kunyanyua vyuma vizito sana na mazoezi mengine ambayo yanapelekea ongezeko la kichocheo cha adrenalini katika damu.

 

Adrenalini huwa ni kichocheo/homoni  cha  “fight and flight” au “kupigana ama kukimbia” ambacho hutolewa pindi mwili unapohisi kuna uhitaji mkubwa wa matumizi ya sukari kwa ajili ya nguvu za mwili, na hii kupelekea utolewaji wa sukari mwilini kwa ajili ya mahitaji ya mwili ya kukimbia ama kupigana.

 

Mfano: Kama unafanya kazi ngumu ya kubeba vitu kizito kama vile chuma (heavyweight lifting), mwili wako hutoa kichocheo cha adrenalini ambayo hupeleka taarifa ya mahitaji ya ongezeko la nguvu kwa ajili ya kazi hio.

 

Nguvu hii humaanisha ongezeko la sukari mwilini kwa ajili ya kazi hii ya kunyanyua vyuma. Hivyo basi unashauriwa kufanya mazoezi mepesi kama kutembea kiasi ili kukusaidia kuepuka ongezeko la sukari mwilini.

 

Taarifa sahihi kuhusiana na vyakula

(Pindi unapogundulika na ugonjwa huu wa kisukari)

Katika ulimwengu tunaoishi sasa kuna taarifa nyingi ambazo sio rasmi zinazoelezea mambo mengi ya kiafya hivyo ni muhimu kuhakikisha unapata taarifa za afya kutoka kwa wataalamu wa maswala ya Afya ambao wana taaluma inayokuwezesha wewe kupata taarifa sahihi.

 

Ukiwa na ugonjwa wowote usioambukiza ni rahisi kutamani kupata suluhisho la haraka ili kuondokana na ugonjwa huo .

 

Watu wengi hufanya mambo mengi ikiwemo kuacha kufuatilia matibabu na ushauri wa watoa huduma wa Afya kwasababu wanakua na imani kwamba njia mbadala zinaweza kuwapatia suluhisho, jambo ambalo huweza kusababisha hatari zaidi na kukomaza magonjwa haya yasioambukiza, na kupelekea kupoteza maisha.

 

 

Kwa kusema hayo, nitaingia moja kwa moja katika kipengele cha namna ya kula kipindi ambacho umegundulika na kisukari.

 

Ukiwa kama mtu mwenye ugonjwa wa kisukari, unapaswa kuwa unakula vyakula kutoka katika makundi yote ya vyakula. Kuelewa kwa undani jinsi ya kula vyakula vyote kwa pamoja, pitia Makala yangu ya sahani inayofaa.

 

Vyakula katika kundi la wanga unavyotakiwa kula ni vyakula vya nafaka ambavyo ni kamili na havijakobolewa yaani (whole grains).

Vyakula hivi vinapaswa kuliwa kwa kipimo cha kiasi cha nusu ya ngumi. Na kama sukari inakua iko juu sana unaweza kupata vyakula kuyoka makundi mengine, hii inawezekezana baada ya kuwasiliana na afisa lishe ili muongozo utolewe kutokana na kiwango cha sukari kwa muda huo.

 

Protini

Mifano ya vyakula vya protini unavyopaswa kula ni nyama isiyo na mafuta, njegere, kunde, na choroko.

Lakini pia kuna jamii za mikunde kunde ambazo unapaswa kuzijua zina protini lakini pia zina asili ya wanga kama vile maharage na njugu hivyo unapaswa kuwa makini katika ulaji wa vyakula hivi, kwani ulaji uliozidi unaweza kupelekea ongezeko la sukari kama utakua katika hali ya sukari ya siku isiyoweza kuvumilia au kustahimili wanga.

 

Kiwango cha protini kinachopaswa kuliwa ni kiasi cha gram 0.8 kwa kila kilo ya uzito wa mwili mpaka gramu 1 ya protini kwa kila kilo.

Hii inategemea na mahesabu yatakayofanyika kipindi cha kufanya mpangilio wa chakula kutokana na mahitaji ya kimetabolisimu ya mteja. Vyakula vyenye protini ni vingi na vinatofautiana kiasi cha protini.

Aidha, vyakula vingine ambavyo vipo katika kundi la vyakula vyenye kirutubisho cha protini ni kama vile samaki, dagaa, mayai, maziwa na vyakula vya baharini (sea foods). Ni mojaw

 

Mbogo mboga

Hili ni kundi ambalo mtu mwenye ugonjwa wa kisukari anapaswa kuzingatia kwa wingi hasa mboga mboga za majani, kachumbari ingawa katika kachumbari na mboga mboga kuna mboga kama karoti ambayo huwa na asili ya sukari na inaweza kupelekea ongezeko la sukari kwa ukubwa kama itatumika kwa kiasi kikubwa siku ambayo mwili unashindwa kuvumilia sukari.

 

Matunda

Mfano wa matunda ambayo mtu mwenye kisukari anapaswa kuyatumia ni maparachichi kwani yana mafuta mazuri ambayo yana manufaa mwilini na hayana tabia ya kuongeza kiwango cha sukari kwa haraka.

 

Jambo la kuzingatia

Pamoja ja kuhudhuria kliniki za sukari na kupata dawa zinazosaidia kupambana na sukari ya juu katika damu, ni muhimu kupata ushauri wa mtaalamu wa lishe pindi tu ambapo utakua umegundulika na kisukari.

 

Hii itakuwezesha kupata muongozo binafsi wa namna ya kula na kwa kiasi gani kutokana na mahitaji ya mwili wako.

 

Nimesisitiza neon binafsi kwasababu ya tofauti za kimwili zilizopo kati ya mtu mmoja na mwingine na pia uvumilivu wa kimchakato ambao hutokea pindi tunapoupa mwili chakula kwa ajili ya mahitaji yetu ya kila siku ambao huyofautiana kati ya mtu mmoja na mtu mwingine.

 

Kwa wagonjwa wenye kisukari na shida kubwa ya kupatiwa mpangilio binafsi wa mlo, unaweza kufanya booking hapa ili uweze kuongeza na mimi kisha nikupatie meal plan yako.

 

Asante sana kwa kusoma makala hii, na ikitokea umeipenda au kuisi kuna mtu itaweza kumsaidia, basi usisite kuisambaza au kumsambazia.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW