“Mgongo wangu umekuwa ukiniuma kwa muda mrefu. Nimetumia dawa mbalimbali na mazoezi, lakini baada ya muda maumivu yanarudi. Je, kweli maumivu ya mgongo au kiuno yanaweza kuisha kabisa?”
Hili ni swali linaloulizwa na watu wengi. Maumivu ya mgongo au kiuno ni tatizo linaloweza kumpata mtu wa umri wowote. Wakati mwingine huanza baada ya kufanya kazi nzito, kunyanyua kitu/vitu vizito, kukaa muda mrefu au kufanya shughuli zisizozoeleka.

Kwa wengine, maumivu yanaweza kuendelea kwa muda mrefu na kuathiri kazi, usingizi na shughuli za kila siku.
Habari njema ni kwamba maumivu mengi ya mgongo na kiuno yanaweza kutibiwa na kudhibitiwa vizuri, na watu wengi hurudi katika shughuli zao za kawaida. Hata hivyo, si kila maumivu yana sababu moja, na si kila mtu anaweza kupata suluhisho kwa kutumia njia ileile.
Kwa Nini Mgongo au Kiuno Huuma?
Mgongo una mifupa, viungo, misuli, mishipa na tishu nyingine zinazosaidia mwili kusimama, kutembea na kufanya shughuli mbalimbali. Tatizo katika sehemu yoyote kati ya hizi linaweza kusababisha maumivu.
Baadhi ya sababu zinazoweza kuchangia maumivu ya mgongo au kiuno ni:
- Kukaa au kusimama katika mkao mmoja kwa muda mrefu.
- Kufanya kazi inayohitaji kuinama au kunyanyua vitu mara kwa mara.
- Kunyanyua kitu/vitu vizito kwa namna isiyo sahihi.
- Misuli ya mgongo na tumbo kuwa dhaifu.
- Kukaa bila kufanya mazoezi au kuwa na shughuli ndogo za mwili.
- Kuumia kutokana na kuanguka, ajali au michezo.
- Mabadiliko yanayotokea kwenye viungo na pingili za mgongo kadiri mtu anavyozeeka.
- Baadhi ya matatizo ya pingili za mgongo yanayoweza kuhusisha mishipa ya fahamu.
- Uzito mkubwa wa mwili, ambao unaweza kuongeza mzigo kwenye mfumo wa mgongo.
- Msongo wa mawazo, usingizi hafifu na uchovu, ambao kwa baadhi ya watu unaweza kuongeza au kuendeleza maumivu.
Muhimu kuelewa ni kwamba maumivu si ugonjwa bali ni ishara ya kuwa kuna jambo haliko sawa katika eneo hilo.
Maumivu hutokea kutokana na mambo tofauti tofauti kwenye mifumo ya mwili. Hivyo maumivu sio kitu kibaya kwani hutusaidia kujitambua kabla tatizo halijaumiza sehemu kubwa ya mwili au halijawa kubwa zaidi.
Ndiyo maana ni muhimu kutafuta sababu inayoweza kuwa nyuma ya maumivu badala ya kutegemea dawa pekee.
Je, Dawa Pekee Zinaweza Kutatua Tatizo?
Dawa zinaweza kusaidia kupunguza maumivu kwa baadhi ya watu, lakini mara nyingi dawa pekee hazishughulikii mambo yote yanayoweza kusababisha au kuendeleza maumivu.
Dawa huondoa tu hisia za maumivu kwa kuzuia zisifike kwenye ubongo kwa tafsiri ili kuweza kuyahisi na sio kutibu tatizo lenyewe. Baadhi ya matatizo hupona yenyewe, hivyo mwili hutumia muda ambao dawa inafanya kazi kujitibu na mara dawa inapoisha nguvu hukuta eneo husika limeshajiponya.
Hivyo dawa pekee pasipo kuondoa chanzo cha tatizo haziwezi kuponya maumivu na huweza kupelekea maumivu kuwa sugu.
Kwa mfano, mtu anaweza kutumia dawa na maumivu yakapungua lakini kama bado anakaa muda mrefu katika mkao usiofaa, hafanyi mazoezi au anaendelea na shughuli iliyosababisha tatizo, maumivu yanaweza kurudi au kukomaa zaidi na hatimae kuwa maumivu sugu.
