Maisha ya kisasa yanawalazimisha watu wengi kukaa kwenye viti kwa saa nane au zaidi kila siku. Watu wengi hutumia muda mwingi wakiwa wamekaa.
Wanafunzi hukaa darasani wakisoma, wafanyakazi hukaa ofisini, na wengi hukaa wakitumia simu au kompyuta.
Ulimwengu tunaoishi sasa sio mkubwa kama ilivyokuwa zamani. Zamani watu walikuwa wakitembea kwenda sokoni, kulima, kuwinda, na kusafiri. Miili ya binadamu iliundwa kwa ajili ya kutembea na kufanya kazi, siyo kutulia mahali pamoja kwa muda mrefu.
Je, Sayansi inasema nini kuhusu kukaa muda mrefu?
Tafiti nyingi za kitabibu zinaonyesha kuwa kukaa zaidi ya saa 6 hadi 8 kwa siku huongeza hatari ya magonjwa ya moyo, kisukari aina ya pili (diabetic mellitus type two), na unene kupita kiasi.
Tafiti za afya ya umma zinaonyesha kukaa zaidi ya saa 6 hadi 8 kwa siku huongeza hatari ya magonjwa sugu. Kwa mujibu wa World Health Organization (WHO), takribani asilimia 27 ya watu wazima duniani hawafanyi shughuli za mwili za kutosha.
Ripoti za Centers for Disease Control and Prevention na American Heart Association zinaonyesha pia maisha ya kukaa muda mrefu yanaongeza vifo vya mapema kwa wastani wa asilimia 15 hadi 20.
Unapokaa muda mrefu, misuli ya miguu hutumia nishati kidogo. Hali hii husababisha mabadiliko makuu manne kwenye mwili na kuleta hatari kwenye Afya yako.
1. Magonjwa ya Moyo
Unapokaa muda mrefu, misuli ya miguu hutumia nishati kidogo. Sukari pamoja na mafuta huongezeka kwenye damu.
Kuongezeka huku husababisha insulin kufanya kazi dhaifu na mafuta mabaya (low-density lipoprotein cholesterol – LDL), kujikusanya kwenye kuta za mishipa. Mishipa inapopungua upana, damu hupita kwa shida na shinikizo la damu huongezeka.
Mafuta ya tumboni huongeza uchochezi wa mwili na kuharibu kuta za mishipa. Mabadiliko haya huongeza hatari ya atherosclerosis, mshtuko wa moyo, na kiharusi.
2. Kisukari Aina ya Pili (Diabetic Mellitus Type Two)
Unapokaa muda mrefu bila kusogea, mwili wako hupunguza matumizi ya sukari kwa sababu misuli haitumii nishati ya kutosha. Sukari hubaki kwenye damu kwa muda mrefu kuliko kawaida.
Kadiri hali hii inavyoendelea, seli za mwili hupunguza mwitikio kwa insulin. Insulin hushindwa kuingiza sukari ndani ya seli kwa ufanisi. Sukari huendelea kuongezeka kwenye damu. Hali hii huongeza hatari ya kupata kisukari aina ya pili.
3. Maumivu ya Mgongo na Shingo
Kukaa kwa muda mrefu kunalazimisha uti wa mgongo na shingo kubeba shinikizo kubwa lisilo la asili, jambo linalosababisha misuli kukaza na kupoteza unyumbufu.
Unapoinama mbele kuelekea skrini, unachosha misuli ya mgongo wa chini na kuivuta mishipa ya shingo kupita kiasi, hali inayopelekea maumivu sugu na uchakavu wa mapema wa pingili za uti wa mgongo.
4. Unene Kupita Kiasi
Unapokaa muda mrefu, mwili wako unazima injini ya kuchoma kalori na kuanza kuhifadhi nishati yote kama mafuta, jambo linalopelekea mlundikano wa nyama uzembe sehemu ya tumbo.
Kitambi hiki kinachotokana na kukaa sana ni hatari zaidi kwa sababu kinazunguka viungo vyako vya ndani na kuvuruga mfumo mzima wa umeng’enyaji wa chakula na nishati.
Kwa hayo yote, kuna ukweli?
Ndio ni kweli! Huu hapa chini ni mfano hai kabisa.
Idadi kubwa ya watu wengi tunapo safiri umbali mrefu kwa basi, treni au ndege (bila kusimama), basi kama sio mwisho ni katikati ya safari miguu huwa inavimba au kupata ganzi.
Sasa ipo hivi, unapokaa muda mrefu bila kusogeza miguu, mzunguko wa damu kwenye miguu hupungua na damu hukusanyika kwenye mishipa ya chini. Hali hii husababisha miguu kuvimba, kufa ganzi, au kuhisi uzito.
Ikiendelea kwa muda mrefu huongeza hatari ya damu kuganda kwenye mishipa ya miguu, hali inayojulikana kitaalamu kama deep vein thrombosis.
Sasa ni makundi yapi ya watu yapo kwenye hatari zaidi?
Haya hapa ni baadhi ya makundi ya watu yalio kwenye hatari zaidi:
● Wafanyakazi wa ofisini.
● Madereva wa masafa marefu.
● Wanafunzi wanaosoma muda mrefu bila mapumziko.
● Watu wanaotumia simu na kompyuta muda mwingi.
Je, Nifanye Nini Kujilinda?
Kama ilivyo kawaida na muhimu kwamba kinga ni bora kuliko tiba, hizi ni baadhi ya njia rahisi sana za kuweza kuzuia madhara na kulinda mwili wako:
● Simama kila baada ya dakika 30 hadi 60 kwa maana ya kwamba kila baada ya dakika 30 za kukaa simama au tembea kwa dakika 2 hadi 5. Hii tunaita kanuni ya 30 ( rule of 30).
● Fanya mazoezi ya kunyosha mwili: Nyosha shingo, mgongo, mabega, na miguu ili kupunguza msongo wa misuli.
● Tumia ngazi badala ya lifti: Hii ni kwasababu hatua ndogo za kila siku huongeza matumizi ya nishati.
● Punguza muda wa kutumia simu ukiwa umekaa, hapa jaribu kusimama au kutembea unapopiga simu.
● Fanya mazoezi angalau dakika 20 kwa siku sawa na Dakika 140 kwa wiki (Tembea
haraka, kimbia polepole, au fanya mazoezi ya nyumbani).
Kama ilivyo kawaida yetu Watanzania: “Kizuri shiriki na mwenzako!” Basi fikisha huu ujumbe kwa jamii.
Kukaa ni sehemu ya maisha ya kila siku, lakini kukaa muda mrefu bila kusimama huongeza hatari ya magonjwa sugu.
Unapobadilisha tabia ndogo kila siku, unapunguza hatari kubwa za kiafya. Mwili wako unahitaji mwendo ili mifumo yake ifanye kazi kwa ufanisi.
I am a healthcare provider. I focus on sharing clear, evidence based health information through articles and social media.
My goal is to help you understand healthily life. I believe accurate health information improves decisions and lives.
