Kuanzishwa kwa “Bima ya Afya kwa Wote” Tanzania: Itanisaidiaje?

Tanzania imeanza utekelezaji rasmi wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHI Act, 2023)  mwanzoni mwa mwaka huu wa 2026. Haya ni mapinduzi katika sekta ya afya yanayolenga kumgusa kila mtanzania.

Kabla ya kutazama kwa undani tuanzie hapa:

Watanzania tuko katika makundi mawili: Kuna wale ambao wakiumwa hawana wasiwasi, wanajua bima yao ipo. Watu hawa huenda hospitali wakiwa na furaha na tabasamu kwa kuwa mara nyingi hawana gharama ya ziada kwenye matibabu au wanatakiwa kuongeza pesa kidogo kukamilisha matibabu yao (top-up).

Kwa asilimia kubwa, kundi hili linajumuisha waajiriwa wa serikali na sekta binafsi imara takribani zaidi ya watu millioni 1.5, ambapo ukiongeza familia na wategemezi wao jumla ni takriban milioni 5 mpaka 7 kati ya watanzania milioni 61.

Kundi la pili ni akina sisi, homa ikipanda na presha inapanda. Sina pesa nitatibiwaje? Kwa shilingi ngapi? 

Kundi hili ni kubwa sana takriban watu millioni 45 mpaka 48, ambao ni wajasiriamali na wakulima. Hapo ongeza na kundi la wazee, vilema na wale walio katika umaskini uliopindukia.

Ni dhahiri kuwa na bima ya afya kunaleta amani fulani na pia msukumo wa mtu kutaka kwenda hospitali kupima mara kwa mara.

Utafiti uliochapishwa katika PLOS One na ripoti za Tanzania Demographic and Health Survey (TDHS) umeonesha kuwa watu wenye bima wana uwezekano wa kwenda hospitali mara 4 mpaka 5 zaidi ikilinganishwa na wasio na bima wanapohisi kuugua.

Kulingana na TDHS, mwaka 2022, takriban 85% ya watu wenye bima walitumia kituo cha afya katika kipindi cha miezi sita iliyopita, kulinganisha na takriban 40% tu ya wasio na bima.

Wasio na bima mara nyingi husubiri mpaka ugonjwa uwe mkubwa. Sababu kubwa  ni ukosefu wa fedha za papo hapo (out-of-pocket spending).

Lengo kuu la bima ya afya kwa wote

Mnamo Novemba 2023 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Sheria hii ilitiwa sahini  na Rais Samia Suluhu Hassan, mwezi Desemba 2023. 

Baada ya maandalizi ya kanuni, usajili wa wanachama na uwekaji wa mifumo ya TEHAMA ulianza kushika kasi mwaka 2025, na kufikia Januari 26, 2026, mfumo ulianza kutumika rasmi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

Serikali imeanza kwa kusajili, kwanza, wale watu wa kaya maskini ambao ni takriban milioni 1.1 mpaka 1.4 (Kwa mujibu wa  takwimu za TASAF)

Maana na dhumuni kuu la bima hii ni kuhakikisha  kila mtanzania awe na bima ya kupata matibabu ya msingi. Bima hii sio hiari, ni lazima kwa kila mtanzania kulingana na sheria ya bima kwa wote iliyopitishwa na Bunge la Tanzania, Novemba 2023.

Bila shaka bima ya afya kwa wote inaleta ukombozi wa afya kutokana na utofauti wake na utaratibu wa bima wa zamani. Hebu tazama utofauti huo hapa:

Zamani, kifurushi cha kawaida kwa mtu mmoja katika kaya ilikuwa walau TSh 192,000 kwa mtu mmoja katika familia. Maana yake kabla ya bima kwa wote, Baba/Mama wa familia alipaswa achangie takriban TSh 576,000 mpaka 1,152,000/= kupata bima ya familia.

Lakini mpango wa bima ya afya kwa wote unaiwezesha familia nzima – yenye mpaka watu sita (mwanachama, mwenza, na watoto/wategemezi 4) kulipa kiasi cha TSh 150,000/= pekee kumuwezesha kila mwanafamilia kupata huduma ya afya bila kikomo mwaka mzima.

Zamani, kaya maskini walitegemea kupata msamaha wa matibabu kutoka hospitali husika na jambo hili lilikuwa linachukua muda mrefu sana lakini sasa kupitia mpango wa bima kwa wote, famili hizi (takriban watu milioni 1.1 mpaka 1.4million) wanatambuliwa na wanaenda hospitali na bima zao maalum kutibiwa bila usumbufu. 