Kwa hiyo, matibabu yanaweza kuhitaji mchanganyiko wa hatua mbalimbali, kulingana na chanzo na hali ya mgonjwa.
Nini Kinaweza Kusaidia?
1. Endelea kufanya shughuli nyepesi nyepesi
Kwa maumivu mengi ya kawaida ya mgongo, kukaa kitandani kwa muda mrefu si suluhisho na huweza kuongeza maumivu zaidi. Kwa kawaida, kuendelea na shughuli nyepesi zinazoweza kuvumilika husaidia mtu kurejea katika hali yake ya kawaida mapema na kuzuia maumivu sugu.
Kutembea ni mfano mzuri wa shughuli rahisi ambayo watu wengi wanaweza kuanza nayo, kulingana na hali zao.
2. Fanya mazoezi yanayofaa
Mazoezi yanaweza kusaidia kuimarisha misuli inayosaidia mgongo, kulegeza misuli iliyokaza, kuongeza uwezo wa mwili kufanya shughuli na kupunguza hatari ya maumivu kujirudia au kuwa sugu.
Hata hivyo, si kila zoezi linafaa kwa kila mtu. Aina ya mazoezi inapaswa kuzingatia sababu ya maumivu, umri, uwezo wa mwili na hali nyingine za kiafya.
Mfiziotherapia atakusaidia kuamua, kukufundisha na kukupa muongozo wa mazoezi sahihi ya kufanya baada ya kukuchunguza na kufanya tathmini ya maumivu unayohisi, kujua aina ya maumivu na chanzo cha maumivu husika.
3. Jifunze kutumia mwili kwa njia sahihi na kwa usalama
Kama kazi yako inahusisha kunyanyua, kusukuma au kubeba vitu, ni muhimu kujifunza namna salama ya kufanya shughuli hizo.
Pia, kama unakaa muda mrefu kazini, jaribu kubadilisha mkao na kusimama au kutembea mara kwa mara badala ya kukaa bila mwendo kwa muda mrefu.
4. Dhibiti uzito na mtindo wa maisha
Kwa mtu mwenye uzito mkubwa, kupunguza uzito kwa njia salama kunaweza kupunguza mzigo unaowekwa kwenye mfumo wa mwili hususani mgongo na kiuno na kusaidia afya kwa ujumla.
Lishe bora, shughuli za mwili, usingizi wa kutosha na kudhibiti msongo wa mawazo ni sehemu muhimu za afya ya mgongo.
5. Usijitibu kwa muda mrefu bila uchunguzi
Ni jambo la kawaida mtu kutumia dawa alizopewa awali au kununua dawa mwenyewe kila maumivu yanaporudi. Hata hivyo, maumivu yanayojirudia au yanayodumu kwa muda mrefu yanahitaji kutathminiwa ili kutafuta chanzo chake.
Matumizi ya dawa kwa muda mrefu bila ushauri wa mtaalamu yanaweza pia kuwa na madhara na hata kutengeneza usugu wa maumivu na kupelekea dawa husika kushindwa kuzuia maumivu husika baada ya muda.
Mfiziotherapia atakusaidia kufanya tathmini ya aina ya maumivu na sababu za maumivu ili kutengeneza mpango sahihi wa matibabu ya maumivu husika.
Je, Maumivu ya Mgongo Yanaweza Kuisha Kabisa?
Ndiyo! Kwa watu wengi maumivu yanaweza kuisha na baadhi ya watu maumivu huweza kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa, lakini hakuna jibu moja linalofaa kwa kila mtu.
Kwa baadhi ya watu, tatizo huisha baada ya muda na matibabu sahihi. Kwa wengine, hasa wenye matatizo ya muda mrefu, lengo linaweza kuwa kupunguza maumivu, kuongeza uwezo wa kufanya shughuli na kuzuia tatizo lisizidi au kujirudia mara kwa mara.
Kwa hiyo, badala ya kuuliza tu “Ni dawa gani itamaliza maumivu yangu?”, ni muhimu pia kuuliza: “Kwa nini mgongo wangu unauma, na ninaweza kufanya nini ili kupona na kuzuia tatizo kurudi?” Hapo ndipo uchunguzi na mpango sahihi wa matibabu unapokuwa muhimu.
