Kinga ni Bora Kuliko Tiba: Jinsi El Niño Inavyoweza Kuathiri Afya Baada ya Mvua Kubwa

Je, umesikia kuhusu El Niño? El Niño ni hali ya mabadiliko ya hali ya hewa inayoweza kusababisha mvua nyingi kuliko kawaida.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeonya kuwa mvua za Vuli za Oktoba hadi Desemba 2026 zitaathiriwa na El Niño yenye nguvu sana.

El Nino Heavy Rains

Mvua zinatarajiwa kuongezeka Novemba na kuendelea hadi Januari 2027. Maeneo yanayotabiriwa kuathiriwa zaidi na mvua hizo ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Unguja na Pemba, mikoa ya kanda ya Ziwa Victoria (Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara) na kaskazini mwa Kigoma.  

Mvua ni baraka kwa wakulima na chanzo muhimu cha maisha. Lakini inaponyesha kwa wingi na kwa muda mfupi, inaweza kuleta mafuriko na kuongeza hatari ya magonjwa. Na hatari za kiafya hazikomi mvua inapokoma.  

Maji machafu na madimbwi yanayobaki baada ya mvua huweka mazingira yanayoweza kusababisha na kueneza magonjwa.

Jiandae kabla mvua haijaanza  

  • Fuatilia taarifa za TMA na maelekezo kutoka kwa mamlaka husika.  
  • Hifadhi maji safi, sabuni, ORS na dawa muhimu za matumizi ya kawaida.  
  • Safisha mifereji ili kuruhusu maji kupita vizuri na kupunguza hatari ya mafuriko.  
  • Andaa mahali salama pa kwenda endapo unaishi katika eneo linaloweza kuathiriwa na mafuriko.  
  • Ikiwa una ugonjwa wa muda mrefu kama presha, kisukari, VVU au TB, hakikisha una dawa zako za kutosha na unazihifadhi sehemu salama.  
  • Ikiwa wewe ni mjamzito, panga mapema mahali pa kujifungulia na usafiri wa kufika kituo cha afya. 

Magonjwa ya Kuangalia kwa Hiki Kipindi:

1. Kipindupindu, Kuhara na Typhoid

Mafuriko yanaweza kuchanganya maji ya kunywa na maji taka, na hivyo kuongeza hatari ya magonjwa kama kipindupindu, kuhara na typhoid. Watoto wako kwenye hatari kubwa ya kupoteza maji mwilini wanapoharisha.  

Hivyo:  

  • Chemsha maji ya kunywa au yatibu kwa kutumia njia salama ya kutakasa maji.  
  • Nawa mikono kwa sabuni na maji safi baada ya kutoka chooni na kabla ya kuandaa au kula chakula.  
  • Mtu anayeharisha apewe ORS mara kwa mara ili kuzuia upungufu wa maji mwilini.  
  • Endelea kumpa mtoto au mgonjwa vinywaji na chakula anachoweza kuvumilia.  
  • Ikiwa mgonjwa anatapika kila kitu, ana dalili za upungufu wa maji mwilini, anapata damu kwenye choo, au mtoto anaonekana dhaifu sana, mpeleke kituo cha afya haraka.  

2. Malaria na Magonjwa Yanayoweza na Mbu

Maji yaliyotuama baada ya mvua hutoa mazingira mazuri kwa mbu kuzaliana. Hii inaweza kuongeza hatari ya malaria na magonjwa mengine yanayoenezwa na mbu, kama dengue na Malaria.  

Hivyo:  

  • Ondoa maji yaliyotuama kwenye matairi, makopo, vyombo na maeneo mengine yanayoweza kuhifadhi maji.  
  • Lala ndani ya chandarua kilichowekwa dawa kila usiku.  
  • Ukipata homa, kutetemeka au dalili nyingine zinazofanana na malaria, nenda kituo cha afya kwa uchunguzi mapema.  
  • Endelea kuzingatia hatua za kujikinga na mbu, hasa baada ya mvua kunyesha.  

