Katika uwekezaji wa sekta ya afya, wajasiriamali wengi huanza kwa kutafuta kiwanja, kujenga au kukodi majengo, kuajiri wataalamu wa afya na kununua vifaa tiba. Hata hivyo, kuna jambo muhimu ambalo wakati mwingine husahaulika:
Kumhusisha Biomedical Engineer tangu hatua za awali za kupanga na kuanzisha kituo cha afya au polyclinic.
Kwanini ni muhimu?
Biomedical Engineer ni mtaalamu anayeunganisha uhandisi na huduma za afya, hasa katika kuhakikisha vifaa tiba na teknolojia zinazotumika kutoa huduma kwa wagonjwa ni salama, zinafaa kwa matumizi yaliyokusudiwa, zinafanya kazi kwa ufanisi na zinaweza kutunzwa kwa gharama zilizo ndani ya uwezo wa muwekezaji.
Kwa mfano, mwekezaji anaweza kujenga chumba cha uchunguzi wa X-ray bila kuzingatia mahitaji ya kinga dhidi ya mionzi, kununua mashine ya maabara bila kutathmini upatikanaji wa vitendanishi na vipuri (reagents and spareparts), au kufunga mashine ya ultrasound bila kuwa na mpango wa matengenezo (PPM) na usaidizi wa kiufundi.

Changamoto hizo zinaweza kusababisha gharama za ziada, kuchelewa kuanza kutoa huduma au vifaa kutotumika ipasavyo hivyo kusababisha hasara kwa muwekezaji na kuhatarisha maisha ya wagonjwa na watumiaji wa vifaa hivyo.
Ndiyo maana ushiriki wa Biomedical Engineer haupaswi kuanza pale mashine inapoharibika. Unapaswa kuanza wakati wazo la kuanzisha kituo cha afya linapokuwa bado katika hatua za mipango.
Yafuatayo ni maeneo sita muhimu yanayoonyesha thamani ya kumhusisha mtaalamu huyu katika safari nzima ya uwekezaji wa huduma za afya:
1. Usanifu wa Majengo na Upangaji wa Miundombinu ya Kituo cha Afya
Jengo la kituo cha afya si sawa na jengo la kawaida la biashara. Huduma za afya zina mahitaji maalumu ya kiufundi, kiusalama na kiutendaji ambayo yanapaswa kuzingatiwa kabla ya ujenzi kuanza.
Biomedical Engineer akihusishwa katika hatua hii, anaweza kushirikiana na wasanifu majengo, wahandisi wa ujenzi, wahandisi wa umeme, wataalamu wa mifumo ya maji na wataalamu wa afya kuhakikisha kuwa majengo yanakidhi mahitaji ya vifaa na huduma zilizopangwa.
- Mifumo ya umeme: Uwezo wa umeme, ubora wa usambazaji, earthing, kinga dhidi ya hitilafu za umeme na mahitaji ya umeme wa akiba kwa vifaa muhimu.
- Mifumo ya maji na mifereji: Upatikanaji wa maji yenye ubora unaohitajika kwa shughuli husika, hasa maabara, huduma ya meno na maeneo ya usafishaji au uchakataji wa vifaa.
- Uingizaji na utoaji wa hewa: Mahitaji ya uingizaji hewa na udhibiti wa mazingira katika maabara, maeneo ya kuhifadhia vifaa na vyumba vinavyotumia teknolojia maalumu kama biosafety carbinate.
- Mpangilio wa vyumba: Nafasi ya kufunga, kutumia, kusafisha na kufanya matengenezo ya vifaa bila kuathiri shughuli za kliniki.
- Usalama wa wagonjwa na wafanyakazi: Mpangilio wa huduma unaozingatia udhibiti wa maambukizi, utiririshaji wa wagonjwa na usalama wa vifaa.
Scenario iliyotokea Arusha Mjini:
Mwekezaji mmoja miongoni mwa wateja wetu aliamua kupanga chumba cha X-ray bila kuhusisha wataalamu wa vifaa tiba na mionzi.
Baada ya jengo kukamilika, anagundua kuwa chumba hakina mpangilio unaofaa kwa mashine, kioo cha chumba cha mtaalam wa mionzi, milango na kuta zinahitaji marekebisho ya kinga dhidi ya mionzi, na mifumo ya umeme haijakidhi mahitaji ya kifaa.
Marekebisho hayo yalipelekea kuongeza gharama na kuchelewesha kuanza kwa huduma, ilikua ni kabla ya kukutana na biomedical engineer na kupata ushauri, mpangilio na ramani sahihi ya jengo hilo la mionzi.
Kwa kumhusisha Biomedical Engineer mapema, mahitaji ya kifaa yanaweza kuingizwa kwenye michoro na nyaraka za ujenzi kabla ya kazi kuanza.
Hata hivyo, usanifu wa kinga dhidi ya mionzi na uthibitishaji wa usalama wake lazima pia ufanywe na wataalamu wenye sifa na mamlaka husika.
Muhimu: Gharama ya kutatua tatizo kwenye michoro mara nyingi huwa ndogo kuliko gharama ya kubomoa, kurekebisha au kujenga upya sehemu ya jengo lililokamilika.
2. Kuchagua na Kununua Vifaa Tiba Vinavyofaa
Kununua vifaa tiba si suala la kuchagua mashine yenye jina kubwa, teknolojia ya kisasa au bei ya chini.
Ni mchakato unaohitaji kutathmini mahitaji ya kitabibu, uwezo wa kifedha, ubora wa kifaa, upatikanaji wa huduma za kiufundi na gharama za kukitumia kwa muda mrefu.
Biomedical Engineer anaweza kusaidia mwekezaji kuandaa mahitaji ya kiufundi ya vifaa, kutathmini wazabuni na kulinganisha chaguo mbalimbali kabla ya kutoa fedha.

Vifuatavyo ni baadhi ya vigezo vya kuzingatia katika tathmini kabla ya mchakato wa manunuzi kuanza rasmi:
- Huduma zipi zitakazotolewa na kiwango cha wagonjwa kinachotarajiwa.
- Uwezo wa kifaa na vipimo vinavyohitajika kwa huduma husika.
- Upatikanaji wa vipuri, vitendanishi na vifaa saidizi (spare parts, reagents and accessories).
- Upatikanaji wa mafundi wenye sifa na msaada wa mtengenezaji.
- Gharama za usakinishaji, mafunzo, matengenezo na matumizi ya kila siku.
- Udhamini, masharti ya huduma na upatikanaji wa nyaraka za kiufundi.
Mfano: Mashine ya Maabara
Fikiria polyclinic inayotaka kununua mashine ya kufanya vipimo vya damu (Hematology analyzer). Mwekezaji anaweza kuvutiwa na mashine yenye uwezo wa kufanya vipimo vingi kwa muda mfupi (high throughput) lakini Biomedical Engineer, kwa kushirikiana na mtaalamu wa maabara, atahitaji kuchunguza mambo mengine kama:
Je, idadi ya wagonjwa inatosha kuhalalisha mashine hiyo?
Je, vitendanishi vinapatikana nchini?
Je, mashine inahitaji maji maalumu au mazingira yenye udhibiti wa joto?
Je, kuna huduma za matengenezo?
Je, gharama ya kila kipimo inaendana na mapato yanayotarajiwa?
Ikiwa mahitaji hayo hayatatathminiwa, mwekezaji anaweza kuishia na mashine ya gharama kubwa inayotumika mara chache au inayokaa bila kufanya kazi kwa sababu ya ukosefu wa vitendanishi.
“Teknolojia ya kisasa nayo inahitaji tathmini“
Vifaa vya kidijitali vinaweza kuwa na faida kubwa, lakini lazima vichaguliwe kulingana na mahitaji halisi. Kwa mfano, mfumo wa digital X-ray unaweza kurahisisha upatikanaji na uhifadhi wa picha, lakini pia unahitaji kompyuta, mifumo ya kuhifadhi taarifa, mtandao pale inapohitajika, usalama wa data na msaada wa kiufundi.
Ushauri wa kitaalamu: Kabla ya kulipia kifaa chochote kikubwa, hakikisha kuna tathmini ya kiufundi na kifedha inayozingatia gharama zote za kukimiliki na kukitumia, si bei ya kununua pekee/ownership contract.
3. Ufungaji, Majaribio na Uthibitishaji wa Usalama wa Vifaa
Kifaa tiba kinapowasili kituoni hakimaanishi kuwa kiko tayari kutumiwa na wagonjwa.
Kuna hatua muhimu za kiufundi zinazopaswa kufanyika kabla ya kuanza kutoa huduma, zikiwemo ukaguzi wa kifaa kilichopokelewa, uthibitishaji wa mahitaji ya eneo la ufungaji kama majina umeme, usakinishaji unaofaa, majaribio ya utendaji, uhakiki wa usalama na mafunzo ya watumiaji.
Biomedical Engineer anaweza kuratibu au kufanya kazi hizi kulingana na aina ya kifaa, mafunzo yake na taratibu husika, kwa kushirikiana na mtengenezaji, msambazaji na wataalamu wengine wanaohitajika.
Mfano: Mashine ya Ultrasound
Baada ya kununua mashine ya ultrasound, hatua za awali hazipaswi kuishia katika kuiwasha na kuona kama picha zinaonekana.
Ni muhimu kuthibitisha kuwa kifaa kimewasilishwa katika hali nzuri, probe zake zinafanya kazi ipasavyo, programu na mipangilio yake ni sahihi, vifaa saidizi vipo, na majaribio yanayofaa yamefanyika kulingana na maelekezo ya mtengenezaji.
Watumiaji wanapaswa pia kufundishwa kuhusu matumizi sahihi, usafishaji wa probe, utunzaji wa nyaya, namna ya kutambua hitilafu na hatua za kuchukua kifaa kinapokuwa na tatizo.
Kwa mashine za X-ray, maabara na vifaa vingine vyenye mahitaji maalumu ya usalama, uthibitishaji unaohitajika lazima ukamilishwe kabla ya kuanza huduma, pamoja na vibali na ukaguzi unaotakiwa na mamlaka husika.
Kwa nini hatua hii ni muhimu? Bila utaratibu mzuri wa ufungaji na uthibitishaji, kituo kinaweza kuanza kutumia kifaa chenye hitilafu, matokeo yasiyoaminika au hatari kwa wagonjwa na wafanyakazi.
Aidha, makosa ya ufungaji yanaweza kuathiri udhamini wa kifaa na kuongeza gharama za marekebisho.
Kanuni ya msingi: Kifaa kinapaswa kuthibitishwa kuwa kimefungwa na kufanya kazi kwa usalama kabla ya kuidhinishwa kuingia kwenye matumizi ya kawaida ya kliniki.
4. Kuanzisha Mfumo wa Matengenezo na Usimamizi wa Vifaa Tiba
Mojawapo ya makosa yanayoweza kuathiri uwekezaji wa afya ni kupanga bajeti ya kununua vifaa bila kupanga namna ya kuvitunza.
Vifaa tiba vinahitaji usimamizi endelevu ili viendelee kufanya kazi kwa usalama na ufanisi. Mfumo huu unajulikana kama medical equipment management na unahusisha usimamizi wa kifaa kuanzia kinaponunuliwa hadi kinapoondolewa kwenye matumizi.
Biomedical Engineer anaweza kusaidia kuanzisha mfumo unaojumuisha:
- Rejesta ya vifaa tiba: Kila kifaa kiwe na namba ya utambulisho, eneo kilipo, mtengenezaji, modeli, namba ya serial, tarehe ya ununuzi na taarifa za udhamini.
- Mpango wa matengenezo kinga: Ratiba ya matengenezo kulingana na maelekezo ya mtengenezaji, matumizi na kiwango cha hatari cha kifaa.
- Mfumo wa kuripoti hitilafu: Watumiaji wajue namna ya kuripoti hitilafu na namna ya kuzuia matumizi ya kifaa kisicho salama.
- Uhakiki wa utendaji na calibration: Vifaa vinavyohitaji calibration au vipimo vya utendaji vikaguliwe kwa utaratibu unaofaa.
- Usimamizi wa vipuri na mikataba ya huduma: Kuwepo na mpango wa kupata vipuri, mafundi na msaada wa kiufundi kwa wakati.
- Mafunzo ya watumiaji: Wauguzi, madaktari na wataalamu wengine wafundishwe matumizi sahihi na utunzaji wa vifaa.
Mfano wa athari za kutokuwa na mfumo
Tuchukulie kituo kina mashine ya Hematology Analyzer inayotumika kufanya vipimo vya damu. Ikiwa hakuna matengenezo yaliyopangwa, hakuna ufuatiliaji wa matumizi na hakuna mpango wa kupata vipuri, hitilafu ndogo inaweza kusababisha mashine kusimama kwa siku kadhaa.
Katika kipindi hicho, kituo kinaweza kulazimika kupeleka sampuli maabara nyingine, kuchelewesha majibu au kupoteza mapato ya vipimo ambavyo kingeweza kutoa.
Kinyume chake, mfumo wa matengenezo unaoweza kutekelezeka unaweza kusaidia kutambua matatizo mapema, kupanga matengenezo na kupunguza muda ambao kifaa hakifanyi kazi.
Shirika la kimataifa linalo jishughulisha na afya, WHO, linaeleza umuhimu wa usimamizi wa vifaa tiba katika kuhakikisha teknolojia ya afya inatumika kwa usalama na ufanisi katika kipindi chote cha matumizi yake.