Ni Wakati Gani Unapaswa Kumuona Mtaalamu wa Afya?
Usipuuzie maumivu makali, yanayoongezeka au yanayoendelea kwa muda mrefu. Tafuta ushauri wa kitaalamu ikiwa:
- Maumivu yanaendelea au yanajirudia mara kwa mara.
- Maumivu yanaathiri kazi, kutembea au usingizi.
- Maumivu yanaenea kutoka mgongoni/kiunoni kwenda mguuni.
- Unapata ganzi, kuchomachoma au udhaifu kwenye mguu.
- Maumivu yameanza baada ya kuanguka au kupata ajali.
- Una homa au unajisikia mgonjwa sana pamoja na maumivu ya mgongo.
- Una matatizo mapya ya kudhibiti mkojo au haja kubwa, au ganzi katika eneo la sehemu za siri/kati ya mapaja. Hii inaweza kuwa hali ya dharura na inahitaji huduma ya haraka.
Fiziotherapi Ina Nafasi Gani?
Fiziotherapi ni mojawapo ya njia zinazoweza kutumika katika kutathmini na kutibu matatizo mbalimbali ya mfumo wa misuli, mifupa na viungo, ikiwemo maumivu ya mgongo na kiuno.
Mtaalamu wa fiziotherapi anaweza kutathmini hali ya mgonjwa, kubaini mambo yanayoweza kuchangia maumivu, kutoa ushauri kuhusu shughuli na mikao, na kupanga matibabu yanayolingana na mahitaji ya mgonjwa ikiwemo mazoezi sahihi.

Lengo si kupunguza maumivu tu, bali pia kumsaidia mtu kurejesha uwezo wa kufanya shughuli zake na kujifunza namna ya kupunguza uwezekano wa tatizo kujirudia.
Matibabu hulenga:
- Kupunguza/kuondoa maumivu
- Kulegeza misuli iliyokaza na kuirudisha katika utendaji wa kawaida
- Kuimarisha misuli ili kukuwezesha kufanya shughuli za kila siku kwa uhuru bila maumivu na kuzuia maumivu kutokurudi mara kwa mara.
Hitimisho
Maumivu ya mgongo au kiuno si lazima yawe sehemu ya maisha yako milele. Watu wengi hupata nafuu kwa uchunguzi sahihi, matibabu yanayofaa, mazoezi na mabadiliko ya mtindo wa maisha.
Hata hivyo, suluhisho la kudumu haliwezi kuahidiwa kwa kila mtu bila kujua chanzo cha maumivu. Usikubali kuishi na maumivu kwa muda mrefu bila kutafuta msaada wa kitaalamu.
Mwili unapotoa ishara ya maumivu, ni muhimu kuusikiliza, kutafuta chanzo na kuchukua hatua sahihi. Misuli iliyo imara huondoa uwezekano wa maumivu kujirudia mara kwa mara.
Karibu Rally Polyclinic katika kitengo chetu cha fiziotherapi tukusaidie kujua chanzo cha maumivu ya mgongo au kiuno na kupata suluhisho la maumivu ya mgongo au kiuno kwa kufuata taratibu na njia sahihi za matibabu.
Wasiliana nasi leo kupitia simu namba +255 769 753 201 kwa taarifa zaidi.

Joseph Kisima ni Mfiziotherapia (Physiotherapist) mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 13 katika tasnia ya fiziotherapi na kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za afya serikalini na sekta binafsi, ikiwemo Aga Khan na CCBRT.
Kwa sasa anaendesha Rally Polyclinic na pia hushirikiana na St. Monica Modern Health Center kutoa huduma za fiziotherapi. Ana utaalamu na uzoefu katika matibabu ya maumivu pamoja na urekebishaji wa wagonjwa wenye magonjwa yanayosababisha kupooza, hususani stroke/kiharusi.
Mbali na taaluma yake, ni mwandishi wa vitabu vya elimu ya afya kwa jamii. Ana kitabu kuhusu kiharusi ambacho hakijachapishwa, na anaandaa kitabu kingine kuhusu mtindio wa ubongo, changamoto zake na huduma kwa watoto.