Pia miaka ya nyumba vifurushi vilikuwa na ukomo wa huduma kulingana na mgonjwa ametibiwa mara ngapi, lakini kwa sasa kifurushi ambacho tayari kimelipiwa kitita cha standard package kinatumika mwaka mzima bila kikomo.

Sasa kwa kifurushi cha familia cha 150,000/= unaweza kupata huduma nyingi tofauti na zamani, mfano kumuona daktari, vipimo vya maabara – karibia vyote, huduma za  mionzi, kulazwa, dawa zote, upasuaji mdogo na mkubwa. Isipokuwa huduma kubwa zaidi kama upasuaji wa urembo (cosmetic surgery), kutibiwa nje ya nchi na kadhalika. Hapo utalazimika kuongeza dau kidogo (top up method).

Bima hii kwa ufupi inawawezesha tajiri na maskini kupata huduma muhimu na lazima kwa binadamu, katika usawa.

Cha kufurahisha zaidi?

Sasa unaweza kulipia kifurushi chako taratibu kwa kuweka kiasi kidogokidogo kwenye account maalumu na kikifikia kiwango cha 150,000/= basi kifurushi chako cha bima kinafunguliwa na unaanza kutibiwa wewe na wategemezi wako.

Tanzania inaingia katika kundi la nchi kadhaa za Africa ambazo tayari zinatekeleza mfumo huu wa bima kwa wote. Mfano nchi ya Rwanda wamekuwa wakitumia mfumo huu na wamefanikiwa kuwahudumia asilimia 90 ya raia wao kupata huduma za afya kupitia bima kwa wote. 

Nchini Ethiopia pia wamefanikiwa  kwa kiwango cha asilimia 111 ya wananchi wao kutafuta na kupata huduma za afya kutokana na kuwa na bima kwa wote. Nchi zingine ni kama Ghana na Kenya.

Nchi zilizoendelea kama Uingereza, huduma ya afya ni bure kabisa kwasababu gharama hulipwa kutoka moja kwa moja kwenye kodi za wananchi kutokana na kwamba wananchi wengi wako katika mfumo unaotambulika na serikali na hivyo ni rahisi kuwakata kodi ya afya.

Kwa tanzania na nchi nilizozitaja za Afrika, bado wananchi wengi wako katika sekta zisizo rasmi (wakulima na wafanyabiashara wadogo) ambao ni ngumu kupata kodi zao kwa ajili ya afya moja kwa moja, hivyo kuchangia kiwango cha kawaida cha 150,000/= kwa familia zenye uchumi wa kawaida, kati na juu.

“Bima  tunayo, huduma tutazipata?”

Baada ya bima kwa wote kuanza ni dhahiri mifumo inatarajiwa kuelemewa kutokana na watanzania wengi kuanza kuhudhuria hospitali kwa wingi.

Pigia picha kwa sasa, hospitali nyingi zinajaa na kuelemewa wagonjwa na kwa asilimia 75% ni wagonjwa wa bima.

Je, baada ya bima kwa wote hospitali zetu zitaweza kubeba idadi hii kubwa ya wagonjwa? Bila shaka hapa kuna mpango maalum wa kuziwezesha hospitali kuwa na idadi kubwa ya dawa, watumishi wa afya na upanuzi wa miundombinu.

Pia mfumo huu wa bima kwa wote utakubaliwa na baadhi ya hospitali ambazo bei elekezi ya serikali haiendani na gharama ya uendeshaji wao? Hapa inaweza kuleta mgongano wa kimaslahi na kupelekea baadhi ya hospitali kushindwa kujiunga.

Lakini yote kwa yote, uwepo wa bima kwa wote ni ukombozi kwa afya zetu watanzania. Watu watakuwa na msukumo wa kutafuta huduma za afya hivyo kuwa na jamii kubwa inayotibiwa kwa ufasaha.

Uwepo wa watu wengi wanaokwenda hospitali utatuonesha wapi kuna changamoto za afya na kuanzia hapo uboreshaji utafuata zaidi na tutakuwa bora zaidi. Waswahili wanasema “Ngoja mvua inyeshe tuone panapovuja, tuzibe!

Serikali inaweza kufanya nini kuongeza ufanisi katika mpango huu?

1. Uwekezaji katika tehama zaidi na mifumo ya kufanya booking watu wakiwa majumbani na kupata appointment kuliko watu kupanga foleni kusubiri kusajiliwa ukiachana na wale wagonjwa wa dharula. 

Huu ni mfumo wa kidigitali na hatuwezi kuukwepa kwa sasa.

2. Serikali ihakikishe inafanya mazungumzo na kupata hospitali nyingi za binafsi kujiunga katika safari hii. Hii itasaidia wagonjwa kutojaa sana kwenye hospitali za serikali na hivyo kuboresha huduma za afya.

3. Serikali ihakikishe swala la dawa, vifaa tiba na watumishi sio kikwazo kwa wagonjwa

Dawa muhimu, manesi, madaktari, wafamasia, maabara na watumishi wengine  wapatikane. Bahati nzuri Tanzania ina mtaji mkubwa wa hawa watu na wengi wako mtaani. 

Wakati tunaingia katika mfumo huu, Tanzania ina uhaba wa watumishi wa afya kwa kiwango cha asilimia 48 mpaka 52. Serikali ijitahidi kupunguza hii dosari kabla bima hii haijaanza kuchangamka la sivyo hali itakuwa mbaya.

4. Kufanya kazi na wadau binafsi wa afya ambao wako katika uwanja wa kidijitali

Mfano wagonjwa waweze kutumia bima zao kupata huduma ya kuongea na daktari kupitia applications zilizosajiliwa na serikali au zinazofanya kazi na serikali mfano application ya TanzMed ambayo inaruhusu wagonjwa kuongea na daktari wakiwa mahala popote. 

Hii itapunguza msongamano wa wagonjwa wanaokuja hospitali kwa changamoto ndogo kama mafua, maumivu ya viungo, msongo wa mawazo, ushauri wa uzazi, ushauri wa mimba, changamoto za awali za uzazi. Kiufupi serikali ifanye kazi na wadau wanaotumia tehama kurahisisha utoaji wa afya.

5. Kufanya kazi kwa ukaribu na wadau wa afya wanaoelimisha jamii

Hii itapunguza safari za hospitali zinazohitaji elimu ya afya tu. Tanzania kuna blog za afya kama abiteafya.com ambao kazi yao kubwa ni kulimisha jamii kwa lugha ya kiswahili kwa kuchambua changamoto ngumu katika lugha rahisi ya kueleweka. 

Elimu kubwa ikiwemo kutafsiri miongozo ya afya kwa lugha rahisi inayoeleweka itasaidia watu kuweza kujikinga na maradhi mengi hivyo kutoumwa mara kwa mara. Hii itapunguza mzigo kwenye vifurushi hivi vya bima na kuwezesha watu wenye shida kubwa na za lazima kupata huduma stahiki.

Nchi kama Marekani zimetumia njia hii kuelimisha jamii zao na kupunguza idadi kubwa ya watu kuja hospitali. Mfano, Marekani wanafanya kazi kwa ukaribu na tovuti kama Mayo Clinic na WebMd kuchapisha makala nyingi za afya ambazo wananchi wanazisoma sana na hivyo elimu kubwa ya afya inawafikia wananchi na kupunguza misongamano mikubwa mahospitalini. 

Tovuti hizi zimekuwa kama chujio la kwanza hasa kwa zile changamoto ambazo mgonjwa anaweza kuzitatua mwenyewe nyumbani. Hivyo kutoa nafasi kwa wale wagonjwa kweli kweli kuja hospitali na kuhudumiwa vizuri.

Wakati wa majanga (kama COVID-19), Google na Serikali ya Marekani  walishirikiana na Mayo Clinic  na WebMD  ili mtu akitafuta dalili, taarifa za kitaalamu zitokee kwanza. Hii ilisaidia zaidi ya watu milioni kubaki nyumbani badala ya kukimbilia hospitali bila sababu ya msingi.

Mwisho

Katika swala la bima kwa wote, serikali itarajie kukutana na vikwazo kadhaa kutoka kwa wananchi kama kusuasua kulipia bima kutokana na mtazamo hasi, ukosefu wa elimu, itikadi za kidini n.k. hivyo lazima iwepo kampeni kubwa ya kutangaza na kuongelea hii bima kwa wote kwa kuelimisha jamii kwa upana zaidi na kwa nguvu kubwa kupitia makanisani, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. 

Hapo ndipo tovuti kama abiteafya.com zitakavokuwa na umuhimu katika kufanya kazi na serikali kuelimisha watu wengi kwa muda mrefu.

Bila kufanya jitihada kubwa za uelimishaji na uhamasishaji, tutakuja kurudi kule kwenye zama za kodi ya kichwa, miaka ya 1960 mpaka 90, wanaume walilazimika kuhama makazi yao kwa kukimbia kodi ya kichwa.

Bila bima kwa wote, wastani wa kuishi kwa mtanzania mpaka kufikia 2026 ilikuwa ni mika 67 mpaka miaka 70. Sasa kuanza kwa bima ya afya kwa wote inaweza kuongeza umri wa kuishi mpaka miaka 80.

Unapenda kuishi muda mrefu? Basi sema “Karibu bima ya afya kwa wote, karibu uibariki familia yangu kwa  uhakika wa matibabu”.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW