Kuna baadhi yetu tunapohisi dalili za malaria, tunakimbilia katika maabara kupima na kwenda kwenye maduka ya dawa kwa ajili ya kupata dawa mseto.
Ni kawaida ya wengi kutafuta tiba mbadala ya malaria kabla ya kwenda hospitali kutokana na sababu mbalimbali za umbali, uchumi na kukwepa adha nyingine.

Je, umeshawahi kujiuliza kwanini unatakiwa kuwahi kituo cha kutolea huduma za afya mara tu unapojihisi una dalili za malaria?
Au wale unaosikia wana malaria kali mpaka wanalazwa chumba cha uangalizi (ICU), ni nini hasa huwa kimewapata?
Kufahamu dalili za malaria kwa ujumla wake, soma makala yangu ya “Malaria: Visababishi, Jinsi ya Kujikinga, na Matibabu”.
Aidha kabla ya kujua ni dalili gani za malaria zinahitaji huduma kwa haraka,tambua kuwa kuna aina mbili za malaria, malaria kali na malaria isiyo kali. Mara zote, aina zote za hizi za malaria zinahitaji kutibiwa kitalaamu kadri inavyohitajika.
Malaria isiyo kali isipopatiwa matibabu isa kwa wakati, vimelea vya malaria vinaendelea kushambulia mifumo mbalimbali ya mwili na kusababisha uharibifu wa viungo na utaratibu wa mwili na kupelekea malaria kali.
Hata kama ikiwa tayari uko ndani ya matibabu ya malaria, dalili zifuatazo zinahitaji huduma ya haraka zaidi:
1. Mwili kuishiwa nguvu kabisa: Bila shaka kama umeshawahi kuumwa malaria, umepatwa na dalili ya mwili kuchoka. Lakini kuishiwa nguvu kabisa ni dalili ya kuwa malaria imekuwa kali.