Kwa hiyo, Biomedical Engineer si mtaalamu wa kuitwa tu mashine inapoharibika; ni mshiriki muhimu katika kuzuia hitilafu, kupunguza muda wa kutofanya kazi na kulinda thamani ya uwekezaji.
5. Kusimamia Mzunguko Mzima wa Maisha ya Kifaa Tiba (Life Cycle Management)
Katika mtazamo wa uhandisi, maisha ya kifaa tiba hayaanzi siku kinapowekwa kwenye chumba cha huduma na hayaishii siku kinapoharibika.
Mzunguko wake huanzia katika kutambua hitaji la huduma, kupanga bajeti, kuchagua teknolojia, kununua, kusafirisha, kufunga, kujaribu, kutumia, kutunza, kukarabati na hatimaye kukiondoa kwenye matumizi kwa utaratibu salama.
Hii ndio life cycle management.
Biomedical Engineer anaweza kusaidia uongozi kufanya maamuzi sahihi katika kila hatua, badala ya kusubiri matatizo yatokee. Zifuatazo ni hatua muhimu katika life cycle management:
Hatua ya 1: Tathmini ya mahitaji
Tambua huduma inayohitajika, idadi inayotarajiwa ya wagonjwa na uwezo wa kituo kutoa huduma hiyo.
Hatua ya 2: Upangaji wa bajeti na ununuzi
Linganisha bei ya ununuzi na gharama za usakinishaji, mafunzo, matumizi, matengenezo, vipuri na uingizwaji wa kifaa.
Hatua ya 3: Usakinishaji na uanzishaji
Hakikisha eneo linafaa, kifaa kimefungwa ipasavyo, majaribio yamekamilika na watumiaji wamefundishwa.
Hatua ya 4: Matumizi na matengenezo
Fuatilia utendaji, gharama za matengenezo, upatikanaji wa vipuri, muda wa kutofanya kazi na historia ya hitilafu.
Hatua ya 5: Tathmini ya kuendelea kutumia au kubadilisha
Tathmini kama kifaa bado ni salama, kinafaa, kinaweza kutengenezwa kwa gharama inayokubalika na kinaweza kukidhi mahitaji ya huduma.
Hatua ya sita: Kuondoa kifaa na kusimamia uteketezaji wake
Kifaa kinapofikia mwisho wa matumizi yake, fuata taratibu zinazofaa za kukiondoa kwenye huduma, kulinda taarifa zilizohifadhiwa ndani yake na kusimamia taka za kielektroniki kwa usalama.
Mfano: Mashine ya X-ray ya kidijitali
Kituo kinaponunua mashine ya X-ray, gharama yake si bei ya mashine pekee. Kuna gharama za ujenzi na kinga dhidi ya mionzi, ufungaji, mafunzo, umeme, matengenezo, mifumo ya picha, leseni au vibali vinavyohitajika na uagizwaji wa vipuri vinapo chakaa.
Baada ya miaka kadhaa, uongozi unaweza kuhitaji kuamua kama uendelee na mashine hiyo, uikarabati, uiboreshe au ununue nyingine.
Biomedical Engineer anaweza kuandaa taarifa za kiufundi zinazosaidia uamuzi huo kwa kuangalia historia ya hitilafu, gharama za matengenezo, upatikanaji wa vipuri, usalama, ubora wa utendaji na mahitaji mapya ya huduma.
Hii husaidia uongozi kuepuka kubadilisha kifaa kwa sababu tu ni cha zamani, au kuendelea kutumia kifaa ambacho hakina tena usalama au ufanisi unaohitajika.
Teknolojia inabadilika: Usimamizi lazima uendane na mabadiliko hayo
Leo, baadhi ya vifaa tiba vina programu zinazosasishwa, mifumo ya kuunganisha data, huduma za mbali na vipengele vinavyoweza kuhitaji leseni za matumizi.
Hivyo, kabla ya kununua kifaa, ni muhimu kujua kama programu zake zitaendelea kuungwa mkono, kama mfumo wake unaweza kuunganishwa na mifumo mingine na kama data za wagonjwa zitalindwa.
Kwa mfano:
Kifaa ESR (Erythrocyte Sedimentation Rate) kwa ajili ya kupima uwezo wa seli nyekundu za damu kushuka na kutengana na sehemu ya umajimaji ya damu, hutumia kadi maalum kuweza kufanya kipimo kwa sampuli kadhaa, baada ya kufikia kikomo mtumiaji hutakiwa kulipia (smartcard) kadi nyingine ili kuendelea kutumia.
