“Nikitumia mto wakati wa kulala, naweza kuharibu shingo au mgongo?”
“Ni bora kulala bila mto?”
“Yapi matumizi sahihi ya mto?”
“Ipi ni mitindo sahihi ya kulala?”
Haya ni maswali ambayo watu wengi hujiuliza.

Ukweli ni kwamba hakuna jibu moja linalofaa kwa kila mtu. Kutumia mto kunaweza kuwa na manufaa, hasa ikiwa unatumika kwa urefu na namna inayosaidia shingo na mgongo kukaa katika mkao unaofaa.
Mto ni kifaa muhimu sana wakati wa kulala. Lengo la mto si kuinua kichwa tu, bali kusaidia kichwa, shingo na mgongo kuwa katika mkao unaofaa wakati wa kulala.
Hatua za Matumizi ya Mto
Hatua ya 1: Tambua Mlalo Unaolalia
Mkao unaotumia kulala una umuhimu katika kuchagua mto.
Ukilala Chali
Kama unapenda kulala chali, tumia mto unaosaidia shingo bila kuinua kichwa kupita kiasi. Mto wenye unene wa wastani unaweza kusaidia kichwa na shingo kukaa katika mkao unaofaa.
Kwa baadhi ya watu, kuweka mto mdogo chini ya magoti kunaweza pia kusaidia kupunguza msongo kwenye sehemu ya chini ya mgongo.
Faida nyingine ya matumizi ya mto katika mlalo wa chali ni kusadia kupumua vizuri na kuzuia ndoto mbaya za kuhisi kukabwa kutokana na kushindwa kupumua vizuri.
Mto unastahili kuwa chini kidogo ya mabega ili kusaidia kichwa kuwa juu kidogo bila kukipindisha katika mkao usio sahihi.

Ukilala ubavu
Kama unalala kwa ubavu, mara nyingi unahitaji mto wenye unene unaotosha kujaza nafasi kati ya kichwa na godoro eneo la shingo. Mto ukiwa mwembamba sana, kichwa kinaweza kushuka kuelekea kwenye godoro. Ukiwa mnene sana, kichwa kinaweza kuinuliwa kupita kiasi.
Hali zote mbili zinaweza kufanya shingo ikae katika mkao usiofaa. Katika mlalo huu mto haupaswi kuwa katika sehemu ya bega bali kuwa baada ya bega kushikilia kichwa.

Ukilala kifudifudi
Kulala kifudifudi kunaweza kulazimisha shingo kugeuzwa upande mmoja kwa muda mrefu. Kwa baadhi ya watu, hali hii inaweza kuchangia usumbufu au maumivu ya shingo na mgongo. Ikiwezekana, jaribu kuzoea kulala chali au ubavu.
Haishauriwi kabisa kulala kifudifudi ili kuepuka maumivu au matatizo ya shingo.
Hatua ya 2: Chagua Mto Unaokufaa
Usichague mto kwa kuangalia ulaini au uzuri wake pekee.
Zingatia:
- Ukubwa wa mto: Usiwe mkubwa sana wala mdogo sana kulingana na mkao wako.
- Ugumu: Mto usiwe mgumu kupita kiasi cha kusukuma kichwa juu, wala laini kiasi cha kupoteza umbo kabisa.
- Mkao wa shingo: Unapolala, kichwa na shingo vinapaswa kuwa katika mkao unaojisikia wa kawaida, bila kuinamishwa sana mbele, nyuma au upande.
- Faraja (comfort): Mto unaofaa mtu mwingine si lazima ukufae wewe.
Kumbuka kwamba mto mzuri si lazima uwe wa gharama kubwa. Muhimu ni kama unakusaidia kupata mkao mzuri na usingizi wenye utulivu.
Kwa wenye matatizo maalumu yaliyothibitishwa na wataalam wa afya, hupendekezwa kutumia mto maalumu kwa ajili ya shingo (cervical pillow).

Hatua ya 3: Angalia mkao wa mwili wote
Usizingatie kichwa pekee. Mkao mzuri wa kulala unahusisha mwili mzima.
Hakikisha godoro na mto vinakupa msaada unaokufanya ujisikie vizuri. Kwa anayelala ubavu, mto kati ya magoti unaweza kusaidia baadhi ya watu kuweka nyonga na miguu katika mkao unaostarehesha.

Kwa anayelala chali, mto mdogo chini ya magoti unaweza pia kuwa wa msaada kwa baadhi ya watu.

Hatua ya 4: Sikiliza Mwili Wako
Mto unaokufaa unapaswa kukusaidia, si kukuongezea matatizo.
Jiulize:
- Je, naamka na maumivu ya shingo au kichwa?
- Je, naamka na maumivu ya mgongo?
- Je, nahisi shingo imekakamaa kila ninapoamka?
- Je, mto wangu unanifanya kichwa kiwe juu sana?
- Je, mto unanifanya kichwa kishuke sana?
- Je, naamka na uchovu sana?
Kama dalili hizi zinajitokeza mara kwa mara, jaribu kurekebisha mlalo au kubadilisha mto.
Hatua ya 5: Usilazimishe mto mmoja kwa kila mtu
Watoto, watu wazima, wazee na watu wenye matatizo mbalimbali ya shingo au mgongo wanaweza kuwa na mahitaji tofauti. Vilevile, mtu mwenye maumivu ya shingo au mgongo anaweza kuhitaji ushauri maalumu kulingana na chanzo cha tatizo.
Kwa hiyo, hakuna sheria kwamba kila mtu lazima atumie mto mmoja, mito miwili au alale bila mto. Kinachofaa ni kile kinachosaidia mwili wako kukaa katika mkao mzuri na kukupa usingizi wenye utulivu ingawa matumizi ya mto ni muhimu kwa milalo ya aina zote mbili.
Ni Wakati Gani Unapaswa Kumuona Mtaalamu?
Kama una maumivu ya shingo au mgongo yanayoendelea, usifikiri kila mara kwamba chanzo ni mto.
Muone mtaalamu wa afya ikiwa:
- Maumivu yanaendelea au yanazidi.
- Maumivu yanarudia mara kwa mara bila sababu inayoeleweka.
- Unapata ganzi, kuchomachoma au udhaifu kwenye mikono au miguu.
- Maumivu yanaenea kutoka shingoni kwenda begani au mkononi.
- Maumivu yameanza baada ya kuanguka, ajali au jeraha.
- Maumivu yanaathiri usingizi au shughuli zako za kila siku.
Mtaalamu wa fiziotherapi anaweza kutathmini mlalo wako, shughuli za mwili na sababu zinazoweza kuchangia maumivu, kisha kukushauri kuhusu mkao wa kulala na hatua nyingine zinazofaa.
Hitimisho
Ndiyo, ni sahihi kutumia mto wakati wa kulala na ni muhimu sana ikiwa unakusaidia kuweka kichwa na shingo katika mkao unaofaa na unakupa usingizi wenye utulivu.
Usiamue kutumia au kuacha kutumia mto kwa sababu tu umeambiwa kwamba “mto ni mbaya” au “kulala bila mto ni bora.” Mahitaji ya mtu mmoja yanaweza kutofautiana na ya mwingine.
Kanuni rahisi ni hii:
“Chagua mto unaolingana na mkao wako wa kulala, unaosaidia shingo na kichwa, na usiosababisha maumivu au usumbufu. Usingizi mzuri hauhusiani na muda wa kulala pekee; mkao unaolala na mazingira ya usingizi pia ni muhimu.”
Karibu Rally Polyclinic kitengo cha fiziotherapi kwa uchunguzi, ushauri na mpango sahihi wa matibabu ya maumivu unayopitia ikiwa ni pamoja na kupata elimu zaidi kuendana na hali uliyonayo.
Unaweza kuwasiliana nasi kupitia simu namba +255 786 240 204 kwa taarifa na maelekezo kamili. Karibu Sana!

Joseph Kisima ni Mfiziotherapia (Physiotherapist) mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 13 katika tasnia ya fiziotherapi na kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za afya serikalini na sekta binafsi, ikiwemo Aga Khan na CCBRT.
Kwa sasa anaendesha Rally Polyclinic na pia hushirikiana na St. Monica Modern Health Center kutoa huduma za fiziotherapi. Ana utaalamu na uzoefu katika matibabu ya maumivu pamoja na urekebishaji wa wagonjwa wenye magonjwa yanayosababisha kupooza, hususani stroke/kiharusi.
Mbali na taaluma yake, ni mwandishi wa vitabu vya elimu ya afya kwa jamii. Ana kitabu kuhusu kiharusi ambacho hakijachapishwa, na anaandaa kitabu kingine kuhusu mtindio wa ubongo, changamoto zake na huduma kwa watoto.
