Je, Fiziotherapi ni Mazoezi, Mazoezi Tiba, au Huduma Jumuishi ya Matibabu?

DHANA ISIYO YA KWELI:

“Fiziotherapi ni mazoezi ya mwili. Mtu anaweza kufanya mwenyewe nyumbani bila kuhitaji mtaalamu wa fiziotherapi!” 

UKWELI:

Fiziotherapi si mazoezi ya kawaida tu. Ni huduma ya kitaalamu ya afya inayolenga kumsaidia mtu kurejesha, kuboresha au kudumisha uwezo wa mwili wa kufanya kazi na kushiriki katika shughuli za kila siku. 

Fiziotherapi huhusisha tathmini ya hali ya mgonjwa, kubaini changamoto zinazohusiana na maumivu, mjongeo wa mwili, nguvu za misuli, usawa wa mwili, uwezo wa kutembea na utendaji wa mwili, kisha kupanga na kutoa huduma inayofaa kulingana na mahitaji ya mgonjwa. 

Mazoezi Tiba ni Nini?

    Mazoezi tiba ni mazoezi yanayochaguliwa na kupangwa kwa madhumuni maalumu ya kitabibu. Hayafanywi tu kwa ajili ya kujenga mwili au kuongeza nguvu, bali hutumika kusaidia kutibu au kudhibiti changamoto mbalimbali za kiafya.  

    Mazoezi tiba ni sehemu ya fiziotherapi/miongoni mwa aina ya matibabu ila sio ukamilifu wa fiziotherapi.

    Kwa mfano, mtu aliyepata kiharusi anaweza kupewa mazoezi maalumu ya kusaidia kurejesha nguvu, usawaziko na uwezo wa kutembea.  

    Mtu mwenye maumivu ya mgongo anaweza kupewa mazoezi yanayolenga kuboresha mjongeo na nguvu za misuli zinazohusika ikiwa ni mojawapo ya matibabu kati ya aina nyingi za matibabu.  

    Mtu aliyefanyiwa upasuaji anaweza kuhitaji mazoezi ya hatua kwa hatua ili kurejesha matumizi ya kiungo au sehemu ya mwili kama sehemu ya matibabu. 

    Hivyo, mazoezi tiba ni sehemu ya fiziotherapi lakini fiziotherapi si mazoezi tiba pekee wala sio mazoezi. 

    Fiziotherapia Hufanya Nini Zaidi ya Kutoa Mazoezi?

      Kulingana na hali ya mgonjwa, mtaalamu wa fiziotherapi anaweza kutumia au kupendekeza njia mbalimbali za matibabu na usimamizi, ikiwa ni pamoja na: 

      • Mazoezi tiba kwa ajili ya kuongeza nguvu, mwendo, usawaziko na uwezo wa kufanya shughuli. 
      • Tiba kwa kutumia mikono (manual therapy) inapofaa, kwa mfano kusaidia kuboresha mjongeo wa viungo na utendaji wa tishu. 
      • Mafunzo ya kutembea na usawa, hasa kwa watu wenye changamoto za kutembea au walio katika hatari ya kuanguka. 
      • Elimu na ushauri kwa mgonjwa, kuhusu namna ya kujitunza, kufanya shughuli/kazi kwa usalama na kudhibiti changamoto yake. 
      • Ushauri kuhusu matumizi sahihi ya vifaa saidizi, kama vile fimbo, magongo au vifaa vya kusaidia kutembea (walking aids), inapohitajika. 
      • Matibabu kwa njia ya umeme au hali joto (baridi au moto). 
      • Huduma za urekebishaji wa uwezo wa mwili (rehabilitation) baada ya magonjwa, majeraha au upasuaji. 
      • Mbinu nyingine za kitaalamu zinazofaa kulingana na hali ya mgonjwa na mpango wake wa matibabu. 

      Je, Kila Anayefanya Mazoezi Anahitaji Fiziotherapi?