Hii teknolojia inatuonesha kua ni muhimu kufahamu undani wa teknolojia iliyotumika na kujua ipo rafiki kiasi gani kwa hali ya kiutumiaji katika kituo husika.
Hivyo, life cycle management ya kisasa inapaswa kuzingatia si afya ya kifaa pekee, bali pia uendelevu wa programu, usalama wa taarifa, upatikanaji wa huduma za kiufundi na gharama za kuboresha teknolojia.
6. Biomedical Engineer ni Strategic Partner wa Mwekezaji, Si Gharama ya Ziada!
Kumhusisha Biomedical Engineer kunaweza kuonekana kama gharama nyingine katika hatua za awali za uwekezaji. Lakini tathmini sahihi inapaswa kuangalia thamani ya huduma hiyo katika kipindi chote cha maisha ya kituo.
Mtaalamu huyu anaweza kusaidia kupunguza makosa ya ununuzi, kuzuia gharama za marekebisho ya majengo, kupanga matengenezo, kupunguza muda wa vifaa kusimama na kuboresha matumizi ya rasilimali.
Kwa kituo kidogo ambacho hakiwezi kumudu Biomedical Engineer wa kudumu, inawezekana kupanga huduma za ushauri na matengenezo kupitia mkataba na mtoa huduma mwenye sifa zinazofaa.
Mpangilio huo unapaswa kuendana na ukubwa wa kituo, aina za vifaa, kiwango cha hatari na masharti ya kisheria.
Ni muhimu pia kutambua kwamba Biomedical Engineer hafanyi kazi peke yake. Ushirikiano na madaktari, wauguzi, wataalamu wa maabara, wahandisi wa majengo na umeme, wataalamu wa mionzi, wasimamizi wa kituo na mamlaka za udhibiti ni muhimu ili kuhakikisha huduma zinakuwa salama na endelevu.
Hitimisho
“Mwekezaji mwenye maono hujenga mfumo, si jengo pekee“
Kuanzisha polyclinic au kituo cha afya ni safari yenye maamuzi mengi ya kitaalamu na kifedha. Maamuzi yanayofanywa katika hatua za mwanzo yanaweza kuathiri gharama za uendeshaji, ubora wa huduma, usalama wa wagonjwa na uwezo wa kituo kukua kwa miaka mingi.
Kwa hiyo, Biomedical Engineer anapaswa kuhusishwa tangu hatua za usanifu wa majengo, tathmini ya mahitaji ya vifaa, ununuzi, ufungaji na uthibitishaji wa utendaji, hadi matengenezo na usimamizi wa mzunguko mzima wa maisha ya vifaa tiba.
Kumhusisha mtaalamu huyu mapema kunatoa fursa ya kutambua changamoto kabla hazijawa gharama, kuchagua teknolojia inayofaa na kuhakikisha kuwa uwekezaji unaendelea kutoa thamani baada ya siku ya uzinduzi.
Ujumbe wa mwisho kwa kila mwekezaji wa sekta ya afya:
Usisubiri kifaa tiba kiharibike ndipo utafute Biomedical Engineer. Mhusishe kabla ya kujenga, kabla ya kununua, wakati wa kufunga na katika kipindi chote ambacho kifaa kinatumika.
Kwa sababu kituo cha afya endelevu hakipimwi kwa idadi ya vifaa vilivyonunuliwa, bali kwa uwezo wake wa kutoa huduma salama, bora na zinazoaminika kwa kutumia teknolojia inayofanya kazi kwa ufanisi kwa muda mrefu.
Kama utahitaji ushauri wa kina & kitaalamu kuhusu usimamizi wa vifaa tiba na teknolojia za afya, usisite kuwasiliana nami kupitia simu namba +255 624 802 843 au “WhatsApp Me”. Asante kwa kutumia muda wako kusoma makala hii.

Haruna Mashaka Banana is a Biomedical Engineer with a Bachelor’s Degree in Electrical and Biomedical Engineering from Arusha Technical College and an Ordinary Diploma in Biomedical Equipment Engineering from the Dar es Salaam Institute of Technology.
He is a registered Biomedical Engineer under ERB and has professional experience in medical equipment maintenance, installation, troubleshooting, preventive maintenance, inventory management, and healthcare technology support.
Eng. Haruna is also a certified trainee in Fundamentals of Organizational Leadership from Uongozi Institute, Mwalimu Nyerere School of Leadership. He has demonstrated leadership through serving as President of the Students’ Organization at Arusha Technical College and as a member of the ATC Board of Directors.
His professional interests include healthcare technology, digital health, public health, medical equipment management, innovation, and youth leadership.
