Je, umeshawahi kujiuliza athari za punyeto kwa wanawake?
Tendo hili mara nyingi linahusishwa na wanaume na mara chache sana kuzungumziwa na hata kufanyiwa tathmini inapokuja kwa jinsia ya kike.
Je, unafahamu ni faida na hasara gani za punyeto zinazoweza kuathiri wanawake? Je, punyeto ni kitu cha kawaida?

Makala hii inazungumzia kwa uwazi ni nini maana ya punyeto, faida zake, hasara zake na ni wakati gani kama mwanamke anahitaji msaada wa kitaalamu.
Punyeto ni kitendo cha kuamsha hisia mwilini mwako mwenyewe kama vile kinena, uke na sehemu nyingine zenye kuamsha ashki ili kupata raha na kufikia kileleni. Unaweza kutumia mikono, vifaa vya tendo la ndoa na hata kwa kufikiria tu.
Kwa ujumla punyeto inakubalika inapofanywa kwa wastani na ina faida kimwili, kiakili na kiafya; japokuwa ni kama tabia nyingine tu, ikifanywa kupita kiasi ina hasara pia.
Faida za Punyeto kwa Wanawake
Kuongeza Hisia Katika Tendo la Ndoa
Punyeto inasaidia mwanamke kufahamu mwili wake vizuri, ni sehemu gani na ni namna gani anaweza kupata raha zaidi. Hii inasaidia kuwasiliana na mweza wake kikamilifu wakati wa tendo na kuleta raha na uhakika wa kufika kileleni.
Kuongeza “Maji Maji” Ukeni
Hasa kwa wanawake wenye changamoto ya uke kuwa mkavu au wanaokaribia kukoma hedhi, mara nyingi hupata changamoto ya mabadiliko ya homoni yanayo pelekea ukavu ukeni.
Punyeto inayofanywa kwa usahihi hasa kabla ya tendo la ndoa inaweza kusaidia kuongeza ute ukeni na kusaidia tendo la ndoa kuwa lenye starehe na kufurahisha.
Kuimarisha Misuli Ya Nyonga
Misuli ya nyonga ndio inasaidia kudhibiti mkojo, choo kikubwa na inahusika katika kupata raha zaidi mwanamke anapofika kileleni.
Punyeto inayofanywa kwa wastani na mara kwa mara inapohitajika inasaidia kuimarisha uwezo wa tendo la ndoa na kudhibiti kibofu cha mkojo vizuri zaidi.
Kupunguza Maumivu Wakati wa Tendo la Ndoa
Kuna baadhi ya wanawake, kutokana na sababu mbalimbali, wana changamoto ya kupata maumivu makali wakati wa tendo la ndoa na wenza wao.
Punyeto inamsaidia mwanamke ku-relax na kumuandaa vema hata kupunguza maumivu makali wakati wa kujamiiana.
Kupunguza Maumivu ya Wakati wa Hedhi
Wakati wa punyeto, hasa mwanamke akifika kileleni, misuli ya mji wa mimba hujifinya na kusaidia damu kutoka vizuri zaidi, pia kuna homoni ya endorphin hutolewa ambayo inasaidia kupunguza maumivu mwilini.
Kupunguza Stress
Wakati wa kilele cha punyeto mwili wa mwanamke hutoa homoni ya dopamine na oxytocin ambazo zinasaidia sio kusikia raha tu bali na kupunguza stress kwa ujumla.

Madhara ya Punyeto Kwa Mwanamke
Kuvimba sehemu za Siri
Punyeto inayofanywa kwa kutumia nguvu au vifaa vya tendo la ndoa kwa muda mrefu husababisha sehemu za siri kuchubuka, kuwasha na hata kuvimba.
Vile vile ikiwa mtu ana kucha ndefu, huenda kukatokea michubuko mingi na vidonda vidogo vidogo.
Magonjwa ya Mfumo wa Mkojo (UTI)
Bila usafi wa kutosha, hasa kwa punyeto inayohusisha kushika uke au kuingiza vifaa vya tendo la ndoa ukeni, inaweza kupelekea magonjwa ya mfumo wa mkojo kwa sababu mrija wa kutolea mkojo uko karibu sana na uke.
Pia usafi hafifu unaweza kusababisha magonjwa mengine kwenye mfumo wa kizazi kama vile uke wenyewe, shingo ya kizazi na mji wa mimba.
Kupata Uraibu (Addiction)
Kama tabia nyingine tu, punyeto inayofanyika mara kwa mara bila kipimo inaweza kupelekea uraibu/uteja na kuathiri mahusiano, kazi na afya ya akili kwa ujumla.
Punyeto sio mbadala wa tendo la ndoa, bali ni njia mojawapo ya mwanamke kujitambua mwili wake na kujisaidia kufurahia tendo la ndoa kikamilifu.
Kupungua kwa ashki/hisia
Ikiwa punyeto inafanyika mara kwa mara, kwa kutumia nguvu au vifaa vya tendo la ndoa vyenye msuguano mkubwa, baada ya muda kinena kinazoea na kuhitaji nguvu nyingi itumike ili kupata raha na kufika kileleni.
Nguvu hii husababisha mishipa ya fahamu kushindwa kuleta raha kwenye tendo la ndoa na mweza, na hata kuhitaji vifaa vyenye nguvu zaidi.
Kulazimisha Kufika Kileleni
Mara nyingi wanawake wenye changamoto ya kufika kileleni kwenye tendo la ndoa na wenza, huweza kupata raha zaidi na kujifikisha kupitia punyeto.
Japokuwa punyeto sio mbadala wa tendo la ndoa, moja ya madhara yake ni kulazimisha kufika kileleni kila wakati.
Ikumbukwe kuwa lengo kuu la punyeto ni kujifunza zaidi juu ya mwili wako linapokuja suala la mapenzi.
Kusikia Aibu na Fedheha
Hii hutokea, hasa, kwa wanawake waliolelewa na kukulia katika mazingira ya dini; na hata mazungumzo ya suala la tendo la ndoa na wazazi/walezi wao ni hafifu. Mara nyingi kujisikiaa fedheha na aibu baada ya kufanya kitendo hicho na kuhisi ni makosa makubwa kufanya punyeto.
Hii ni moja ya madhara makubwa ya kufanya punyeto na huenda kupelekea mtu kukosa kujiamini kabisa.
Ni Wakati Gani Unahitaji Msaada?
Hata kwa wanawake, uraibu/uteja wa punyeto hutokea; ni pale ambapo unajisikia hamu ya kufanya punyeto mara kwa mara mpaka inaathiri utendaji wako kazini au shuleni, mahusiano yako na hata namna unavyojisikia binafsi.
Mara nyingi mwenye uteja hujisikia vibaya na fedheha na kujuta kufanya kitendo hicho au kupata msongo wa mawazo baada ya punyeto. Mtu anafikia mahala kushindwa kujizuia kuendelea na majukumu yake ya kawaida kila siku ili apate muda tu wa kufanya punyeto.
Na mwisho kabisa kuwa na matarajio makubwa sana ya tendo la ndoa kutoka kwa mweza wake ambayo sio halisi kufikiwa kama vile anapofanya punyeto yeye mwenyewe.
Hizi ni dalili mbaya na zinaashiria uraibu. Ikiwa una dalili hizi ni vyema kupata msaada wa kitaalamu hasa kutoka kwa madaktari wabobezi kwenye masuala ya uraibu (addiction) au wataalamu wa masuala ya jinsia na mapenzi hasa tendo la ndoa.

Analytical, energetic, and detail-oriented medical doctor and researcher with experience supporting qualitative and quantitative research-related activities. My skill set spans from conducting interviews, coding qualitative data materials, and analyzing qualitative and quantitative data materials as well as English- Swahili transcription and translation.
Also, I have experience in stakeholder meetings, workshop facilitations, evidenced-based dissemination and policy and strategic planning.
