Fiziotherapia (Physiotherapy) ni taaluma ya afya inayosaidia watu kurejesha, kuboresha na kudumisha uwezo wa mwili wa kufanya shughuli za kila siku.
Mtaalamu wa fiziotherapi, anayejulikana kama Mfiziotherapia (physiotherapist), hutumia njia mbalimbali za kutambua tatizo la mgonjwa kama vile:
Kuchukua taarifa za mgonjwa kwa njia ya mahojiano na mgonjwa au ndugu wa mgonjwa (history taking), uchunguzi kwa vitendo (physical examination), kupitia vipimo vya maabara (laboratory investigation), kumbukumbu za dawa (medication history), kupitia vipimo vya picha (radiological investigation) kama vile X – ray, CT – scan, MRI – scan, pamoja na kupitia kumbukumbu za nyuma za wataalamu wengine waliowahi kumhudumia mgonjwa kama zinapatikana (past medical history).

Mfiziotherapia hutumia njia tofauti tofauti za matibabu kama vile mazoezi maalumu, matibabu kwa njia za umeme, njia za hali joto (joto/baridi), tiba kwa kutumia mikono, ushauri wa namna sahihi ya kutumia mwili na mbinu nyingine salama za kitabibu.
Fiziotherapia inaweza kusaidia mtu mwenye maumivu, jeraha, ulemavu au changamoto za mijongeo mwili, pamoja na kusaidia kuzuia matatizo yanayoweza kuathiri uwezo wa mtu wa kutembea, kufanya kazi au kujihudumia.
Kwa mfano, kumsaidia mtu aliyepata kiharusi kurejesha uwezo wa kutembea na kutumia mkono, mtu aliyefanyiwa upasuaji kuanza kutumia kiungo vizuri, au mtu mwenye maumivu ya mgongo kuondokana na maumivu pamoja na kujifunza namna sahihi ya kujilinda, kufanya mazoezi na kutumia mwili.
Nini husababisha mtu kuhitaji fiziotherapi?
Kuna sababu nyingi zinazoweza kumfanya mtu kuhitaji huduma ya fiziotherapi. Baadhi yake ni:
- Majeraha ya michezo au ajali.
- Kupooza (kwa mkono, Kiharusi)
- Maumivu ya mgongo na shingo.
- Maumivu au matatizo ya viungo kama goti, bega na nyonga.
- Kurejesha mwili katika utimamu baada ya kuvunjika kwa mfupa/mifupa.
- Matatizo yanayotokea baada ya upasuaji.
- Magonjwa yanayoathiri mfumo wa fahamu na uwezo wa mwili kutenda kazi.
- Ulemavu wa kuzaliwa au unaotokea baadaye.
- Udhaifu wa misuli na kupungua kwa uwezo wa mwili kutokana na kukaa au kulala muda mrefu.
- Baadhi ya matatizo ya kupumua na moyo.
- Matatizo ya ukuaji na mijongeo kwa watoto.
- Haja ya kuzuia majeraha au kupunguza hatari ya kuanguka, hasa kwa wazee.
Dalili gani zinaweza kuashiria kuwa mtu anaweza kuhitaji fiziotherapia?
Mtu anaweza kufaidika na tathmini ya Mfiziotherapia ikiwa ana:
- Maumivu yanayoendelea au yanayorudia mara kwa mara.
- Hitilafu ya kutembea au kusimama.
- Kushindwa kutumia mkono, mguu au kiungo fulani vizuri.
- Kupungua kwa nguvu za misuli.
- Kukakamaa kwa misuli au viungo.
- Kupoteza usawa wa mwili.
- Ugumu wa kufanya shughuli za kawaida kama kuvaa, kuoga au kupanda ngazi.
- Changamoto za mijongeo baada ya kiharusi, jeraha au upasuaji.
Ni muhimu kutambua kuwa si kila maumivu yanahitaji fiziotherapi pekee. Wakati mwingine tathmini ya daktari au mtaalamu mwingine wa afya huhitajika kwanza ili kubaini chanzo cha tatizo.
Nani anaweza kuhitaji huduma ya fiziotherapi?
Fiziotherapi ni kwa watu wa rika zote – watoto, vijana, watu wazima na wazee.
Inaweza kumsaidia mtu mwenye ugonjwa au jeraha, lakini pia inaweza kutumika kwa ajili ya kuongeza uwezo wa mwili, kuzuia majeraha/maradhi na kudumisha afya na uhuru wa kufanya shughuli za kila siku.
Wanariadha, wafanyakazi wanaofanya kazi zinazohitaji nguvu za mwili, watu wanaokaa muda mrefu, wazee na watu wanaopitia kipindi cha kupona baada ya ugonjwa au upasuaji wanaweza pia kunufaika na huduma hizi.
Ipi nafasi ya fiziotherapi katika timu ya wataalamu wa afya?
Fiziotherapi ni sehemu muhimu ya timu ya wataalamu wa afya. Mfiziotherapia hafanyi kazi kwa kujitegemea pekee; mara nyingi hushirikiana na wataalamu wengine kulingana na mahitaji ya mgonjwa.
Kwa mfano:
- Daktari anaweza kutambua ugonjwa au tatizo la kiafya na kupanga matibabu.
- Mfiziotherapia huchunguza uwezo wa mwili wa mgonjwa na kusaidia kurejesha mijongeo, nguvu, usawa na uwezo wa kufanya shughuli.
- Muuguzi hutoa uangalizi wa kila siku na kusaidia katika utekelezaji wa mpango wa huduma.
- Mtaalamu wa tiba kwa vitendo (Occupational Therapist) humsaidia mtu kurejesha uwezo wa kufanya shughuli za kila siku na kazi.
- Mtaalamu wa lishe husaidia katika mahitaji ya lishe yanayohusiana na afya na kupona.
- Mtaalamu wa saikolojia anaweza kusaidia changamoto za kihisia na kisaikolojia zinazoweza kuambatana na ugonjwa, jeraha au ulemavu.
- Wataalamu wengine wanaweza kushirikishwa kulingana na hali na mahitaji ya mgonjwa.
Kwa hiyo, Mfiziotherapia ni mshiriki muhimu katika timu ya afya, hasa pale ambapo tatizo linaathiri mijongeo, nguvu, usawa, maumivu au uwezo wa mtu kufanya shughuli za kila siku.
Mchango wa fiziotherapi kwa jamii ni upi?
Mchango wa fiziotherapi hauishii hospitalini au kliniki. Taaluma hii ina mchango mkubwa katika kuboresha afya na ustawi wa jamii.

- Kurejesha uwezo wa kufanya shughuli za kila siku: Fiziotherapi huwasaidia watu waliopoteza uwezo kutokana na ugonjwa, jeraha au ulemavu kurejesha uwezo wao wa kutembea, kufanya kazi na kujihudumia.
- Kupunguza maumivu na ulemavu: Kwa kutumia njia sahihi za matibabu na mazoezi, fiziotherapi inaweza kusaidia kupunguza maumivu na kuboresha uwezo wa mwili.
- Kuzuia matatizo ya afya: Miziotherapia hutoa elimu kuhusu mkao sahihi, matumizi salama ya mwili, mazoezi na namna ya kuzuia majeraha.
- Kuongeza uhuru wa mtu: Mtu anapoweza kutembea, kuoga, kuvaa, kufanya kazi na kujihudumia mwenyewe, anakuwa na uhuru zaidi na utegemezi kwa familia unapungua.
- Kusaidia watu wenye ulemavu kushiriki katika jamii: Fiziotherapi inaweza kusaidia mtu mwenye ulemavu kuongeza uwezo wake wa kushiriki katika familia, elimu, kazi na shughuli nyingine za kijamii.
- Kupunguza mzigo kwa familia: Mgonjwa anapopata nafuu na kuwa na uwezo mkubwa wa kujihudumia, mzigo wa kimwili, muda na gharama kwa walezi na familia unaweza kupungua.
- Kusaidia watu kubaki na afya na uwezo wa kufanya kazi: Kwa watu wanaofanya kazi, fiziotherapi inaweza kusaidia kuzuia na kudhibiti baadhi ya matatizo ya misuli na mifupa yanayoweza kuathiri uwezo wa kufanya kazi.
Ni wakati gani mtu anapaswa kumuona Mfiziotherapia?
Mtu anapaswa kufikiria kupata ushauri au tathmini ya Mfiziotherapia anapokuwa na tatizo linalohusu au linaloathiri maumivu, mijongeo ya mwili, nguvu, usawa au uwezo wa kufanya shughuli za kawaida.
Hata hivyo, baadhi ya dalili zinahitaji huduma ya haraka ya kitabibu, badala ya kuanza fiziotherapi bila uchunguzi. Kwa mfano:
- Kupooza au udhaifu wa ghafla wa upande mmoja wa mwili.
- Kushindwa kuzungumza au kuelewa maneno ghafla.
- Maumivu makali ya kifua au kupumua kwa shida.
- Kupoteza fahamu.
- Jeraha kubwa baada ya ajali.
- Maumivu makali yanayoambatana na udhaifu au kupoteza hisia kwa ghafla.
- Dalili nyingine zozote zinazotokea ghafla na kuhatarisha maisha.
Katika hali hizi, mtu anapaswa kwenda kituo cha afya au hospitali mara moja.
Hitimisho
Fiziotherapi ni sehemu muhimu ya huduma za afya inayosaidia watu kurejesha na kuboresha uwezo wa mwili, kupunguza maumivu, kuzuia matatizo na kuongeza uwezo wa kufanya shughuli za kila siku.
Huduma hii inaweza kuwa na manufaa kwa watu wa rika na hali mbalimbali, kuanzia wenye majeraha na magonjwa hadi wale wanaotaka kudumisha uwezo na afya ya mwili.
Kwa hiyo, kama una maumivu yanayoendelea, changamoto za kutembea, kupungua kwa nguvu za misuli, kukakamaa kwa viungo au ugumu wa kufanya shughuli zako za kawaida, ni muhimu kupata tathmini ya Mfiziotherapia ili kujua chanzo cha tatizo na hatua zinazofaa.
Kumbuka, kupata msaada mapema kunaweza kukusaidia kurejesha uwezo wa mwili na kuendelea na maisha yako kwa uhuru zaidi.

Joseph Kisima ni Mfiziotherapia (Physiotherapist) mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 13 katika tasnia ya fiziotherapi na kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za afya serikalini na sekta binafsi, ikiwemo Aga Khan na CCBRT.
Kwa sasa anaendesha Rally Polyclinic na pia hushirikiana na St. Monica Modern Health Center kutoa huduma za fiziotherapi. Ana utaalamu na uzoefu katika matibabu ya maumivu pamoja na urekebishaji wa wagonjwa wenye magonjwa yanayosababisha kupooza, hususani stroke/kiharusi.
Mbali na taaluma yake, ni mwandishi wa vitabu vya elimu ya afya kwa jamii. Ana kitabu kuhusu kiharusi ambacho hakijachapishwa, na anaandaa kitabu kingine kuhusu mtindio wa ubongo, changamoto zake na huduma kwa watoto.

Well said, ahsante kwa kutuelimisha mkuu