Malaria kali pia hunapelekea upungufu mkubwa wa damu ambao dalili yake kubwa ni kuchoka sana kwa sababu mwili unashindwa kulisha nishati misuli yake. Hivyo basi, unapoona mwili unakosa nguvu kabisa au kuchoka sana ambapo hupati nafuu hata baada ya kupumzika, ni wazi unahitaji huduma kwa haraka zaidi.
2. Ngozi kuwa ya njano: Dalili nyingine inayohitaji huduma ya afya kwa haraka hata kama tayari umeshaanza kupata matibabu ya malaria ni rangi ya ngozi yako kubadilika kuwa njano; kama una ngozi nyeusi dalili hii ni ngumu kuonekana katika ngozi ila inaonekana vizuri zaidi kwenye macho na viganja.
Unapoona dalili hii basi tambua kuwa unahitaji huduma ya afya na uangalizi wa kitaalamu kwa haraka.
3. Kuchanganyikiwa: Ulishawahi kusikia wanasema “malaria imempanda kichwani?”, hii ni pale mtu amachanganyikiwa, anapata degedege au kupoteza fahamu kabisa (coma).
Ni kwa sababu katika mchakato wa vimelea vya malaria kuendelea kusambaza ugonjwa mwilini na kusababisha mishipa midogo inayopeleka damu kwenye ubongo kuziba.
Ubongo unakosa oksijeni na chakula cha kutosha, maji kujaa na kupelekea ubongo kuvimba, seli zake kushindwa kufanya kazi vizuri. Kitaalamu hii huitwa Malaria ya Ubongo (Cerebral Malaria) , ni dalili hatari kabisa na isipopatiwa matibabu mapema na kwa haraka, husababisha madhara makubwa zaidi kwenye mfumo wa fahamu hata baada ya malaria kutibiwa.
Ndio pale unasikia, “Baada ya malaria kumpanda kichwani hajakaa sawa mpaka leo hii!”.
4. Kupumua kwa shida: Malaria kali inaweza kusababisha changamoto za upumuaji kwa mgojnwa. Yaani kama ulishawahi kuumwa malaria na hujapatwa na hii dalili ni jambo la kushukuru.
Kwa sababu, vimelea vya malaria vinasababisha mapafu kujaa maji na kupelekea kushindwa kufanya kazi yake vizuri. Unajisikia kama unabanwa kifua, hewa haingii vizuri.
Pia mapafu yako yanaweza kuvimba na kushindwa kuingiza hewa, hali hii ni lazima uwe katika uangalizi na kuwekewa mashine ya kukusaidia kupumua.
Unaweza kushangaa malaria tu inaweza kumpelekea mtu kuwekwa ICU na mashine ya kupumulia juu? Ndio. Hivyo, ukiona unapata dalili hii ya kupumua kwa shida wahi hospitali haraka.
5. Kutapika kila kitu unachokula: Mara nyingi kutapika ni dalili inayoonekana mara kwa mara kwenye malaria kutokana na homa na sababu nyingine.
Lakini kutapika kila kitu maana yake hata dawa za kumeza za malaria kama mseto ni ngumu kufanya kazi mwilini kwa kuwa unazitapika kabla ya kuchakatwa, hivyo unahitaji dawa za sindano au dripu.
Vile vile kutapika sana kunapelekea maji na madini mengine mwilini kupungua kwa kasi. Hali hii inapelekea hali ya mwili kudhoofika zaidi.
Ukiona unatapika na una dalili nyingine za malaria , wahi haraka katika kituo cha kutolea huduma za afya kabla malaria haijawa kali.
6. Kushindwa kula (au kunywa) na kushindwa kunyonya kwa watoto wachanga
Kwa watoto wachanga inaweza kuwa ni ngumu kutambua kama malaria imewapanda kichwani maana huwezi ona kama amaechanganyikiwa.
Pia dalili kama ya ngozi kuwa ya njano inaweza kuwa ni changamoto kugundua kwa haraka. Kutapika na kushindwa kupumua au kupumua kwa shida inaweza ikawa rahisi kwako mzazi kuona.
Kushindwa kunyonya pia ni dalili hatari sana kwa mtoto, zaidi ya kuwa ana malaria kali, ina maana hawezi kurejesha nguvu ya mwili wake, anakosa chakula na virutubisho vingine na anahitaji msaada wa kitaalamu ili aweze kupata chakula kwa wakati huo na dawa.
Mwisho
Haijalishi ni malaria kali au la, unahitaji msaada wa kitabibu kurejesha hali ya afya yako na kuzuia vimelea vya malaria kuendelea kuharibu mifumo mingine ya mwili na viungo muhimu kama vile figo, ini, moyo na kadhalika.
Usisubiri hadi malaria iwe kali au mpaka uone au kuhisi dalili za malaria kali. Unatakiwa kuwahi haraka kwenye Kituo cha huduma za Afya mara tu unapoona dalili ili uweze kupatiwa vipimo na matibabu sahihi. Kuchelewa kuwahi kupata huduma kutapelekea kufikia dalili tajwa hapo juu na hivyo mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
Ni muhimu kukamilisha dozi yote ya vidonge ili upone. rudi kwa mtaalamu wa afya kwa muda aliokupangia kufuatilia maendeleo yako kwani usipofanya hivyoi hivyo kuna hatari ya hizi dalili za hatari kurejea maradufu zaidi au/na kupelekea usugu wa dawa kwa mdudu wa malaria.
Kauli mbiu ya mwaka huu kwenye Siku ya Malaria Duniani, Aprili 25, ni“Tumedhamiria Kutokomeza Malaria, Wakati ni Sasa, Tunaweza!”.
Vipimo, dawa na huduma nyingine za Malaria sasa zinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma nchini Tanzania, hivyo basi usisite kumshirikisha na mwingine baada ya kusoma makala hii ili na yeye aweze kuchukua hatua stahiki pale atakapoona dalili hizi hatari za Malaria.
Kumbuka, sio kila homa ni malaria! Unapoona dalili hizo, wahi kituo cha kutolea huduma za afya kwa uchunguzi zaidi na matibabu sahihi wakati wote.

Analytical, energetic, and detail-oriented medical doctor and researcher with experience supporting qualitative and quantitative research-related activities. My skill set spans from conducting interviews, coding qualitative data materials, and analyzing qualitative and quantitative data materials as well as English- Swahili transcription and translation.
Also, I have experience in stakeholder meetings, workshop facilitations, evidenced-based dissemination and policy and strategic planning.
