Safari ya Tanzania katika kupambana na ukoma ni mfano mzuri wa mafanikio kwenye afya ya jamii. Miaka ya nyuma, ugonjwa huu ulileta ulemavu mkubwa, unyanyapaa, na changamoto nyingi za kijamii.
Hali hii imebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji wa Serikali kupitia NTLP, ukisaidiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), WHO, na jamii zenyewe.
Hata hivyo, mafanikio haya yanatuletea swali moja la msingi: Je, tumemaliza safari yetu au sasa ndio tunaingia kwenye hatua ngumu zaidi?
Ukweli ni kwamba Tanzania imepata matokeo makubwa. NTLP imefanya kazi kwa miaka zaidi ya 50 na kufanikiwa kushusha maambukizi mapya kutoka visa 2,457 mwaka 2015 hadi visa 1,511 mwaka 2021.
Mapema mwaka 2006, nchi yetu ilifikia lengo la WHO la kutokomeza ukoma kitaifa. Huu ulikuwa ushindi mkubwa wa afya ya jamii unaostahili pongezi.
Ushindi huo haumaanishi kuwa kazi imeisha, bali umetufungulia njia ya safari ndefu zaidi. Hadi sasa, Tanzania bado ipo kwenye orodha ya nchi 12 duniani zinazoripoti zaidi ya maambukizi mapya 1,000 kila mwaka.
Mbaya zaidi, mgonjwa 1 kati ya kila wagonjwa 10 anagundulika akiwa tayari ana ulemavu wa kudumu. Hali hii ingeweza kuepukika kabisa kama wangepata utambuzi na matibabu mapema.
Kutokana na hali hii, Tanzania kupitia NTLP imejiwekea lengo thabiti la kutokomeza kabisa maambukizi mapya ya ukoma na kufikia sifuri ifikapo mwaka 2030, ili kuendana na mkakati wa kimataifa wa WHO.
Tujiulize Kwanza: Tumetoka Wapi, Tunaenda Wapi?
Fikiria daktari wa zahanati ndogo huko vijijini mwaka 1985. Ana wagonjwa wa ukoma wanaokuja wakiwa wamejificha uso, wakiingia usiku ili majirani wasije wakawaona. Huyu daktari ana dawa, lakini hana mfumo wa kuwapata watu ambao bado hawajafika mlangoni mwake. Vilevile ana ujuzi, lakini hana njia ya kuwafikia.
Picha hiyo imebadilika kwa kiasi kikubwa. NTLP, iliyoanzishwa na Wizara ya Afya mwaka 1977, imekuwa nguzo ya mapambano dhidi ya ukoma na kifua kikuu kwa wakati mmoja na kwa ushirikiano na wadau kama Novartis, GLRA (German Leprosy Relief Association), Swiss TPH, na Global Partnership for Zero Leprosy (GPZL).
Kwa miaka mingi, mfumo huu umeweza kupeleka matibabu ya bure (MDT – Multidrug Therapy) hadi maeneo ya mbali, kutoa mafunzo kwa watoa huduma ya Afya, na kupunguza unyanyapaa kwa kiwango fulani.
Juhudi za Tanzania zimezaa matunda ya kweli. Nchi yetu ilishinda vita dhidi ya ukoma katika ngazi ya kitaifa tangu mwaka 2006, jambo ambalo lilishangaza wengi. Hatua hii ina maana kuwa ugonjwa huo umepungua hadi kufikia chini ya kisa kimoja kwa kila watu 10,000, kama WHO inavyoelekeza.
Mafanikio haya makubwa yanathibitisha kazi kubwa iliyofanyika na yanastahili kupongezwa sana.
Lengo la Leo si Lile la Jana
Hapa ndipo changamoto kubwa inapoanza kujitokeza. Kutokomeza ukoma kitaifa, ambalo lilikuwa lengo letu mwaka 2006, kulimaanisha kupunguza kasi ya maambukizi. Hali hii ni kama kupunguza nguvu ya moto mkubwa wa nyikani ili uweze kudhibitiwa kwa urahisi.
Hata hivyo, lengo jipya la Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mwaka 2021 hadi 2030 lina mwelekeo tofauti kabisa. Safari hii tunataka kuuzima moto huo kabisa, kwa kukata mnyororo wa maambukizi ili kuzuia ugonjwa huu usienee tena kwa mtu yeyote.
Mkakati huo mpya wa WHO unasisitiza kuwa na dunia isiyo na ukoma kabisa kupitia nguzo kuu 4:
- Kutengeneza na kufuata mipango ya kitaifa ya kutokomeza ukoma kabisa
- Kuongeza nguvu katika kuwatafuta na kuwatambua wagonjwa mapema
- Kusimamia matibabu kwa ukaribu na kuzuia ulemavu mpya
- Kupiga vita unyanyapaa dhidi ya wagonjwa
Tanzania ilionyesha nia thabiti kwa kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa wa kutokomeza ukoma, hatua ambayo ni muhimu sana kisheria na kimkakati. Kupitia mpango huu, Tanzania inaenda sambamba na mkakati wa kimataifa wa kufikia Malengo Matatu ya Sifuri ifikapo mwaka 2030:
- Sifuri kwenye maambukizi mapya
- Sifuri kwenye ulemavu mpya kwa watoto
- Sifuri kwenye unyanyapaa au ubaguzi
Kuna tofauti kubwa kati ya kuwa na maandishi mazuri ya sera na utekelezaji halisi wa mipango hiyo. Hilo ndilo pengo kubwa linalozungumziwa hapa. Kubadilisha mwelekeo kutoka kwenye ‘kudhibiti’ ugonjwa na kwenda kwenye ‘kuutokomeza’ kabisa si sawa na kuongeza mwendo wa gari lilelile unaloendesha.
Hatua hii ni sawa na kubadilisha injini nzima ya gari hilo. Mbinu zilizosaidia kudhibiti ugonjwa huko nyuma hazitoshi kuutokomeza kwa sasa, na hapo ndipo kazi nzito inapoanza.
“Ni kweli tumepiga hatua kubwa, lakini safari hii inayomalizia ndiyo yenye milima mirefu zaidi. Vita hii ya mwisho dhidi ya ukoma haihitaji mazoea yetu ya kila siku, inahitaji mapinduzi ya kweli. Tunahitaji nguvu mpya, ari mpya, na mbinu mpya kabisa zitakazotutoa hapa tulipo na kutufikisha kwenye ushindi wa mwisho.” – Shirika la Afya Duniani (WHO)
Changamoto ya Sasa: Pengo la Mfumo
Kuna swali moja ambalo wasimamizi wa afya wanajiuliza wenyewe usiku wa manane: “Kama dawa zipo, kama matibabu yanatolewa bure, kama watoa huduma tumepatiwa elimu”, Sasa ni kwa nini bado kuna watu wanaogundulika na ulemavu wa kudumu?
Jibu halionekani kwenye takwimu peke yake. Linaonekana ukiangalia mfumo mzima, kutoka vijiji hadi hospitali kuu za mjini.
Wagonjwa Wanafika Hospitali Wakiwa Wamechelewa
Kipimo kikubwa cha ufanisi wa mapambano dhidi ya ukoma ni idadi ya wagonjwa wapya wanaofika hospitalini wakiwa tayari wamepata ulemavu wa kudumu unaoonekana kwa macho, kama vile vidole vilivyolika na kuwa vifupi, vidonda visivyopona, au matatizo ya kuona.
Hali hii inajitokeza wazi nchini Tanzania ambapo takriban asilimia 8 hadi 10 ya wagonjwa wote wapya wanaogundulika kila mwaka wanakuwa tayari wamepata ulemavu huu wa kudumu.
Hii ina maana kwamba mgonjwa mmoja kati ya kila wagonjwa 10 anachelewa kufika hospitalini, kiwango ambacho ni kikubwa sana ikilinganishwa na malengo ya kimataifa yanayotaka kusiwe kabisa na ulemavu mpya, jambo linaloonyesha uhitaji mkubwa wa jamii kuwahi vituo vya afya ili kuzuia ulemavu kabla haujatokea.
Hii si takwimu tu bali ni hadithi, hebu fikiria mtoto wa miaka 13 anayefika kliniki leo akiwa tayari na vidole vilivyolika na kufupika. Huu si ulemavu uliotokea usiku mmoja. Ni matokeo ya ugonjwa uliomuingia mwilini miaka mingi iliyopita, ukajificha chini kwa chini bila kuonyesha dalili kwani Ukoma una kipindi kirefu sana cha uatamizi (incubation period), mara nyingi huchukua miaka 3 hadi 5, na wakati mwingine hadi miaka 20 kabla ya dalili kuanza kuonekana.
Mtoto huyu hakuwa na kosa, alipata maambukizi haya utotoni kutoka kwa mtu wa karibu anayemnyanyua na kumkumbatia kila siku. Vidole vyake kufupika leo ni ushahidi wa wazi kwamba tulichelewa kumtafuta na kumtibu yule aliyemuambukiza mapema vya kutosha.
Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Public Library of Science One (PLOS ONE) la mwaka 2024 na watafiti wa Chuo cha Muhimbili Health and Allied Science (MUHAS) kwa ushirikiano na NTLP, ulichunguza wagonjwa wa ukoma 6,963 nchini kati ya mwaka 2017 na 2020 na kuthibitisha kuwa ulemavu huu unazuilika.
Kikwazo kikubwa hapa nchini si ukosefu wa dawa au wataalamu, bali ni matumizi ya mifumo ya kizamani ya ufuatiliaji inayoshindwa kuendana na kasi ya mahitaji ya sasa ya jamii.
Hali hii inakuwa mbaya zaidi tunapoangalia maambukizi mapya kwa watoto, ambayo ni kiashiria tosha kwamba ugonjwa bado unaenezwa kikamilifu kwenye ngazi ya familia kwa sababu wagonjwa wazima hawagunduliki mapema.
Jinsi Unyanyapaa Unavyozuia Matibabu ya Ukoma
Kuna nguvu moja ambayo haionekani kwenye takwimu lakini inazuia maendeleo ya kupambana na ugonjwa huu kuliko chochote kingine: unyanyapaa.
Hii si hisia tu ya ndani, bali ni nguvu kubwa ya kijamii inayowaendesha watu na kuathiri maamuzi yao ya kila siku.

Fikiria mtu anayepata madoa kwenye mguu wake na kudhani ni ugonjwa wa kawaida wa ngozi. Wiki mbili zinapita madoa yakiendelea kusambaa, na anapomwambia mke wake, anajibiwa, ‘Usimwambie mtu, watafikiria ni ukoma.’
Baada ya miezi sita ya kuficha ugonjwa kwa hofu ya maneno ya watu, anafika kliniki akiwa tayari na ulemavu unaoanza, ambapo daktari anamweleza kuwa dawa ni bure na zinatibu vizuri, lakini athari iliyohofiwa imeshajitokeza.
Taarifa ya mapitio ya kati ya mwaka 2023 ya NTLP inabainisha wazi kwamba unyanyapaa na ubaguzi ndizo sababu kuu zinazofanya watu wasiende kutafuta matibabu mapema. Hili si tatizo la ukosefu wa elimu pekee, bali ni imani za kina za kijamii zilizojengwa kizazi hadi kizazi, ambazo utatuzi wake unahitaji mkakati wa mawasiliano unaogusa roho za watu na kutumia sauti za wale wanaofahamika katika jamii zao.
Ufuatiliaji wa Mawasiliano: Mstari wa Mbele wa Kutokomeza Ukoma
Kuna ukweli muhimu ambao mara nyingi haupewi uzito unaostahili katika mapambano dhidi ya ukoma. Watu wanaoishi au kuwa karibu na mgonjwa wa ukoma wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi kuliko watu wengine katika jamii.
Wakati huohuo, ushahidi wa kisayansi unaonesha kuwa dozi moja ya Rifampicin yani Single -Dose Rifampicin inayotolewa kwa watu hawa inaweza kupunguza hatari ya kupata ugonjwa kwa karibu asilimia 60. Hii inaifanya contact tracing kuwa moja ya silaha muhimu zaidi katika hatua ya kuelekea kutokomeza ukoma.
Kwa mtazamo wa afya ya umma, kila mgonjwa mpya anayegunduliwa hapaswi kuonekana kama mgonjwa mmoja pekee. Anawakilisha mtandao mzima wa watu waliowahi kuwasiliana naye ambao wanaweza kuwa katika hatari ya kuambukizwa.
Hivyo, kila kisa kipya kinatoa fursa ya kufanya uchunguzi wa waliokaribiana naye, kugundua wagonjwa wengine mapema, na kutoa kinga kwa wale ambao bado hawajaonyesha dalili.
Endapo hatua hizi zitafanyika kwa ukamilifu na kwa wakati, uwezo wa kukatiza mnyororo wa maambukizi utaongezeka kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo, hapa ndipo changamoto kubwa ilipo. Kwa mujibu wa National Strategy Plan Six (NSP VI) 2020–2025, mfumo wa Tanzania kwa muda mrefu umeegemea zaidi katika passive case detection, ambapo wagonjwa husubiriwa kufika kwenye vituo vya afya. Ingawa sera mpya imeanza kuhimiza active case finding pamoja na matumizi ya SDR-PEP, utekelezaji wake bado haujafikia kiwango kinachohitajika.
Uzinduzi wa mradi wa Morogoro Leprosy Elimination Project (MoLEP) ya mwezi Septemba 2024 mkoani Morogoro umeonesha mwelekeo mzuri kwa kuanza kujaribu mfumo wa contact tracing katika wilaya tatu.
Hata hivyo, Tanzania ina zaidi ya wilaya 180. Hali hii inaonesha wazi kuwa bado kuna pengo kubwa kati ya sera tulizonazo na kiwango cha utekelezaji kinachohitajika ili kufikia lengo la kutokomeza ukoma.
Kutoka Ukusanyaji Data Kwenda Maamuzi ya Wakati Halisi
Tanzania imepiga hatua muhimu katika kuimarisha mifumo ya taarifa za afya kupitia matumizi ya District Health Information software 2 (DHIS2), ambayo imeongeza uwezo wa kukusanya na kuhifadhi takwimu za ukoma kutoka ngazi mbalimbali za huduma.
Hata hivyo, thamani ya data haipo katika kukusanywa kwake pekee. Thamani yake halisi inaonekana pale inapogeuzwa kuwa taarifa zinazoweza kuongoza maamuzi, kuelekeza rasilimali, na kusaidia hatua za haraka za afya ya umma.
Mapitio ya Kati ya NTLP ya mwaka 2023 yalibainisha hitaji la kuimarisha miundombinu ya intaneti na mifumo ya ukusanyaji wa taarifa kwa wakati halisi. Katika hatua ya kuelekea kutokomeza ukoma, viongozi wa afya wanahitaji kuona kinachoendelea wakati kinatokea.
Msimamizi wa afya wa wilaya anapaswa kuwa na uwezo wa kufuatilia mwenendo wa visa vipya ndani ya wiki husika, huku ngazi ya mkoa ikitambua mapema maeneo yanayoonesha ongezeko la maambukizi ili hatua zichukuliwe kabla changamoto haijapanuka zaidi.
Kadri idadi ya wagonjwa inavyopungua, ndivyo umuhimu wa taarifa za wakati halisi (real time data) unavyoongezeka. Maamuzi yanayotegemea data iliyochelewa mara nyingi huja baada ya fursa ya kuzuia maambukizi kupita.
Katika hatua hii ya safari ya kutokomeza ukoma, kasi ya kupata taarifa na kasi ya kufanya maamuzi ni mambo yanayoweza kuamua tofauti kati ya kudhibiti ugonjwa na kuutokomeza kabisa.
Kuziba Pengo la Uzoefu Katika Utambuzi wa Ukoma
Moja ya changamoto zisizoonekana kirahisi katika hatua ya sasa ya mapambano dhidi ya ukoma ni kwamba mafanikio yenyewe yamezalisha changamoto mpya. Kadri idadi ya wagonjwa ilivyopungua, ndivyo nafasi za watoa huduma wengi wa mstari wa mbele kukutana na wagonjwa wa ukoma zilivyopungua pia.
Wengi wamejifunza kuhusu ugonjwa huu darasani au kwenye vitabu, lakini hawajawahi kuuona katika mazingira halisi ya kazi. Matokeo yake, dalili za awali ambazo mara nyingi huwa dhaifu na zisizo wazi, kama madoa, kupotea kwa nywele katika baadhi ya maeneo ya ngozi, au mabadiliko madogo ya hisia kwenye vidole, zinaweza kupuuzwa au kuchanganywa na magonjwa mengine ya ngozi au hata neva.
Programu ya MoLEP imeanza kushughulikia changamoto hii kwa kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya na wahudumu wa afya ngazi ya jamii, hatua ambayo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa utambuzi wa mapema.
Hata hivyo, katika mazingira ambayo wagonjwa wa ukoma wanaonekana mara chache, mafunzo ya muda mfupi pekee hayawezi kutosha.
Kinachohitajika ni mifumo endelevu ya usaidizi wa maamuzi, rejea za kidijitali, na mbinu za kujifunza kazini zinazomwezesha mhudumu kufanya uamuzi sahihi hata miezi au miaka baada ya mafunzo, na hata pale ambapo hajawahi kukutana na mgonjwa wa ukoma kwa muda mrefu.
Kwenye makala yangu mpya ya “Mapambano Dhidi ya Ukoma Tanzania: Mapendekezo ya Kimkakati“, nimeelezea kwa kina njia muhimu zinazounganisha teknolojia, wananchi na wadau mbalimbali kwenye mapambano dhidi ya ukoma. Unaweza kuisoma hapa.
I am a healthcare provider. I focus on sharing clear, evidence based health information through articles and social media.
My goal is to help you understand healthily life. I believe accurate health information improves decisions and lives.