        Hapana! Mazoezi ya kawaida kwa mtu mwenye afya yanaweza kufanywa bila kuwa chini ya huduma ya fiziotherapi, japokuwa ni vyema mfiziotherapia akahusishwa katika mazoezi ya kawaida ili kutoa elimu ya njia sahihi ya kufanya mazoezi binafsi kwa usalama.  

        Hata hivyo, mtu mwenye maumivu, jeraha, udhaifu wa misuli, changamoto ya kutembea, usawa au tatizo la kufanya shughuli za kawaida anaweza kunufaika zaidi kwa kutathminiwa na mtaalamu wa fiziotherapi. 

        Jambo muhimu ni kwamba, si kila mazoezi yanafaa kwa kila mtu. Mazoezi yanaweza kubadilishwa kulingana na umri, hali ya afya, uwezo wa mwili, aina ya tatizo na hatua ya kupona. 

        Je, Fiziotherapi ni Huduma Inayojitegemea au Sehemu ya Timu ya Afya?

          Fiziotherapi ni taaluma ya afya inayoweza kutolewa kama huduma maalumu, lakini mara nyingi fiziotherapi hufanya kazi kama sehemu ya timu jumuishi ya wataalamu wa afya. 

          Kwa mfano, mgonjwa aliyepata kiharusi anaweza kuhitaji huduma za daktari, muuguzi, mfiziotherapia, mtaalamu wa tiba ya shughuli za kila siku (occupational therapist), mtaalamu wa lugha na kuongea (speech and language therapist), mtaalamu wa lishe na wataalamu wengine kulingana na mahitaji yake. 

          Katika mfumo huu, kila mtaalamu huchangia ujuzi wake ili kumsaidia mgonjwa kufikia matokeo bora ya kiafya na kurejea katika maisha ya kawaida kadiri inavyowezekana. 

          Kwa Nini ni Muhimu Kumwona Mtaalamu wa Fiziotherapi?

            Kufanya mazoezi bila mwongozo kunaweza kuwa na manufaa kwa baadhi ya watu, lakini kwa mtu mwenye tatizo maalumu la kiafya, tathmini ya kitaalamu ni muhimu. 

            Mfiziotherapia anaweza kutathmini tatizo na kusaidia kuamua: 

            1. Tatizo linaweza kuwa linatokana na nini. 
            2. Ni aina gani ya mazoezi au matibabu yanafaa. 
            3. Mazoezi yafanywe kwa kiwango gani. 
            4. Ni mambo gani yanapaswa kuepukwa. 
            5. Mgonjwa anaendeleaje baada ya kuanza matibabu. 
            6. Ni wakati gani mgonjwa anahitaji kupewa rufaa kwa mtaalamu mwingine wa afya. 

                      Hitimisho 

                      Fiziotherapi si mazoezi, wala si mazoezi tiba pekee. Ni huduma ya kitaalamu ya afya inayotumia tathmini, mbinu mbalimbali za matibabu kama vile: Umeme, hali joto, mazoezi tiba, elimu, ushauri na mbinu nyingine zinazofaa kumsaidia mtu kuboresha au kurejesha uwezo wa mwili na kushiriki katika shughuli za maisha ya kila siku. 

                      Kwa hiyo, tunaposema “fiziotherapi” tusifikirie tu mtu anayefanya mazoezi bali mtaalamu wa afya anayemtathmini mtu, anatambua changamoto za utendaji wa mwili, anaweka mpango wa matibabu na humsaidia mgonjwa katika safari yake ya kupona na kurejea katika maisha yenye uwezo na uhuru zaidi. 

                      4 thoughts on “Je, Fiziotherapi ni Mazoezi, Mazoezi Tiba, au Huduma Jumuishi ya Matibabu?”

                      1. Paulo Festo Malyosi

                        Asante Kwa elimu nzuri,Mimi kama mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya fiziotherapia nimejifunza kitu kutoka kwenye post hii

                        1. Karibu kwenye ulimwengu wa Fiziotherapi. Endelea kunifuatilia utajifunza vingi zaidi visivyofundishwa vyuoni ila ni msaada mkubwa kwa jamii endapo wakipata msaada sahihi na elimu ya kutosha

                      Leave a Comment

                      Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

                      swSW