Kila mtu atakufa, hilo halina ubishi kabisa. Swali ni kwamba, utakufa lini? Utakufaje ? Katika mazingira yapi? Je, unaamini kuna vifo vinavyosababishwa na ukosefu wa elimu?
Leo hii ukipatwa na dharula ya mtu wako kuanguka ghafla au ukikutana na mtu amedondoka ghafla utachukua hatua gani? Kuwa mkweli, utaita gari ya dharula au utamuitia bajaji?

Katika familia nyingi za kitanzania, mgonjwa akianguka au kuzidiwa ghafla huwa hawakumbuki gari ya dharula (ambulance) bali watampakia haraka kwenye gari au boda na kumkimbiza hospitali.
Kulingana na makadirio ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mwaka 2025/2026, takriban watu 10,000 hupoteza maisha kila mwaka nchini Tanzania kutokana na ajali za barabarani.
Ripoti ya World Bank na UN Road Safety Fund (2024) inaonyesha kuwa idadi kubwa ya vifo hivi hutokea kabla ya kufika hospitalini (pre-hospital deaths).
Wagonjwa wengi husafirishwa kwa kutumia bodaboda, taksi, au magari ya polisi ambayo hayana vifaa vya kuimarisha hali ya mgonjwa (resuscitation equipment) wala watumishi wenye ujuzi.
Udhaifu mkubwa wa mpango wa dharula kuanzia kwenye elimu kwa jamii, mpango mzima wa kuchukua hatua za mapema, ukosefu wa elimu ya huduma ya kwanza (First Aid) kwa madereva na miundombinu kama barabara ambayo sio rafiki kwa dharula ni vyanzo vikubwa vya vifo hivi.
Tanzania imechukua hatua gani katika kuongeza ufanisi wa huduma za dharula?
Tanzania kupitia Wizara ya Afya inafanya juhudi kubwa kuhakikisha inaboresha kitengo cha dharula lengo likiwa ni kupunguza idadi ya vifo nchini.
Baadhi ya mambo ambayo Wizara ya Afya inafanya kazi kubwa kuboresha katika idara ya dharula ni kama ifuatavyo:
1. Ujumuishaji huduma ya dharula katika Sera ya Kitaifa
Tanzania ni nchi ya kwanza kurasimisha Huduma Muhimu za Dharura na Mahututi (EECC) katika sera ya kitaifa.
Hii inahakikisha kuwa huduma za msingi za kuokoa maisha (oksijeni, maji ya mwilini, na ufuatiliaji wa mgonjwa) zinapewa kipaumbele katika wodi zote za hospitali, siyo tu kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU). Mpango huu ulianza kufanyiwa kazi tangu 2023.
2. Upanuzi wa Idara za Dharura (EMD)
Kupitia mipango ya kukabiliana na COVID-19, Tanzania imejenga na kuboresha zaidi ya Idara za Tiba ya Dharura (EMDs) 80 katika vituo vya afya vya msingi na 35 katika hospitali za mikoa.
3. Mafunzo Maalum
Tangu mwaka 2013, Tanzania imefundisha zaidi ya madaktari bingwa 88 wa tiba ya dharura na maelfu ya wauguzi, wahudumu wa dharura (paramedics), na wataalamu wa afya, hasa kupitia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
4. Usambazaji wa Huduma ya Msingi ya Dharura (BEC)
Chama cha Tiba ya Dharura Tanzania (EMAT) kinashirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya zaidi ya 1,600 katika huduma za msingi za dharura kwa mwaka 2024, kikizingatia mbinu za kuokoa na kuimarisha hali ya mgonjwa.
5. Ukuaji wa Idara za Tiba ya Dharura (EMD)
Sekta hii inazidi kukua, huku Idara ya Dharura katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ikitoa mfano wa huduma kwa wagonjwa wengi, jambo ambalo limepunguza vifo kwa kiasi kikubwa.
Ni dhahiri Tanzania kupitia Wizara ya Afya inafanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba watu wanapata huduma ya dharula hasa katika kuhakikisha wataalamu na miundombinu ya dharura inawezeshwa.
Pamoja na hayo yote, bado kuna dalili kubwa ya watu kutotambua na kutotumia fursa hizi kwa kiwango cha juu.
Tatizo liko wapi sasa?
Tatizo kubwa ni elimu ya dharula. Jamii haina elimu ya kutosha kuhusu mambo ya dharura.
Tarehe 11 Machi, tasnia ya habari ilimpoteza Mhe. Denis Busulwa, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi mwenza wa kituo cha redio cha EFM na televisheni ya E-TV.
Alikuwa mmoja wa wafanyabiashara na wabunifu mashuhuri katika sekta ya habari na burudani nchini Tanzania.
Mr. Denis alipata dharula na akafariki nyumbani kwake. Katika maelezo ya dereva wake, alianza kujiskia vibaya na akapelekwa nyumbani. Presha yake ilikuwa imeshuka.
Badala ya dereva kupiga simu kitengo cha dharula, alichagua kumfanyia maombi na presha ilipokuwa bado haipandi aliongeza maombi na baadaye Mr. Denis akafariki akiwa nyumbani kwake.
Unadhani hakukuwa na haja ya dereva wake kuomba msaada wa dharula huku akiendelea na maombi?
Familia ya marehemu walikuwa na uwezo wa kukodi gari la dharula binafsi (ambulance) hivyo shida hapa sio uchumi bali ni kukosekana kwa uelewa wa mambo ya dharula.
Wengi tumemlaumu sana kwanini hakuita gari la dharula? Hapa tunarudi pale pale, pamoja na ujuzi wa kuendesha gari, dereva hajawahi kupata mafunzo ya elimu ya dharura kama ilivyo kwa madereva wengi katika nchi yetu. Nani analaumiwa hapa?
Kwanini hili linajitokeza?
Serikali na wadau wanafanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu lakini namna ya kufikisha elimu kwa watu imekuwa ngumu sana kwasababu sehemu kuu ambapo watu wanatakiwa kupata elimu (mfano, mashuleni, vyuoni, kanisani na vyombo vya habari), mada ya dharula haifundishwi kwa muendelezo wa kiwango cha kujenga uwezo.
Somo la huduma ya kwanza shuleni ni mada moja tu amabayo husomwa na kufanyiwa mtihani na kufunikwa. Ni dhahiri tuna kazi kubwa ya kufanya.
Bila elimu ya kutosha kuhusu dharula bado tutaendelea kumsingizia Mungu kwa vifo ambavyo hata sisi tunaweza kuvipunguza.
Sote tulishuhudia namna ambavyo uelimishaji mkubwa umepunguza kabisa vifo vya albino na ukeketaji wa wanawake Afrika.
Nini kifanyike kwenye dharula (emergency) Tanzania?
1. Elimu ya huduma ya kwanza iwe somo darasani
Kama ambavyo kuna somo la stadi za kazi, hisabati au sayansi, kuwe pia na somo la dharula ambapo wanafunzi watafundisha namna tofauti za kupambana na dharula ikiwemo kujifunza namna ya kutoa huduma za kwanza kwa changamoto za mara kwa mara katika jamii.
Hii itatengeneza kizazi ambacho kinajua maana ya dharura na umuhimu ya utaalamu katika dharula. Somo hili likisomwa kuanzia darasa la kwanza mpaka la sita na sekondari tutakuwa na kizazi ambacho kiko tayari kuokoa uhai. Tutaongeza nguvu kazi ya taifa.
Mfano mzuri ni nchi kama Norway, Uingereza na Marekani. Nchi hizi katika mtaala wake wa elimu, somo la huduma ya kwanza ni lazima kwa kila mwanafunzi.
2. Vyanzo vikuu vya elimu kama vituo vya redio, taasisi binafsi zipewe ulazima wa kuongelea na kuelimisha maswala ya dharula
Ukiangalia katika vituo vingi vya redio, swala la afya hupewa muda wa nusu saa tu, na ni marachache kupata mada hizi za dharula. Radio zetu hutumia muda mwingi kwenye kuzungumzia michezo, sanaa ya muziki, mapishi na mapenzi.
Serikali iweke sera ambapo vyombo hivi viwe na mada za afya za dharula mara kwa mara. Hii ndio njia ya kuelimisha sehemu kubwa ya jamii.
3. Serikali iweke sera inayozuia wagonjwa walio katika dharula au hatari kubebwa kwa usafiri holela
Hii iwe kama ile sheria ya barabarani inayolazimisha abiria kutobebwa kwenye malori au pick up. Sera hii ikiwa na sheria kali itailazimisha jamii kuanza kuzipa kipaumbele gari za dharula (ambulances).
Sababu kubwa inayofanya wadau wengi binafsi wasiikuze huduma ya dharula ni kwasababu ya muitikio mdogo wa jamii na hivyo kufanya biashara hii kuwa ya gharama sana na kuwepo gari chache za dharula katika miji.
Sera hii itaongeza huduma ya gari za dharula kuwa kubwa na gharama za usafiri kuwa chini na vifo vitapungua. Nchi kama Afrika Kusini, Rwanda na Misri wamejitahidi kwa kiwango kikubwa kulitekeleza hili kwenye sera zao.
4. Ushirikiano na wadau binafsi wa afya
Serikali ishirikiane na wadau wa afya kusaidia kutafsiri shughuli wanazozifanya kuwa katika kuelimisha na kuongeza nguvu kazi ya uelimishaji. Tasisi ya kiserikali OSHA Tanzania inajitahidi sana kutoa elimu na mafunzo kwa wafanyakazi wengi wa taasisi takriban 5,000 mpaka 8,000 kila mwaka, lakini bado idadi ni ndogo ukiangalia idadi ya watanzania million 70.
Bila shaka ni wakati sahihi wa taasisi kama OSHA kushirikiana na wadau wengine wa afya kama blogu ya Abite Afya kufikia watu wengi zaidi tanzania.
Mfano mzuri hapa ni namna ambavyo nchi ya Marekani wanafanya kazi na tovuti maarufu kama Mayo Clinic na WebMD kuchapisha maelfu ya makala za afya zinazosaidia sana kuelimisha jamii kwa ukubwa.
Uingereza wao hufanya upatikanaji mkubwa wa elimu ya afya kupitia uchapishaji wa makala nyingi za afya kupitia tovuti ya First Aid – NHS. Tovuti hii imekuwa ndio maktaba ya elimu ya afya ya dharura kwa jamii.
Mashirika ya kiserikali yakishirikiana na taasisi za uelimishaji tanzania tutakuwa na hazina kubwa ya uelimishaji ambayo ndio itakuwa uti wa mgongo wa changamoto za dharula.
5. Kuhakikisha madereva wa vyombo vya moto wote nchi nzima wamepitia mafunzo ya huduma ya kwanza
Madereva wakiwa na elimu na ufahamu wa dharula itasaidia sana kupunguza vifo kabla ya kufika mahospitalini. Kuna mifano kadhaa ya nchi zilizoendelea, tunaweza kuiga hapa na tukapiga hatua, mfano:
Ujerumani na Austria wamefanya lazima kwa kila mwombaji wa leseni ya udereva kupitia mafunzo ya huduma ya kwanza. Hii inahakikisha kuwa karibu kila dereva barabarani ni “first responder” anayeweza kusaidia ajali inapotokea.
Huduma ya kwanza Tanzania bado inaonekana ni kwa ajili ya watu wa afya tu kama madaktari, manesi, na kadhalika. Hii ndio dhana potofu ambayo inabidi tupambane kuiondoa.
Mwisho
Wewe ni mmiliki wa taasisi tanzania ? Usikubali kukaa na wafanyakazi ambao hawana mafunzo ya huduma ya kwanza. Jiulize siku ukijikuta katika mazingira ya marehemu Mr. Dennis Busulwa utaokolewa? Huduma ya kwanza sio kwaajili ya watu wa afya tu bali kila mwananchi mwenye akili timamu.
Wasiliana na moja kati ya taasisi hizi hapa kujua utaratibu wa taasisi yako kupatiwa mafunzo hayo.
Taasisi ya “OSHA” huendesha mafunzo haya nchi nzima kupitia kanda zake. Kwa mujibu wa kalenda ya mafunzo ya 2025/2026. Tembelea tovuti yao kuona ratiba zao.
Taasisi ya “City Ambulance Tanzania – Inspired To Save Life” pia wanatoa huduma ya gari la dharula na mafunzo ya huduma ya kwanza kwa taasisi na watu binafsi. Tembelea tovuti yao kuona ratiba zao.
Taasisi ya “Emergency Medicine Association of Tanzania” pia wanatoa mafunzo hayo kwa wafanyakazi wa afya katika taasisi mbali mbali, polisi na hata raia wa kawaida.
“Abiteafya.com” ni tovuti ya kitanzania amabyo inatumia makala za afya kuelimisha jamii. Huduma zetu za uandishi wa makala na health campaign management zinaweza kuisaidia taasisi yako kufikia watu wengi zaidi na kuisaidia nchi hii kufika mbali katika uelimishaji wa jamii kiafya.
Tunazikaribisha taasisi za kiserikali na binafsi kufanya kazi na sisi kuifikia jamii kwa ukubwa. Pamoja tunajenga!
Tumia Links Hizi kwa Ajili ya Reference:
- Global status report on road safety 2023
- Pan-African Med Journal
- The impact of introducing ambulance and delivery fees in a rural hospital in Tanzania
- Public Health Matters
- First aid – Mayo Clinic
- African Journal of Emergency Medicine | ScienceDirect.com by Elsevier

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.