3. Ngozi 

Maji ya mafuriko yanaweza kuwa na uchafu na vijidudu vinavyoweza kusababisha maambukizi ya ngozi. Kutembea kwenye maji ya mafuriko bila kinga huongeza hatari ya kupata changamoto mbalimbali za ngozi.

Hivyo:  

  • Epuka kutembea kwenye maji ya mafuriko bila viatu. Vaa viatu au buti zinazofunika miguu.  
  • Osha sehemu ya mwili iliyogusana na maji ya mafuriko kwa maji safi na sabuni.  
  • Safisha na funika majeraha au michubuko mapema ili kupunguza hatari ya maambukizi.  
  • Badilisha nguo zilizolowa na uoshe mwili baada ya kugusana na maji ya mafuriko.  
  • Ukipata homa, maumivu ya misuli, kichwa kuuma au dalili nyingine baada ya kugusana na maji ya mafuriko, nenda kituo cha afya kwa uchunguzi.  

4. Kikohozi na Magonjwa ya Njia ya Hewa

Makazi ya muda yenye msongamano huongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa ya njia ya hewa. Hewa safi na mzunguko mzuri wa hewa husaidia kupunguza hatari hii.

Hivyo:  

  • Hakikisha hewa inapita vizuri ndani ya makazi na epuka msongamano inapowezekana.  
  • Funika mdomo na pua unapokohoa au kupiga chafya.  
  • Mtu mwenye kikohozi kinachoendelea, kikohozi kikali au kupumua kwa shida afike kituo cha afya kwa uchunguzi.  
  • Watoto, wazee na watu wenye magonjwa sugu wanahitaji uangalizi zaidi wakianza kupata dalili za njia ya hewa  

5. Chakula na Usalama wa Chakula 

Mafuriko yanaweza kuchafua chakula na kuongeza hatari ya magonjwa ya tumbo. Chakula kilichoguswa na maji ya mafuriko kinaweza kuwa na vijidudu hatari, hivyo hakifai kuliwa.  

  • Tupa chakula kilichoguswa na maji ya mafuriko.  
  • Pika chakula vizuri na funika ili kukilinda dhidi ya uchafu na wadudu.  
  • Nawa mikono kwa sabuni kabla ya kuandaa au kula chakula.  
  • Hifadhi chakula sehemu safi na salama, mbali na maji ya mafuriko.  
  • Chakula kinapopungua, watoto na wajawazito wapewe kipaumbele ili kupunguza hatari ya utapiamlo.  

Afya ya Akili

Baada ya mafuriko, si nyumba na mali pekee zinazoweza kupotea. Watu wanaweza pia kupoteza wapendwa wao, usalama na utulivu wa maisha.

Hali hii inaweza kuleta hofu, huzuni, msongo wa mawazo au kukosa usingizi.  

Usimwache mtu anayepitia hali hii peke yake. Msikilize, mpe moyo na msaidie kupata mahitaji ya msingi. Ikiwa huzuni, hofu au kukosa usingizi vinaendelea na kuathiri maisha ya kila siku, msaidie kupata huduma kutoka kwa mhudumu wa afya.

Kwa Ufupi:

  • Fuatilia taarifa za TMA na maelekezo ya mamlaka husika.  
  • Kunywa maji salama.  
  • Nawa mikono kwa sabuni.  
  • Ondoa maji yaliyotuama.  
  • Lala ndani ya chandarua.  
  • Epuka kugusa au kutembea kwenye maji ya mafuriko.  
  • Tafuta huduma ya afya mapema unapopata dalili za ugonjwa.

Mwisho

El Niño haiwezi kuzuiwa, lakini madhara yake kwa afya yanaweza kupunguzwa kwa maandalizi na tahadhari za mapema.

Linda afya yako, linda familia yako, na wasaidie walio karibu nawe. Kinga ni bora kuliko tiba.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW