Kuna Athari Zozote za Kuongezewa Damu Mwilini?

Kama nilivyoeleza kwenye makala iliyopita (unaweza kuisoma kwa kubonyeza hapa), watu mbalimbali wanahitaji damu kwa mahitaji tofauti tofauti ikiwa ni pamoja na ujauzito, kufanyiwa upasuaji (operation) mkubwa, watoto kutokana na sababu mbalimbali, wagonjwa wa kansa, waliopata ajali na kupoteza damu nyingi kwa wakati mfupi, na kadhalika.

Sio mara zote mtu anapatiwa damu yote kama ilivyotoka kwa mtu mwingine. Damu ikitolewa kwa mtu inatenganishwa kuwa sehemu tofauti tofauti na anapatiwa mgonjwa kulingana na mahitaji.

Kuna Seli nyekundu za damu ambazo mara nyingi tunaizungumzia kama damu yenyewe. Kuna Plasma iliyogandishwa; hii inatumika maalumu kwa watu wanaohitaji damu nyingi kwa wakati mmoja, magonjwa ya ini, na magonjwa ya kuganda damu. 

Pia kuna Seli sahani; hii inawafaa wagonjwa wenye upungufu wa seli sahani kutokana na sababu mbalimbali kama vile kansa ya damu au wenye changamoto ya seli sahani zisizofanya kazi.

Kwa sababu seli sahani zina kazi kubwa katika kuganda damu, wagonjwa wanaovuja damu nyingi bila kujali sababu pia wanapatiwa sehemu hii ya damu. 

Pia huduma nyingine za kupokea damu ni pamoja na Krayopresipitatate, kusaidia damu kuganda; Thromboelastografia kwa ajili ya kuangalia uwezo wa viambata vya damu na kwenye upasuaji wa ini; vile vile Kuongeza damu kwa wingi wakati mmoja ikiwemo seli hai nyekundu, plasma na seli sahani na huitaji mtu kupatiwa mpaka chupa 50 za damu ndani ya masaa 24 mpaka 48. 

Nini Kinatokea Mwilini Baada ya Kupokea Damu?

Faida za kuongezwa damu ni nyingi kulingana na mahitaji ya mgonjwa husika na aina ya bidhaa ya damu aliyopatiwa. Japokuwa kuna athari tofauti tofauti za muda mfupi na muda mrefu zitokanazo na kuongezwa damu, kama ifuatavyo:

1. Kupata magonjwa ya kuambukiza

Ingawa ni aghalabu sana hii kutokea kulingana na vipimo vya awali vinavyofanyika kabla ya damu kukubaliwa na kutumika kuwekewa mgonjwa; kuna magonjwa yanayotokana na virusi, bakteria na vijidudu vingine yanaweza kuambukizwa kwa kupokea damu.

Mfano ni UKIMWI, Homa ya Ini, Virusi vya Saitomageli, Virusi vya Epstein Barr, Malaria n.k. Magonjwa haya kwa kawaida yanapimwa kwa mchangiaji ili kuzuia maambukizi.  

2. Kuchochea kwa Ulinzi wa Mwili

Hali hii huwa si ya kutisha. Mara nyingi ni homa, kutetemeka, kusikia baridi na hutokea hasa pale mgonjwa anapopatiwa plasma au bidhaa ya damu  yenye kiasi kikubwa cha seli nyeupe za damu (seli nyeupe za damu ndio zinahusika kupigana na magonjwa mwilini).

Kwa sasa teknolojia inatenganisha seli hai nyeupe za damu ili kuzuia maambukizi na pia kuzuia uchochezi wa  mfumo wa kinga mwilini. Moja kati ya dalili zake ni pamoja na kuwashwa. 

3. Majeraha kwenye Mapafu Baada ya Kuongezwa Damu

Hii ni moja ya changamoto kubwa sana inayotokana na kuongezwa damu hasa kukiwemo seli mahususi kwenye damu ya aliyechangia ambazo zinaingiliana na seli za aliyepokea na kusababisha uharibifu wa mishipa midogo midogo ya damu kwenye mapafu.

Dalili zake ni kupata changamoto ya kupumua baada ya kupokea damu.

4. Transfusion-associated graft-versus-host disease (TA-GVHD)

Tatizo hili linatokea, mara nyingi, pale ambapo seli za kinga (mwilini) za aliyetoa damu zinashambulia seli za aliyepokea damu na hasa hutokea kwa wagonjwa wenye kinga dhaifu. Pia inatokea pale ambapo mgonjwa amepokea damu kutoka kwa ndugu wa karibu ya ndugu wa damu.

Hali hii ni hatari na mgonjwa anaweza kupoteza maisha ndio maana damu unayotoa sio anayopokea ndugu yako, yeye hupatiwa mbadala inayoendana na group lake la damu.

Athari nyingine hatarishi pale mgonjwa anapopokea damu ni pamoja na kuzidiwa kwa mzunguko wa damu kutokana na kuongezwa damu pamoja na kufeli kwa mifumo mbalimbali ya mwili na viungo muhimu mwilini

Athari hizi nyingi zinahusishwa na seli hai nyeupe za damu na ndio maana duniani kuna mchakato maalumu wa kupunguza selihai nyeupe kwenye damu kwa zaidi ya 99% kabla ya damu haijatenganishwa katika bidhaa tofauti tofauti na kupatiwa muhitaji.

Hivyo kupokea damu ni salama na ndio maana kuchangia damu kuna okoa maisha mengi zaidi. 

Tone la Damu! Tone la Huruma! Changia Damu! Okoa Maisha!

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW