Umewahi kujikuta unatumia/umetumia saa moja (au zaidi) uki’scroll Instagram, Facebook, au TikTok bila kufahamu ni muda gani ulianza?
Au umeshindwa kulala kwa sababu akili yako bado “inatafuna” habari, video na ujumbe uliovipokea mchana kutwa? Hujakosea na haupo peke yako!

Kila siku, ubongo wako unapokea kiasi kikubwa cha taarifa kupitia mitandao ya kijamii, habari, ujumbe na programu mbalimbali – kiasi ambacho hakikuwahi kutokea kwa vizazi vilivyopita.
Tatizo si kwamba taarifa ni nyingi tu. Tatizo ni pale kasi ya taarifa inapozidi uwezo wa akili yako kuzichakata na kupumzika.
Makala hii inaelezea jinsi hali hii inavyoweza kuathiri afya yako ya akili, dalili za kuzitambua, na hatua za vitendo unazoweza kuchukua.
Kwa Nini Taarifa Nyingi Zinaweza Kukuathiri
Akili inapopokea taarifa nyingi kuliko inavyoweza kuchakata, matokeo ni uchovu wa kiakili – hata bila kufanya kazi ngumu.
Akili ya binadamu haikuundwa kupokea maelfu ya vipande vya taarifa kila siku. Notification moja inapokatiza kile unachosoma, halafu video moja inafuatiwa na nyingine, akili yako inabaki katika hali ya “kuruka” kutoka jambo moja kwenda jingine bila kupumzika kikamilifu.
Hali hii ikiendelea, kwa muda mrefu, inaweza kusababisha:
- Umakini uliogawanyika — kushindwa kukaa na jambo moja kwa muda mrefu
- Uchovu wa kufanya maamuzi — maoni na taarifa nyingi zinazopingana zinakuchelewesha kuamua
- Kukosa muda wa akili kutulia na kutafakari, hasa jioni au usiku.
Ni muhimu kuelewa: kupata taarifa nyingi si sawa na kuwa na maarifa mengi. Mtu anaweza kusoma makala kumi kwa siku bila kuelewa hata moja kwa kina.
Dalili za Kuzidiwa na Taarifa (Information Overload)
1. Kuhisi uchovu wa akili bila kufanya kazi ngumu: Umekaa tu, lakini akili yako imepokea habari nyingi kiasi kwamba unahisi kama umefanya kazi nzito.
2. Kushindwa kuzingatia jambo moja kwa muda mrefu: Unaanza kusoma au kufanya kazi, kisha akili yako “inaenda” kwenye simu bila wewe kuamua hivyo.

3. Wasiwasi wa kukosa taarifa (kuhisi lazima ufuatilie kila kitu): Unahisi hofu ya kukosa habari mpya, hata kama haihusiani na maisha yako moja kwa moja.
4. Ugumu wa kulala au kutulia usiku: Akili inaendelea “kutafuna” taarifa za mchana hata baada ya kuzima simu.
5. Kuchoka kufanya maamuzi madogo: Maoni na taarifa nyingi zinazopingana zinakufanya uchelewe hata kuamua mambo rahisi.
Ukijitambua katika dalili tatu au zaidi kati ya hizi, huenda ni wakati wa kubadilisha jinsi unavyotumia taarifa.
Nini Unachoweza Kufanya? – “Lishe ya Taarifa”
Kama unavyochagua chakula unachokula, chagua pia taarifa unazoruhusu ziingie akilini mwako.
Kabla ya kutumia muda kwenye taarifa yoyote, jiulize:
- Chanzo: Nani ametoa taarifa hii?
- Umuhimu: Je, kweli ninahitaji taarifa hii sasa?
- Ubora: Je, chanzo hiki kinaaminika?
- Matumizi: Nitaitumiaje taarifa hii katika maisha yangu?
Hatua Nyingine za Vitendo:
- Weka muda maalum wa kuangalia mitandao ya kijamii, badala ya kufanya hivyo mfululizo mchana kutwa
- Tenga angalau saa moja kabla ya kulala isiyo na simu, ili akili ipate nafasi ya kutulia
- Chagua vyanzo vichache vinavyotegemeka badala ya kufuatilia vyanzo vingi visivyo na uhakika
- Jikumbushe: Si lazima ujue kila kitu kinachotokea ili uwe na hekima
Wakati wa Kutafuta Msaada wa Kitaalamu
Zungumza na mshauri wa afya ya akili endapo dalili zinaendelea kwa wiki kadhaa au zinaathiri maisha yako ya kila siku.
Kuhisi uchovu wa taarifa mara kwa mara ni jambo la kawaida katika zama hizi. Hata hivyo, unapaswa kuzungumza na mshauri wa afya ya akili endapo:
- Wasiwasi au msongo unaotokana na matumizi ya mitandao unaathiri usingizi wako kwa wiki kadhaa mfululizo
- Unahisi huwezi kudhibiti muda unaotumia kwenye simu hata unapotaka
- Hali hii inaanza kuathiri kazi, masomo au mahusiano yako ya kila siku
Dalili hizi hazimaanishi kuna tatizo kubwa la kiafya, lakini zinastahili tathmini ya mtaalamu badala ya kujaribu kujitibu peke yako.
Hitimisho
Wimbi la taarifa ni changamoto ya kweli ya zama hizi za kidijitali – lakini si lazima likuathiri. Kwa kujenga nidhamu ndogo ya jinsi unavyotumia taarifa, unaweza kulinda umakini wako, usingizi wako, na afya yako ya akili kwa ujumla.
Ikiwa unahisi kuzidiwa na taarifa kunaanza kuathiri maisha yako ya kila siku, zungumza na mshauri wa saikolojia badala ya kuendelea kubeba mzigo huo peke yako.

Abel Isdory Mwakitosi is a Counseling Psychology student, Certified Financial Educator (BOT), educator, and youth leader from Tanzania. He combines training in psychology, education, financial literacy, and community leadership to support youth development, psychological wellbeing, personal growth, and responsible financial decision-making.
He is passionate about empowering individuals and communities through education, counselling-related skills, leadership, and practical financial knowledge.
